Featured Post

ADC: WANAOMPINGA MAGUFULI WAJITAFAKARI



NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
CHAMA cha Alliance for Democratic Change (ADC) kimepongeza uamuzi wa Serikali wa kununua ndege mpya, ikiwemo ya Boeing 787-8 Dreamliner, na kuwataka wale wote wanaombeza Rais Magufuli wajitafakari upya.
Mwenyekiti wa ADC, Hamad Rashid Mohamed, amesema hakuna nchi duniani inayoweza kutangaza utalii wake bila kuwa na shirika la ndege imara linaloendeshwa kwa ufanisi ili kukuza uchumi wake, biashara na mawasiliano.

Jumapili, Julai 8, 2018, Rais John Magufuli aliwaongoza Watanzania kuipokea ndege ya abiria aina ya Boeing 787-8 Dreamliner kutoka Seattle, Marekani ambayo imenunuliwa na Serikali kwa fedha taslimu, ikiwa miongoni mwa ndege saba zilizopangwa kununuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano.
Mpaka sasa tayari ndege nne zimekwishawasili nchini na nyingine zinafanya safari katika miji takriban 12 pamoja na Visiwa vya Comoro, wakati ndege nyingine mbili zinatarajiwa kuwasili Novemba mwaka huu na Dreamliner nyingine itawasili mwaka 2020.
Hamad amesema, jitihada za Rais Magufuli kulifufua Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) zinahitaji kuungwa mkono kwani kuimarika kwake kutafungua milango  na  kutanua wigo wa uchumi, utalii, kuvutia wawekezaji na kukuza biashara za ndani na nje.
Alisema utalii ni moja kati ya sekta inayoongoza duniani na alama mojawapo ya nchi kujitangaza kimatiafa ni kuwa na shirika lake la ndege kama anavyotaka Rais Magufuli.
Hamad alisema, ni jambo la ajabu nchi ndogo kama Rwanda na Shelisheli zina mashirika imara ya ndege huku nchi kubwa kama Tanzania ikiwa haina ndege hata moja kama ilivyokuwa kabla ya ujio wa ndege mpya. 
"Nchi inapokuwa na shirika lake la ndege ni kukuza teknolojia na kuzalisha ajira mpya za ndani na nje, kwa wahandisi, marubani, wahudumu pia biashara zitapanuka," alisema Hamad.
Alisema, wanasiasa wanaobeza hatua hiyo ya Rais wanahitaji kutafakari maradufu kwani mpango wa kuwa na shirika ulikuwepo toka awamu ya kwanza na anachokifanya Rais Magufuli sasa ni uthubutu wake wa kulifufua na kuitakia mema nchi yake.
"Ipo haja ya kuwa makini katika kuwekeza mtaji wa kutosha, umakini wa menejimenti, matengenezo ya huduma za ndege, tuna nafasi ya kufanya vizuri, mfano mzuri wa mashirika madogo ya ndege za ndani yalivyoanza na sasa yanavyotoa huduma bora," alieleza.
Alisema, Tanzania ina nafasi kubwa ya kutumia viwanja vyake vyenye idadi ya wakazi  wanaofikia milioni  3 hadi 6 na iwapo vitatumika kwa kujali soko la ndani na nchi jirani kama kongo, Rwanda, Uganda, Kenya na Burundi na wanaobeza pengine hawatambui  umuhimu wa usafiri wa anga na reli.
"Anayebeza hajui misingi ya uendeshaji wa kibiashara, miundombinu ni msingi mkubwa wa kukuza biashara zikiwemo barabara, reli, usafiri wa majini na anga ni mambo yanayohitaji kutazamwa kwa muhimu wake," alieleza.
Mwenyekiti huyo  wa ADC alisisitiza kuwa, maeneo hayo ni lazima yapewe kipaumbele kwani hata wakati wa utawala wa Mwalimu Julius Nyerere kulikuwa na mashirika mengi kama Tacoshil, Nasaco, Dahaco, TRC, ATC, Kamata  na UDA.
