Featured Post

KAYA ZAIDI YA 50 ZAISHI CHINI YA MITI



NA MOSES NG’WAT, KATAVI
HALI  si shwari katika Kijiji cha Kamalampaka, wilayani Mlele baada ya kaya zaidi ya 50 kukosa makazi, kufuatia  nyumba zao kuchomwa moto kwa kile kilichoelezwa kuwa walivamia hifadhi ya msitu wa serikali.

Gazeti hili lilishuhudia wakazi hao waliokuwa wakiishi katika kitongoji cha Katobagula kijijini hapo, wakiendelea na maisha chini ya miti, huku watoto wakishindwa kuendelea na masomo yao.
Wakizungumza kwa masikitiko, wananchi hao walisema zoezi hilo lililoanza Agosti 15, 2018 liliongozwa na Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) pamoja na watu wanaodhaniwa kuwa ni askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Walisema mbali na nyumba zao kuchomwa moto na nyingine kubomolewa, katika oparesheni hiyo baadhi yao wamepoteza idadi kubwa ya mifugo kama ng’ombe na mbuzi, ikiwemo kuporwa chakula walichozalisha.
Mmoja wa waathirika wa oparesheni hiyo, Lushu Lutunga (64), alisema ameshangazwa na hatua hiyo ya kuchomewa moto nyumba zake sita kwa madai zilijengwa ndani ya hifadhi wakati ukweli ni kwamba yeye yuko nje ya alama za mpaka.
“Nimelipa jumla ya shilingi milioni 12 baada ya kukamata ng’ombe zangu 128, na sasa mimi na familia yangu tunaishi chini ya mti hapa kijijini na hatujui hatima yetu,” alilalamika Lutunga.
Aliongeza kuwa, hadi sasa hajui hatima ya chakula walichobeba jumla ya magunia 128 ya mpunga, pamoja na mahindi zaidi ya magunia 40 walichokuwa wamezalisha kwa ajili ya chakula na biashara.
Naye Malapala Matoboki, alieleza kuwa, jumla ya nyumba zake kumi zilichomwa moto huku yeye akikamatwa na kuwekwa ndani kwa siku mbili kabla ya kufikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa makosa mawili ya kuvamia misitu na kukata miti ambapo alitozwa faini ya shilingi 150,000.
“Kabla ya kuzingira nyumba yangu na kunikamata, niliuliza kwanini viongozi wa kijiji huja kuomba michango ya maendeleo ilhali wanajua naishi isivyo halali, nikatoa risiti ikiwemo niliyochangia mbio za mwenge mwaka huu kwa kutoa ng’ombe mzima, lakini hawakunielewa,” alibainisha Matoboki.
Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Anthony Maganga, alithibitisha kufanyika kwa oparesheni hiyo na kwamba jumla ya watu 500 wamefurushwa ndani ya eneo hilo.
“Ni kweli tumekuwa tukiomba michango ya maendeleo kutoka kwa wakazi hao, lakini haimaanishi kuwa wakitupatia michango ndio wanahalalisha uvunjaji wa sheria,” alisema.
Kuhusu baadhi ya wananchi kupoteza mali zao ikiwemo vyakula vyao kuporwa, Mtendaji huyo wa kijiji alisema, hadi sasa hakuna mwananchi aliyetoa taarifa katika uongozi wa kijiji.
Diwani wa Kata ya Inyonga kilipo kijiji hicho cha Kamalampaka, Sudi Mlolwa, alisema baadhi ya wananchi wamefikisha malalamiko yao na kwamba aliwaelekeza kuyapeleka kwa Mkuu wa Wilaya ili kutafutiwa ufumbuzi.
Aliongeza kuwa, tatizo la mipaka katika kijiji hicho ni kubwa na tayari kupitia vikao mbalimbali wamewasilisha maombi ya kuongezewa eneo kutokana na ongezeko la watu kijijini hapo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Damas Nyanda, alipoulizwa juu ya tukio hilo alisema ndio anapokea taarifa hizo kwa mara ya kwanza na kushauri suala hilo lizungumziwe na Mkuu wa Wilaya kwa kuwa ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama.
Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Recho Kasanda, alipotafutwa hata wa njia ya simu hakupatikana na taarifa kutoka ofisi yake zilieleza kuwa alikuwa nje ya ofisi kikazi katika Halmashauri nyingine ya Mpimbwe.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Mlele anaongoza halmashauri mbili za Mpimbwe na Mlele.
Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, Ofisi ya Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) Wilaya hiyo ya Mlele haikuwa tayari kuzungumzia suala hilo licha ya mwandishi wetu kufika ofisini hapo.

Comments