Featured Post

MADIWANI TABORA WAPEWA SIKU 14 KUREJESHA VIWANJA WALIVYOJIMILIKISHA

MADIWANI wa halmashauri ya Manispaa ya Tabora wamepewa muda wa siku 14 kurejesha viwanja vyote walivyojimilikisha kiyume na utaratibu.

Agizo hilo limetolewa  na Mkuu wa wilaya ya Tabora Komanya Eric Kitwala alipokuwa akizungumza na Madiwani, Wakuu wa Idara na Vitengo na Watendaji wa halamashauri ya manispaa hiyo.
Alisema manispaa hiyo inakabiliwa na migogoro mingi ya ardhi isiyoisha ambayo kwa kiasi kikubwa imesababishwa na baadhi ya watumishi na madiwani wa halmashauri hiyo kujimilikisha viwanja vingi kinyemela na kinyume na utaratibu.
Alisema kitendo cha diwani au mtumishi yeyote aliyepewa dhamana ya kusimamia maendeleo ya wananchi kutumia wadhifa wake kwa maslahi binafsi ni kwenda kinyume na maadili ya utumishi.
‘Natoa siku 14 kwa madiwani wote waliojimilikisha viwanja kinyume na utaratibu katika maeneo mbalimbali ya manispaa hii kujisalimisha, la sivyo sheria itachukua mkondo wake’, alisema.
Kitwala alisisitiza kuwa amedhamiria kumalizia migogoro yote inayohusiana na mambo ya ardhi katika wilaya yake na kwa kuanzia ametenga siku ya Ijumaa ya kila wiki kuwa siku maalumu ya kusikiliza malalamiko ya wananchi na kuyatafutia ufumbuzi.
Aliwataka wananchi wote wenye malalamiko ya viwanja kufika ofisini kwake wakiwa na vielelezo husika ili aweze kumaliza mgogoro huo, aliagiza wataalamu wa idara husika kufika ofisini kwake siku ya kusikiliza malalamiko ya wananchi ili haki itendeke.
Aidha aliagiza Wakuu wa Idara na Watendaji wote kutokaa Ofisini bali waende vijijini kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na kusikiliza kero za wananchi kwa kuwa kila siku amekuwa akipokea meseji za malalamiko ya wananchi.
Diwani wa Kata ya Ndevelwa (CCM) Seleman Juma Maganga ambaye ndiye Msemaji wa madiwani wote wa CCM alimshukuru Rais John Pombe Magufuli kwa kuwaletea DC mwenye maono makubwa ya maendeleo.
Aliwataka wataalamu wa manispaa hiyo kuwajibika ipasavyo na kujiepusha na uzembe wa aina yoyote ile ili kwenda na kasi ya Mkuu wao mpya wa wilaya vinginevyo  atawawajibisha.

Comments