Featured Post

TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE YASAINI MKATABA WA USHIRIKIANO NA HOSPITALI YA FUWAI YA NCHINI CHINA

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imesaini  mkataba wa kushirikiana na jimbo la Shandong na Hospitali ya magonjwa ya Moyo ya Fuwai iliyopo mjini Beijing nchini China. 

Mkataba huo ulisainiwa hivi karibuni nchini China na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Prof. Mohamed Janabi na Prof. Shengshou Hu wa jimbo la Shandong mbele ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,  Jinsia, Wazee  na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu na Waziri wa Afya wa China Mhe. Xiaowei Ma.
Makubaliano yaliyosainiwa  katika mkataba huo ni kutolewa kwa  mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa madaktari, wauguzi na wataalam wanaoendesha mashine za moyo (Technician) na kufanya kambi maalum za matibabu ya moyo ambazo zitasaidia kuwajengea uwezo wataalam wa hapa nchini. 
Katika kutekeleza makubaliano hayo kabla ya kumalizika kwa mwaka huu wataalam watatu ambao ni Daktari, Muuguzi na mtaalam wa kuendesha mashine za moyo (Technician) watakwenda katika Hospitali hiyo kwa ajili ya mafunzo ya muda mfupi. 
Hospitali ya Fuwai ni  kituo cha kitaifa cha kutibu na chuo cha kufundisha wataalam wa magonjwa ya moyo ilianzishwa mwaka 1956  ina wodi 41, vyumba vya upasuaji wa moyo 28, vyumba vya kufanya upasuaji wa bila kufungua kifua kwa njia ya kutoboa tundu dogo katika mshipa mkubwa wa paja au mkono (Cath lab) 13 na vitanda vya kulaza wagonjwa 1238.
Imetolewa na:
Kitengo cha Uhusiano
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
29/08/2018

Comments