Featured Post

RELI MPYA YA SGR NCHINI KENYA ILIOFADHILIWA NA CHINA YASABABISHA HASARA YA $100M

Mradi wa reli mpya ya kisasa nchini Kenya SGR umesababisha hasara ya $100m (£76m) katika kipindi cha mwaka wa kwanza wa operesheni zake , kulingana na wizara ya uchukuzi nchini humo.
Mradi huo uliofadhiliwa na serikali ya China ambao unaunganisha mji wa pwani wa Mombasa na Nairobi ulifadhiliwa kwa mkopo wa kima cha $3bn kutoka kwa benki ya China ya Exim katika kipindi cha miaka 15.

Serikali ya Kenya ilipinga madai kwamba bei ya ujenzi wa mradi huo wa reli iliongezwa, haiwezi kudumishwa na haifai kiuchumi.
Reli hiyo ya SGR ni miongoni mwa miradi muhimu ilioahidiwa na rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wake, ukizinduliwa mwezi mmoja kabla ya uchaguzi wa urais uliopita.
Huku treni za abiria zikijaa mara kwa mara, waziri wa uchukuzi James Macharia aliambia kamati ya bunge kwamba ilikuwa vigumu kuwarai wenye mizigo kusafirisha mizigo hiyo kupitia reli kutoka kwa barabara.
Mipango ya kuanza kulipa deni hilo inatarajiwa kuanza mwaka ujao, na iwapo reli hiyo itashindwa kujilipia deni hilo basi huenda walipa kodi wa Kenya wakalazimika kulipa deni hilo.
Wanauchumi wanakadiria kwamba China sasa inamiliki asilimia 70 ya deni la Kenya.
Hatahivyo serikali inatumai kwamba reli hiyo itaanza kupata faida katika kipindi kijacho cha fedha.

Tanzania yaanza kujenga reli ya kisasa

Nchini Tanzania Rais wa Tanzania John Magufuli aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa awamu ya kwanza ya mradi mkubwa wa reli ya kisasa ya Standard Gauge ambayo hapo baadae itaunganisha nchi za Rwanda na Burundi pia.
Lakini katika awamu hii ya kwanza, ujenzi utakuwa wa reli yenye urefu wa kilomita takribani 300, ambayo itatoka jijini Dar es Salaam na kuishia mkoa wa jirani wa Morogoro.
Ni reli ya kisasa, na ya kwanza Afrika Mashariki na kati itakayokuwa na uwezo wa kupitisha treni zitakazoendeshwa kwa nguvu ya umeme.
Reli hiyo itajengwa kwa awamu ya kwanza na kampuni kutoka nchi mbili, uturuki na Ureno kwa gharama ya takriban dola bilioni 1.2 za Kimarekani.
Reli hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba treni yenye kuvuta mabehewa 100 na kubeba mzigo wa mpaka tani 10000 kwa mkupuo sawa na uwezo wa Malori 500 ya mizigo.
Mradi huu utaleta ahueni kwa wasafiri wa Dar es Salaam mpaka Morogoro ambpo wataweza kusafiri kwa mwendo kasi kwa saa 2 na dakika 50 pekee
Rais wa Tanzania Dokta John Pombe Magufuli katika sherehe hizo amesema kuwa Tanzania itanufaika kutokana na Mradi huu kwa maendeleo ya uchumi,
Hivi sasa Serikali ya Tanzania inaelekeza jitihada zake za ujenzi wa reli wa awamu ya pili yenye urefu wa kilometa 336 kutoka Morogoro mpaka Dodoma yalipo makao makuu ya nchi na tayari serikali ya Uturuki imeonyesha nia ya kushirikiana na Tanzania kujenga sehemu hiyo.

Comments