Featured Post

KAMATI YA MISS MORO YATOA MABATI KWA SHULE YA MSINGI

Kamati ya maandalizi ya shindano la Warembo wa Morogoro (Miss Morogoro 2018) imeanza kutoa misaada mbalimbali kwa jamii ambapo kwa imetoa bati 35 katika shule ya  msingi Muungano iliyopo kata ya Mafisa manispaa ya Morogoro.


Mkurugenzi wa Miss Morogoro Farida Kulususu akizungumza wakati wa kukabidhi mabati shuleni hapo,alisema wao kama kamati kwa kushirikiana na warembo wao wameonelea kutoa mabati hayo kwa ajili ya kuezeka chumba cha darasa moja ambalo lilikuwa wazi kwa muda mrefu.
Farida ambaye pia ni mkurugenzi wa Nyumbani Park/Samaki Spot Morogoro, alisema pamoja na kuwepo kwa changaamoto nyingi katika shule za msingi hasa katika ujenzi wa madarasa, na uhaba wa madawati aliwaomba wahisani wengine kujitokeza kusaidia katika maeneo hayo kwa shule hiyo na shule nyingine zenye mahitaji.
“Sisi kama kamati yaa Miss Morogoro kwa kuanzia tumeona tutoe mchango wetu wa bati ambazo zitasaidia kwa darasa moja na tutajitahidi kusaidia katika maeneo mengine kwa kadri tutakavyo jaliwa,”alisema Farida.
Kaimu mwalimu mkuu wa shule ya msingi Muungano Clemence Mgana akishukuru baada ya kupokea bati hizo alisema, shule bado imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya kutokamilika kwa majengo manne ya vyumba vya madarasa.
Mgana alisema shule hiyo pia inakabiliwa na uhaba wa madawati kwa darasa la tatu ambao baadhi yao wamekuwa wakikaa chini.
“Madawati yaliyopo sasa ni 305, mahitaji ni 503 upungufu 196 huku wanafunzi walioandikishwa kwa darasa la kwanza 2018 ni 296,hatuna ofisi ya walimu kwani kwa sasa walimu wanatumia darasa moja wapo,” alisema Mgana.
Mmoja wa wanafunzi katika shule hiyo Fatuma Athumani alizungumzia tatizo la maji katika shule hiyo ambayo imedumu kwa muda mrefu jambo linalowalazimu wanafunzi kubeba maji kwenye dumu ndogo na kwenda nayo shule.

Comments