Featured Post

WATOTO WANAODAIWA KUWA WACHAWI WAUAWA KIKATILI

 Tahadhari: Baadhi ya simulizi na picha zinaogofya
Akiwa amekalia benchi la mbao, mtoto huyu mwenye umri wa miaka mitatu anaonekana mwenye furaha. Anatazama kipindi cha vibonzo cha Ninja Turtle.
Ni vigumu kuamini kwamba Comfort anadaiwa kuwa mchawi.

Hii ndiyo sababu kwamba yeye na nduguze wakubwa wawili wanaishi katika makao ya dharura katika mji wa Calabar, kusini mashariki mwa Nigeria.
Ni nyumba ndogo iliyotengenezwa chini ya ardhi na iliyo na runinga. Mlango hufungwa mara kwa mara kwa usalama wa watoto hao.
Makao hayo ni ya muda hadi pale watoto hao watakapoanza kuishi na familia zao.
Lakini hakuna mtu anayetaka kuishi na watoto hao wanaoitwa wachawi katika nyumba zao.
Baada ya kipindi chake cha vibonzo kujisha, Comfort anaonekana nje na kuinua shati lake linaloonyesha makovu ya vidonda mgongoni mwake.
Makovu hayo yanatokana na kisu cha moto kilichotumiwa na jirani ili kumlazimu kukubali kuwa mchawi.
Majina ya watoto katika hadithi hii yamebadilishwa. Maelezo yamefichwa juu ya picha ili kuwalinda

Kuelekezwa gizani
Mapema mwezi Februari, Comfort na dadake Hope, 15, na ndugu yao mdogo, 5, Godbless walikuwa wakiishi na bibi yao Christiana karibu na eneo la Akampka.
Wazazi wao walifariki katika hali isiyoeleweka, na huku hilo likiwa limemefanya Christina kuwa na wasiwasi kuhusu watoto hao aliamua kuwachukua.
Huku akiwa na virusi vya HIV na kukosa kunywa dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo, hali ya kiafya ya Christiana ilikuwa inadorora na alikuwa akiendelea kukonda.
Huku akiwalaumu watoto hao kwa kusababisha hali yake mbaya, Christiana aliwapeleka katika kanisa lao kwa uongozi.
Wakiwa kanisani, nabii mmoja alithibitisha hofu yake kwamba wasichana hao walidaiwa kuwa wachawi.
Kwa Christiana, hilo lilithibitisha chanzo cha kifo cha mwanawe wa kike na mkwewe, ugonjwa wake na tabia mbaya ya watoto wake.
Muda mfupi baadaye, jirani kwa jina Rankin alimsikia Christiana akiwashutumu watoto hao kwa kukata kamba ya kuanikia nguo katika ua wa familia hiyo wakiwalaumu kuwa wachawi.
Baada ya kuzungumza na Christiana na kugundua maelezo zaidi kuhusu shutma hizo, Rankin alirudi siku iliyofuta na rafikiye.
“Alianza kutupiga na kutwambia kumuondoa bibi yetu kutoka kwa ulimwengu wa uchawi," alisema Hope.
Watoto hao walijaribu kutoroka kupitia minazi iliokuweko, lakini walizingirwa na wanaume hao wawili na kupelekewa katika nyumba za majirani.
Mikono yao na miguu ilifungwa kwa pamoja na Rankin akiweka chuma motoni.
“Baadaye walituuliza iwapo sisi ni wachawi," anasema Hope "na tukawaambia hapana."
“Hivyo basi alianza kutupiga mmoja baada ya mwengine akitumia chuma hicho cha moto kuanzia alfajiri hadi mchana.”
Damu ilimwagika ardhini huku wakilazimishwa kukiri.
“Hatimaye tulisema ndio," anasema Hope. "Baadaye walituuliza iwapo ni sisi tuliomuua baba yetu na mama yetu-tulisema ndio."
“Walituuliza iwapo matatizo haya yoyte katika familia yetu - ni sisi tulioyasababisha- tulisema ndio."
Baada ya kutembelea kanisa lililojengwa kwa udongo ambapo watoto hao wanasema kuwa walipigwa na kuchomwa, nabii aliyewaita kuwa wachawi hakuweko.
