Featured Post

AfDB YARIDHISHWA NA MIRADI YA NISHATI MIUNDOMBINU MIBOVU NA CHAKAVU KUONDOLEWA DODOMA


 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika( AfDB) nchini Marekani,Steve Dowd(kulia), baada ya viongozi hao kufanya mazungumzo kuhusu miradi ya nishati inayofadhiliwa na AfDB katika ofisi ya Waziri wa Nishati jijini Dodoma.



Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa pili kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini Marekani, Steve Dowd (wa pili kulia), wakikagua kituo cha kusambaza umeme cha Zuzu jijini Dodoma, ikiwa ni moja ya miradi ya nishati inayofadhiliwa na AfDB kwa kushirikiana na Serikali.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ( katikati) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini Marekani,Steve Dowd (wa pili kulia), wakikagua kituo cha kusambaza umeme cha Zuzu jijini Dodoma.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ( katikati) akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Benki ya maendeleo ya Afrika ( AfDB), watendaji wa Wizara ya Nishati, pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) baada ya kufanya ziara katika kituo cha kusambaza umeme cha Zuzu jijini Dodoma.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ( wa pili kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika( AfDB) nchini Marekani,Steve Dowd (wa pili kulia), wakiwa katika picha ya pamoja katika moja ya Transfoma zilizopo katika kituo cha kusambaza umeme cha Zuzu jijini Dodoma.

………………….

AfDB yaridhishwa na utekelezaji wa miradi ya nishati ya umeme wanayoifadhili

Yaahidi kuendelea kutoa ufadhili utakaohusisha uondoaji wa miundombinu mibovu ya umeme jijini Dodoma

Na Zuena Msuya, Dodoma
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), imeahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Tanzania katika kuimarisha miundombinu ya umeme nchini hususan katika Mkoa wa Dodoma ili kuboresha upatikanaji wa huduma ya umeme kutokana na kuongezeka kwa shughuli za uwekezaji.
Uboreshaji wa hali ya umeme mkoani Dodoma unahusisha  uondoaji wa miundombinu mibovu na chakavu zikiwepo takribani transifoma 75, kujenga njia ya kusafirisha umeme yenye urefu wa kilometa 135 kuzunguka Jiji, pamoja na kujenga vituo viwili vya kupokea na kupoza umeme katika eneo la Msalato na Kikombo vitakavyokuwa na uwezo wa kufua umeme wa takribani Megawati 200.
Waziri wa Nishati, Dkt.  Medard Kalemani alisema hayo katika kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Zuzu jijini Dodoma,wakati wa ziara  ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini Marekani, Steve Dowd, aliyekuwa akikagua utekelezaji wa baadhi ya miradi ya nishati ya umeme inayofadhiliwa na Benki hiyo katika mikoa mbalimbali nchini.
“Katika mazungumzo yangu na AfDB kabla ya kufanyika kwa ziara hii, pia wameonyesha nia ya kujenga kituo cha kuzalisha umeme wa Jua wa megawati 100 katika eneo la Zuzu jijini Dodoma katika kipindi cha miaka miwili ili umeme huo uingizwe katika Gridi ya taifa,” alisema Dkt Kalemani.
Akizungumzia miradi ya nishati, Dkt. Kalemani aliutaja mradi mkubwa wa umeme na wa kwanza nchini wa megawati 400 (National Backbone), kuwa ni miongoni mwa miradi mikubwa iliyotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali ikiwemo AfDB.
Alifafanua kuwa, katika utekelezaji wa mradi huo, Serikali ya Tanzania ilitoa shilingi Bilioni 18, Benki ya Maendeleo Afrika ( AfDB) ilitoa Dola za Marekani milioni 64.5 kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan( JICA), Benki ya Uwekezaji Ulaya (EIB), Benki ya Dunia( WB) na Benki ya Korea.
Aliongeza kuwa mradi huo wa Backbone unahusisha ujenzi wa Kituo cha kupoza umeme cha Zuzu ambacho kitaongezwa uwezo wa kusambaza umeme kutoka Megawati 48 za sasa hadi kufikia Megawati 200.
Alisema kuwa, baada ya kukamilika kwa miradi hiyo, mji wa Dodoma utakuwa mahitaji ya umeme wa megawati 70 kwa kipindi cha miaka 5 ijayo, na megawati 108 kwa miaka kumi ijayo, huku Mpango wa serikali kwa miaka kumi na mitano ijayo, ni kuwa na zaidi ya megawati 210, ili mkoa uweze kujitosheleza.
“Tunataka Mji wa Dodoma uwe ni mji wa mfano kwa kuwa na umeme mwingi na wa kutosha,na wa uhakika kwa kuwa viwanda vingi sasa vitaanzishwa katika Mkoa wa Dodoma, na uwekezaji mkubwa utafanyika kwa muda mfupi, kutokana na mkoa huo sasa kuwa na hadhi ya Jiji na Makao Makuu ya nchi, hivyo umeme ni lazima uwepo wa kutosha na wa uhakika,” alisisitiza Dkt. Kalemani.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) nchini Marekani, Steve Dowd alisema kuwa ameridhishwa na utekelezaji wa miundombinu ya umeme inayofadhiliwa na Benki hiyo hapa nchini baada ya kukagua na kuona namna ambavyo inavyotekelezwa.
Dowd alisema kuwa, Benki hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kufadhili utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati ya umeme kwa kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoendelea  kiuchumi ambazo zinafanya vizuri katika utekelezaji wa nishati hiyo kulingana mahitaji na ubora unaotakiwa na kwa wakati.
“Nimefurahi kutembelea baadhi ya miradi hii ya nishati inayofadhiliwa na AfDB ambayo inatumia fedha nyingi. Kwa kweli mnafanya vizuri, nimeridhishwa na kasi ya kuwaletea wananchi wenu maendeleo kupitia sekta ya nishati, AfDB itaendelea kuwaunga mkono katika hili, tuendelee kushirikiana,” alisisitiza Dowd.
Akizungumzia namna ambavyo AfDB inashirikiana na Tanzania, Dowd aliishauri serikali ya Tanzania, kuendelea kuomba fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo kutoka katika nyanja mbalimbali, kwa kuwa inatekeleza miradi hiyo kama ilivyotarajiwa.

Comments