Featured Post

AIBU ALBINO KUWINDWA KAMA WANYAMA PORI!



NA MWANDISHI WETU
PAMOJA na kwamba alitoka kijijini ambako ni mbali na ambako alivamiwa akiwa ndani kwake kutokana sababu tu ya rangi ya ngozi yake, na kwamba hivi sasa yupo mbali na kijiji hicho Jane (22), huogopa kutembea peke yake labda akiwa kwenye kundi la watu anapokuwa kwenye shughuli za manunuzi jijini Dar es Salaam.

Watu wengi walio na ulemavu wa ngozi au maalbino, ulemavu ambao umekuwa unamtokea mtu mmoja kati ya 1,400 wamekuwa wakijificha na kujitenga ikiwa ni kujihami dhidi ya watu wanaoamini kwamba viungo vya miili yao ni vyanzo vya bahati au utajiri.
“Naogopa sana kutokana na matukio mengi yanayotokea hivi sasa,” alisema Jane ambaye sio jina lake halisi na dada yake ndiye analifahamu.
Jane anaishi kwenye makazi salama  katika kituo cha Under the Same Sun kinachofadhiliwa na serikali ya Canada kwa ajili ya maalbino.
“Ni hivi karibuni tu  mtoto wa kiume mwenye umri wa  miaka sita alikatwa mkono, aliletwa hapa na ameshapelekwa Canada kwa ajili ya upasuaji,”, alisema Jane, ambaye mkono wa kulia wa shati lake unaning’inia kwa kupwaya ndani kutokana na kukatwa kwa mkono wake.
Jane anaamini kua mjomba yake ndiye aliyemkata mkono wakati akiwa amelala kijijini kwao katika eneo kanda ya ziwa miaka sita iliyopita.
Kama ilivyo kwa wote wanaonusurika kwenye matukio haya ya uvamizi wa albino kwamba wahusika na hata washukiwa bado wanatembea kwa uhuru, na wakati huo huo matukio mengine yakiendelea bila hatua zozote madhubuti kuchukuliwa.
“Mjomba pamoja na shemeji yangu walikamatwa na polisi, nilipofika kituoni polisi waliniambia niwasamehe ili waachiliwe huru nilikataa, lakini waliwaruhusu hivyo hivyo bila idhini yangu” alisema Jane.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Kituo cha Utafiti cha Pew chenye  makazi yake nchini Marekani katika Afrika imani za kishirikina ni kubwa sana nchini Tanzania   ambapo mwaka 2010 iligunduliwa kuwa idadi kubwa ya watu sawa na asilimia 93  nchini Tanzania bado wanaamini katika nguvu za giza.
Mkurugenzi wa Under the Same Sun, Vicky Mtetema alisema kwamba imani hiyo si tu kwamba imedhoofisha demokrasia nchini kutokana na watu  wengi kuendelea kulalamika kuhusu hali ngumu ya kimaisha na kutupia lawama hizo kwamba imesababishwa na mizimu, bali pia kutoa fursa kwa waganga na wapiga ramli kutoa tiba zinazosababisha mauaji ya watu wasio na hatia kama njia ya kuondokana na umaskini.
“Ni asilimia saba  ya idadi ya watu ambayo haijihusishi na waganga hao. Kama waganga hao wakiwaelekeza kwamba ni lazima walete kiungo cha ambaye ni albino huamini, na hata kama watambiwa walete kichwa cha mtoto wake mwenyewe, mtu huamini na kufanya aliyoambiwa na mganga,” alisema.
Kijana mmoja ambaye yupo kwenye makazi hayo salama anaamini kabisa kwamba wazazi wake ndio walikuwa wamepanga alipokuwa na umri wa miaka tisa mpango wa yeye kuvamiwa nyumbani kwao na hatimaye kukatwa mkono wake na mtu asiyemfahamu.
Mwanamke mwingine ambaye hana mikono yake yote miwili alisema kuwa jirani yake wa muda mrefu ndiye aliyemfanyia ukatili huo. Anafikiri kuwa pia mchumba wake pamoja na baba wa mtoto wake walipanga yeye kufanyiwa ukatili huo kwa zaidi ya wiki tatu kabla ya ndoa yao, na miezi michache kabla ya kuzaliwa mtoto wake wa pili.
“Bila kujali kwamba unakaribia kufunga ndoa, au ni mchumba wako, au ni mke wako  wanafanya unyama huo,” alisema Ntetema akitoa orodha ya albino waliuawa usiku wa ndoa zao, au kuuzwa wakiwa hai kwa waganga wa jadi.
“Mara nyingine wanataka mahusiano na wewe kwa sababu wanakuhitaji, ili wakuuze kwa bei kubwa au waweze kukata viungo vyako,” alisema.
Lakini inaumiza sana pale watu waliopendana wanapofumbia macho suala hili huku akilini zao zikiwa zinaongozwa na waganga pamoja na tamaa ya utajiri.
Ni watu matajiri ndiyo wanaoweza kununua viungo hivi vya albino huku wakitegemea kupata nguvu za kimaajabu, alisema Ntetema ambaye alikuwa mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) ambapo mwaka 2008  katika shughuli zake za uandishi wa habari alipewa mguu wa albino kwa dola 2000 za Marekani.
Shirika la Msalaba Mwekundu linasema kuwa seti nzima ya viungo vya albino inaweza kuuzwa hadi dola 75,000 za Marekani, wakati Ntetema anasema mtu mmoja hivi karibuni alijaribu kumuuza albino kwa dola 350,000 za Marekani.
“Ni watu matajiri, na maarufu, na ni watu ambao wana nguvu za kisiasa na kiuchumi  ndiyo ambao wanaweza kuwa na kiasi hicho cha fedha kiwe dola 2000 au dola 350,000. Mtanzania wa kawaida hawezi kuwa na kiasi hicho cha fedha,” alisema.
Madhila yanayowakabili walemavu hao yalishawahi kujadiliwa Bungeni na maonyo makali yakawa yanatolewakwa wanasiasa na jamii kwa jumla.
Waganga nao wamekuwa wanafahamu dhahiri watu wanafika kwao kwa ajili ya huduma za kiganga  na wamekuwa wakipata pesa nyingi kulingana na msimu  ambayo wanasiasa hufurika kwao.
Inakuwa ni jambo la kuskitisha kwamba binadamu anawindwa kama mnyama pori na thamani ya uhai wake kuwa umepuuzwa na kuonekana kama taka zisizo na thamani.
Wengi ambao tayari wana ulemavu huu wa ngozi wamekuwa wanakimbilia  kwenye makazi haya salama  ambayo tayari yamejaa kwani wanaona hata kama ni kufa ni sawa kuliko kuwa hai na kukumbana na ukatili huo wa kutisha.

Comments