Featured Post

FEDHA ZA DIASPORA KUWEKEZA, SI MBADALA WA MISAADA



NA ALOYCE NDELEIO
Kila mwaka Diaspora kutoka nchi zinazoendelea wanaoishi na kufanya kazi  nchi zilizoendelea hutuma nyumbani mamilioni ya Euro ili kusaidia  familia sanjari na miradi mingine midogo inayozinufaisha jamii au familia zenyewe hususan katika sekta ya kilimo.

Kutokana na hali hiyo linakuwepo shinikizo la kuboresha njia za kuhamisha fedha hizo pamoja na msukumo wa kuwekeza katika vitega uchumi  vinavyozalisha zaidi.
Kwa mujibu wa Umoja wa Ulaya takwimu za misaada ya maendeleo   kwenda  nchi zinazoendelea katika kipindi cha mwaka 2008 -2013 ambayo  ilipitia kwenye  Mfuko wa Maendeleo wa Ulaya (EDF) ilifikia jumla ya Euro bilioni 22.98 au Euro bilioni 4.6 kwa mwaka.
Zilibainisha kwamba kiwango kilichopelekwa nchini mwao na diaspora hao baada ya kipindi hicho kilikadiriwa kufikia euro bilioni  20 kwa mwaka.
Fedha hizo zinawakilisha kiasi kikubwa cha fedha ambazo zimekuwa  hazihusishwi au kutiliwa maanani  licha ya kutoa  mchango mkubwa  katika uchumi wa nchi nyingi zinazoendelea.
Nchi  zenye  raia wake  wengi  diaspora  mtiririko wa fedha wanazotuma nyumbani zimekuwa zinachangia kiwango kikubwa katika pato la ndani la taifa. Mfano nchi  kama Lesotho  zinachangia asilimia 60 na takribani  theluthi moja  kwa visiwa vya Caribbean na asilimia 25 hadi 30 kwa Cape Verde.
Utafiti wa Benki ya Maendeleo ya Afrika  (AfDB) unabainisha  kiasi hicho huchangia  asilimia 346 ya misaada ya maendeleo kwa visiwa vya Comoro na asilimia 200 kwa Kenya.
Vyanzo vikuu vya fedha hizo ni kutoka  diaspora waishio Ulaya Magharibi kwenda Afrika, Marekani  kwenda visiwa vya Caribbean na Australia na New Zealand  kwenda  visiwa vya Pasifiki.
Hata hivyo takribani  asilimia 40 ya fedha zote ni kutoka diaspora  wa nchi za kusini mwa Afrika. Mfano kutoka  Botswana  au Afrika Kusini  kwenda  nchini  nyingine za Afrika hususan majirani.
Takwimu za Benki ya Dunia zinaonesha kuwa baadhi ya kiwango kinachotolewa  kikiwa wastani wa  euro 100 hadi 300 kwa kila mtu kwa mwaka  kiliongezeka  katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.
Matokeo ya mapato hayo yanatofautiana kwani takribani asilimia 80 inatumiwa kwa matumizi mbalimbali, asilimia 15 au zaidi  kutegemeana  na  nchi hujenga miundombinu kama vituo vya afya, shule  na misikiti; na kiwango kidogo cha asilimia moja kinawekezwa kwenye  miradi ya  faida kwa jamii.
Hakuna shaka kwamba fedha hizo hutumiwa kuboresha maisha ya jamii  maskini na hususan katika maeneo ya vijijini, hivyo huwa kama njia ya usalama na uhakika wakati wa mavuno haba au matatizo ya afya.
Hali hiyo pia imekuwa inasaidia kuhakikisha kuwa zinakuwepo fursa za  kupata elimu hususani kwa watoto wa kike na kwa mujibu wa Mtafiti Flore Guibert, wa  taasisi ya Maendeleo na Utafiti ya Ufaransa,  “Aina hii ya uwekezaji ni muhimu kwa manufaa na kuimarisha mtaji wa nguvu kazi.”

