Featured Post

WAKULIMA WA KOROSHO TANGA WAISHUKURU SERIKALI KWA KUWAJALI KWA PEMBEJEO



WAKULIMA wa korosho katika Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga wamepongeza juhudi za serikali za kuwapelekea kwa wakati dawa za kupuliza mashamba yao na kwamba zimekuja kipindi ambacho miti ya zao hilo inahitaji kutibiwa.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzake kwenye uzinduzi wa kampeni ya matumizi ya dawa za kutibu mikorosho uliyofanyika katika kitongoji cha Bawa, mkazi wa kijiji cha Gezani, Mbwana Mwaroho aliishukuru
serikali kwa kuwaletea dawa hizo kwa wakati kwa kuwa kipindi hiki ndicho ambacho mikorosho inaanza kutoa maua na wanahitaji dawa.
Mwaroho alisema  suala la upatikana wa dawa limekuwa changamoto lakini kwa sasa Serikali ya awamu ya tano imekuwa ikileta dawa hizo kwa wakati.
Akizindua kampeni hiyo Meneja wa Bodi ya Korosho tawi la Tanga, Ugumba Kilasa  aliwataka wakulima wa zao hilo kulima kisasa badala ya kuendelea na kilimo cha mazoea ambao hauna tija.

Alisema kampeni hiyo itafanyika  kwenye Wilaya za Mkinga, Pangani na Muheza na kwamba lengo ni kuhamasisha matumizi ya dawa ili kukabiliana na milipuko ya magonjwa ya miti ya mikorosho na hivyo kuwafanya wakulima kubadilisha maisha yao kupitia zao hilo.
Aliwataka wakulima kutumia dawa kwa usahihi kwa maelekezo ya wataalamu hali ambayo alidai kuwa itawanufaisha na kubadilisha maisha yao kwa kutumia kilimo.
Alieleza kuwa kwa kuwatumia wataalamu zao hilo litawabadilisha kimaisha na hivyo kwenda sambamba na mpango wa serikali wa kumfanya mkulima kuwa na maendeleo kwa kulima kitaalamu na kuvuna kwa wingi na gharama nafuu.
Kilasa alisema kuwa jumla ya lita  elfu 20 za dawa ya maji na tani 60 za dawa ya safa ya unga zimeshapokelewa na kwamba lengo ni kutaka zitumike muda huu kwa kuwa ni kipindi cha mikorosho kutoa maua na ambacho wadudu waharibifu hukitumia kuyashambulia.
Naye Mratibu wa zao la Korosho Wilaya ya Mkinga, Nzaro Kijo alieleza zoezi hilo kuwa litafanyika katika mashamba ya mfano na kwamba dawa kwa ajili ya wakulima zimehifadhiwa kwenye ghala la Gezani ambako matangazo na taratibu za upatikanaji zimeshawekwa.
Kijo  aliwataka wakulima ndani ya Kata 22 za Wilaya hiyo kutumia fursa hiyo kutibu mazao yao ili kuyanusuru na magonjwa na kuongeza pato ambalo sasa limeshuka kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo magonjwa ya miti ya mikorosho.
Naye Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Wakulima wa  Korosho Mkoa wa Tanga, Mashi Sopa aliwahakikishia wakulima wa zao hilo usalama wa mazao yao na kwamba chama hicho kimejipanga kukabiliana na changamoto ya walanguzi wa korosho.


Comments