Badala yake nilikutana na mchungaji Israel Ubi. Anasema kuwa hakuna hata mtu mmoja kutoka kanisa hilo anayeweza kutoa madai kama hayo ama hata kufanya matambiko kuwakamata watu wanaodaiwa kuwa wachawi.
“Hakuna uchawi hapa,” anasema.
Aliposukumwa zaidi kuzungumzia suala hilo, alikiri kwamba kanisa hilo lilikabiliana na mashetani na majini ambapo watu wengi katika eneo la Niger Delta wanaamini kuwa yapo katika maeneo ya bahari na miti.
Ni mjomba wao watoto hao Sunday ambaye aliripoti kuhusu kisa hicho cha chuma cha moto kwa polisi.
Dereva wa teksi, ambaye anasema haamini uchawi upo alimshutumu nabii aliyedai kwamba watoto hao ni wachawi.
“Kutokana na hali yake ya kiafya, mamangu aliamini maneno yake. Manabii hawa ni wahalifu, ni watu wanaoharibu maisha ya watu.”
Unyanyapaa wa kuwataja watoto kuwa wachawi ni suala la hivi karibuni katika jimbo la Delta , ambalo lililibuka miaka ya 1990. Kabla ya hilo, wanawake wakongwe walikuwa wakilengwa na madai ya kuwa wachawi.
Kufikia 2008, ilikadiriwa kuwa watoto 1500 walibandikwa kuwa wachawi katika majimbo ya Akwa Ibom na Cross Rivers kusini mashariki mwa Nigeria.
Kulingana na utafiti tangu wakati huo, visa ambavyo vilikuwa vimenakiliwa vinashirikisha visa vya watoto na watoto wachanga ambao walidungwa misumari vichwani, kulazimishwa kula simiti, kuchomwa kwa moto, kuchomwa na tindi kali, kupewa sumu na hata kuzikwa wakiwa hai.
Ripoti ya shirika la watoto la Umoja wa Mataifa Unicef mwaka 2010 inasema kuwa ni watoto wasioweza kujitetea kwa mfano walio na ulemavu wa maumbile na wenye magonjwa kama vile kifafa ambao wanalengwa zaidi.
Wengine wamebandikwa kuwa wachawi kwa kuonekana hawashughuliki sana na mambo yanayoendelea, ni wavivu ama walio na tabia mbaya.
Sheria dhidi uhalifu nchini Nigeria inazuia kumtuhumu mtu ama hata kutishia kumtumu mtu kwamba ni mchawi. Na sheria ya kuwalinda watoto ya mwaka 2003 inasema kuwa ni makosa kumpiga mtoto ama kumuumiza kwa njia yoyote.
Hata hivyo huku sheria hiyo ikiidhinishwa katika ngazi ya kitaifa, majimbo 36 ya taifa hilo bado hayajaidhinisha. Hii inayapatia majimbo husika haki ya kibinafsi mbali na majukumu ya kuunda sheria zao zitakazoweza kusaidia kukabiliana na matatizo kama hayo. Ni majimbo robo tatu pekee ya Nigeria ambayo yameidhinisha sheria hizo za kuwalinda watoto na ni jimbo la Akwa Ibom pekee ambalo limeweka sheria muhimu zinazohusiana na unyanyasaji wa wanaodaiwa kuwa wachawi. Sheria yake ya mwaka 2008 imesema kiuwa wale watakaowaita wenzao wachawi watahukumiwa hadi miaka 10 jela. Na licha ya shinikizo, Jimbo la Cross River bado halijabadilisha sheria ya mwaka 2009 ili kuharamisha vitendo kama hivyo.
Lakini licha ya kujaribu kutangaza kitendo hicho kuwa cha uhalifu, tatizo la watu kuitwa wachawi linaendelea mbele ya macho ya serikali za majimbo hayo na maafisa wa polisi wa Akwa Ibom na Cross River.
Oliver Orok, Waziri wa maendeleo na masuala ya kijamii wa jimbo la Cross River aliambia BBC kwamba wizara inafanya kazi kuhakikisha kuwa tatizo hilo linaangamizwa.
