Featured Post

KISWAHILI KINAJITOSHELEZA KUWA LUGHA YA KIMATAIFA



NA MWANDISHI WETU
KISWAHILI  ni moja ya lugha kuu tatu maarufu miongoni mwa jamii za Afrika ambapo nyingine ni pamoja na Kihausa na Kiarabu. Hata hivyo, Kiswahili kimekuwa kinapata umaarufu na hata kukubalika kuliko ilivyo kwa  Kihausa na Kiarabu kote Barani Afrika na hata miongoni mwa nchi nyingine nje ya bara la Afrika.  Kutokana na hali hiyo, Kiswahili kinaonekana kuwa moja ya lugha kubwa ndani ya Afrika.

Inakadiriwa kuwa idadi ya watu wanaozungumza Kiswahili kwa sasa inafikia milioni 110 na katika uzungumzaji wake. Kiswahili ni lugha inayozungumzwa na kufundishwa miongoni mwa Waafrika wenyewe, Mashariki ya Mbali, Ulaya na Marekani.
Mada iliyowasilishwa na Dk. Sigalla Huruma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hivi karibuni kwenye Mkutano wa Jamii Anuai inabainisha kwamba miongoni mwa jamii za Afrika Mashariki, Kiswahili kimeibuka kuwa lugha ya Afrika Mashariki katika mazingira ya kawaida.
Kwa mfano, nchini Uganda, Kiganda kinatumika zaidi na hata hivyo kimeshapoteza umaarufu kutokana na kujikita zaidi miongoni mwa kabila la Baganda.
Katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ambako kuna lugha za kienyeji zaidi ya 120 serikali ya nchi hiyo imependekeza lugha kuu za taifa ziwe nne ambazo ni Choking, Chilumba, Lingala na Kiswahili. Miongoni mwa lugha hizo nne Kiswahili ndio kimekuwa kinapata umaarufu na kinakua zaidi na kwa haraka miongoni mwa jamii za nchi hiyo.
Aidha Kiswahili hakipanuki tu miongoni mwa jamii bali pia kinapanuka kama lugha ya biashara na katika mkondo huo inaelezwa kuwa tangu mwaka 1959 kimetokea kuwa daraja lililowaunganisha viongozi wa harakati za ukombozi Afrika.
Washiriki kwenye harakati hizo walitoka miongoni mwa nchi zilizozungumza Kifaransa na zilizozungumza Kiingereza. Aidha wanaharakati hao waliweza kuwasiliana kwa msaada wa wajumbe kutoka kila upande ambao walikuwa wanakifahamu Kiswahili na  hivyo kuwatafsiria wenzao.
Dk. Huruma anabainisha kuwa madai kwamba Kiswahili sio tu lugha ya Taifa ya Tanzania na Kenya bali ni lugha ya Afrika Mashariki na Kati ni ya kweli na inakubalika hivyo.
Wasomi wengi ndani ya Afrika Mashariki na Kati na hata nje wanabainisha ukweli kwamba Kiswahili kinazungumzwa na kueleweka Mashariki na Kati na sehemu nyingine duniani na wanabainisha ukweli kwamba ni lugha ambayo katika Afrika ina mchango muhimu kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiteknolojia, hivyo inafaa kutumika si kama lugha rasmi Afrika Mashariki na Kati pekee bali katika bara lote la Afrika.
Kwa mfano wataalamu wa lugha ya Kiswahili kama Mulokozi, Ryanga na Chacha wanatoa mifano halisi inayoonesha kwamba Kiswahili kinatumika Afrika Mashariki na Kati katika majadiliano na mihadhara ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Zipo nchi zaidi ya 11 katika eneo la Afrika Mashariki na Kati  ambako Kiswahili kimepanuka na kinazungumzwa kueleweka.  Katika msingi wa aina hiyo nchi  hizo ambazo zinaunda kundi la nchi zinazozungumza Kiswahili  ni pamoja na Burundi, Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Kenya, Malawi, Msumbiji, Rwanda, Tanzania, Uganda, Zambia na Zimbabwe
Kwa jinsi Afrika Mashariki ilivyo ni muhimu kuweka wazi kwamba mfumo wa kisiasa na kiuchumi katika Afrika kama vile Umoja wa Afrika na Jumuia ya Afrika Mashariki kimsingi hauwezi kufanikiwa  na kuwa na ufanisi kwenye malengo yake kama hakutakuwepo na kupewa kipaumbele kwa masuala ya utamaduni na lugha ambavyo vitakuwa ni gundi ya kushikamanisha umoja.
Ushiriki wa watu wa kawaida kwenye mijadala na maamuzi kuhusu masuala muhimu yanayoathiri maisha yao kunaweza kuwa njia  moja nzuri ya kufanikisha Kiswahili kuwa na lugha ya pamoja. Katika hali hiyo ni muhimu kusema kuwa mawasiliano ya lugha moja yanaweza kuimarisha hali ya mshikamano na undugu.
Kutokana na baadhi ya nchi za Afrika kuegemea au kutegemea  kwenye lugha za kigeni au kwa maana nyingine lugha za kikoloni  kwa namna moja kumesababisha athari kwenye mawazo na hivyo kuathiri maamuzi makubwa ambayo yanazihusu.

