Featured Post

HISPANIA, RWANDA ZAONGOZA KWA KUWA NA WANAWAKE WENGI KWENYE UONGOZI WA SERIKALI



LONDON, ENGLAND
REKODI ya idadi ya wanawake wanaowania nafasi mbalimbali wakati wa uchaguzi duniani inabadili uso wa siasa na kuchochea uwepo wa usawa wa jinsia katika mabunge.
Mexico imechagua idadi sawa ya wanawake na wanaume bungeni katika mabunge yote mawili, hatua inayodhihirisha kuwa nchi hiyo imepiga'' hatua kubwa''.

Serikali ya Hispania, ilichaguliwa mwezi Juni, ni ya kwanza tangu nchi hiyo ilipokuwa ya kidemokrasia kwa kuwa na wanawake wengi kuliko wanaume kwenye Baraza la Mawaziri.
Waziri Mkuu wa New Zealand, Jacinda Ardern, alijifungua mtoto wa kike Juni 21, 2018 na kuwa mwanamke wa pili pekee kuwa na mtoto akiwa madarakani, baada ya Waziri Mkuu, Benazir Bhutto, wa Indonesia mwaka 1990.
Je, mwaka 2018 ni mwaka wa wanawake kushika nyadhifa mbalimbali?
Mwaka mmoja baada ya Hillary Clinton kushindwa nafasi ya urais nchini Marekani, kumekuwa na wanawake ambao wanawania nafasi mbalimbali nchini humo kuliko ilivyokuwa zamani.
Mgombea wa chama cha Democrat, Alexandria Ocasio-Cortez, alimshinda mwanasiasa mkongwe Joe Crowley mwenye miaka 56, jijini New York mwezi Juni.
Binti huyo mwenye miaka 28 aliwashangaza wengi kwa kuwa hakuwa na historia ya kuwa kwenye siasa, lakini alipambana na mtu aliyetumika kwenye siasa kwa awamu 10.
Profesa Farida Jalalzai, Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa katika Chuo cha Oklahoma, anaamini kuwa uthubutu wa wanawake kuwania nafasi mbalimbali ni kwa sababu pia hawapendezwi na Donald Trump.
Anasema kuwa wanawake wanafanya vizuri sana mwaka huu kwenye Bunge la Congress. Lakini kuna safari ndefu bado kwa kuwa kuna 20% pekee kwenye Bunge la Wawakilishi.

Vipi kuhusu Ulaya?
Wanawake wako mpaka 30% kwenye mabunge ya mataifa ya Ulaya ikiwemo Monaco.
Mwaka 2017 idadi kubwa ya wanawake ilijitokeza kwenye chaguzi duniani, lakini hakukuwa na mafanikio makubwa. Ulaya ilipata wanawake wengi waliokuwa na uwakilishi bungeni, lakini wengi walikosa nafasi hizo.
Karibu kila nchi duniani imerekodiwa kuwa na ongezeko la idadi ya wabunge wanawake tangu mwaka 1997 baada ya Umoja wa Mabunge (IPU) kukusanya matokeo.
Miongo miwili iliyopita Sweden, Norway, Finland, Denmark na Uholanzi zilikuwa na zaidi ya 30% ya wabunge wanawake-huku Sweden ikiongoza kwa 40.4%.
Miaka 21 baadaye, nchi zinazoongoza sambamba na nchi za Scandnavia zimepitwa na Rwanda na nchi kadhaa za America ya Kati na Kusini, Bolivia, Grenada, Mexico, Nicaragua, Costa Rica na pia Visiwa vya Caribbean kama vile Cuba, pia ni miongoni mwa nchi 10 zenye zaidi ya 40% ya wabunge wanawake.
Lakini Zeina Hilal, ambaye ni kiongozi wa masuala ya mpango wa jinsia ndani ya IPU, anasema maendeleo katika kuhakikisha kuwa kuna usawa kati ya wanawake na wanaume katika uwakilishi yanaonyesha kuzorota katika kipindi cha miaka miwili au mitatu.
''Tunasikitika kwa kuwa miaka michache iliyopita ilikuwa ongezeko la kiasi cha 0.6% kwa mwaka 2016 na 2017, kwa miaka miwili mfululizo tumefikia uwiano wa 0.1% hii inaogofya''.
Ikiwa uwiano huu utaendelea, IPU inakisia kuwa itachukua miaka 250 kufikia usawa wa jinsia kwenye mabunge.
Nchi nyingi duniani hazina viongozi wanawake, kwa sasa kuna viongozi wa juu wanawake 11 duniani-ukijumuisha marais idadi inafika 21.
Angela Merkel ni kiongozi pekee aliyehudumu muda mrefu kwenye serikali ya Ujerumani, amekuwa kiongozi tangu mwaka 2005.
Mbali na Sheikh Hasina Wajed wa Bangladesh, ambaye kwa sasa yuko kwenye muhula wa tatu, wanawake wengine walio viongozi wa serikali wamekuwa kwenye nafasi hizo kwa miaka mitano au chini ya hapo. Jacinda Ardern wa New Zealand, Kiongozi wa Iceland Katrin Jakobsdottir na Ana Brnabic wa Serbia wote walichaguliwa mwaka 2017.
Erna Solberg alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Norway mwaka 2013.
Nchini Namibia, Saara Kuugongelwa aliingia madarakani mwaka 2015, Theresa May akawa Waziri Mkuu wa pili mwanamke wa England mwaka 2016, mwaka sawa na aliochaguliwa Aung San Suu Kyi nchini Myanmar.
Viorica Dancila ni mwanamke wa kwanza katika historia kuwa Waziri Mkuu wa Romania, alichaguliwa Januari mwaka 2018.

