Featured Post

MISAADA NI MAVAZI YA KUAZIMA HAITATUSITIRI



NA ALOYCE NDELEIO
MIONGONI mwa mikakati inayojionesha na kupewa kipaumbele na serikali ni pamoja na kuhakikisha jitihada za kujinyanyua kiuchumi zinakuwa na ufanisi ili kuondokana na utegemezi wa misaada.
Hali hiyo ni pamoja na kuzitumia rasilimali zilizopo nchini  kuinua uchumi pamoja na kuanzisha  nyenzo za kuufanya uchumi huo uwe endelevu ka kuwa na uchumi wa viwanda.
Lakini hoja moja  inafanya au kuonesha kuwa jamii ilisokomezwa katika usingizi kwa kutegemea misaada na papo hapo wanaotoa misaada  kuwa na upeo unadhihirisha kuisoma jamii namna ambavyo inajiendesha.

Hoja ni kwamba hivi Tanzania ya leo ingekuwa katika hali gani kama wahisani wanaoipa misaada toka ipate uhuru wasingekuwepo? Swali hili na mengine ambayo yamekuwa yakiuumiza vichwa vya watu  linatokana ‘kilio’ ambacho kimetolewa hivi karibuni na viongozi waandamizi wa serikali.
Wahisani nao kwa kugundua matendo yanayofanywa na nchi kuwa hayana tija waliamua kuikatia Serikali misaada ya  shilingi trilioni moja kutokana na kashfa ya IPTL pamoja na kitendo cha fedha kuchotwa katika Akaunti Maalum ya Tegeta Escrow, zaidi ya sh bilioni 200, zilizohifadhiwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Hali hiyo ilisababisha serikali kusema, “Hawa wahisani mara nyingi wamekuwa na sababu mbalimbali na hata huko nyuma walishawahi kufanya hivyo, lakini safari hii wanasema wamekata misaada yao kutokana na kashfa ya IPTL na wanasema wanasubiri ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ije, hili ni jambo linalonisononesha sana kwa sababu uamuzi huo utaathiri watu wengi.”
Hoja inayoibuka hapa ni kwamba machungu ya kutegemea misaada  hapo ndipo  yanapoanza kuonekana. Hadi miaka ya karibuni ilifahamishwa kuwa toka mwaka 1961 Serikali za Tanzania [Bara na Zanzibar] zimeomba, kupokea na kutumia mikopo na misaada toka nje ya nchi inayozidi jumla ya Dola za Kimarekani bilioni 20 (zaidi ya Shilingi  milioni 26,000).
Hiyo ni taarifa ya utafiti uliofanywa na wataalamu watatu waandamizi katika Benki ya Dunia ambayo inaonesha kwamba katika kipindi cha miaka 26 tu (1970-1996), Tanzania ilipewa jumla ya dola milioni 16,632 (shilingi 21,621.6 bilioni) na wafadhili mbalimbali wa nje. Fedha hizo ni zaidi ya asilimia 80 ya jumla ya mapato yote ya Tanzania ya fedha za kigeni kwa kipindi hicho.
Mtiririko wa misaada na mikopo kwa Tanzania ulikuwa unaongezeka kutoka dola milioni 37.7 mwaka 1970 hadi kufikia dola milioni 1,158 mwaka 1992 na kushuka tena kidogo hadi dola milioni 830 mwaka 1996, inasema ripoti hiyo.
Inakadiriwa kwamba kati ya 1970 na 1980, Tanzania ilikuwa inapata misaada (sio mikopo) mingi kupita nchi yoyote miongoni mwa nchi zinazopokea misaada ya Jumuiya ya Kimataifa ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo iitwayo kwa Kiingereza Organization for Economic Co-operation & Development (OECD). Kamati maalumu ya OECD inayogawa misaada ilitaarifu kwamba Tanzania ilikuwa inapata asilimia 8.3 ya jumla ya misaada yote ya OECD katika kipindi hicho cha muongo mmoja (1970-80).
Tunaarifiwa kwamba utafiti wa wataalamu hao wa Benki ya Dunia ulifanywa katika nchi 10 za Afrika zilizopata uhuru takribani miaka 50 iliyopita na ambazo zimepokea misaada na mikopo mingi ya nje. Nchi hizo ni Tanzania, Uganda, Kenya, Zambia, Ethiopia, Nigeria, Ghana, Cote de’ Ivoire, Mali na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Katika mtazamo mwingine ni kwamba Tanzania imekuwa na ‘bahati kubwa ya kupendwa’ na wafadhili kwani hata wakati sera za serikali kuhusu maendeleo zilipokuwa mbaya na kuwachukiza (1985-90), baadhi yao bado waliendelea kuipa misaada.
