- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NEW YORK, MAREKANI
Mbunge wa Kyandodo Mashariki Bobi Wine ameiambia BBC kuwa
atarudi Uganda na kuendelea na shughuli za kisiasa akimaliza matibabu yake
ughaibuni.
Bobi Wine ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi
amesema hana woga wa kukabiliana na mkono wa dola katika harakati zake
alizosema zinalenga kumuweka yeye na Waganda wote huru.
Mwanasiasa huyo ambaye pia ni mwanamuziki maarufu nchini
Uganda kwa sasa yupo Marekani anapopatiwa matibabu baada ya kupigwa na vyombo
vya dola.
Bobi Wine na wenziwe 32 walikamatwa baada ya kudaiwa
kushambulia msafara wa Rais wa Yoweri Museveni mjini Arua mwezi uliopita na
kuwekwa katika kizuizi cha jeshi.
Mwanzo alipandishwa katika mahakama ya kijeshi kabla ya
kuhamishiwa kwenye mahakama ya kiraia na kushtakiwa kwa kosa la uhaini.
Akiongea na mwanahabari wa BBC Zuhura Yunus aliyemtembelea
nchini Marekani Bobi Wine amesema alipokuwa kizuizini "askari walinipiga,
walinidunda na kunifanyia mambo mengi."
Bobi Wine aliruhusiwa kuondoka Uganda Ijumaa baada ya
kuzuiliwa awali na ameiambia BBC kuwa punde tu madaktari wake watakapomruhusu
atarudi Uganda kuendelea na harakati za kisiasa.
"Nimekuja hapa kupata matibabu, lakini nitarudii
nyumbani kwasababu Uganda ni nyumbani kwangu," amesema Bobi Wine na
kuongeza, "Mimi ni kiongozi, baada ya matibabu nitarudi kuendelea na mambo
ya siasa."
Alipoulizwa kama hana woga baada ya kupigwa na kudundwa, amesema:
"Siwezi kuogopa kwasababu kila kitu wamefanya wanaweza kufanya lakini mimi
siogopi."
Serikali ya Uganda imekuwa ikikanusha toka mwanzo ripoti
kuwa Bobi Wine amepigwa na kuumizwa. Raisi Museveni alivinyooshea vidole vyombo
vya habari kabla ya mbunge huyo kuachiwa akidai vinapotosha umma.
Hata baada ya kuachiwa na kuruhusiwa kwenda nje kwa matibabu
serikali ya Uganda imeendelea kushikilia msimamo wake kuwa hawakumtesa.
"Hawa watu (serikali) wanajua mambo ya kudanganya tu.
Wanaweza kufanya kitu halafu wanaongea kitu kingine. Lakini ukweli upo
wazi," amesema.
Ndoto za Urais
Baadhi ya wachambuzi wanaona vuguvugu linaloendelea Uganda
linaweza likwa chanzo cha kumng'oa Museveni Madarakani. Lakini je Bobi Wine ana
ndoto za kuwania urais.
"Sina ndoto za kuwa rais kwa sasa. Sasa hivi nataka
kuwa huru, na watu wa Uganda wanataka huwa huru bila kujali nani ni rais,"
amesema na kuongeza, " Haijalishi kama mtu yupo upande wetu (upinzani) au
wa Museveni, wala mambo yetu si ya kumtoa Museveni. Tunataka kuwa huru katika
nchi yetu."
Kwa mujibu wa Bobi Wine hata kuachiwa kwake na kuruhusiwa
kwenda Marekani kwa matibabu si kielelezo cha uhuru wa mahakama ambayo iliamuru
hivyo bali nguvu ya umma.
"Ilikuwa presha ya watu wa Uganda na nje ya Uganda iliowalazimisha
serikali kutuachia. Bila presha ile sidhani kama wangetuachia. "
Comments
Post a Comment