Featured Post

KIHUNZI KWA UTAWALA BORA NI WAPANGA SERA



NA MWANDISHI WETU
UTAWALA bora unaainishwa kuwa ni utawala unaofanya kazi kwa uwazi, unaowajibika, wenye kutawala kwa sheria, wenye ufanisi na ulio na taasisi zilizo halali.

 Katika hali hiyo  inaaminika kuwa utawala wa aina hiyo ni nyenzo muhimu kwenye maendeleo ya kiuchumi ambapo utawala dhaifu husababisha uchumi kukua taratibu ambapo wakati wengine wakikimbia utawala huo huwa unachechemea.
Utawala wa aina hiyo ni muhimu kwenye kupata maendeleo na wakati huo huo ushirikishwaji kidemokrasia kwa kuhakikisha kwamba maendeleo yanawiana na ni endelevu.
Taasisi za umma zinatakiwa zimudu kusimamia rasilimali za umma na kuendesha masuala ya umma kwa njia ambazo zinakuwa huru dhidi ya rushwa na matumizi mabaya  ya madaraka kwa kuzingatia utawala wa sheria na ambazo zinalinda na kukuza uelewa wa watu  kuhusu haki zao.
Kipimo halisi cha utawala bora ni uwezo wa serikali kutambua haki za binadamu na kuipatia jamii maendeleo kwa uwiano na kwa uendelevu. Utawala bora unatolewa kupitia uwazi, uwajibikaji na ushirikishaji pamoja na mwitiko kwa mahitaji ya maskini, walioko pembezoni na walio na uwakilishi mdogo.
Hata hivyo dhana ya utawala bora imekuwa inapotoshwa na baadhi ya wapanga sera ambao ndio wameshikilia taasisi za umma  ili kukidhi matakwa au maslahi yao.
Wengi wamekuwa wakitumia mwanya wa utandawazi kujenga mazingira ya rushwa na hivyo kuifanya isambae kwa kiwango kikubwa. Sasa ndio hapo inapotokea  shinikizo kutoka  nchi wahisani, mashirika ya misaada na wawekezaji kufuata sera zinazaendana na ajenda za uliberali mamboleo.
Ajenda za uliberali mambo leo zimezifanya nchi maskini kuwajibika kwa mashirika ya misaada kuliko ambavyo zinawajibika kwa watu wao. Aidha nyingi zimekuwa zinafanya shughuli zao ili kuwapendezesha wahisani kwa kujikomba na kuombaomba na hata kuzigawa rasilimali kwa mikataba ya kilaghai.
Licha ya kwamba utawala bora ni kichochea cha kukua kwa uchumi baadhi ya watendaji wamekuwa wanawajibika kwa wawekezaji zaidi kuliko kwa wananchi wao na hali hiyo ndio imekuwa inakwaza upatikanaji wa maendeleo.
Takwimu mbalimbali duniani zinaonesha kuwa  kukua kwa kasi na ufanisi mzuri kwenye maendeleo kunahusiana na hali nzuri ya utawala bora na hususani kwenye ufanisi wa serikali, ubora wa usimamizi, utawala wa sheria na udhibiti wa rushwa.
Kiungo kati ya kukua kwa uchumi na vidokezo viwili vya ufanisi wa serikali na ubora wa usimamizi ni mkubwa miongoni mwa nchi za Asia kuliko sehemu nyingine duniani. Lakini inakuwa ni vigumu mno  kuanzisha uhusiano wa kawaida kati ya vipengele hivyo.
Mfano nchi nyingi za Afrika, Tanzania ikiwemo zimekuwa zinajibainisha kuwa zilikuwa kwenye kiwango  sawa na nchi za Mashariki ya Mbali wakati zilipopata uhuru. Lakini leo hii nchi kama Malaysia na Indonesia zimepiga hatua  kubwa zaidi ya maendeleo kuliko zile ambazo zilikuwa sawa kwenye miaka ya 1960.
Katika mazingira hayo tafsiri inayoweza kupatikana kuhusu uhusiano kati ya  ubora wa serikali  na ufanisi mkubwa kwenye maendeleo ni kwamba  kila kimoja kinachangia kukiboresha kingine.
Jambo jingine ni kwamba umuhimu wa vipengele vya utawala bora  unatofautiana ndani ya nchi kulingana na hatua ya maendeleo iliyofikiwa. Katika nchi ambayo ina kipato cha chini  inatakiwa kupambana ili kuwa na serikali yenye ufanisi usimamizi mzuri ulio bora na utawala wa sheria na udhibiti mkubwa wa rushwa.
Kwa mfano inatakiwa  kujiepusha na migogoro, kuzingatia haki za binadamu na kutoa huduma muhimu za umma.
Ili nchi iweze kuingia kwenye orodha ya nchi zilizo na kipato kikubwa inatakiwa kuboresha utawala bora kwa kuzingatia  na kuheshimu ushirikishwaji wa wananchi  na uwajibikaji wa serikali.
Nchi zilizo na kipato cha kati na kikubwa zinaweza kunufaika na zawadi hii kubwa  kutokana na kutumia sauti za wananchi wake, uimara wa kisiasa na kuwepo kwa taasisi zinazokubalika duniani.
Mfano wa taasisi hizo ni pamoja na mfumo wa kisheria ulio na ufanisi, huduma zenye ubora wa hali ya juu katika sekta ya afya na elimu na mfumo wa kifedha ambao umekaa katika mpangilio unaokubalika.
Rushwa kwenye  mageuzi ya kuingia kwenye utawala bora  hutofautiana kulingana vidokezo binafsi vya maendeleo. Rushwa huzuia programu za huduma za umma  zisiwafikie maskini, wakati udhaifu kwenye mamlaka za usimamizi na ufanisi serikalini huingia kwenye ulegevu.
Hali kadhalika tabia za kijamii huathiri matokeo ya kijinsia na ushiriki kwenye masuala kama ya usafi. Katika nchi ambayo inakabiliwa kwa mapana na soko kushindwa, serikali ni lazima kuangalia namna kuondoa au kufanyia mageuzi  vikwazo vyote vinavyozuia maendeleo. Kwa kuwa nchi zinakuwa na mifumo  tofauti ya mazingira ya mwanzo huwa na  namna tofauti ya kukabiliana na vikwazo, zinahitaji kuwa na sera za mageuzi  zinazofuatilia utawala bora.
Kama malengo ya maendeleo yalivyo, vipimo vyote vya utawala bora  lazima vifuatwe. Wapanga sera si tu kwamba wanatakiwa kufuata  kile ambacho ni rahisi kukitekeleza lakini pia kwa utaratibu kwa kuangalia zaidi kwenye  athari za maendeleo.
Taasisi zilizo na ubora wa hali ya juu  zitasaidia uchumi unaokua kwa haraka kuepuka  mitego inayotoka kwa nchi zilizo na kipato cha kati  na kuwezesha uchumi unaokua taratibu  kuanzisha mazingira ambayo ni  muhimu kwa uendelevu wa ukuaji wa uchumi.
Utawala bora unawezesha kuwepo kwa mgawanyo zaidi wa kazi ulio na ufanisi, tija kubwa kwenye uwekezaji na utekelezaji wenye ufanisi wa  sera za kiuchumi na kijamii na njia nyingine muhimu za kukua kwa uchumi kuliko endelevu.

Comments