Featured Post

KUTOFAUTIANA, KUKOSOANA KUSIKENGEUE DEMOKRASIA



NA ALOYCE NDELEIO
DHANA ya kukosoana ni jambo endelevu ndani ya jamii katika mambo yanayohusu ustawi wake na nyanja inayoonekana kuwa na ukosoaji mara nyingi ni uwanja wa siasa. 
Mara nyingi kunakuwepo kutofautiana katika dhana hii kutokana na upande mmoja kuuona upande mwingine kuwa haufahamu jambo linalolengwa na mara nyingine kuonekana ni kukiuka kanuni au kuipotosha jamii.

Inawezekana kuwa  kinachotokeza katika hali hiyo ni kutoonekana kwa hoja katika ukosoaji au malengo ya ukosoaji huo yakiwa ni kudhoofisha mitazamo chanya inayoonekana ndani ya jamii yenyewe.
Kimsingi wanaoingia katika ukosoaji wamekuwa ni wawakilishi wa wanajamii na hivyo pale ukosoaji unapokuwa haulengi mkondo chanya  husababisha taswira ya kuzigawa jamii.
Msingi mama wa kukosoana ni kurekebishana, kusahihishana, kuelekezana na hitimisho linalofikiwa ni kukubaliana hivyo kwamba yanayokosolewa kuingia katika mkondo ulio sahihi, wenye tija na maridhiano  kwa jamii yote.
Makubaliano yanapofikia hitimisho sahihi huonesha uwepo demokrasia na mambo mengi  yakiwemo michakato, mipango na mikakati hufanyika kwa ufanisi na maendeleo hupatikana.
Mtazamo kama huo ndio unaowafanya baadhi ya wanasiasa kusema kuwa kama hakutakuwepo kukosoana iwe ndani ya vyama au taasisi  kunasababisha uwepo usimamizi wa kiimla katika chama au taasisi yenyewe.
Lakini wapo ambao wanatumia kukosoana kujenga taswira ya kukashifiana ama baina ya viongozi wenyewe au makundi ya wanajamii kutokana na kutofautiana kiitikadi. Hilo linaibua uadui wa kifikra ambao unakwaza dhima nzima ya kuiletea jamii maendeleo.
Katika kuonesha kuwa kauli hizo zina ukweli ndani yake Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere  alisema katika Kitabu cha Maongozi , “Lakini kuna mambo mawili ya lazima katika demokrasia; ukiyakosa hayo demokrasia hakuna. La kwanza  ni kwamba kila mtu lazima aweze kusema kwa uhuru kabisa, na maneno ya kila mtu lazima yasikilizwe.
“Hata kama mawazo ya mtu huyu  hayapendwi kiasi gani, au walio wengi wanamdhania amepotoka kiasi gani, si kitu. Kama mtu anapendwa kwa wema wake, au hapendwi kwa visa vyake, hayo si kitu. Kila Mtanzania, kila mtu kijijini, kila mjumbe wa Halmashauri ya wilaya, kila Mbunge n.k. lazima aweze kusema  kwa uhuru bila hofu ya vitisho – ama katika mkutano  ama nje ya mkutano.”
 Andiko hilo lililotoka  kabla ya mfumo wa vyama vingi linasadifu mazingira ya sasa, ni mawazo  endelevu ambapo aliongeza, “Watu wenye mawazo  tofauti, hata wakiwa wachache, lazima wawe na haki  ya kutoa mawazo yao katika majadiliano  bila ya hofu ya kusumbuliwa; mawazo yao na yashindwe  katika hoja za majadiliano, sio kwa vitisho au mabavu.
“Majadiliano yenyewe yatakayoleta uamuzi  lazima yawape   nafasi  watu kusema kwa uhuru kabisa. Na hata baada ya  kuamua  jambo  watu wawe na uhuru kuendelea kulizungumza  jambo hilo.
“Maana wale wachache  wenye mawazo tofauti  lazima wafahamu  kuwa kama wanayo mawazo  yenye maana, na kama wakiyaeleza mawazo hayo vizuri, wanaweza kubadili mawazo ya wale  wengine walio wengi.”
