Featured Post

KABURI LA ALBINO LAFUKULIWA, MIFUPA YAIBIWA KYELA, MBEYA ILI KUSAKA UTAJIRI


 Mtuhumiwa mmoja aliyeuawa na wananchi wenye hasira baada ya kukutwa akichimbua kaburi la marehemu Sisala Simwali huko Mbeya.



WATU wasiofahamika wamefukua kaburi la Bandusamile Mwalyebe 'Kanjanja' (65) mlemavu wa ngozi (albino) aliyefariki mwaka 2012 katika Kitongoji cha Mbande, Kijiji cha na Kata ya Ngonga wilayani Kyela mkoani Mbeya, kisha kuondoka na mifupa na baadhi ya viungo  kwa kile kilichodaiwa ni imani za kishirikina kwa lengo la kupata utajiri.

Mashuhuda wa tukio hilo juzi walilieleza gazeti hili kuwa imani za kishirikina ndiyo chanzo cha kufanya unyama huyo kwa watu hao ambao bado hawajafahamika wakiwa na lengo la kusaka utajiri baada ya kwenda kwa mganga wa kienyeji (Sangoma) aliyepiga ramli katika nchi jirahi ya Malawi.
Hatua hiyo ya kufukuliwa kaburi la mtu mwenye ualbino limezua taharuki kwa wakazi wa wa eneo hilo huku wakidai kuwa tukio hilo halijawahi kutokea katika kijiji hicho toka dunia ianze, huku wakieleza kuwa watafanya msako ili kuwatambua wahusika wa tukio hilo.
Betina Buruma, mtoto wa kaka wa marehemu, alisema alipoamka asubuhi, aliona kaburi limefukuliwa alipokuwa akichuma majani ya mchaichai, hivyo akatoa taarifa kwa mwenyekiti wa kitongoji ambaye naye alitoa taarifa kituo cha polisi wilaya ambao walifika eneo la tukio.
Alisema polisi walipofika walifanya upekuzi na kugundua kuwa jeneza (sanduku) limevunjwa huku mifupa ikichukuliwa na watu hao wasiojulikana na kuwa baba yake alikuwa muasisi wa kucheza ngoma za asili aina ya Mang'oma.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Malima Mwaisango, alisema kuwa baada ya kupokea ttaarifa hiyo alipiga simu polisi ambao walifika eneo la tukio kujionea hali halisi na kusema kuwa kitendo kilichofanyika ni chukizo kwa mungu kwani imetokana na imani za kishirikina.
Mmoja wa walemavu wa ngozi katika kata hiyo, aliyejitajwa kwa jina la Gwantwa Mwalyaje, alisema imani za kishirikina zimewafanya waishi kwa hofu kwani maeneo mbalimbali amesikia wenye ualbino wakikatwa viungo na kuuawa kinyama.
''Hali hii inatufanya tuishi kwa hofu na kutokuwa na uhakika na maisha yetu,kutokana na watu wenye imani za kishirikina wamekuwa wakisema Albino ni dili,wamekuwa wakituua kinyama huku wengine wakiwa hawana viungo baada ya kukatwa na watu hao kisha kutokomea navyo," alisema Mwalyaje.
Mwalyaje alizungumza kwa taabu huku akibubujikwa na machozi,aliiomba serikali kuwachukuliwa hatua watu hao pindi watakapobainika huku akiomba waongezewe ulinzi ili waweze kuishi kwa uhakika akieleza kuwa wanalazimika kurudi nyumba mapema pindi waendapo kwenye shughuri mbalimbali wakihofu kutekwa.
Akizungumza na wananchi mara baada ya kubaini kuchukuliwa kwa mifupa ya mremavu wa ngozi,mkuu wa upepelezi wa jeshi la pilisi wilayani humo, Modestus Chambu, alithibitisha tukio hilo,na kusema kuwa wamefungua jarada la uchunguzi ili kuwabaini watu waliousika na tukio hilo ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Aidha amewaomba wananchi kutoa ushirikiano na jeshi la polisi kuwasaka wathusika na kudai kuwa vitendo kama hivyo havipaswi kufanyika kwani ni aibu kwa kijiji na wilaya nzima kwa tukio hilo la kuwawinda kama wanyama watu wenye ulemavu wa ngozi.
Alisema vitendo kama hivyo ni chukizo kwa mungu havipaswi kufanywa, kwani watu hao ni sawa na watu wengine ''hii dunia inakoelekea si kuzuri watu wanapaswa kuwa waungwana kuacha kutegemea imani hizo za hovyo wakidhani kufanya hivyo watapata mafanikio ya kimaisha," alisema.
Imebainika kuwa matukio kama hayo ya ufukuaji wa makaburi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (ALBINO) ni muendelezo wa matukio baada ya mwaka 2017 katika Wilaya ya Mbeya Vijijini baadhi ya watu walikamatwa wakituhumiwa kufukua kaburi la Sisala Simwali, mwenye ulemavu wa ngozi, ambapo walifikishwa mahakamani huku mmoja akiuawa na wananchi wenye hasira katika eneo la tukio.
Na pia mwaka huo huo katika Kata ya Miyovizi, wilaya ya Mbozi, kaburi la mtu mwenye ulemavu wa ngozi aliyekufa miaka sita iliyopita pia lilifukuliwa na kuchukuliwa mifupa na watu wasiofahamika ambapo hadi leo hakuna mtu ama watu waliokamatwa wakihusishwa na tukio hilo.
Machungaji wa Kanisa la Temple of Pray For All Nations, Nabii Charles Mkuvasa, wilayani Kyela alisema kutokana na kuwepo kwa matukio haya ipo haja ya viongozi wa dini mbalimbali kuongeza maombezi kuliombea Taifa hili ili watu wenye imani za kishirikina waache kufanya ukatili huo.
Nabii Mkuvasa alisema Watanzania baadhi wenye tabia kama hizo waache kwani mambo hayo ni chukizo kwa Mungu, badala ya kutegemea kupata mali kwa njia za kishirikina kwa kudhuru wenzao, badala yake wamshirikishe mungu na wafanye kazi za kihalali na kuachana na ushirikina ambao hauna tija.

Comments