Featured Post

ELIMU NI NGUZO YA UFANISI, UTENDAJI BORA WA SERIKALI



NA ALOYCE NDELEIO
Elimu imekuwa ni moja ya nguzo zinazoleta ufanisi kwenye utendaji wa serikali ikizingatiwa kuwa ndiyo inayosimamia sehemu kubwa ya sekta za umma.
Lakini kuporomoka kwa kiwango cha elimu kunakuwa tishio kwamba elimu itakuwa duni na sekta za umma zitakuwa na watendaji dhaifu ambayo watashindwa kupambana na vikwazo katika uzalishaji na ukuzaji wa uchumi.
Katika mazingira hayo ni kwamba kundi la watendaji wa serikali watakaokuwepo kwenye uongozi wataendesha mambo kisanii na hivyo kuathiri dhana nzima ya utawala bora.

Ufanisi wa serikali  ni muhimu kwenye  maendeleo kiuchumi. Kwa ujumla  ustawi wa maendeleo ya kiuchumi kwenye nchi zilizoko pembezoni ambako serikali zinashindwa kupunguza kiwango cha rushwa, utekelezaji wa sheria na kuboresha mazingira kwa maendeleo ya sekta binafsi kumekuwa kunachangiwa na ukosefu wa elimu bora.
Takwimu zinaonesha kwamba upo uhusiano chanya kati ya elimu bora miongoni mwa wafanyakazi wa serikali na wigo tofauti wa ufanisi wa serikali kwa maana kwamba  watumishi wa serikali wanapokuwa na elimu nzuri, kiwango cha rushwa kinakuwa kidogo wakati kiwango cha ukusanyaji kodi kikiwa kikubwa.
Kwa upande mwingine usimamizi wa fedha za umma unakuwa mzuri na huungwa mkono zaidi na soko binafsi au sekta buinafsi.
Kiwango kikubwa cha elimu kwenye usimamizi na utawala huwa kinahusiana na kuwepo kwa kiwango kidogo cha rushwa ndani ya utawala husika.
Kwa mujibu wa mwongozo wa kimataifa wa mwaka 2012 unaohusu kuondokana na athari zinazozikabili nchi ambao unajulikana kwa kiingereza kama International Country Risk Guide2012 ni kwamba  upo uhusiano kati ya kiwango cha elimu anachokuwa amekipata mtumishi na vidokezo vya rushwa.
Kutokana na hali hiyo kiwango cha elimu  kwenye uongozi wa umma  kinaendelea kufungamana na kiwango kidogo cha rushwa.
Vidokezo hivyo vinabainisha kuwa sehemu kubwa ya nguvu kazi iliyopata elimu inaweza kuchangia kwenye kiwango kikubwa cha maendeleo kwa kusaidia kupunguza  matumizi mabaya ya ferdha za umma na hivyo kuwezesha sekta binafsi kufanya kazi.
Aidha inaelezwa kuwa pindi watumishi wa umma wanapokuwa na elimu nzuri nchi husika zinakuwa na uwezo wa  kukusanya kodi ya mapato. Uhamasishaji wa mapato ni moja ya changamoto kubwa kwenye uchumi unaoendelea na ukiwa mkubwa ni lazima uchukuliwe  kama alama ya uwezo wa kujenga taifa.
Uhusiano katika ya vigezo vya elimu inayopatikana na kodi ya mapato inayokusanywa kwa asilimia ya Pato la Ndani la Taifa (GDP) ni chanya miongoni mwa nchi nyingi. Tafiti zinabainisha kuwa watumishi wa umma waliopata elimu nzuri wamekuwa na ufanisi katika kusimamia kodi, kuhakikisha uwepo wa uadilifu, uelewa na kuwezesha maendeleo kwenye sekta binafsi.
Wigo mwingine wa ufanisi wa serikali ni katika kuangalia uwezo wa nchini katika  kuunga mkono maendeleo, usimamizi na uendeshaji wa soko binafsi kama vile sekta ya fedha za ndani ambazo baadaye hugeuzwa na kutoa mchango muhimu  katika kukuza na kukua kwa uchumi.
Mwongozo huo  unabainisha kuwepo kwa  mkondo hasi wa uhusiano wa  kitakwimu na kiuchumi  kati ya elimu na uongozi ukiwemo usimamizi na ushindani ambapo inaelezwa kwamba nguvu kazi iliyo na elimu ya uongozi wa umma inasaidia kukuza viwango vya sekta ya fedha za ndani na hivyo kuhuisha maendeleo ya sekta binafsi na kukua kwa uchumi.

