Featured Post

CHELSEA YAMTIMUA ANTONIO CONTE, KOCHA MAURIZIO WA NAPOLI KUTUA



LONDON, ENGLAND
CHELSEA inatarajiwa kuweka wazi uamuzi wake wa kutengana na Conte baada ya kuwatumikia kwa miaka miwili hivi karibuni.
Kufikia sasa, klabu hiyo imekataa kufunguka kuhusu hatma ya meneja huyo wa Italia mwenye umri wa miaka 48 lakini inafahamika kwamba amefutwa kazi na hata wachezaji wa Chelsea wamekuwa wakimtakia heri na kumshukuru kwa muda aliokaa Chelsea.

Conte aliwasaidia kutwaa mataji ya ligi ya Premia msimu wake wa kwanza pamoja na Kombe la FA.
Licha ya Conte kuwaongoza wachezaji mazoezini wiki hii, hatma yake imekumbwa na taharuki huku mkufunzi wa zamani wa Napoli, Maurizio Sarri, akitarajiwa kujaza pengo lake.
The Blues wa Chelsea tayari wamefikia makubaliano ya kuwasili kwa Sarri mwenye umri wa miaka 59.
Iwapo usajili wa Sarri utadhibitishwa, atakuwa mkufunzi wa tisa wa Chelsea tangu Mrusi Roman Abramovich aliponunua timu hiyo 2003.
Licha ya kutoinua taji lolote na Napoli miaka mitatu aliyowaongoza, Sarri amerudisha hadhi ya Napoli na kuwawezesha kumaliza nafasi ya pili, tatu, na pili nyuma ya Juventus msimu uliomalizika wa 2017-18.
Aidha, Sarri, kocha wa zamani wa Empoli, alitajwa kocha bora wa mwaka Serie A, msimu wa 2016-17.
Aslimia ya ushindi wa Conte mechi za Premier League ni bora kuliko wakufunzi wote waliowahi kuinoa timu hiyo.
Hata baada ya kubeba Kombe la FA mwezi Mei kwa kuizamisha Manchester United, mustakbali wa Conte ulizidi kutapatapa.
Hakupoteza matumaini na aliweza kurudi kuinoa timu hiyo wakati ikijiandaa kwa msimu ujao.
Isitoshe, dalili za kuondoka kwake ziliongezeka kuanzia mwisho wa msimu uliopita baada ya Blues kukosa kufuzu kwa Champions League kwa kumaliza nafasi ya tano Premier League.
Hata ubingwa wa Chelsea mwezi Mei Kombe la FA ilimaanisha kuwa Conte - aliyeifunza Juventus kutoka 2011 hadi 2014 - hajawahi kuondoka mikono mitupu katika misimu mitano iliyopita ambapo alihudumu kuwa meneja.
Lakini mambo yalibadilika msimu uliopita na Chelsea ilimaliza alama 30 nyuma ya Manchester City, mabingwa wa Premier League pamoja na kutemwa nje ya Champions League, hatua ya mchujo baada kufungwa 4-1 na Barcelona katika mechi za mikondo miwili.
Matokeo hayo yalizamisha ufanisi wa klabu hiyo ya London Magharibi huku Conte akilaumu msongamano wa mechi kwenye ratiba katika msimu wa Krismasi.
Mnamo mwezi Oktoba, Blues walidhalilishwa na Crystal Palace ambayo hata haikusajili pointi moja katika mechi saba na kumchochea Conte kujitetea dhidi ya kuwepo kwa mgomo baridi kutokana na mbinu zake za mazoezi.
Baada ya Krismasi, Chelsea ilifungwa mechi nne - mbili mfululizo - mwanzo dhidi ya Bournemouth na Watford, kabla ya kudunishwa na timu za Manchester City na Manchester United.
Hata baada ya kufufua fomu yake baadaye kwa kushinda mechi nne mfululizo msimu ukikaribia kukatika, haikuiwezesha Chelsea kumaliza kati ya timu nne za kwanza.
Kasoro ya Conte ni kukosa kuwasajili mastaa?
Miezi miwili tu baada ya kuiongoza Chelsea kutwaa taji la ligi ya Premier 2016-17, Conte alizidisha mkataba wake ikiwemo kurefusha muda wake Stamford Bridge miaka miwili zaidi.
Lakini alionywa dhidi ya kufuta rekodi yake kwa kumuiga Mourinho ambaye, msimu mmoja tu baada ya kuisaidia Chelsea kunyakua ligi 2015-16, aliwarudisha nyuma kwa kumaliza nafasi ya 10 kwenye jedwali msimu uliofuata.
Msimu wa 2017 ulikumbwa na kuondoka kwa viungo muhimu wa timu hiyo akiwemo nahodha John Terry aliyeitumikia Chelsea miaka 22, na Diego Costa aliyefahamishwa kupitia arafa kuwa hakuoana na mipango ya Conte.
Hali hiyo ilipelekea Costa kujiunga na to Atletico Madrid ambapo walibeba Kombe la Europa League msimu uliokamilika 2018.
Uhamisho huo wa Chelsea uliendelea huku ikiagana na kiungo mkabaji wake Nemanja Matic na kumpiga bei kwa mahasimu wake Manchester United kwa kitita cha pauni milioni £40.
Chelsea ilijaribu kuokoa chombo kwa kumsajili Alvaro Morata, lakini haikufanikiwa kumshawishi nyota wake wa zamani Romelu Lukaku, kujiunga nao.
Lukaku aliishia kutua Old Trafford.
Sakata hizi zilipelekea kuibuka kwa maswali kuhusu kusalia kwa Conte klabu hiyo na tangu mwezi Januari mwaka huu, maswali haya yalizidi.
Conte hakukosa kuyajibu na kila alipoulizwa, alisisitiza kuwa alikuwa mwenye furaha huku akitaka klabu hiyo imuunge mkono na kumhakikishia uwepo wake kiti cha Ukufunzi.

Comments