Featured Post

JARIBIO LA DAWA YA UKIMWI LAWAPATIA MATUMAINI WANAOSHIRIKI NGONO ISIYO SALAMA



CARDIFF, WALES
JARIBIO la dawa ya HIV ambayo inapunguza viwango vya maambukizi limekuwa likileta matumaini nchini Wales kulingana na takwimu mpya.
Vituo vya afya nchini Wales vilianza kutoa dawa hiyo ya Pre-Exposure Prophylaxis (Prep) mnamo mwezi Julai 2017.

Katika mwaka wa kwanza wa majaribio, takriban watu 559 waliopo katika hatari ya maambukizi walitumia dawa hiyo ambayo imeelezewa kuleta matumaini ya kinga dhidi ya HIV.
Kati yao hakuna aliyepatikana na virusi vya HIV.
Kumekuwa na visa vya magonjwa ya zinaa miongoni mwa wale wanaoshiriki katika majaribio ya dawa hiyo, ambayo wanasayansi wamegundua inaweza kuwalinda watu waliopo katika hatari ya kupata maambukizi iwapo itatumiwa kila siku.
Phil alianza kutumia dawa hiyo baada ya kutoka katika uhusiano wa muda mrefu na kuona kwamba itakuwa njia nzuri ya kutahadhari.
"Inaondoa wasiwasi wa mtu kuambukizwa HIV," aliambia BBC Radio Wales.
Inakupatia fursa ya kushiriki tendo la ngono bila wasiwasi.
Takriban watu 150 hupatikana na ugonjwa wa HIV nchini Wales kila mwaka, nusu ya idadi hiyo ikiwa maambukizi ya ngono kati ya wanaume.
Utafiti huo wa miaka mitatu wa Prep ama Truvada, uliofanywa nchini Wales ulitangazwa mwaka uliopita na waziri wa afya Vaughan Gething.

Je Prep ni dawa gani?
Jina kamili la Prep ni Pre-exposure prophylaxis ambapo inalinda seli katika mwili na kuharibu virusi ili kuvizuia kusambaa iwapo vitainbgia mwilini.
Ikitumiwa kila siku imeonekana kupunguza hatari ya maambukizi kwa asilimia 86.
Kwa sasa inatumika nchini Marekani, Canada, Australia na Ufaransa ili kulinda watu waliopo katika hatari ya kupata maambukizi ya HIV.
Mnamo mwezi Agosti 2017 ilitangazwa kwamba Prep itapatikana kwa wagonjwa waliopo Uingereza ikiwa ni miongoni mwa majaribio.
Dkt. Olwen Williams, rais wa muungano wa afya ya ngono na HIV alisema kwamba licha ya ufanisi huo ni muhimu kutumia mipira ya kondomu unaposhiriki ngono.
"Kile tulichogundua wakati tukijadili Prep na watu binafsi ni kwamba mawazo yao, maumbile yao na vile wanavyofurahia ngono kuimeimarika," anasema.
Nchini Wales, dawa hiyo inapatikana kwa mtu yeyote anayehisi yupo katika hatari ya kuambukizwa virusi vya HIV, hususan watu ambao hushiriki tendo la ngono lilsilo salama.
CHANZO: BBC 

Comments