Featured Post

VISIMBUZI VYOTE SASA KUONYESHA CHANELI ZA NDANI BURE - SERIKALI



NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imesema kuanzia sasa, visimbuzi vya Starmedia, Digtek, Continental na TING vitaanza kuonyesha chaneli zote za ndani bila kutoza gharama yoyote kwa mtazamaji.

Akizungumza na  waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi alisema serikali imefikia uamuzi huo baada ya visimbuzi vya Azama, Zuku na DSTV kuzuiwa  kuonyesha chaneli za ndani kulingana na aina ya leseni zao.
Akifafanua kuhusu mazungumzo kati ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, na wadau pamoja na wamiliki wa  vituo mbalimbali vya televisheni  nchini yaliyofanyika mapema jana, Dkt. Abbasi alisema kuwa  kuanzia sasa chaneli zote za ndani zinapaswa kuonekana bila kutoza gharama yoyote kwa mtazamaji.
“Ningependa Watanzania wafahamu kwamba kuanzia sasa visimbuzi vya TING, Starmedia, Continental na Digtek vitaonyesha takriban chaneli 34 za ndani bure, ili kutoa fursa ya kila mwananchi kuwa na haki ya kupata taarifa,” alisema Dkt. Abbasi.
Aidha, alielezea kuwa wadau hao pamoja na wamiliki wa vituo vya televisheni wameonyesha kuridhishwa na hatua hiyo ya kwa vile Serikali imetengeneza miundombinu itakayoruhusu chaneli zao kuonekana nchi nzima.
Dkt. Abbasi, alisisitiza kuwa “tayari nchi imeandaa mifumo ya kuhakikisha kwamba bila kutegemea kampuni za nje, au zilizosajiliwa nje ya nchi, tulishajenga mifumo ya ndani ya kusaidia kurusha matangazo nchi nzima”
Vilevile, aliwatoa hofu watazamaji kwa kusema kuwa kufikia Septemba 5, mwaka huu visimbuzi vyote vitakuwa na chaneli zote za ndani bila kutoza gharama yoyote kwa mtazamaji.
Kuhusu baadhi ya wateja kulalamikia visimbuzi vya Starmedia, kutoonyesha chaneli za ndani, Dkt. Abbasi alisema wameshaagizwa kuvifungua vyote na zoezi hilo litaendelea hadi Septemba 5 ambapo wataonekana nchi nzima.
Dkt. Abbasi, alisema visimbuzi vya Azama, Zuku na DSTV hao wataendelea kuonyesha maudhui mengine lakini siyo chaneli za ndani kama leseni zinavyowataka.

Comments