Featured Post

BOBI WINE: AWAKILISHWA NA WAKILI WAKE MAHAKAMANI UGANDA



KAMPALA, UGANDA
MBUNGE wa Uganda na msanii Bobi Wine hakuhudhuria kikao cha mahakama hii leo kuhusiana na kesi ya uhaini iliyowasilishwa dhidi yake na serikali.
Mmoja wa mawakili wake, Tonny Kitara, anasema kuwa Bobi Wine bado amelazwa katika hospitali moja mjini Kampala kufuatia majeraha aliyopata wakati alipokamatwa na wanajeshi.

Mwanamuziki huyo anatarajiwa kusafirishwa kwa matibabu ijapokuwa haijulikani anatarajiwa kupelekwa wapi.
Watu 25 waliokuwa wameshtakiwa pamoja naye katika mahakama ya hakimu mkuu mjini Gulu waliwasili mahakamani humo kaskazni mwa Uganda kulingana na Kitara.
Jumla ya watu 33 wameshtakiwa na uhaini kufuatia madai kwamba waliupiga mawe msafara wa rais Yoweri Museveni.
Baadhi ya washukiwa hao hawakuonekana mahakamani kwa sababu ya hali mbaya ya kiafya ama mkanganyiko wa siku ya kusikizwa kwa kesi hiyo .
Stakhabadhi zao za dhamana kwa makosa zilisema kuwa wanatarajiwa kuwasili mahakamani Septemba 30 na sio Agosti 30. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba Mosi.
Baadhi ya washtakiwa wanaendelea kupata matibabu hospitalini na huenda wakashindwa kuhudhuria mahakamani ambapo watawakilishwa na mawakili wao.
Bobi Wine ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi ni mwakilishi wa Jimbo la Kyadondo Mashariki na ni msanii maarufu wa muziki nchini Uganda.
Alikamatwa wiki mbili zilizopita kwa tuhuma za uvamizi wa msafara wa Rais Museveni mjini Arua na kupokea kipigo kikali yeye na wenzie 32 kutoka kwa vyombo vya ulinzi na usalama. Dereva wa Bobi Wine alipigwa risasi na kuuawa katika purukushani hizo.
Watuhumiwa hao waliwekwa chini ya ulinzi wa jeshi huku Bobi Wine awali akipandishwa katika mahakama ya kijeshi kwa tuhuma za kumiliki silaha kinyume cha sheria.
Rais Yoweri Museveni alijitokeza na kukanusha taarifa kuwa Bobi Wine ameumizwa vibaya na kuvishutumu vyombo vya habari kwa kueneza taarifa za uongo.
Baada ya kelele za upinzani kupazwa ndani na nje ya Uganda pamoja na kwenye mitandao ya kijamii, kesi yake mbele ya mahakama ya kijeshi ilifutwa na kuachiwa huru kabla ya kukamatwa tena na kufunguliwa mashtaka ya uhaini katika mahakama ya kiraia.
Jumatatu wiki hii, Bobi Wine na washukiwa wengine wote waliachiwa kwa dhamana.

Comments