Featured Post

KOCHA EMMANUEL AMUNIKE AWATIMUA NYOTA SITA WA SIMBA NDANI YA TAIFA STARS



NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WACHEZAJI sita wa Simba, mabeki Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, viungo Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Hassan Dilunga na mshambuliaji na nahodha, John Bocco, wameenguliwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kinachojiandaa na mechi dhidi ya Uganda Septemba 8, mwaka huu mjini Kampala kwa utovu wa nidhamu.

Kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike amechukua hatua hiyo baada ya wachezaji hao kushindwa kuripoti kambini juzi, hoteli ya Sea Scape, eneo la Kunduchi jijini Dar es Salaam bila taarifa yoyote, huku mwenzao, kipa, Aishi Salum Manula pekee akiripoti
Badala yake, Amunike, winga wa zamani wa kimataifa wa Nigeria, amewachukua mabeki, Ally Sonso, Paul Ngalema wa Lipuli ya Iringa, Salum Kimenya wa Tanzania Prisons ya Mbeya, David Mwantika, viungo Frank Domayo wa Azam, Salum Kihimbwa na mshambuliaji Kelvin Sabato, wote wa Mtibwa Sugar.
Wachezaji walioripoti kambini hadi sasa ukiondoa walioongezwa ni makipa Aishi Manula wa Simba na Mohammed Abdulrahman  wa JKU, mabeki ni Aggrey Morris, viungo Mudathir Yahya na mshambuliaji Yahya Zayed wa Azam.
Wachezaji wa Yanga, kipa Benno Kakolanya, mabeki Gardiel Michael, Kelvin Yondan na Andrew Vincent ‘Dante’ na kiungo Feisal Salum ambao wapo na timu yao mjini Kigali, Rwanda ambako jana walimenyana na wenyeji, Rayon Sport katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika, watajiunga na timu wakirejea kuanzia kesho Iiumaa.
Nyota wanaocheza nje wanatarajiwa kuwasili kuanzia Septemba 1 ambao ni mabeki Hassan Kessy wa Nkana FC ya Zambia, Abdi Banda wa Baroka FC ya Afrika Kusini, Himid Mao wa Petrojet FC ya Misri, Simon Msuva wa Difaa Hassan El-Jadida, Morocco, Farid Mussa, Shaaba Iddi wa CD Tenerife  ya Hispania, Rashid Mandawa wa BDF XI ya Botswana, Thomas Ulimwengu wa El HIlal ya Sudan na nahodha Mbwana Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji.
Amunike aliyesaini mkataba wa kufundisha Taifa Stars mapema mwezi huu, ambaye anasaidiwa na Mnigeria mwenzake, Emeka Amadi na Mzalendo, Hemed Suleiman ‘Morocco’, baada ya mechi na Uganda Septemba 8, mwaka huu mjini Kampala, atawafuata Cape Verde Oktoba 10 kukamilisha mechi zake za mzunguko wa kwanza kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Comments