Featured Post

KIMENUKA - RAIS MAGUFULI AMSHUKIA PAULO MAKONDA, ASEMA LAZIMA ALIPE KODI



Kauli ya Rais Magufuli juu ya sakata la Makontena

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka viongozi wote nchini kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria sambamba na kuhakikisha wanasimamia ipasavyo matumizi ya rasilimali za umma kwa maslahi ya wananchi.

"Kwa mujibu wa sheria ya Madeni, Dhamana na Misaada Namba 30 ya mwaka 1974 (kama ilivyorekebishwa na sheria namba 9 ya mwaka 2003) kifungu cha 3, 6, 13 na 15, Waziri wa Fedha na Mipango ndiye mwenye mamlaka ya kukopa nje na ndani, kutoa dhamana na kupokea misaada kwa niaba ya Serikali.
Kwa msingi huo, hakuna mtu yoyote mwenye mamlaka ya kukopa, kutoa dhamana na kupokea misaada kwa niaba ya Serikali bila mtu huyo kukasimiwa mamlaka hayo na Waziri wa Fedha kwa mujibu wa sheria hiyo" amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo tarehe 30 Agosti, 2018 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato mkoani Geita, wakati akizungumza na viongozi na wafanyakazi wa wilaya hiyo, ambapo amesisitiza kuwa viongozi wote wajenge utaratibu wa kusoma sheria na kujiepusha kutumiwa kwa maslahi ya watu binafsi.
Kauli hiyo imekuja leo baada ya siku chache zilizopita, viongozi wawili wa serikali ya Tanzania wamekuwa wakitupiana maneno hadharani. Viongozi hao ni Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda.
Majibizano hayo yamekuwa yakifuatiliwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii pamoja na kuchukua sehemu kubwa ya vichwa vya habari katika magazeti, kwa takriban wiki nzima.
Chanzo cha mvutano huo ni kuhusu makontena 20 ya samani zenye thamani ya shilingi bilioni 1.4 ambapo licha kuingizwa nchini kwa jina la Paul Makonda, lakini mkuu huyo wa Mkoa anadai mali ni kwa ajili ya msaada katika shule mbalimbali kwa lengo la kuboresha elimu.
Hata hivyo, Mamlaka ya Mapato nchini Tanzania imelishikia kidedea suala hilo na kumtaka mkuu huyo kulipigia kodi ya kiasi cha shilingi 1.2 bilioni, kwa madai kwamba, kontena hizo, ziko kwa jina la mtu binafsi na zimekaa bandarini kwa zaidi ya siku tisini.
Maswali mengi pia yaliibuka juu ya mzigo huo wa samani baada ya kusambaa mtandaoni kwa barua iliyokuwa ikionesha Paul Makonda kuomba msamaha wa kodi ambao halikuridhiwa mpaka sasa.
BBC imefanya mazungumzo na mtaalamu wa masuala ya siasa Goodluck Ng'ongo, ambae anasema kila kitu ambacho kinachozua mjadala sheria yake ipo wazi.
"Waziri Mpango anasimamia sheria na kanuni na Mkuu wa Mkoa anaonekana kuweka siasa."
Kwa mujibu wa sheria ya Bodi ya Afrika Mashariki, Mtu anaweza kusimama kama taasisi au kusimama kama mtu binafsi katika kusafirisha mzigo ukiwa unaonesha ni wa nani na umetokea wapi?
Mchambuzi huyo pia ameendelea kusema kuwa asasi za kiraia na taasisi za dini peke yake ndio zina msamaha wa kodi tena kwenye bidhaa ambazo zinahusu afya na elimu lakini vilevile msamaha huo upo kwenye bidhaa ambazo hazizalishwi nchini.
Kisheria hakuna msamaha kwa mtu mmoja na kwa vitu vinavyotengenezwa ndani ya nchi, ameongeza kusema Goodluck.
Samani katika makontena hayo ishirini ambazo ni viti na meza vinaweza kutengenezwa nchini Tanzania.
Ameendelea kufafanua, kuwa, aidha ofisi ya Mkuu wa Mkoa sio taasisi ya kidini au asasi ya kiraia hivyo hata kama samani hizo ni kwa ajili ya elimu bado hivyo vifaa vinapaswa kulipiwa kodi.
Fungu la serikali pia haliwezi kuhusika katika njia zote mbili.
Jambo jingine lililozua mjadala ni kuwepo kwa majibu yanayokanganya kutoka kwa Makonda, ambae awali aliyakana kuwa makontena hayo sio yake lakini baadae alinukuliwa kusema kwamba atatakayenunua atalaaniwa yeye pamoja na uzao wake.
Mamlaka ya Kodi nchini humo TRA bado ina matumaini kwamba watapata mteja wa makontena hayo watakaporudia kufanya mnada jumamosi ijayo mara baada ya zoezi hilo kushindwa jumamosi iliyopita.
Makontena hayo ya mkuu wa mkoa wa Dar es salaam,Paul Makonda yalikuwa yanadiwe jumamosi iliyopita laikini yalikosa wanunuzi ya watu wengi baada ya watu wengi kushindwa kufikia bei iliyotangazwa.

Comments