Chambo cha kutegemeana
Lakini  baadhi wanakosoa kuwa aina hiyo ya mtiririko wa fedha kwamba  unapingana na uzalishaji linapotokeza suala la kuhamasisha kufanya kazi na  kuongeza tija katika kilimo kwa nchi zinazozipata.
Miongoni mwa mataifa madogo miongoni mwa  mataifa ya Caribbean  mtiririko wa fedha kutoka kwa diaspora wake umewawezesha kuishi maisha bora kiasi kwamba hakuna anayejali kuendeleza sekta ya kilimo ambayo imezidi kuporomoka.
Mtiririko  huo pia  umeanzisha au kuunda utegemezi miongoni mwa familia nyingi. Aidha  hali hiyo imewafanya  ndugu walio nje ya nchi  kuwa wanaweka akiba  kwa ajili ya kuwapelekea ndugu  au wadogo zao  hali inayowafanya wadundulize kile wanachokipata kwa shida na kukitenga kama vile matoleo ya sadaka.
Wakiwa wanajua kuwa wao ni sehemu muhimu ya familia zao, jamaa  wengi huwa wamepoteza matumaini  ya kurudi nyumbani, na matokeo yake  ni kuwepo mzunguko wa kudumu na ambao umekuwa ni jambo la kawaida  miongoni mwa nchi za Sahel  ambako uhamaji umekuwa ni utamaduni wa  muda mrefu.
Kwa mujibu wa Jean-Pierre Garson mtaalamu wa masuala ya uhamiaji  kwenye Umoja wa Ushirikiano wa Uchumi na Maendeleo (OECD)   “Mtazamo wa jumla wa utoaji wa fedha hizo unawawezesha wale waliobakia nyumbani kuibuka kutoka katika lindi la umaskini.
“Lakini athari zake kwenye maendeleo bado haziko wazi na hususani ikizingatiwa kuna kupotea kwa nguvu kazi kutokana na uhamaji  unaozikumba nchi hizo.”
Hili ni tatizo kubwa katika maeneo ya vijijini ambako  hukumbwa na uhamaji mkubwa na ambako kukosekana kwa wanaume kunadhoofisha mafanikio yanayopatikana kwenye kilimo.
Lakini hoja ni kwamba ni kwa namna gani fedha hizo zinaweza kugeuzwa  na kuwa zana halisi ya maendeleo kwa wale waliobakia nyumbani na kwa  upana zaidi kwa nchi za maskini kwa jumla?
Suala hili  limechukua mtazamo mpya katika miaka ya hivi karibuni na kwamba sababu ya kuwepo kwa mvuto huo mpya ni nyingi ikiwa ni pamoja na ushawishi wa kuwezesha watu kujitegemea na hivyo kupunguza  uhamiaji.
Hali hiyo inaendana na matumaini ya kuwepo udhibiti mzuri wa kupeleka fedha kimataifa na kuepuka mitandao ya utakatishaji wa fedha na ambayo pia ni ya kigaidi.