“Serikali ya Jimbo hilo kwa ushirikiano na Unicef na washirika wengine wa kimaendeleo walipanga mkutano kuzungumzia kuhusu kufanyia marekebisho sheria, miongoni mwa vitu vingine suala la kuwaita watoto kuwa wachawi na madhara yake, alisema Bwana Orok.
Waziri huyo anasema kuwa sheria ya uhalifu imefutilia mbali vitendo kama hivyo. Hatahivyo miaka 10 baadaye hakuna mtu aliyeshtakiwa mahakamani.
Kumekuwa na ongezeko la kampeni katika jimbo hilo ili kukabiliana na tatizo hilo. Kulingana na Bwana Orok, fedha pia zimetolewa kujenga nyumba ya watoto waliopo hataraini.
Ameongezea kwamba iwapo serikali itapelekewa kesi kama hizo itakabiliana na makanisa kama hayo na manabii wake. Wakili james Ibor anasema kwamba maafisa wa polisi hawapati ufadhili wa kutosha ili kuweza kufanya uchunguzi kama huo.
“Kila mara tunalazimika kuweka shinikizo kuhakikisha kufanyika kwa uchunguzi," anasema Ibor anayesimamia shirika moja lisilo la kiserikali mjini Calabar kwa jina Basic Rights Counsel Initiative (BCRI). Shirika hilo huangazia visa vinavyohusu unyanyasaji wa haki za watoto mbali na kusimamia nyumba ambayo Comfort na nduguze wanaishi.
Ananiambia kuhusu watoto wawili ambao walipewa sumu na baba yao ambaye aliamini kwamba walikuwa wachawi. Alikiri kuwaua lakini hakukuwa na vifaa vya kutuma sampuli za damu mjini Lagos ili kuthibitisha sababu za kifo za watoto hao.
Mwaka mmoja baadaye, miili yao ipo katika chumba cha kuhifadhia maiti na baba yao bado hajashtakiwa.
Ibor anasema kuwa kesi zao zimekwama kwa miaka sasa.
Anasema kuwa kazi yake imefanywa kuwa ngumu kutokana na uzembe wa maafisa wa polisi na serikali kuchunguza masuala tata mbali na jamii na familia kuonyesha ishara za kutotaka kutoa ushahidi.
Robo ya kesi zinazoendelea zinahusiana na uchawi anasema. Lakini suala hilo linashirikishwa sana na majimbo ya mashambani nchini Nigeria.
Miezi sita iliyopoita, vyombo vya habari vya Nigeria viliripoti kuhusu watoto 40 ambao waliokolewa kutoka kwa kambi za unyanyasaji za waganga katika mji mkuu wa Abuja.
Na Mwezi Mei mjini lagos, mvulana mmoja alipigwa vibaya na mamake kwa kutumia kiboko.
Tunazo sheria, alisema Ibor. ''tatizo sio sheria - tatizo ni kuzitekeleza sheria hizo na hadi hilo lifanyike watoto wetu hawako salama''.
Na amewalaumu baadhi ya manabii na wachungaji kwa kuleta hofu miongoni mwa wakazi wa jimbo la Niger delta ambapo umaskini na imani za kichawi imesambaa.

Kufukuza mashetani
Jasho linaonekana likidondoka katika uso wa msichana anayegaagaa akiwa sakafuni.
Mtu mmoja anamshika kiunoni kabla ya kumzungusha. Lakini hii sio densi, ni mbinu ya kumfanya mtoto huyo kuondokwa na uchawi.
Wachungaji watatu wameunda timu ya kumponya msichana huyo mwenye umri wa miaka 15.
Kwa muda wa dakika 30 wanamchapa kichwa chake mara kadhaa, wakimfinya masikio mbali na kumshika tumbo.
Nguo zako zinachomeka, kichwa chako kinachomeka tumbo lako linachomeka, walirejelea matamshi hayo usoni mwake huku wakimpindua sakafuni.
Joy anaenua mikono yake kujikinga. watoto wanne wamewekwa katika orodha ya mchungaji Emmanuel kutolewa mashateni jioni hii, mdogo wao kabisa ana umri wa miaka minane.
Nguvu zinatoka kwa mtakatifu, anaelezea kabla ya tambiko hilo kuanza la kupunga mapepo kuanza.
Anatupatia nguvu kufanya kazi yetu ili kuwaokoa watoto. Unapowaombea watoto unaona mapepo - ukizungumza nao utasikia yakizungumza.