Kiswahili kuingia Gabon
Hivi karibuni serikali ya Gabon imefikia uamuzi wa kuanza  kufundisha Kiswahili kwenye shule zake kuanzia shule za msingi, hivyo kuiomba Tanzania kubuni na kuanzisha mitaala inayofaa kuanzisha ufundishaji wa lugha ya Kiswahili nchini humo.
Rais Ali Bongo Ondimba wa nchi hiyo alimwomba Rais wa Tanzania wakati huo, Jakaya Mrisho Kikwete kumpatia mwalimu binafsi wa kumfundisha lugha ya Kiswahili ikiwa ni jitihada zake za kuonesha mfano wa kuimarisha ufundishaji wa lugha ya Kiswahili kwa wananchi wake.
Kutokana na hali hiyo Gabon inakuwa ni nchi nje ya nchi zinazounda Jumuia ya Afrika Mashariki kuazimia lugha hiyo kufundishwa mashuleni.
Katika mazingira hayo ni dhahiri Kiswahili kunapanuka kwa kasi na itakuwa ni nchi ya 12 kutumia Kiswahili kama moja ya lugha muhimu ya mawasiliano barani Afrika.

Changamoto za sasa
Zipo changamoto kadhaa ambazo Kiswahili kimekuwa kinakubaliwa  kama lugha ya taifa. Changamoto ya kwanza ni katika elimu. Kumekuwepo majaribio ya kupendekeza Kiswahili kiboreshwe zaidi na kutumiwa kama lugha ya kufundishia katika elimu ya sekondari na hata elimu ya juu.
Changamoto inayokikabili ni kwamba vyanzo na utaalamu wa kutafsiri vitabu vya msingi na hususani kwenye masomo ya sayansi katika ngazi hiyo kwa sasa hali hiyo inabakia kuwa ni tatizo.
Changamoto nyingine ni kutokana na ukweli kwamba hivi sasa  jamii inaishi kwenye dunia iliyojikita kwenye utandawazi kiuchumi na kiteknolojia ambapo Kiingereza kinabakia na kuendelea kutumiwa sana hususani kwenye biashara na kuwafanya wanaopinga matumizi ya Kiswahili kutumiwa katika ngazi za elimu kutumia kigezo hicho kukatisha tamaa maendeleo yake.
Zipo sababu za kijamii zaidi na hususani wimbi la sasa baada ya  kuhurishwa kwa huduma za kijamii kuanzia miaka ya 1990 ambapo mfumo wa elimu nao haukupitwa na hali hiyo.
Kuanzishwa kwa shule binafsi kuanzia ngazi ya shule za awali hadi msingi, sekondari na hata vyuo kumesababisha kuibuka kwa shule  nyingi binafsi ambazo zinatumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia.
Katika mazingira hayo imekuwepo tabia miongoni mwa wazazi hivi sasa wakiongozwa na wasomi kuchukulia kuwa kujua kuzungumza Kiingereza kama kigezo muhimu kwa maendeleo ya kitaaluma ya  watoto.
Jambo la aina hii sio tu kwamba linawanyima watoto haki ya kujifunza lugha bali pia inamomonyoa fursa za kujifunza na kuzoea  utamaduni ambao unapatikana na kuimarishwa kupitia lugha yenyewe.
Kisiasa ni kwamba kuwepo mabadiliko kwenye umuhimu wa  kuunganisha utambulisho wa uasilia kunaakisi mabadiliko ya kisiasa,  kwa mfano kuanzishwa kwa sera mpya za kiliberali na siasa za mfumo wa vyama vingi kwa Tanzania uasilia umekuwepo kwa kuhisi kuongezeka kwa mabadiliko japo utekelezaji wake sio kwa  kiwango kikubwa.