Katika ukosoaji ambao umekuwa unafanyika  miongoni mwa wanasiasa walio wengi uchache wa walio na mawazo  hata kama yana maana umekuwa  hauwekwi kwenye mizania  kuangalia tija yake, na kama ni kukubalika hakuwi ni moja kwa moja kwani kufanya hivyo ni kumpaisha mkosoaji badala ya kumridhisha.
 Kitabu hicho kinaendelea,  “Kadhalika  wale walio wengi lazima wawe tayari  kuyashikilia  mawazo yao  mpaka wale wachache  waridhike kuwa uamuzi uliofanywa  juu ya jambo lile  ulikuwa sawa. Majadiliano lazima   yaruhusiwe kuendelea, kwa uhuru kabisa. Hiyo ni sehemu ya maana ya uhuru wa mtu binafsi.”
Hata hivyo alibainisha,“Lakini ile lazima ya  uhuru wa mazungumzo haiwezi kuzuia  uamuzi kufanywa. Kuna wakati  utafika  mazungumzo yakatike na kitendo kifuate; ama sivyo hatutafanya kazi yoyote  ila kubwata tu. Uamuzi ukishafanywa lazima ukubalike kuwa ni uamuzi wa watu wote; na wote, hata wale  waliokuwa wakipinga, hawana budi  kushiriki  kutimiza jambo lile.
“Kwa hiyo, jambo la pili katika  demokrasia  ni kwamba sheria ikishapitishwa  lazima kila mtu aitii sheria ile, pamoja na wale walioipinga  na wasiotosheka  na hoja  zilizotolewa  kutetea sheria ile. Isitoshe, mara sheria  ikipitishwa kuikubali peke yake  hakutoshi, lazima kila mtu aitetee.”
Kukosoana ni kuimarisha mshikamano ndani ya jamii kwa kuuweka katika mazingira sahihi, licha ya kwamba walioegemea katika uhafidhina huwa na mawazo ya kiimla hivyo kuwa vigumu kukubaliana na  hilo kwani kwa kiwango kikubwa huwa hawashauriki.  
Lakini wakati ukosoaji unapofanyika baina ya wanajamiii lazima kuangalia pia vigezo vingine vikiwemo vya kitaaluma na kifundi ambapo wataalamu wa masuala ya kitaaluma na kiufundi  wanatakiwa kufanya mabadiliko, badala ya kudhani kuwa wanafahamu vilivyo bora.
Hata hivyo  ni lazima wapambane kuelewa uhalisia wa watu maskini. Hilo linawezekana kwa kuwashirikisha wanasiasa maswali hayo ili nao wayatafakari kwa kuwa ni wawakilishi wao.
Ili kupata suluhisho katika masuala ya kijamii makundi hayo lazima yawe tayari kuwasikiliza, kufahamu uelewa wa watu maskini, vipaumbele vyao na shughuli zao; baadaye watumie uelewa wao wa kiteknolojia kushughulikia yale yanayowakabili maskini, iwe katika ngazi ya mitaa, taifa au ngazi nyingine ya juu.
Ni lazima wajiulize kila mara ni kitu gani kinafanyika ndani ya kaya na jumuia, hivyo kwamba sera kuu na ndogo ziwe zinapanga namna zitakavyoshughulikia kuwasaidia wanawake, wanaume au watoto kuyaona matamanio yao. Ushiriki katika sera za kupanga maamuzi ni lazima ziwe na msingi mpana.
Kujiuliza maswali hayo kunaweza kutokana na hoja za ufafanuzi kutoka kwa maskini  ambapo wakati  wanapozungumza kuhusu hali nzuri wanabainisha mitazamo ya malighafi, kijamii, kimaumbile, kisaikolojia na kiroho, usalama na uhuru wa kuchagua na kutekeleza.
 Hali ya aina hiyo inamaanisha kuwa pale ambapo kukosoana na kukubaliana  kunachangia ustawi wa jamii tofauti na mtazamo kwamba  kukosoana na kujengeana uadui.
Aidha taswira inatakiwa kutoa dira chanya kwa kufanya pande zote kufungamana na kufanikisha malengo ya kijamii katika mfumo wa demokrasia.
CHANZO: FAHARI YETU 

Comments