Featured Post

BOMA LA CHIFU MERERE WA USANGU LINAVYOWAVUTIA WAGENI KUTEMBELEA


Chifu wa sasa wa Wasangu, Salehe Alfeo Merere akiwa na mwandishi wa makala haya.

NA INNOCENT NG'OKO, MBARALI
HISTORIA ya kiongozi wa kabila la Wahehe, Mkwavinyika Munyigumba, maarufu kama Chifu Mkwawa, haiwezi kukamilika bila kumtaja Chifu Merere wa kabila la Wasangu.

Hii ni kwa sababu machifu hao wawili wa historia ya pekee, kwani licha ya wao wenyewe kupigana, lakini kwa Chifu Merere ndiko mahali ambako kulitumika pia kudhoofisha nguvu za Mkwawa hadi Wajerumani wakamshinda.
Chifu Merere ni miongoni mwa machifu maarufu nchini Tanzania, hususan katika Nyanda za Juu Kusini, pamoja na Mkwawa na Mbeyela wa Njombe.
Huyu Merere alikuwa kiongozi wa kabila la Wasangu aliyetawala katika Bonde la Usangu, Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, bonde maarufu hivi sasa kwa kilimo cha mpunga pamoja na kuwa ndiyo chanzo cha Mto Ruaha Mkuu wenye manufaa makubwa katika kilimo pamoja na uzalishaji wa umeme katika mabwawa ya Mtera na Kidatu.
Ukifika Wilaya ya Mbarali katika Kata ya Utengule-Usangu katika eneo la Mbalino utakuta Ngome kubwa ya Chifu Merere, ambako ndiko chifu huyo alikotengeneza himaya kubwa.
Ngome ya Chifu Merere ndiyo pekee  inayouweka Mkoa wa Mbeya kwenye ramani ya mmoja wa machifu madhubuti waliokuwa na himaya kubwa na utawala imara ambao ulifanikiwa kuwaogopesha wakoloni wa Kijerumani kabla hawajarejea tena kwa mbinu mpya za Umisionari.
Ukifika eneo hilo la Mbalino kwenye Kata ya Utengule-Usangu utaona magofu ya ngome ya Chifu Merere iliyojengwa tangu mwaka 1896 na Waarabu.
Hapa utapata simulizi nyingi zikiwemo mbinu za Chifu Merere alizotumia kujiimarisha kijeshi dhidi ya mahasimu wake wakiwemo Wahehe, Wasafwa na Wajerumani.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa hadi kufikia mwaka 1830, Chifu Merere alikuwa amejiimarisha kijeshi na kuwa moja ya machifu tishio wakati wa Ukoloni, hivyo kufanikiwa kutanua himaya yake baada ya kuwapiga majirani zake, hasa Wasafwa.
Katika eneo la Utengule, Mji wa Mbarizi Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini, kuna ngome nyingine ndogo ambayo ilijengwa chifu huyo wa Wasangu baada ya kuwashinda majirani zao Wasafwa. Ngome hiyo ndogo  aliitumia kujificha alipokuwa akizidiwa kivita.
Historia inaonyesha, himaya ya Chifu Merere ilianzia katika eneo la Ngelyama lililopo ndani ya Hifadhi ya Ruaha ambapo Chifu Merere aliyefahamika kwa jina la Mwahavanga alikuwa amejiimarisha.
Baada ya kifo cha Chifu Merere Mwahavanga hatimaye utawala ulichukuliwa na mwanaye aliyefahamika kwa jina la Chifu Merere Mgandilwa, ambaye alijikita kuimarisha ngome iliyopo eneo la Utengule-Usangu.
Ngome ndogo katika eneo la Utengule katika Mji wa Mbarizi wilayani Mbeya Vijijini ilikuwa inasimamiwa na ndugu yake Mgandilwa, Chifu Merere Tovela Mahamba, ambapo mpaka sasa unaweza kuliona kaburi lake katika eneo hilo.
Chifu wa sasa wa kabila la Wasangu, Salehe Merere, ambaye alitawazwa akiwa na miaka 20 tu mwaka  1988, anasema ngome ya machifu karibu wote waliowahi kutawala katika Bonde la Usangu imekuwa kivutio kikubwa kutokana na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wanaotembelea eneo hilo.
Anasema, mbali na kuwepo kwa ngome hiyo, wageni wanaofika hujionea makaburi ya baadhi ya machifu wa Wasangu, akiwemo Chifu Alfeo Merere Nkahanga, na machifu wengine waliopita katika tawala mbalimbali za kabila hilo.
Ukifika katika Ngome ya Chifu Merere, utapata simulizi mbalimbali zenye kusisimua za nyumba maalum zenye makaburi ndani yake, ambayo ni ya machifu waliowahi kutawala kwa nyakati tofauti.
