- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NAIROBI, KENYA
KENYA imemkamata na kumrudisha kwao mfanyabiashara mmoja
raia wa China, baada ya mkanda wa video kusambaa katika mitandao ya kijamii,
ukimuonesha akitoa matamshi ya ubaguzi wa rangi.
Liu Jiaqi, alirekodiwa wakati alipokuwa akizozana na mmoja
wa wafanyakazi wake raia wa Kenya, na akamtukana Rais Uhuru Kenyatta pamoja na
Wakenya wote kwa kuwaita nyani, masikini na wajinga.
Polisi ilimtia nguvuni mfanyabiashara huyo siku ya Jumatano
baada ya kusambaa kwa video hiyo mitandaoni. Video hiyo ilipokewa kwa ghadhabu
na Wakenya wengi.
Liu ni muuza pikipiki na ameonekana kwenye video hiyo
akimwambia mfanyakazi wake kuwa naichukia Kenya kwa sababu "inanuka."
Mfanyakazi huyo alipomuuliza kwanini yupo Kenya akajibu kuwa
yupo hapo kwa kutafuta pesa tu.
Video hiyo ilirekodiwa kwa usiri na mfanyakazi huyo ambaye
alikuwa akitishiwa kufutwa kazi.
Liu na washirika wake hawajazungumzia chochote kuhusu video
hiyo ambayo ubalozi wa Uchina jijini Nairobi unasema ilirekodiwa mwezi Juni
mwaka huu.
Msemaji wa ubalozi huo Zhang Gang ameliambia shirika la
habari la AFP kuwa Bw Liu tayari ameshaadhibiwa na kampuni yake na amemwomba
radhi aliyemtolea matamshi hayo.
"Mazungumzo na hisia binafsi za za kijana huyu
haziakisi mawazo ya watu wa Uchina kwa ujumla wao," amesema Gang.
Wafanyakazi wa raia wa Kenya katika mradi wa reli ya kisasa
SGR waliripoti kwa wingi vitendo vya kibaguzi kutoka kwa Wachina.
Japo hii ni mara ya kwanza kwa mtu kufurushwa kwa ubaguzi,
kumweripotiwa visa vingi vya ubaguzi kutoka kwa raia wa Uchina wakati wa ujenzi
wa reli ya kisasa ya SGR kutoka Mombasa mpaka Nairobi.
Mwaka 2015, kuliripotiwa kisa cha kukataliwa Wakenya kuingia
kwenye mgahawa mmoja wa Kichina jijini Nairobi ifikapo usiku. Mmiliki wa
mgahawa huo alipandishwa kizimbani kwa kosa la kutokuwa na leseni ya kuuza
pombe na si ubaguzi.
Comments
Post a Comment