Featured Post

BILA KUWA NA DHAMANA, NDOTO KUPATA PEMBEJEO



NA DANIEL MBEGA, DODOMA
LICHA ya msimu wa masika kwa mwaka huu 2017 kukumbwa na hali ya ukame, lakini upatikanaji wa pembejeo za kilimo umekumbwa na changamoto kubwa inayoashiria uzalishaji duni wa mazao ya chakula na biashara.
Safari hii siyo changamoto ya ubadhirifu na ucheleweshaji wa pembejeo hizo, bali ni wakulima wenye dhamana tu ndio wanaoruhusiwa kupatiwa vocha za pembejeo.

Uchunguzi uliofanyika mkoani Dodoma umebaini kwamba, ingawa wakulima wengi mkoani humo siyo wanufaika wakubwa wa pembejeo hizo, lakini wale wanaostahili kupata safari hii wameshindwa baada ya kuwepo kwa sharti la dhamana ya kuwa na shamba lisilopungua ukubwa wa ekari moja.
Aidha, wakulima wengi ambao mara nyingi huhitaji pembejeo hizo, hususan mbegu na mbolea, na wale wanaojihusisha na kilimo cha mpunga, mahindi na vitunguu, wengi wao wakiwa katika maeneo ya mabonde ambayo yanahusisha kilimo cha umwagiliaji.
Zuberi Saidi Mlinji, Ofisa Ugani wa Kata ya Malolo, anasema, utaratibu wa ugawaji wa vocha za pembejeo umebadilika ambapo sasa si wote watakaonufaika kama ilivyokuwa zamani bali ni wale tu watakaokidhi masharti.
“Kwa mfano, katika Kijiji cha Malolo vocha zitakazokuja ni 100 tu na zitatolewa kwa wakulima ambao wanakidhi vigezo vya kuwa na shamba lisilopungua ekari moja,” anasema ofisa huyo.
Anasema serikali imefanya hivyo baada ya kugundua kwamba, baadhi ya wakulima waliokuwa wakipata vocha za pembejeo hawakuwa pia na uwezo wa kulipia hata nusu ya gharama na wengine hawakuwa kabisa na mashamba, hatua ambayo iliwafanya baadhi yao kuzigeuza mtaji kwa kuuza kwa wenye uwezo.
“Wengi walikuwa wakiziuza tena vocha hizo kwa sababu ama hawakumudu gharama, hawakuwa na mashamba na wengine waliamua tu kutotumia na kugeukia kwenye kilimo cha asili walichokizowea kwa kutumia mbegu za asili na hawakutumia mbolea kabisa,” anabainisha ofisa ugani huyo wakati akizungumza na mwandishi wa makala haya kijijini Malolo.
Anasema hivi sasa wameamua kutoa pembejeo hizo kwa wakulima baada ya kujiridhisha kwamba wana uhitaji na wanayo mashamba yanayokidhi vigezo.
Aidha, anasema kwamba, kupungua kwa idadi ya vocha hizo za pembejeo ni jambo la kawaida, kwani mpango huo wa serikali ulilenga kuwawezesha wakulima kupata mbegu bora pamoja na mbolea ili kukuza uzalishaji na kuongeza kipato.
Kupitia mpango huo wa ruzuku ya pembejeo ulioanza mwaka 2008, serikali ililenga kuwapunguzia mzigo wakulima kwa kubeba nusu ya gharama za pembejeo hizo wakati kiasi kingine kilipaswa kulipwa na wakulima wenyewe.
Kwa mujibu wa maelezo ya maofisa kutoka wizara ya kilimo, idadi ya vocha hizo ilikuwa ipungue kila mwaka kwa kuamini kwamba, walau katika kipindi cha miaka mitatu wakulima hao wangekuwa na uwezo wa kujinunulia wenyewe pembejeo.
“Watu wanakosea, ni kwamba, mpango huu ulipanga kuwawezesha wakulima wote walau kwa miaka mitatu, na baada ya hapo vocha zisingeweza kuja kwa idadi sawa, bali zingeendelea kupungua kwa kuwa serikali iliamini katika kipindi hicho tayari wakulima wangeweza kumudu kununua pembejeo wenyewe, jambo ambalo linaonekana kama limeshindikana,” anasema ofisa mmoja wa wizara hiyo anayeshughulikia masuala ya pembejeo, ambaye aliomba hifadhi ya jina lake.
Lakini kupungua kwa vocha hizo za ruzuku, na kwa utaratibu wa sasa wa kuhakikisha wakulima wanakuwa na dhamana, kutaleta changamoto kubwa ya mpango wa serikali kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo.
Licha ya kupungua kwa idadi hiyo, lakini mara kadhaa pembejeo zimekuwa zikichelewa kuwafikia wananchi na mpango huo umekumbwa na ufisadi mkubwa kwa watendaji pamoja na mawakala, ambapo inaelezwa kwamba, baadhi yao walishtakiwa katika mahakama za kisheria.
Kila mwaka, bajeti kuhusu pembejeo za kilimo imekuwa ikipungua na wakulima, ambao wanaamini ni haki yao kupata vocha hizo bila kujali idadi yao, wanaona kwamba serikali imewatelekeza.
Kwa mfano, katika bajeti ya kilimo ya 2015/2016, makadirio ya mahitaji ya pembejeo yalikuwa tani 485,000 za mbolea, tani 60,000 za mbegu bora, miche ya chai 1,700,000, miche ya kahawa 5,000,000, viuatilifu vya korosho tani 25,000 na viuatilifu vya pamba ekapaki 1,500,000.
Aidha, kwa mwaka 2015/2016 Serikali ilitoa ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa mfumo wa vocha ambapo kaya za wakulima 999,926 zilinufaika kwa kutumia tani 99,993 za mbolea, tani 10,270.86 za mbegu bora za mahindi na mpunga vyote vikiwa na thamani ya Shs. 78 bilioni.
Idadi hiyo ilipungua kwa mwaka 2016/17, serikali ilisema ingewezesha upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwa kuhakikisha upatikanaji wa tani 400,000 za mbolea, tani 40,000 za mbegu bora, miche bora ya kahawa na chai pamoja na kuwezesha upatikanaji wa viuatilifu vya zao la korosho, pamba na mazao mengine.
Licha ya sekta ya kilimo kuchangia asilimia 29 ya Pato la Taifa kwa mwaka 2015, lakini ukuaji wake ulipungua ulipungua kwa asilimia 2.3 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 3.4 katika mwaka 2014 kwa shughuli za kiuchumi za kilimo zinazojumuisha mazao, ufugaji, uvuvi na misitu.
Wakati ambapo mahitaji ya pembejeo yanaongezeka kila mwaka kutokana na wananchi kuhamasika kujishughulisha na kilimo, serikali imeshindwa kuongeza nguvu katika utoaji wa vocha za ruzuku hasa kwa kuzingatia kipato halisi ya mwananchi wa kawaida, hususan mkulima, ambaye hana uhakika na soko la mazao yake huku hali ya mabadiliko ya tabia nchi nayo ikimuathiri kutokana na uhaba wa mvua.

Comments