Elimu na taasisi
Hata hivyo moja ya suala muhimu ni iwapo kiwango cha kupata elimu  miongoni mwa wafanyakazi wa umma huwa ni chimbuko la utawala bora au elimu ni matokeo ya kukua kwa taasisi.
Kama taasisi ndio inakuza kiwango cha elimu inayopatikana, basi sera za umma lazima ziangalie uimarishaji wa taasisi mahsusi ili kuhakikisha kuwa watumishi wa umma walio na vipaji wanachaguliwa kujiunga  kwenye uongozi wa umma na hivyo mfumo wa elimu wa nchi kuwa umekuza stadi zinazotambulika.
Kwenye mada moja ya wataalamu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF)  kuhusu mchango wa taasisi kwenye kuimarisha uchumi inabainisha kuwa uhusiano wa kawaida kati ya ubora wa mpangilio wa kitaasisi kama vile  kulenga kupunguza athari za wawekezaji kuhamisha rasilimali na kipato cha sehemu kubwa ya nchi.
Kwa maana hiyo kuna uhusiano  mkubwa kati watumishi wa umma walioelimika vizuri ndani ya sekta za umma na kiwango kikubwa cha ustawi miongoni mwa jamii kwa ujumla.
Aidha maana ya hali hiyo ni kwamba maamuzi yanayofanywa na watumishi wa umma walio na vipaji huboresha ubora wa upatikanaji wa huduma na matokeo yake ni kukua kwa uchumi.
Katika mazingira ya aina hiyo ni kwamba wakati taasisi zikiwa imara kwenye sekta za umma  kunawezesha  kupunguza kiwango cha utajiri ambao ungeibwa na wafanyakazi wa umma ambao ni wabadhirifu jambo ambalo husababisha wafanyakazi wabadhirifu kuondoka kwenye sekta za umma.
Wafanyakazi hao huwa ni wanaoguswa na maslahi ya umma na hutoa huduma kwa umma kwa kuwa wanakuwa na maarifa mazuri  lakini pia wakiwa wazuri kwenye kufanya maamuzi na hivyo kufikia hitimisho kuwa kiwango kikubwa cha elimu  alichopata mtumishi wa umma kinahusiana na kiwango kidogo cha rushwa ndani taasisi.
Katika hali hiyo inamaanisha kuwa kadri watumishi wa umma wanavyokuwa na maarifa zaidi ndivyo kiwango cha utoaji wa huduma huwa bora pamoja na kuongezeka kukua kwa uchumi.
Fedha ambazo hutolewa kama motisha kwa watumishi huleta ustawi kwa jamii na hususani inapotokea kwamba taasisi ni dhaifu. Kuwepo kwa programu za motisha  kunaifanya sekta ya umma kuwa na mvuto kwa umma kwa jumla na matokeo yake  kuboreka kwa huduma za umma na uchumi kukua.
Kwenye msimamo wa sera ni kwamba ufanisi katika utendaji wa serikali unaweza kupatikana na njia mojawapo ni kuimarisha  mfumo wa mahakama. Mfumo wa mahakama ulio na ufanisi ambao unatekeleza sheria kwa haki unaweza kuwaondoa  watumishi kwenye kujaribu kuchezea sheria  na mifumo ili kujitajirisha wenyewe kwa kutumia mali za umma na hali kadhalika kusababisha watu binafsi kupambana na rushwa  sehemu yoyote yenye huduma za umma.
Inapokuwepo motisha husaidia kuwavuta watu walioelimika. Nchi mbalimbali duniani na hususan kwenye uchumi unaoinukia ni muhimu kujikita kwenye mtazamo wa kuvutia watu waliopata elimu nzuri kwenye utawala  ili kuboresha utoaji wa huduma na kukuza maendeleo ya uchumi.
Hali hiyo ndio iliyowezesha nchi za Mashariki ya Mbali zikiwemo Malaysia na Singapore kupiga hatua za haraka za maendeleo jambo lililowezesha sekta ya umma  kuwa kuvutio kwa wafanyakazi bora  ambao walitoa mchango mkubwa kwenye  kukuza ubora  wa shughuli za serikali na mwishowe kuwa na uchumi mzuri ulio na ufanisi.

Comments