Katika kipindi hicho Tanzania ilipata misaada zaidi ya mara mbili ya ile iliyopewa Ghana ambayo kwa kipindi hicho ilikuwa ndio nchi ya Afrika inayosifiwa na wafadhili kwa kufanya vizuri mageuzi ya kiuchumi.
Kabla ya 1970, Serikali ya mwanzo ya Tanzania chini ya Mwalimu Julius Nyerere ilikuwa imefanikiwa kuvutia sana wafadhili wa nje na kupewa misaada na mikopo mingi  ili kutekeleza sera zake za maendeleo chini ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.
Falsafa ya Mwalimu Nyerere ya kujenga nchi ya usawa na msisitizo wake katika kujitegemea vilivutia sana viongozi wa nchi za Ulaya Kaskazini (Scandinavia) waliokuwa wameegemea kwenye siasa za Ujamaa wa Kijamii (Social Dermocrats). Hata kiongozi maarufu wa Ujeumani wakati huo Willy Brandt na Waziri Mkuu wa Canada walivutiwa sana na Ujamaa wa Tanzania, inasema ripoti hiyo.
“Benki ya Dunia ilizidisha mara mbili mikopo kwa Tanzania kati ya 1973 na 1977 kwa sababu Bwana Robert McNamara aliyekuwa rais wake wakati huo alikuwa anatekeleza sera ya ukuaji sawa kiuchumi iliyokuwa inashabihiana na mikakati ya maendeleo ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Nyerere,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Hata hivyo, Benki ya Dunia na wafadhili wengine walianza kupingana na sera za Ujamaa wa Tanzania ilipokaribia mwaka 1980. “Kulijitokeza ushahidi kwamba licha ya mipango mizuri chini ya Azimio la Arusha hakukuwa na mafanikio ya Ujamaa wala Kujitegemea na hivyo misaada toka nje ilikuwa inafujwa,” inasema ripoti ya Watafiti wa Benki ya Dunia.
Misaada kwa Tanzania imekuwa inatoka katika nchi zipatazo 50 wakati mikopo mingi inatoka Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Benki ya Maendeleo kwa Afrika (AfDB) na Umoja wa Ulaya (EU). Wafadhili wakubwa wa misaada (isiyo mikopo) kwa Tanzania ni nchi nne za kaskazini mwa Ulaya (Skandinavia) ambazo ni Sweden,  Norway, Denmark na Finland).
Nchi hizi zimetoa zaidi ya asilimia 30 ya misaada yote iliyofika Tanzania kati ya 1970 na 1996. Sweden peke yake imetoa nusu (asilimia 15) ya misaada iliyotolewa na nchi za Scandinavia. Nchi hizo ndio zimekuwa na tabia ya ung’ang’anizi wa kutoa misaada hata wakati sera za serikali zilipowachukiza wafadhili wengine.
Wafadhili wengine wakubwa kwa Tanzania ni nchi za Ujerumani na Uholanzi ambazo zimetoa asilimia nane ya misaada. Wafadhili wengine maarufu ni Canada, Uingereza na Marekani. Nchi hizo zilitoa asilimia sita ya misaada yote kwa Tanzania katika kipindi cha 1970 – 96.
Pamoja na nchi wafadhli misaada mingi kwa Tanzania imekuwa inatoka katika Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo (UNDP), Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi (UNHCR) na asasi tanzu ya Benki ya Dunia (IDA).
Leo hii wahisani hao wameonesha makali yao na huenda ni kwa kuona kuwa  misaada inayotolew  kuwa haiwafikii walenga. Hiyo ni sehemu tu je, wakifunga milango kabisa tatasononeka kiasi gani?
Je, hatuwezi kutumia rasilimali zetu kujitegemeza badala ya kutegemea hisani? Kama wahisani hao wanachukizwa na ukwapuaji mbona baadhi wanaonesha kutochukizwa na hali hiyo?
Hapa ndipo panatakiwa kuzimuliwa kwamba tunaweza kutumia rasilimali zetu na kujitegemea na kuachana na utegemezi wa misaada kwani misaada hiyo ni nguo ya kuazima haiwezi kuisitiri nchi.

Comments