Tunapokamilisha shughuli hiyo mtoto anakuwa kama mwendawazimu ambaye amepona wazimu.
Mchungaji anaelezea kwamba kanisa lake la Calabar linatoa huduma kwa jamii yote kwa jumla.
Maombi haya huwazuia wazazi kuwakataa watoto wao, huzuia mapepo hao kuwapoteza, anasema.
Nani anayejua huenda wakawaoa watoto wao wa kike, anaongezea, hivyo basi kabla ya wewe kugundua, uchawi tunaokabiliana nao tayari upo nyumbani kwako.
Mchungaji Eunice anazungumzia kuhusu mapepo anayomtuhumu Joy kuwa nayo.
“Ulihudhuria mkutano wa wachawi? Wewe ni mchawi? Huwa unakunywa damu ya watu? Huwa wala nyama ya binadamu? Huwa unauwa?”
“Nimemwangamiza mtu mmoja pekee," Joy mwishowe anasema kwa sauti akilia.
Ni baada tu ya msichana huyo kuzirai na kuanguka sakafuni ambapo shughuli ya kumtoa mashetani na uchawi huaminika kuwa imefanikiwa.
Wakili James Ibor anasema makanisa ya Kipentekosti kama hayo huwahamasisha waumini wake kulaumu uchawi kwa masaibu yanayowakumba maishani au kwa taabu wanazopata.
Kisa hicho cha karibuni kinahusisha mvulana aliyechapwa na wazazi wake baada ya pikipiki ya familia hiyo kuharibika; katika kisa kingine, msichana alituhumiwa kuwa mchawi, na kuchapwa viboko na babake baada ya babake huyo kufutwa kazi.
“Huwa wanatumia hofu kuwadumisha waumini wao ambao kila wakati hutoa sadaka na fungu la kumi (mchango wa kila wiki).
“Hiyo ndiyo njia pekee ambapo wanaweza kuendelea kuwa na maana kwenye jamii na kujipatia pesa.”
Mwaka uliopita UN iliandaa warsha yake ya kwanza iliyoangazia uchawi, nchini Nigeria na mataifa mengine.
Katika ripoti baada ya warsha hiyo, umoja huo ulisema "idadi kamili ya waathiriwa na ukatili huu haijulikani, na inaaminika kwamba visa vingi huwa haviripotiwi”.
Umoja huo pia ulieleza mchango ambao hutekelezwa na "wajasiriamali wa kiroho" katika kueneza na kuhalalalisha wasiwasi unaohusiana na itikadi za uchawi katika jamii, na sana, kuwepo kwa watoto wachawi.

Kufungwa kwenye mti
Bassey anakumbuka jinsi wasichana wawili walivyotuhumiwa na mchungaji miaka miwili iliyopita katika kanisa la Divine Zion of God Church katika mji mdogo wa Akpabuyo, jimbo la Cross River.
Muumini aliyekuwa na uja uzito alikuwa amepitisha muda wake wa kujifungua kwa wiki kadha, na wasichana hao wa miaka saba na 10 walidaiwa kuhusika na wakadaiwa kuwa wachawi.
Mwanamke huyo alikuwa amekwenda kwa mchungaji katika kanisa lake na kulipa pesa apewe ufunguo. Ingawa alijifungua vyema muda mfupi baadaye, tayari madhara ya kitendo chake yalikuwa yametendeka.
Wiki moja baadaye, Bassey alisikia kilio cha wasichana hao alipokuwa anarejea nyumbani kutoka shambani.
Walikuwa wamefungwa kwenye mnazi, na walikuwa wanapigwa kwa vijiti na panga na wanaume watatu.
Ebe Ukara, afisa katika Kamati Tekelezi ya Haki za Watoto eneo la Akamkpa, anasema 60% ya visa vya kudhalilishwa kwa watoto ambavyo hufikishwa katika meza yake huwa vinahusiana na uchawi, na mara nyingi hutokana na tamko la mchungaji.
Wachungaji hao, anasema, wanaweza kujipatia pesa nyingi sana kutoka kwa watu wanaokimbilia kwao kuomba msaada, ingawa anasisitiza kwamba si makanisa yote ya Kipentekoste ambayo yanahusika katika kuwatapeli waumini.
