Featured Post

MAALIM SEIF SHARIF HAMAD ‘AMEITOSA’ Z’BAR



NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
WAZANZIBARI wameshauriwa kutomtafuta mchawi  aliyeikwamisha nchi hiyo isijitoe katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Anayestahili kubeba lawama zote ni Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, aliyemsaliti Rais wa Zanzibar Hayati Mzee Aboud Jumbe Mwinyi. 
Hayo yameelezwa jana na Mwanaharakati anayejihusisha na Masuala ya Kisiasa, Kijamii na Utamaduni, Ali Makame Issa, katika mkutano  wake na waandishi wa habari.

Mkutano huo ulifanyika nyumbani kwake Malindi, Mkoa Mjini Magharibu, Kisiwani Unguja. 
Aliwahimiza Wazanzibari kujenga umoja, kukataa siasa za mgawanyiko, uhasama na chuki zinazofanywa na Maalim Seif tangu akiwa mwanachmawa CCM na sasa CUF.
Aliongeza kuwa, Maalim Seif alivujisha siri ya waraka ulioandikwa kitaalamu na Mzee Jumbe aliotaka ujadiliwe na Halmashauri Kuu ya CCM, kupatikana ufumbuzi wake ambapo Zanzibar ingejiendesha kama nchi huru.
Alifafanua kuwa, hoja zilizoanishwa kwenye waraka wa Hayati Mzee Jumbe, zilifanyiwa utafiti wa kitaalamu na maswali ya msingi ambayo yasingeweza kujibiwa.
“Badala yake mfumo wa Muungano ungebadilika kuwa wa serikali tatu au Zanzibar ingepata kiti chake Umoja wa Mataifa, Wazanzibar hasa kizazi kipya kisidanganywe na Maalim Seif anayejifanya mtetezi wa Zanzibar wakati ameshiriki usaliti.
“Asilalamike Zanzibar kumezwa na Muungano wakati yeye ndiye aliyeikwamisha isijitoe bila kutokea mikiki ya kisiasa au kiusalama,” alisema.
Issa alisema; “Nawahimiza vijana wakisome kitabu cha "partnership" kilichoandikwa na Hayati Mzee Jumbe. Kina hoja za msingi na sehemu ya madai hayo yalitakiwa kuwalishwa NEC ya CCM.
“Badala yake ukaporwa na Maalim Seif na kukwamisha mpango mzima,” alifafanua.
Alisema kama si njama dhidi ya Mzee Jumbe hadi kuvuliwa madaraka mwaka 1984, maelezo yanayotolewa sasa na Maalim Seif amenakili hoja za Mzee Jumbe aliyetaka usawa katika muundo wa Muungano.
"Malim Seif alimwambia Hayati Mwalimu Nyerere maneno makali dhidi ya Jumbe. Mwalimu kama unampenda Jumbe tuvunje Muungano. Kama unataka Muungano udumu Jumbe atupishe.
“Madai ya Serikali tatu si sera ya CCM, Mzee Jumbe akalazimishwa kujiuzulu kwa kuwajibika,” alisema.
Pia Issa alisema ni jambo la kushangaza kumuona Maalim Seif baada ya kumtosa mwenzake, akawa Waziri Kiongozi na miaka michache baadae akazitumia hoja za Mzee Jumbe kudai Muungano wa Serikali tatu kabla hajabadili msimamo wake na kutaka Muungano wa mkataba. 
Mwanaharakati huyo ambaye alishiriki siasa CUF na ADC, alimtaka kiongozi huyo kutohamisha athari za mitafaruku ya kisiasa CCM hadi kugombana na wenzake, kuiileta kwenye jamii ili kuwagawa wananchi kwa mitazamo.
"Ninawasihi Wazanzibari tukatae kugawanywa na Maalim Seif. Mwenzetu amekosa msimamo imara. Tuheshimu mazingira ya Muungano uliotupa fursa nyingi za kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa miaka 54," alisema.
Juhudi za kumpata Maalim Seif kujibu tuhuma hizo zimegonga mwamba baada ya simu yake ya kiganjani kuita bila kupokelewa.
Alipotafutwa Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Omar Ali Sheikh, alisema anayeweza kujibu hoja hizo na nyingine ni Maalim Seif mwenyewe. 

Comments