Featured Post

BIOTEKNOLOJIA ASILIA ZINACHANGIA KUBORESHWA BIOTEKNOLOJIA MPYA



NA ALOYCE NDELEIO
BIOTEKNOLOJIA asilia au za kitamaduni inamaanisha njia za asili na zamani zilizotumiwa na viumbe hai kutengeneza bidhaa mpya au  kuboresha iliyokuwepo.
Katika uhalisia wake zaidi ni kwamba chimbuko la njia hizo linaweza kuonekana kwenye mifumo ya maisha ya binadamu tangu alipoanza  kuhama kutoka uwindaji na ukukusanyaji wa matunda kama chakula na kuzalisha mahitaji yake kupitia kilimo.

Binadamu akiwa ni mkulima aliweza kukusanya mimeapori na kuanzisha kilimo chake na kuwa na mbegu nzuri kwa ajili ya kuotesha msimu wa uliofuatia ambazo zilichaguliwa kutoka mazao yaliyopatikana  msimu wa mavuno.
Jinsi binadamu alivyozidi kugundua aina mbalimbali za mimea basi ndio  wakati huo alianza kutafuta mbegu zake na kuzikuza ili kupata mbegu bora ambazo zilitumika kwa miaka kadhaa.
Mara nyingine mbegu hizo zilittumika kutoka kizazi kimoja hadi kingine, aidha ni katika kipindi hicho binadamu aliweza kufahamu tabia mbalimbali  za mimea na jinsi inavyoweza kuhimili aina kadhaa za magonjwa.
Katika bioteknolojia hizo za asili ndiko binadamu aliweza kubaini ni aina  ipi ya mbegu iliyo na ladha nzuri na inayotoa mazao mengi.
Hali kama hiyo pia ilikuwepo kwa upande wa wanyama waliowafuga, ambapo mbinu  kama zilizotumika kwenye mbegu za mimea zilitumika  kupata aina nzuri ya wanyama kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Karne zilizopita watu waligundua njia za usindikaji wa asili ambao ulitokea katika seli zilizokuwa hai kwa bahati mbaya. Japo hawakuwa na maelezo ya kisayansi kuhusu hatua hizo walitumia matokeo waliyokuwa wanayaona katika maisha yao ndani ya kaya zao.
Kwa mfano waligundua chakula kilikuwa kinaweza kubadilika ladha na hata viambatanisho vyake na kwamba inakuwa si rahisi kuharibika.
Kadhalika waligundua kuwa ipo haja ya kuvundisha unga wa ngano,  kuukanda kwa  ajili ya kuoka mikate, zabibu zikavundishwa na kuzalisha  mvinyo na kupata siagi kutoka kwenye maziwa.
Kufutia majaribio ya hapa na pale, na baadaye kuingia kwa teknolojia ya juu, watu walijifunza kudhibiti hatua hizo na kutengeneza bidhaa nyingi  zinazotokana na bioteknolojia.
Maendeleo ya sayansi yaliwezesha kuhamishwa kwa teknolojia nyingi  zilizokuwa zinatumika majumbani na kuziingiza katika matumizi na hivyo kugundua mbinu mpya.
Kwa hali hiyo baioteknolojia za asili ni pamoja na kuchagua mbegu, kutafuta mbegu nzuri na hata kuvundisha baadhi ya mazao.

Bioteknolojia mpya
Bioteknolojia ya kisasa inahusisha mbinu kadhaa ambazo zinajumuisha  kwa makusudi matumizi ya vinasaba, seli na tishu hai katika njia  zinazotabirika na zinazodhibitika kuleta mabadiliko katika muundo wa  vinasaba katika kuunda  kiumbe au kutengeneza tishu mpya.
Mfano wa mbinu hizi ni pamoja na kuunganisha DNA au uhandisi  vinasaba, kuboresha tishu n.k.
Bioteknolojia ya kisasa ilianza mwaka 1953 baada ya kugundulika kwa DNA (deoxyribonucleic acid) na jinsi mawasiliano ya vinasaba yanavyotoka kizazi kimoja hadi  kingine.
Ugunduzi huu uliwezekana kutokana na ugunduzi wa awali wa vinasaba uliofanywa na Mwanasayansi Gregor Mendel, ambao uliweka misingi ya mpito kutoka bioteknolojia ya asili na ya kisasa.
Aidha, uliwezesha kuzalisha mabadiliko yaliyotakiwa ndani ya viumbe kwa kubadili moja kwa moja vinasaba kwa njia iliyodhibitiwa na inayochukua muda mfupi ikilinganishwa na mbinu za asili.
Ugunduzi huo ulikuwa sanjari na kupanuka kwa teknolojia na sayansi kama  vile biokemia na saikolojia, na hivyo kufungua uwezekano wa matumizi mapya ya biotekonolojia ambayo yalikuwa hayafahamiki kwenye mifumo  ya asili.