Lakini kwa "manabii wa uongo", watoto ndio rahisi zaidi kusingiziwa. Wanaweza kusingiziwa kwa umaskini na madhila yanayokumba familia nyingi na jamii.
Kwa kuangalia tu mabango makubwa ambayo yametundikwa kwenye mizunguko ya barabara - kuanzia jiji kuu la Abuja hadi kwenye Niger Delta - pombe na ukombozi wa kiroho ndizo biashara kuu zaidi Nigeria, bidhaa zinazonunuliwa na kuuzwa.
Kila bango linaahidi muujiza - jinsi ya kupata kazi, kumpata mchumba, kukabiliana na kuharibika kwa mimba, utasa au ugumba, na bila shaka pia kukabiliana na uchawi.
Lakini mabango haya pia yanaonyesha mambo mawili makuu kuhusu imani za Kipentekoste ambazy imeenea sana nchini Nigeria tangu miaka ya 1970.
Kwanza, aina hii ya Ukristo husisitiza zaidi ufanisi na pesa au mali tele - iwapo mtu hajafanikiwa maishani, basi hiyo ni ishara kwamba kuna jambo ambalo haliko sawa pahali.
Pili, makanisa haya ya Kipentekoste huuonesha ulimwengu kama ukumbi wa vita kati ya nguvu za Mungu na nguvu za kishetani.
Kwa hivyo, makanisa haya ya Kipentekoste yameendeleza na kuvumisha dhana kwamba mali inapatikana kwa urahisi, lakini kwa wengi huzuiwa kuipata na nguvu za kishetani.
Lakini viongozi hawa wa makanisa Nigeria si kwamba wameanzisha dini ya kipekee Afrika au kwamba wanafuata utamaduni na itikadi za Kiafrika.
Badala yake, wanaiga wenzao wa Marekani ambao makanisa yao hufanya kazi zaidi kama majukwaa ya kuunda himaya za kiuchumi zaidi badala ya kuwa makundi ya kidini.
Hili limesababisha kuwepo kwa imani mahuluti hivi, ambapo wameunganisha itikadi za wenyeji hasa imani katika ushirikina na aina kali ya Ukristo ambayo wakosoaji wanasema huwafanya waumini kuwa kama watumwa wa kiroho.
“Makanisa haya ya 'uyoga' ni tatizo kubwa sana - manabii wao huongozwa na pesa," anasema Ukara.
Msemo huu wa 'makanisa ya uyoga' hutumiwa kurejelea makanisa haya kutokana na hali kwamba ni makanisa madogo madogo yenye vyumba visivyo rasmi na huchipuka popote pale kama uyoga na kukua haraka sana.
Kwa kiwango kikubwa huwa hayadhibitiwi na serikali.
Moja ya makanisa hayo ni Ark of Noah (Safina ya Noah), kanisa linalopatikana Calabar Kusini.

Nyumba ya Mungu
Ndala dogo za aina ya Winnie the Pooh zilizo nje ya mlango ndiyo ishara pekee kwamba ibada ya wokovu ya utakasaji inaendelea ndani.
Huku akiwa amevalia shati la rangi ya njano, Nabii Gideon Okon anasimama huku akiwaombea watoto watatu waliotuhumiwa kuwa wachawi.
“Mungu huyafungua macho yangu kuniwezesha kuyaona matatizo ya watu hawa," Okon anasema. "Hivyo ndivyo ninavyoweza kubaini nani mchawi.”
Anasema kwamba hakuna anayewaleta watoto kwake, kwamba huwa anapata ufunuo anapofunga na kujinyima chakula na kufanya maombi.
“Iwapo mtu huyo yuko tayari na anataka kukombolewa na kutakaswa, basi huwa tunaanza kujadiliana kuhusu malipo," anasema.
Okon anasema malipo hutegemea aina ya tambiko linalohitajika kufanywa kumtakasa mhusika.
“Walio na nguvu na hatari zaidi kuwaua huwa ni mapepo wa baharini,” anasema. "Kwa hao huwa natoza naira 200,000 ($556), lakini ni bei ya kuzungumza na wazazi.”