Kuwezesha kuhamisha fedha
Hatua ya kwanza kwenye mkakati wowote unajumuisha kuwa na uhamishaji wa kawaida ili kuwezesha kuwajua na kuwarekodi lakini pia kupunguza gharama zake na kuwafanya wawe kwenye mazingira ya usalama zaidi.
Hivi sasa  fedha zinazopelekwa zinapitia njia rasmi na sahihi za benki hususan kwa Afrika. Malipo mengi yanashughulikiwa na mawakala wa kuhamisha fedha wanaendesha shughuli zao katika maeneo mengi na huduma zao ni salama na safi. Hata hivyo zinagharimu  kutokana na kamisheni  inayokatwa  kulingana na kiasi cha fedha kilichotumwa ambayo ni kutoa asilimia kumi hadi 15.
Kwa mujibu wa utafiti  wa hivi karibuni wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD)  ulibaini kuwa  asilimia 70 ya fedha zinazopokelewa  Afrika Magharibi zinapitia mikononi mwa wakala halali.
Aidha diaspora kutoka Comoro na Mali wanapendelea  kutumia  njia zisizo rasmi na mara nyingine njia za hatari kwa kutumia wafanyabiashara, mfumo ambao ni rahisi wa kutumia  simu.
Hatua au  njia hizo  ni wazi kuwa zinaweza  kuongeza kiasi kinachohamishwa  ikiwa ni pamoja na kutoa msukumo wa ushirikiano kati ya mabenki katika nchi  ambako fedha zinatoka na zinakopelekwa.
Ethiopia imeonyesha kuwa mafanikio yanaweza kupatikana  kwa  kuruhusu  wateja wake  kufungua  akaunti za fedha za kigeni na matokeo yake ni kwamba mabenki yameanzisha  mifumo  ambayo inawezesha  wahamaji   kupeleka  fedha  nyumbani  kwa kutumia tu mfumo rahisi wa kupiga simu.
Hili linawezekana  kwa kutumia mitandao ya vyama vya ushirika  au taasisi ndogo za fedha  na katika hili simu zinawezesha  utoaji huo wa fedha.
Katika juhudi za aina hiyo za kubuni suluhisho kwa maeneo ya vijijini IFAD kwa kushirikiana na mashirika mengine ilizindua  pendekezo la aina takribani miaka kumi iliyopita a liliungwa mkono kwa Euro milioni  saba.
Mabadiliko kwenye mfumo pia kulipunguza  gharama za kupeleka fedha  jambo ambalo limeshafanikiwa kwenye nchi kadhaa zinazoendelea.
Wahamaji hao wanataka  mabenki  kutoa kiwango cha  riba kinachovutia, garantii na  mikopo  hivyo kwamba wanaweza kuanzisha ubia mkubwa zaidi.
Hata hivyo inaelezwa kuwa fedha peke yake  hazitaweza kuanzisha  mfumo na ubia endelevu utakaowezesha kuanzishwa kwa fursa za ajira na utajiri.
Ni muhimu kwamba  wale walio nyuma ya mkakati huo wanaungwa mkono na nchi na watu wanaofanya kazi katika sekta hiyo katika nchi wanamotoka na ambao hawawezi kuhamasishwa, au kupata msaada sahihi au mafunzo.
Mamlaka za ndani  pia zinaweza kuchangia kutoa mazingira  ya  kiuchumi, kijamii na  kisiasa  na ambayo   inafaa na imara.

Miradi ya kilimo shughuli adimu
Miradi ya kilimo na mikakati mingine ya kusaidia kilimo kwenye familia  imekuwa ni michache  miongoni mwa nchi zinazoendelea na hata ile iliyopo mingi inaendeshwa kwa mitazamo yake.
Tofauti muhimu inayotokeza imo kwenye visiwa vya Pasifiki na Caribbean  ambako baada ya kukamilisha mahitaji ya msingi diaspora wao huanzisha  mipango ya kuwekeza inayolenga kilimo, uvuvi na utalii vijijini.
Kwa nchi za Afrika Magharibi mikakati hiyo haipo, bali ni  mitambo michache ya umwagiliaji iliyoanzishwa kwenye kingo za mto Senegal katika vijiji vya wakazi wa Mali na Senegal.
Kwa nchi za Afrika Mashariki wahamaji hao hupendelea kuwekeza kwenye viwanda vidogo vya usindikaji wa mazao mbalimbali na hata hivyo  kwa msaada wa wataalamu waliobobea miradi michache imeanza kwa kuwekeza kwenye kilimo.
Wapo wahamaji ambao  wamebahatika  kuwa na upeo wa kuona  haja ya kuwepo kwa uhakika wa chakula na haja ya kuboresha hali hiyo  na wamekuwa wanatoa mafunzo kwa kinamama ambao  huweza kununua  mazao na kuyahifadhi ili kuepuka  bei ndogo au za chini na unyonyaji  unaofanywa na wafanyabiashara.
Hata hivyo wahamaji wengi wamekuwa wakidhibiti  kiasi cha fedha wanazopeleka au kuingiza kwenye miradi ili kuepuka matumizi mabaya.
Lakini mashirika kadhaa ya kimataifa ambayo yamefanya utafiti katika sekta ya kilimo hivi karibuni yanaonya kuwa fedha zinazopelekwa kutoka kwa diaspora haziwezi kuchukua nafasi ya misaada ya maendeleo ya taifa  au kufidia pengo lililokosekana katika kuboresha maendeleo ya serikali za mitaa.

Comments