Rwanda inaongoza kwa kuwa na wawakilishi wanawake
IPU imeorodhesha nchi tatu zenye mambunge madogo zenye uwakilishi wa zaidi ya 50% wa wanawake nazo ni Rwanda, Cuba na Bolivia. Ingawa Mexico ina kiasi cha 48.6%.
Rwanda inaongoza kwa kuwa na uwiano mkubwa wa wanawake katika bunge kuliko nchi nyingine yoyote.
Mabadiliko ya katiba mwaka 2003 yameruhusu 30% ya viti kuwa vya wanawake bungeni. Tangu wakati huo wanawake wamekuwa wakijitokeza katika chaguzi mbalimbali.
Mabadiliko hayo yalikuja baada ya Mauaji ya Kimbari mwaka 1994 ambapo watu 800,000 wengi wanaume walipoteza maisha, wanawake walilazimika kufanya majukumu mapya mengi ili kuijenga upya nchi yao.
Rwanda hivi sasa ni moja kati ya nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi barani Afrika ingawa Rais Paul Kagame amekuwa akikosolewa kuwa amekuwa akiwabana wapinzani.
Nchi nyingine iliyo na uwiano mzuri wa jinsia ni pamoja na Bolivia na Mexico.

Nchi gani ina wawakilishi wachache wanawake bungeni?
Miongoni mwa nchi zilizo na rekodi mbaya kwa uwakilishi wa wanawake bungeni ni Yemen, Oman, Haiti, Kuwait, Lebanon na Thailand-nchi zote zikiwa na 5% ya uwakilishi au chini ya hapo.
Kuna visiwa kadhaa ambavyo havina uwakilishi wa wanawake kabisa kama vile Vanuatu, Micronesia na Papua New Guinea na nchi nyingine kama El Salvador na Sierra Leone ambayo idadi ya uwakilishi wa wanawake haifahamiki.
Yingluck Shinawatra aliweka historia ya kuwa Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke wa Thailand mwaka 2011.
Wakati huo alikuwa mmoja kati ya wawakilishi wanawake kwa 16% bungeni-namba kubwa katika Bunge la Thailand-lakini mwaka 2015 alishtakiwa kwa shutuma za ufisadi na kutoroka nchini humo.
Tangu wakati huo idadi imeshuka mpaka kufikia 5%.
Nchini Yemen kuna mwanamke mmoja tu aliyechaguliwa bungeni kati ya wabunge 301. Mpango wa kuhakikisha kunakuwa na uwakilishi wa angalau 30% haukufanikiwa.
Professor Franceshet anasema anaamini hali itabadilika ikiwa wanawake wataendelea kuweka msukumo kwa vyama vya kisiasa na kwa viongozi wa kisiasa kwa ajili ya kuwapa nafasi zaidi wanawake.
BBC

Comments