Katika eneo la Niger Delta, mtu mwenye pato la wastani huwa na bahati sana akijipatia pauni moja kwa siku.
Lakini Okon, ambaye zamani alikuwa anafanya kazi katika kampuni ya ujenzi, baadaye anakanusha kwamba huwa anawatoza watu pesa kwa huduma zake. Anasema huwa anapokea "mchango".
Baada ya saa kadha za maombi na nyimbo, watoto hao watatu - wa miaka kati ya 10 na 15 - wanalazimishwa kunywa majimaji ya rangi ya kijani kutoka kwa chupa ya soda.
Ndicho kitu cha kwanza wameruhusiwa kula au kunywa baada ya kufunga kwa lazima kwa siku tatu.
Okon anasema ni mchanganyiko, wa maji, mafuta ya mchikichi (mawese), mchanga, majani na tandu saba waliokaushwa na kusagwa kama unga.
“Mungu aliniambia viungo vinavyofaa kuvitumia," anasema.
“Huwa ni tofauti kwa kila mhusika.”
Ni baada ya watoto hao kutapika, ndipo inapoaminika kwamba "wameponywa" kabisa.

Mwisho wa waovu
Sekta ya filamu Nigeria - ambayo hufahamika kama Nollywood - inaendelea kunawiri.
Huwa inatoa filamu zaidi ya 2,500 kila mwaka, na kuifanya kuwa ya pili kwa kuzalisha filamu kila mwaka baada ya Bollywood ya India.
Filamu hizi kwa kawaida huwa katika makundi matano tofauti - za mapenzi, za ucheshi, za historia, za uhalifu na ujambazi, na za “halleluyah” ambazo huwa na ujumbe mzito wa kidini.
Unaweza ukazitazama katika vituo vya kupumzikia, migahawa, baa na kwenye mabasi. Huwa maarufu sio Nigeria pekee bali pia kote Afrika, na hata nje ya bara hili.
Evil School (Shule ya Maovu), Family of Witches (Familia ya Wachawi), School of Witches (Shule ya Wachawi) ni mifano tu ya filamu za hivi majuzi za Nollywood ambazo zinawaonesha watoto wakiwa kama wachawi.
Iliyozidi zaidi ni End of the Wicked (Mwisho wa Waovu), ambayo huangazia familia ya Amadi ambayo huishi na bibi mzaa baba - ambaye tunagundua kwamba ni mwanachama wa kundi la wachawi.
Watoto wa familia hiyo wanashawishika kujiunga na kundi hilo la wachawi, na kwenye filamu hiyo wanaoneshwa wakila nyama ya binadamu na kupanga njama ya kuwaua wazazi wao.
Filamu hiyo ya mwaka 1999 iliandaliwa na kanisa la Liberty Gospel Church, na miongoni mwa waigizaji alikuwa kiongozi wa kanisa hilo Helen Ukpabio aliyeigiza kama mchungaji ambaye kwa njia ya kishujaa anawafichua wachawi hao na kuwaangamiza.
Filamu hiyo ilizua utata na, wakati huo, ililaumiwa kutokana na kuongezeka kwa visa vya watoto kutuhumiwa kuwa wachawi katika miaka iliyofuata.
Ilishutumiwa kwa kufunika mpaka kati ya maisha ya uhalisia na uigizaji. Sio tu kwamba ilimhusisha mchungaji halisi ambaye alijiigiza mwenyewe, bali pia ilianza kwa ujumbe kwamba ilikuwa sehemu ya msururu wa makala za ufichuzi.
Wanigeria wenyewe wamezishutumu filamu kama hizo kwa kuendeleza dhana potofu kuhusu maisha Nigeria kte barani Afrika.
Katika sura kwenye kitabu kilichochapishwa majuzi kuhusu athari za filamu za Nollywood katika utamaduni, msomi Françoise Ugochukwu anakariri mtazamo wa raia mmoja wa Nigeria aliyekuwa akilalamika katika ukumbi mtandaoni.
“Filamu za aina hii zimeeneza picha mbaya kuhusu Nigeria...na kulifanya lionekane kama taifa linalotatizwa na ushirikina na imani na itikadi za kale," unasema ujumbe mmoja katika jukwa hilo. "Haijatosha kwa mataifa ya Magharibi kuzibandika tamaduni zetu sifa za kishetani, kwamba sasa tunajitendea hayo sisi wenyewe?