Alisema, katika nchi yoyote ikiwa watu hawazungushi biashara kitaifa na kimataifa, uchumi hauwezi kukua.
"Kama huna usafiri wa ndege, barabara na reli utakwama. Kuna Watu hawawezi kupanda treni, kwa muda mrefu wanapatanda ndege, lazima fursa kama hizo ziwepo katika nchini," aliongeza.
Alitoa mfano wa China ambayo imeanzisha treni inayokimbia kwa kasi kuliko zote duniani ili kuwafanya wafanyabiashara wake kuwafikia watu wengi, lengo likiwa ni kuwapa nafasi kufanya biashara kwa uharaka na usahihi.
Katika hatua nyingine, chama hicho kimesema mradi wa uzalishaji umeme wa maji wa Stigler's Gorge utamaliza matatizo ya nishati nchini na kuchochea shughuli za maendeleo.
Chama hicho kimesema, ni aibu kwa Tanzania kutokuwa na megawati 5,000 wakati vyanzo vya kuzalisha nishati hiyo vipo vya kutosha, hivyo uamuzi wa sasa unastahili kuungwa mkono.
Mwenyekiti wa ADC Taifa, Hamad Rashid Mohamed, alisema jana kwenye Makao Makuu ya chama hicho huko  Bububu, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi kisiwani hapa kwamba, suala la kujenga miradi kama huo wa Stigler's Gorge katika Bonde la Mto Rufiji ni la muhimu kwa kuwa umeme ni nishati muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa Taifa.
"Tumeshuhudia wenyewe namna umeme kidogo ulopelekwa vijijini ulivyosaidia kubadilisha hali za masiha ya watu kiuchumi na kijamii, kwahiyo kukamilika kwa mradi huu wa Stigler's Gorge kutakuwa na manufaa makubwa kwa Taifa zima," alisema.
Hamad alisema, licha ya kuwa umeme ni usalama wa nchi, lakini pia ni fursa pekee ya kufikiwa kwa maendeleo ya kweli kwani ndoto ya Tanzania ya Viwanda  haiwezi kufikiwa ikiwa hakuna umeme wa uhakika.
Alisema, kukamilika kwa mradi huo wa umeme wa maporomoko ya maji huko Rufiji bila shaka kutakuwa na tija kubwa ya kupatikana umeme  wa kutosha, jambo ambalo litatoa nafasi kwa wananchi kujituma, kuzalisha mali na kufanya kazi kwa bidii.
"Huwezi kupata maendeleo ikiwa unatumia umeme usio na uhakika, wataalam wanasema ili nchi ipate maendeleo ya kweli, lazima kuwe na matumizi ya umeme na akiba ya megawati asilimia 35 kwa tahadhari," alisema Hamad.
Alisema, kutengemaa kwa mradi huo kuna faida nyingi kuliko kutokuwepo kwake, hivyo ni lazima kwanza tutazame manufaa ya mradi wenyewe na tija yake kwani kunahitajika nchi iwe na vyanzo vingi kama vya umeme wa gesi, mawimbi ya bahari, upepo na maji.
Akizungumzia uamuzi wa hivi karibuni wa Rais John Magufuli kukutana na viongozi wastaafu ili  kupata maoni na ushauri, alisema ni jambo jema kwani viongozi hao wamebahatika kushika nyadhifa za juu na sasa wamepanuka maarifa na kuwa na uzoefu kuliko mtu mwingine ambaye hajashika nafasi hizo.
"Viongozi wastaafu wameongoza nchi na kushika nyadhifa kadhaa za juu, sasa wako nje ya uwanja ni rahisi kutazama makosa na kumpa ushauri, uzoefu waliopata unatosha wanajua makosa yao na mafanikio, hivyo wamemshauri kwa nia njema," alisema.
CHANZO: FAHARI YETU

Comments