Tofauti ya bioteknolojia mpya na ya zamani
Kabla ya kugundulika kwa vinasaba na DNA mabadiliko ya vinasaba ndani ya viumbe ikiwemo mimea. Kwa mfano mmea uliokuwa na muonekano wa kufanana uliweza kupandikizwa kwenye mmea mwingine kwa matumaini kwamba kupitia njia ya chavua tabia  hiyo au ukuaji wake ungehamishiwa kwenye machipukizi ya mimea mama.
Hata  hivyo katika bioteknolojia ya kisasa kufikia malengo tarajiwa ndani ya kiumbe hufanyika katika kiwango cha kinasaba.
Kutokana na hali  hiyo  kinasaba kilichokusudiwa kwenye mabadiliko kinatambuliwa, kuhamishwa na  kupandikizwa kwenye seli za kiumbe ili kuzalisha mabadiliko ya kinasaba.
Kadhalika katika mbinu nyingine mpya za bioteknolojia ni kama vile kuweka vinasaba kwenye  joto kubwa ili kuleta mabadiliko yaliyokusudiwa katika muundo wa kinasaba au tishu za mmea.
Katika hali hiyo kubadilisha mbegu ni  mbinu ya bioteknolojia ambayo imekuwa inatumika kuuweka mmea katika tabia mpya, ili ziweze kutumiwa  baadaye kuendana na mabadiliko yanayokuwepo.

Matumizi ya bioteknolojia
Bioteknolojia ya kisasa ipo katika matumizi mengi kuliko ilivyo kwa bioteknolojia ya asili. Kwa uhalisia ni kwamba  bioteknolojia ya asili ililenga katika mahitaji ya chakula na  kilimo kwa kutumia mbinu kama vile  kuchagua mbegu au kuziloweka.
Kukua kwa Sayansi na Teknolojia kumepanua mtazamo ambao baioteknolojia inaweza kutumia kwa kuhusisha mazingira, afya ya  binadamu na wanyama kama  vile  maendeleo ya chanjo na dawa na kutambua vyanzo vya magonjwa; nishati kama vile kuzalisha dizeli; misitu kama vile kuzalisha viuatilifu na upandikizaji wa miti katika miti mingine na maeneo mengine.

Mbinu za baioteknolojia
Kukua kwa Sayansi na Teknolojia kumeibua  maendeleo ya  aina  mpya ya  mbinu za bioteknolojia ambazo zilikuwa hazipo katika mbinu za  asili za bioteknolojia.
Mfano bioteknolojia ya sasa inajumuisha mbinu kama vile kuunganisha DNA sanjari na masuala ya kutengeneza vinasaba.
Miongoni mwa mbinu  zinazotumika katika bioteknolojia  za kisasa zimeanzishwa kutokana na matokeo ya kuongezeka kwa uelewa wa  vinasaba na viumbe wadogo. Mfano bioteknolojia  ya asili ya kuchagua mbegu kutoka mimea inayofanana pindi inapochanganywa.
Hata hivyo kupitia teknolojia ya kuunganisha DNA ndani ya bioteknolojia za kisasa, vinasaba vinaweza kuhamishwa  kati ya  aina mbili  zisizofanana, mfano kati ya bakteria na binadamu. 
Mbinu za kisasa pia kama vile kuunganisha DNA kumewezesha kupatikana kwa  bidhaa mpya kwa kiwango kikubwa kuliko inavyowezekana katika mbinu za asili za  bioteknolojia.

Muda na usahihi
Kugundulika kwa  muundo wa chembechembe za DNA na namna ambavyo habari za vinasaba zinahamishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine  kumewezesha kuhamisha vinasaba, hivyo tofauti  zilizopo  kati viumbe kwa kutumia  teknolojia ya kisasa kunakuwa ni kwa kasi na hutumia muda mfupi kuliko kutumia teknolojia za asili.
Japo sio lazima sana kwamba kila seli inayotumika katika hatua mojawapo  inajumuisha kuhamisha kinasaba lakini ukweli ni kwamba uwezekano wa  kujumuisha seli na kinasaba kinachokusudiwa  kwa  kiwango kikubwa  inatumika kwa kutumia mbinu mpya za baioteknolojia kuliko kutumia  bioteknolojia za asilia.
Lakini kwa kutumia mbinu za asili itachukua muda wa vizazi vingi na muda mwingi wa kuzalisha mimea na wanyama walio katika mkondo  unaotakiwa miaka  mingi kwani inakuwa ni kujaribu kwa kubahatisha .
Uelewa wa vinasaba halisi unaweza kuhamishwa pamoja na teknolojia za kisasa  kumeweza kupunguza muda unaotumika katika kupata matokeo kuliko ambavyo  ingetumika katika mbinu asilia za bioteknolojia.

Comments