“Kwa kweli kuna mtu anayefikiria kwamba walichofanya mababu zetu ni kuketi tu siku zote na kufanya matambiko ya kishetani?”
Mwanasheria James Ibor anasema ni filamu kama vile End of the Wicked ambazo sio tu zimeendeleza dhana kwamba watoto wanaweza kuwa wachawi, bali pia kwamba watu wanaweza kuwa wachawi kwa kula chakula kilichotiwa nguvu za kichawi.
“Mtazamo ulibadilika kutokana na kuanza kuenea kwa filamu za Nollywood miaka ya 1990," anasema. "Ingia katika duka lolote la filamu hapa, na uchague bila kufuata utaratibu wowote filamu 50, na nakuhakikishia kwamba 80% kati ya utakazozichagua zitakuwa zinazungumzia uchawi na juju."
Lakini linaloshangaza zaidi ni kwamba moja ya sababu ya filamu za Nollywood kuwa maarufu ni kwamba huwa zinatoa jukwaa kwa Waafrika kusimulia hadithi kuhusu maisha yao wenyewe.
Mmoja wa waandaaji wa filamu Nollywood, Orok Atim, anasema ingawa mada ya uchawi ni mbaya, ni suala ambalo huathiri maisha ya watu wengi Nigeria - na hivyo basi huwa wanatarajia kukutana nayo wanapokuwa wanatazama filamu za Nigeria.
Orok Atim ameketi mbele ya 'madhabahu' yake ya muda, akiigiza filamu yake ya karibuni zaidi.
Ingawa filamu hiyo anayoiandaa ni hadithi ya mapenzi (pichani), Atim huwa anapenda sana kuandaa filamu kuhusu mambo ya kiroho na ushirikina.
Filamu yake itakayofuata itakuwa kuhusu rafiki yake ambaye kwa sasa ni marehemu alivyokumbana na uchawi.
“Uchawi upo katika jamii yetu hata wa leo," anasema. "Usipoonyesha kinachofanyika katika jamii bado utakuwa unapoteza muda wako.
“Huwa natumia filamu zao kuelimisha, kuburudisha na kuueleza ulimwengu kwamba uchawi upo.”
Hakuna filamu hata moja inayowaonyesha watoto bayana kama wachawi.
Atim anasema filamu zake huwa zinawawezesha watazamaji wake Nigeria kukabili woga walio nao, na si kuendeleza itikadi za kichawi na ushirikina.
Kwa kutumia ubunifu wa kompyuta, filamu zake hufanya vitu visivyoonekana kuonekana; na huwapa watu taswira au muonekano wa kitu cha kiroho ambacho huwa hakionekani lakini huzungumziwa sana.
Na Atim anapinga dhana kwamba filamu kama vile End of the Wicked zinachangia katika kuenea kwa visa vya watoto kutuhumiwa kuwa wachawi.
“[Lakini unachokisema ni] uvumi tu wa kutaka kuua filamu za Nollywood,” anasema. "Hakuna mtu anaweza kutoa hadithi kuhusu mambo ambayo hayapo.”
Diana-Abasi Udua Akanimoh, anayefanya kazi na shirika lisilo la kiserikali kwa jina Way to the Nations katika jimbo la Akwa Ibom, anasema amejionea mwenyewe madhara ya filamu hizo zenye mada za kichawi.
“Nilikwenda katika kanisa moja hapa Eket na mchungaji alikuwa anazungumzia jinsi ya kuwazuia mapepo wa baharini na uchawi," anasema. "Alianza kwa kuwaambia waumini wake kwamba alikuwa ameyaona mambo kama hayo katika filamu aliyokuwa ameitazama majuzi.”
“Kwa hivyo, watu wasio na habari au wasiofikiria kwa undani watakuwa wanafikiria, 'Oh, iwapo mchungaji anasema haya, basi hilo lina maana kwamba ndio ukweli’.”
Akanimoh, ambaye husimamia jumba salama ambalo ni kimbilio kwa watoto wanaotuhumiwa kuwa wachawi, anasema ingawa filamu hizo sio chanzo hasa cha tuhuma hizo, bila shaka hukuza na kuendeleza utamaduni unaotumiwa kutetea vitendo kama hivyo.
