Featured Post

UFARANSA BINGWA WA DUNIA 2018



* Yaishindilia Croatia 4-2, Mbappe aendelea kung'ara

MOSCOW, RUSSIA
HII ni zaidi ya 1998! Ufaransa imetwaa Kombe la Dunia leo huku ikitoa kipigo kwa Croatia cha mabao 4-2 katika fainali, ikiwa ni mara mbili ya kipigo ilichokitoa kwa timu hiyo katika nusu fainali ya michuano hiyo miaka 20 iliyopita.

Mechi hiyo imedhihirisha wazi kwamba, Ufaransa ni mbabe wa Croatia, lakini kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps ameweza kuifikia rekodi ya Mario Lobo Zagallo wa Brazil kwa kutwaa taji hilo kama mchezaji na kama kocha.
Mwaka 1998 Ufaransa iliitandika Croatia mabao 2-1 katika nusu fainali wakati Deschamps akiwa nahodha na kuiongoza hadi kunyakua taji kwa kuifunga Brazil mabao 3-0.
Bao la kujifunga la Mario Mandzukic katika dakika ya 18 lilifungua njia ya ubingwa kwa Ufaransa, kwani dakika 20 baadaye Antoine Griezmann alipachika la pili kwa mkwaju wa penati na kuifanya Ufaransa iendelee kuongoza licha ya bao la kusawazisha la Ivan Peresic katika dakika ya 28.
Jitihada za Ufaransa kusaka taji lao la pili la dunia ziliendelea kipindi cha pili ambapo kunako dakika ya 59 Paul Pogba alipachika la tatu akimalizia rebound baada ya shuti lake la kwanza kugonga mwamba.
Wakati Croatia ikitafuta upenyo wa kusawazisha mabao hayo, ghafla kijana yosso mwenye kasi na mkabaji, Kylian Mbappe-Lotin akapachika bao la nne dakika ya 65 lililodidimiza matumaini ya Croatia kunyakua taji hilo kwa mara ya kwanza.
Mario Mandzukic alipachika bao la pili dakika ya 69 'akilipia' bao lake alilojifunga mapema.
Deschamps aliweka matumaini makubwa kwa nahodha Olivier Giroud, ambaye amedhihirisha kuwa muhimili imara na kiunganishi maridhawa kwa Mbappé na Griezmann ingawa hakuweza kuifungia Ufaransa hata bao moja.
Katika mechi tatu zilizopita za mtoano, Croatia ilicheza kwa dakika 120, lakini kocha Zlatko Dalic hakuweza kukibadilisha kikosi chake kilichoiondoa England kwenye nusu fainali.
Vikosi vya jana vilikuwa:
Ufaransa: Lloris, Pavard, Varane, Umtiti, Lucas, Mbappe-Lottin, Pogba, Kante, Matuidi, Griezmann na Giroud.
Croatia: Subasic, Vrsaljko, Lovren, Vida, Strinic, Rebic, Rakitic, Brozovic, Perisic, Modric na Mandzukic.
Harry Kane wa England amenyakua Kiatu cha Dhahabu kwa kuibuka Mfungaji Bora baada ya kupachika mabao sita - ikiwa ni miaka 28 tangu Mwingereza mwingine, Garry Lineker, alipoibuka mfungaji bora kule Italia kwa kufunga idadi kama hiyo ya mabao.
Mlindamlango wa Ubelgiji, Thibaut Courtois, ameibuka kipa bora na kunyakua tuzo ya Golden Glove.
Luka Modric ndiye Mchezaji Bora wa Mashindano, wakati yosso Kylian Mbappe ametwaa tuzo ya Mchezaji Chipukizi wa mashindano.


Comments