Utandawazi na fursa ya kupanuka
Lugha ya Kiswahili kama zilivyo lugha nyingine duniani imepitia kwenye mikono mbalimbali kuanzia chimbuko lake, kukua na inaelekea kwenye kukomaa kutokana na kutumiwa na watu wengi  duniani hivi sasa.
“Nina uzoefu na lugha ya Kiswahili na nimesikia kwamba Kiswahili  kinakua na kupata umaarufu mkubwa kama lugha ya kimataifa na hilo ni juu yenu watu mnaozungumza Kiswahili kuhakikisha kuwa umaarufu wake unaongezeka”
Kauli hiyo ilitolewa na Meya wa zamani wa jiji la London, Ken  Livingston kwenye mahojiano na Mtanzania mmoja ambaye alitaka kufahamu mambo ambayo anayafahamu kuhusu Tanzania.
Kiswahili kama lugha ya taifa imeweza kuibuka na kuwa hivyo  kutokana na sababu za kiutamaduni ambazo zilikuwepo kabla na  ambazo zilisababisha kuyaweka makundi ya watu pamoja.
Biashara ilikuwa pia ni kichocheo kwa baadhi ya watu kujifunza lugha, lakini sera za kikoloni pia ziliendelea kuboresha au kukuza  lugha ambayo imeendelea kuimarisha umoja miongoni mwa makundi mbalimbali ya jamii.
Baada ya uhuru serikali ilikuwa makini kwenye kukuza lugha na hivyo kuifanya lugha ya taifa na sera kadhaa, hatua na taasisi zilianzishwa kuunga mkono maendeleo ya Kiswahili.
Katika mazingira hayo ni dhahiri kuwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitoa mchango mkubwa na wa aina yake kwa kutumia Kiswahili kujenga taifa imara licha ya kuwa na makundi mengi ya kikabila na ya kidini.
Kwa namna ambavyo Afrika Mashariki ilivyo wimbi la sasa hivi la utandawazi kupitia biashara huria, kukuza uwekezaji kutoka nje, ushirikiano wa kiuchumi miongoni mwa nchi na kanda za bara la Afrika ambazo zinatoa fursa kuendeleza, kupanua na kupenyeza Kiswahili katika maeneo mbalimbali kama ilivyokuwa kwa Tanzania.
Ukweli ni kwamba moja ya sababu zilizowezesha maendeleo ya Tanzania kuanzia kwenye karne ya 19 ni biashara na leo hii pamoja na mambo mengine utandawazi kwa ujumla umejikita kwenye ushirikiano wa kiuchumi hivyo basi ipo haja ya kukiingia kifua Kiswahili katika mkondo wake wa kupanuka.
Ushirikiano wa kiuchumi kati ya sekta mbalimbali za kiuchumi, mashirika na nchi lazima kuongozwe na wapanga sera wetu (kisiasa) kwa kukitumia Kiswahili kama lugha rasmi ya biashara.
Zipo njia nyingi ambazo zinaweza kutumiwa katika kufanikisha hatua ya Kiswahili kutumiwa kama lugha rasmi ya biashara kama vile shule au vyuo vya biashara kuhakikisha kuwa Kiswahili kinajumuishwa kama lugha ya biashara.
Aidha njia nyingine ni kuyafanya matangazo kuwa kwa Kiswahili, nembo za bidhaa iwe ni lazima kuandikwa kwa Kiswahili, mawasiliano ya kibiashara na misamiati ya kisheria kwenye biashara itafsiriwe na kutolewa kwa Kiswahili pamoja na mambo mengine mengi ambayo yanahusiana na biashara yawe kwa lugha hiyo.
Hivi sasa hakuna ambaye anafikiria kuwa Kiswahili kinaweza kuwa ni lugha ya kimataifa lakini hoja ni kwamba ni kwa kasi gani kinaweza kuendelezwa, kupanuliwa na kukiwezesha katika hatua za kujenga utambulisho kwa watu wote wanaozungumza Kiswahili.
Katika sekta hii ya kiuchumi ni dhahiri sekta ya utalii inaingia moja kwa moja kwamba inaweza kukikuza Kiswahili kutokana na kuhusisha idadi kubwa ya watalii kutoka nje ya nchi. Hali hiyo inawezekana kupitia utambulisho wa tamaduni mbalimbali zilizo nchini.
Kutokana na watalii wengi kupendelea kufahamu tamaduni za sehemu wanakotalii hiyo ni moja ya fursa ambapo Kiswahili kama sehemu ya utamaduni kinaweza kuenezwa kwa kasi nzuri.
Hali hiyo inatokana na jinsi kauli ya Meya huyo wa zamani wa jiji la London kusema kwamba ni juu ya wanaozungumza Kiswahili  kuhakikisha kuwa kinapanuka na moja ya njia  ni kupitia sekta ya utalii.
Kwenye ulingo huu wa utandawazi imeshajidhihirisha kuwa Kiswahili kinapanuka kutokana na kutumika kwenye vyombo vya habari vya kimataifa vikiwemo vituo vya redio vya Sauti ya Ujerumani, BBC, Redio ya Kimataifa ya China, Redio VaticanRedio Japan na Sauti ya Amerika.

Malema iwe lugha ya Afrika
Licha ya kuwa lugha rasmi ya Umoja wa Afrika (AU), Kiongozi wa Chama cha Watetezi wa Uhuru wa kiuchumi (EFF) cha Afrika Kusini, Julius Malema, ametoa wito wa kupitishwa kwa lugha moja itakayotumika barani Afrika, huku akipendekeza lugha inayofaa kutumika iwe ni Kiswahili.
Malema aliyasema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa na EFF, ambapo aliongelewa mambo mbalimbali ikiwemo ujumbe wa Rais wa Marekani Donald Trump kwenye mtandao wa Twitter kuhusu marekebisho ya sheria ya ardhi Afrika Kusini.
"Tunatakiwa kuanzisha lugha moja ambayo itatumika kwenye bara zima. Kwa mfano Kiswahili, kinaweza kukuzwa ili kitumike barani kote," alisema Malema.
Lugha ya Kiswahili ni lugha inayotumika sana barani Afrika, ambapo kinatumika sana Afrika Mashariki na Kati. Ni lugha rasmi kwa nchi ya Tanzania na Kenya.

Comments