Na mfanyakazi wa kijamii Ebe Ukara anadai kwamba "watu hutazama filamu hizi na kuiga yale wanayoyaona manabii hawa wakifanya."
Ukara alihusika katika kuokolewa kwa Comfort na ndugu zake baada yao kupigwa na nabii huyo na kushambuliwa kwa panga.
“Filamu siku hizi zinafunza mambo mengi sana ambayo watu hawakuyafanya zamani," anasema. "Kumpeleka mtoto kanisani ukampige - hilo halikuwepo.”
Lakini waziri Oliver Orok anasema serikali haiamini filamu za Nollywood ndizo zinazofaa kulaumiwa. Badala yake inaamini tatizo ni "itikadi za muda mrefu za baadhi ya jamii”.

Kufukuzwa
Charity ni mmoja tu miongoni mwa watoto wengi wanaoishi barabarani baada ya kutuhumiwa kuwa mchawi.
Kwa miaka miwili iliyopita, msichana huyu wa miaka 13 amekuwa akiishi kwenye kibanda katika jaa la taka viungani mwa mji wa Calabar.
Ndani ya kibanda hicho, wasichana wengine wanne wa umri karibu na wake bado wamelala - hakuna godoro, na pia hakuna vyandarua vya kujikinga dhidi ya mbu.
Maisha ni magumu, lakini siku nzuri ninaweza kujipatia Naira 1,500 ($4) kwa kutafuta chupa za soda za plastiki na mikebe ya chuma inayoweza kutumiwa tena kutoka kwenye jaa hilo la taka.
“Najihisi vyema kuishi hapa," ananong'oneza Charity. "Kurejea kuishi katika nyumba ya mjomba wangu itakuwa ni kama kujiweka motoni.”
Baada ya babake kufariki dunia, alikwenda kuishi na mjomba wake.
Alipojaribu kumnajisi, alituhumiwa na mke wake kwamba alikuwa amemroga.
“Walinifunga mikono, na kutishia kunitupa ndani ya choo," anasema.
“Waliniweka hivyo kwa siku moja," anasema. "Kwa hivyo, ilinilazimu kusema kwamba nilikuwa mchawi ili wanifungue mikono."
Baada yake "kukiri", mjomba wake aliacha kumpa chakula, na akaamua kutoroka.
Jaa la Lemna ni makao kwa watoto wa mtaani mia kadha ambao hufahamika kama skolombo - watoto kama Charity.
Wengi wana hadithi zinazoshabikiana - walifukuzwa au wakatoroka nyumbani baada ya kutuhumiwa kuwa wachawi.
Makundi kadha yasiyo ya kiserikali Nigeria kama vile Basic Rights Counsel Initiative (BRCI) na Way to Nations hujaribu kufanya zaidi ya kuwaokoa tu watoto waliotuhumiwa kuwa wachawi - huwa wanajaribu kuwakutanisha tena na jamaa wale wale ambao waliwatuhumu watoto hao kuwa wachawi.
Juhudi kama hizo huwa nadra kufanikiwa, hata kwa jamaa wasio wa karibu sana.
Tukirudi tena Calabar, James Ibor anakabiliwa na tatizo la afanye nini na Comfort na ndugu zake wawili.
Wanataka kuondoka kituo chake, lakini hakuna jamaa anayetaka kuwachukua.
“Tutawafahamishaje taarifa hizi kwa watoto hao, kwamba shangazi zao na wajomba wao hawako tayari hata kuwaona?" anasema.
“Watoto hawa basi wakati huo wanaweza hata wakaanza kufikiria pengine kwamba ni kweli wao ni wachawi.”

Shukrani:
Makala hii ilifanikishwa kupitia ufadhili kutoka kwa Pulitzer Center on Crisis Reporting.
Mwandishi, Mpiga picha & Mpiga video: Marc Ellison
Michoro: Ozo Ezeogu (Comic Republic)
Tafsiri: Abdalla Dzungu na Peter Mwai
Mwandalizi: James Percy
Mhariri: Kathryn Westcott
Imeundwa kwa kutumia Shorthand
Picha zote zina Hakimiliki


Comments