Featured Post

TAMKO LA MHE. UMMY MWALIMU (MB) WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA TIBA ASILI YA MWAFRIKA TAREHE 31/8/2018 – DODOMA.


Ndugu wananchi,
Maadhimisho ya Siku ya Tiba Asili ya Mwafrika yalianza rasmi mwaka 2003 baada ya Mawaziri wa Afya wa nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika kuridhia kuwepo kwa sherehe hizo. 
Maadhimisho haya hufanyika katika nchi 46 za kanda ya Afrika ambazo ni wanachama wa Shirika la Afya Duniani tarehe 31/08 ya kila mwaka na huu ni mwaka wa 16 tangu maadhimisho haya yafanyike.

Ndugu wananchi,
Tanzania, imekuwa inaadhimisha maadhimisho haya kwa malengo makuu manne. Kwanza ni kufufua ari na kujenga heshima ya huduma za tiba asili ambazo kwa mujibu wa historia zimekuwa zikikandamizwa na kudharaulika. Kuanzia wakati wa ukoloni hadi leo na kuzifanya tiba zetu za asili na Waafrika wenyewe kuzinyanyapaa tiba hizo. Hali hiyo imetufanya tuyumbe, tukose dira na mwelekeo katika suala zima la kuboresha  Tiba Asili katika nchi zetu.

Pili kwa kupitia maadhimisho Waganga wa Tiba Asili wamekuwa wakihamasishwa kujiepusha na migongano katika jamii kwa kutohusisha ushirikina na uchawi kama chanzo cha ugonjwa. Aidha, wataalamu wa tiba ya kisasa nao wamekuwa wakihamasishwa kushiriki katika kuendeleza na kuboresha huduma za tiba asili.

Tatu, maadhimisho haya yanahimiza masuala ya uboreshaji wa dawa za asili na utengenezaji wa dawa hizo kiviwanda. Aidha,  utafiti endelevu wa dawa za asili kwa magonjwa mbalimbali unahimizwa kwa madhumuni ya kupata dawa ambazo zinaweza kupatikana kiurahisi  ili mwenye kuhitaji aweze kuzipata.

Nne, kwa kupitia maadhimisho haya Waganga wa Tiba Asili wanahimizwa kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili ya taaluma na huduma za afya.

Ndugu wananchi,
Katika kuadhimisha Siku ya Tiba ya Asili ya Mwafrika kila mwaka tunakuwa na ujumbe maalum au kauli mbiu. Ujumbe maalum wa mwaka huu ni Utengenezaji wa dawa za asili katika Afrika” (Local manufacturing of traditional medicine products in the African Region).

Kauli mbiu hii inalenga kuanzisha viwanda vya kutengeneza dawa za asili nchini. Kauli mbinu hii inaendana na mkakati waSerikali ya awamu ya tano inayohimiza uanzishwaji wa viwanda nchini. Kwa sasa kutoka mwezi Oktoba mwaka 2017, vituo vitatu vya uzalishaji wa dawa vilivyopo Dar es Salaam, Moshi na Arusha vilikaguliwa na kukidhi vigezo vya kutengeneza dawa za asili. Vituo hivyo vitatu vimetengeneza dawa ambazo zilikidhi vigezo vya kusajiliwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala. Dawa hizo ni pamoja na: (1). Ujana; (2). Sudhi; (3). IH- Myoon; (4). Apamol; na (5). Vatari. Dawa nyingine kumi za (1). Billyd Formular Power; (2). Vission 2; (3). JC; (4). Fiwemu; na (5). 4A9; (6) Joy Natural Herbal  (7) Mshana; (8). Life; (9). Detoxcer na (10). Low oxygen zipo katika chakato wa kusajiliwa.

Aidha, dawa za asili zilizosajiliwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ni (1). Ravocream; (2). Mangifera cream; (3). Morizella® juice sweet; (4). Morizella® juice (Sugar free); zinazotengenezwa na Taasisi ya Madawa Asili iliyo chini ya MUHAS. Pia, Mansoordaya Chemicals Ltd inayotengeneza dawa za (1). Ayu Koff; (2); Herbal health tonic     na (3).Ayu DD syrup.

Pia, hadi tarehe 30 Julai, 2018; waganga 19,141; vituo 221 na dawa za asili tano zimesajiliwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala.

