Featured Post

MAONYESHO YA SAYANSI KWA WANAFUNZI 2018 KUAKISI 'TANZANIA YA VIWANDA'

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Profesa Simon Msanjila akikabidhi zawadi kwa Prosper Gasper na Erick Simon kutoka Shule ya Sekondari St. Jude's jijini Arusha baada ya kuibuka washindi wa jumla wa Mashindano ya Wanasayansi Chipukizi (YST) yaliyofanyika Agosti 8-9, 2017 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.


Na Daniel Mbega
SHIRIKA la Young Scientists Tanzania (YST) linaandaa kwa mwaka wa nane sasa Maonyesho ya Sayansi yanayowahusisha wanafunzi wa shule za sekondari kote nchini ambayo yatafanyika kuanzia Jumatano, Agosti Mosi hadi 2, 2018 kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Kama ilivyokuwa kwa miaka mitatu iliyopita, maonyesho ya mwaka 2018 yatawashirikisha jumla ya wanafunzi 200 na walimu 100 kutoka katika shule 100 za Tanzania nzima - yaani Bara na Visiwani.
Wanafunzi na walimu wa shule hizi wamegharimiwa kila kitu - kuanzia nauli za kutoka huko makwao, malazi na chakula - hali inayotokana na ufadhili kutoka kwenye taasisi mbalimbali zinazoguswa na ubunifu wa watoto wetu katika kuandaa kizazi cha wanasayansi.
Haijawekwa wazi ni shule zipi zitakazoshiriki, lakini kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtandaji wa YST, Dkt. Gozbert Kamugisha, kunatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa katika kazi za ubunifu za mwaka huu kutokana na wanafunzi na walimu kila mwaka kuboresha kazi zao kwa kurekebisha makosa yaliyotokea huko nyuma.
Lengo kubwa la mashindano ama maonyesho hayo ya sayansi kwa wanafunzi ni kuhamasisha watoto wetu waweze kuyapenda masomo ya sayansi licha ya ukweli kwamba, mitaala yetu haitoi nafasi kwa watoto kufanya ubunifu.
Na ubunifu uliopo hapa kwa wanasayansi hao chipukizi ni kazi zilizo katika nyanja mbalimbali za sayansi kama Kemia, Fizikia na Hisabati, Baolojia na Mazingira, Sayansi ya Jamii na Teknolojia.
"Ugunduzi wa wanasayansi chipukizi umejikita zaidi katika kutafuta mbinu za kukabiliana na changamoto za maendeleo kwenye afya, kilimo na usalama wa chakula, usalama wa mawasiliano na uchukuzi, nishati na mazingira, elimu, mahusiano ya kijamii na matatizo ya kijamii," anasema Dkt. Kamugisha.
Wanasayansi hawa chipukizi hawaji bure, kwani miongoni mwao watakaoshinda watazawadiwa fedha taslimu, medali na vifaa vya maabara na wanne kati yao watapewa ufadhili wa kusomeshwa mpaka elimu ya chuo kikuu, ufadhili ambao hutolewa na taasisi ya Karimejee Jivanjee Foundation ili waweze kuendelea kuimarisha vipaji vyao vya ugunduzi wa kisayansi.
"Maonyesho ya wanasayansi chipukizi ya 2018 yanalenga kuwahamasisha wanafunzi wa sekondari kupenda sayansi na ugunduzi na kujenga utamaduni wa kisayansi kwa vijana wa Kitanzania, ni fursa nzuri kwa wanafunzi kuonyesha njia madhubuti za kukabiliana na changamoto za kijamii na kiuchumi," anasema Dkt. Kamugisha.

Tanzania ya Viwanda
Ukiacha malengo hayo yanayoelezwa na waandaaji, lakini taswira chanya iliyopo sasa inaonyesha yanakwenda sambamba na Sera ya Serikali ya kuifanya Tanzania ya Viwanda.
Wakati maonyesho haya yanaanza mwaka 2011, hakukuwa na mtazamo wowote wa kusema kwamba nchi yetu inaweza kubadilishwa kuwa ya viwanda zaidi ya wahusika kulenga kutengeneza kizazi cha wanasayansi.
Hata hivyo, tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani na kuja na kauli mbiu ya 'Tanzania ya Viwanda', ni dhahiri kwamba maonyesho haya sasa yanafaa kutiliwa mkazo na kuungwa mkono na wadau wote wapenda maendeleo ili Tanzania ianze sasa kuwaandaa wataalamu wake ambao ndio watakaoijenga Tanzania ya Viwanda.
Ni wazi kwamba, wanafunzi waliotangulia miaka nane iliyopita kupata ufadhili, hivi sasa wengine watakuwa wanasomea shahada za uzamivu kama waliendelea moja kwa moja, japo walio wengi wamehitimu shahada za kwanza na uzamili.
Hawa wasomi kama watajengewa mazingira mazuri na wezeshi kwa kuzingatia sera nzuri, hakika wanaweza kuwa wataalamu tunaowahitaji kwa sababu hatuwezi kuzungumzia Tanzania ya Viwanda bila kuwa na wataalamu, hata kama tutakuwa na malighafi za kutosha.
Washindi wa mwaka 2017, kwa mfano, Prosper Gasper na Erick Simon, wanafunzi wa shule ya sekondari ya St. Jude’s kutoka Arusha, ambao wazo lao la “Kutumia Simu za Mkononi kama Mfumo wa Kubaini Ajali za Moto” (The Use of Mobile Network as a Fire Alert System) liliyashinda mawazo mengine 99 yaliyowasilishwa mwaka huo, walifanya vizuri hata kimataifa baada ya kuibuka washindi wa kwanza katika Mashindano ya Ubinifu wa Sayansi na Teknolojia barani Afrika yaliyofanyika jijini Johannesburg, Afrika Kusini 2017, Tanzania ikishiriki kwa mara ya kwanza kabisa.
Vijana hao walibuni mfumo wa kubaini, kwa kutumia simu za mkononi, uwepo wa moto pamoja na wizi kwa kuweka ving’amuzi vinavyoweza kubaini mapema hata kama mtu hayuko nyumbani au akiwa amelala.
YST ni kama jiwe la msingi katika kukuza vipaji vya wanasayansi nchini, na maonyesho haya yameonyesha ongezeko kubwa la ushiriki wa shule za sekondari kutoka shule 4 mwaka 2011 hadi 100 mwaka sasa, hatua ambayo imetokana na hamasa ya kuendeleza masomo ya sayansi kwa shule mbalimbali za sekondari nchini.
Kwa maana hiyo, baada ya YST kuibua vipaji, serikali na wadau wengine wanapaswa kuunga mkono jitihada hizi na wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha vipaji hivi vinaendelezwa hata baada ya mashindano.
Lazima serikali na wadau wengine waweke mazingira mazuri yatakayowapa fursa na hamasa watoto wetu siyo tu kupenda masomo ya sayansi, bali pia kuonyesha ubunifu na vipaji vyao.
Tunapozungumzia Tanzania ya Viwanda tunamaanisha kwamba lazima tuwe na wataalamu ambao watabuni na kuendeleza viwanda vilivyopo.

Comments