Kwa mgeni yeyote atakayetembelea eneo hilo atajionea kaburi la Binti wa Mkwawa wa kabila la Wahehe, aliyefahamika kwa jina la Mapuga, ambapo Chifu Merere na Chifu Mkwawa walibadilishana mabinti kwa lengo la kumaliza mapigano ya kivita baina yao.
Katika  eneo la Ngelyama ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ndiko kuna eneo la kufanya ibada za kimila (matambiko) ya kabila la Wasangu ambayo yanatajwa kuwa na zaidi ya miaka 200. Machifu wote wa kabila hilo wamekuwa wakienda kufanya matambiko katika eneo hilo.
Miongoni mwa machifu wa Wasangu waliowahi kutawala katika himaya hiyo ni Mui'Gumbi Merere I –(1834-1860), Tovelamahamba Merere II (1860-1893), Mugandilwa Merere III (awamu ya kwanza 1893-1896 ), Mugandilwa Merere III (awamu ya pili 1896-1906), Mxabuwoga Merere IV (1906-1950).
Wengine ni Myotishuma (1950-1953), Alfeo Mugandilwa Merere V (1953-1962), Yusuf Merere VI (awamu ya kwanza 1962-1988), Ahmed Merere VII (1989 – 2002), Yusuf Merere VI (awamu ya pili 2002 – 2003) na chifu wa sasa - Salehe Alfeo Merere VIII (2003-mpaka sasa).
Ili kuhakisha mazingira ya Ngome ya Chifu Merere yanaboreshwa na kuwa imara zaidi, Mbunge wa Jimbo la Mbarali, Haroon Pirimohomed ameanza kuonyesha njia kwa kutoa fedha ambazo zitasaidia ukarabati wa jengo la boma hilo ambalo lilianza kubomoka.
Mbunge huyo anasema, sehemu hiyo ndiyo ya historia ya Wasangu ambayo inapaswa kulindwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya vizazi vijavyo na kuwa  wageni mbalimbali  wanaoembelea  eneo hilo wataweza kujifunza mambo  mbalimbali  kuhusiana na historia ya machifu wa kabila hilo.
Ofisa Utalii katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Patrick Charles, anabainisha kuwa, Ofisi ya Mkurugenzi imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha eneo la Himaya ya Chifu Merere inaboreshwa kwa kuyafanyia ukarabati majengo yake.
"Ofisi ya Mkurugenzi imejipanga kuhakikisha majengo katika himaya ya Chifu Merere yanaboreshwa kwa kuyafanyia ukarabati  ili kuligeuza eneo hilo kuwa la kitalii kutokana na kuwa mpaka sasa kuna wageni wengi ambao wanakwenda kutembelea," anasema Charles.
Aidha, anasema, katika Shule ya Msingi Ibara katika Mji wa Rujewa, kuna eneo ambalo halmashauri imetenga kwa ajili ya mambo ya kihistoria yakiwemo ya Chifu Merere na vivutio mbalimbali vya kitalii vilivyopo katika Wilaya ya Mbarali.
Anasema, Ofisi ya Utalii imejipanga kuhakikisha inavitangaza na kuviboresha vivutio vya utalii vilivyomo katika wilaya hiyo kwa lengo la kuwawezesha wageni kutembelea kwa wingi na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wakazi wa Mbarali.
Ofisa Utalii huyo anasema, mbali na kivutio cha utalii cha Ngome ya Chifu Merere, Wilaya ya Mbarali imejaliwa kuwa na vivutio vingi na miongoni mwake ni Mlima Ngoni wenye historia ya Wangoni uliopo katika Kijiji cha Chamoto, Kata ya Igurusi.
Anavitaja vivutio vingine kuwa ni Mti mkubwa wenye historia ya kufanyika mapatano na usuluhishi kati ya Chifu Mkwawa na Merere katika Kijiji cha Luwango, Kata ya Ipwani na Masalia ya Kiwanda cha kutengenezea zana za Kale katika Kijiji cha Mlungu, Kata ya Miyombweni.
Pia anasema, kuna mabaki ya Ngome ya Wajeruman iliyopo katika Kiiji cha Ibelege, Kata ya Ipwani.
Wilaya hiyo imepakana na Hifadhi za Taifa za Ruaha na Kitulo na Pori la Akiba la Mpanga Kipengere ambapo mgeni yeyote anayefika anaweza kutembelea hifadhi hizo kwa urahisi zaidi.
CHANZO: TANZANITE

Comments