Nawashauri Watengeneza dawa za asili kuzingatia Sheria, kanuni, miongozo na taratibu zinazowasimamia katika kuhakikisha kuwa bidhaa zitengenezwazo zinakidhi usajili. Aidha, mjiepushe na matangazo  yanayokizana na sheria, kanuni, miongozo na taratibu ikiwa pamoja na matangazo ya dawa ambazo hazijafanyiwa uthibitisho kuwa ni salama.

Ndugu wananchi,
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatambua huduma za tiba asili kuwa tiba rasmi kwa mujibu wa Sera ya Afya. Tanzania inayo mitidawa mingi na mingi inatumika kutibu magonjwa mbalimbali.  Pia ni ukweli usiopingika kuwa  dawa nyingi za kisasa hutengenezwa kutokana na mitidawa, na elimu ya mwanzo kabisa juu matumizi ya miti hiyo kutumika kama dawa inatokana na waganga wa tiba asili. Tanzania ina rasilimali kubwa ya mitidawa na wapo waganga wenye ujuzi katika hilo. Hivyo basi, ni vyema  wataalam wa tiba ya kisasa na waganga wa tiba asili shirikianeni kwa lengo la kuboresha na kuendeleza huduma na dawa za tiba asili.

Kwa kuzingatia ukweli huo, Serikali imekuwa na itaendelea kuhakikisha kuwa tiba asili inaboreshwa na kuendelezwa. Kuanzia sasa vyuo vyote vya afya vya Serikali vitakuwa vinawafundisha Waganga wa Tiba Asili kwa kutumia kitabu kilichaandaliwa na Wizara ili kuwa na uelewa wa pamoja baina ya Wataalam wa afya wa kisasa na waganga wa tiba asili. Kwa kuanzia vyuo vifuatavyo vitaanza; (1). Chuo cha uuguzi Mirembe, (2). Chuo cha Waganga Wasaidizi Mafinga, (3). Chuo cha uuguzi Njombe, (4). Chuo cha uuguzi Mtwara, (5). Chuo cha Waganga Wasaidizi Kibaha, na (6). Chuo cha uuguzi Morogoro.

Ndugu wananchi,
Fomu za usajili zinapatikana katika Ofisi za Waganga Wakuu wa kila Halmashauri nchini. Kila Halmashauri ina Mratibu wa Tiba ya Asili na Tiba Mbadala anayesimamia namna ya kufanya USAJILI wa mganga, kituo na dawa za asili.

Nitoe wito kwa Waganga na Wadau wa Tiba Asili kuzingatia Sera, Sheria, kanuni, miongozo na taratibu zinazowasimamia katika kutoa huduma za tiba asili kwa wateja wao. Aidha, nawataka waganga kujiepusha na matangazo  yanayokizana na sheria, kanuni na taratibu ikiwa pamoja na kuondoa mabango yaliyozagaa mitaani yanayoonyesha kuwa wanaweza kutibu na kuponya magonjwa mbalimbali kwa mfano UKIMWI. 

Pia, Waganga wa Tiba Asili acheni kutumia vifaa msivyojua matumiazi yake kwa mfano mashine za QUANTUM. Mnawadanganya wananchi kuwa mnafahamu matumizi ya mashine hizo. Tuliishatoa maelekezo kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kutoa elimu kwa waganga wa tiba asili na tiba mbadala. Sheria zilizopo zitumike kuhakikisha kuwa mashine za QUANTUM haziendelei kutumika nchini.

Ndugu wananchi,
Napenda kuwakumbusha wananchi kwamba huduma za tiba asili zinatambuliwa kwa mujibu wa Sera ya Afya na Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala, Namba 23 ya mwaka 2002. Madhumuni ya sheria hiyo ni kusimamia, kudhibiti na kuendeleza tiba asili ya Tanzania. Vilevile, udhibiti wa maadili ya uganga na ukunga wa tiba asili nchini umepewa kipaumbele.

Kwa mujibu wa Sheria hiyo, Baraza la Waganga wa Tiba za Asili na Tiba Mbadala limeundwa kama chombo cha Serikali kitachosimamia na kuratibu shughuli za usajili wa watoa huduma, wasaidizi wa watoa huduma, vituo vya huduma vya tiba asili na dawa za asili. Ni muhimu kwa kila mdau wa tiba asili kuzingatia Sera, Sheria, Kanuni, Miongozo na taratibu zilizowekwa, kuachana na matangazo yasiyofaa, kuacha kuweka mabango hovyohovyo barabarani, matangazo katika vyombo vya habari ni lazima yapate kibali cha Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala.

Ahsanteni



Comments