Featured Post

ZIWA VICTORIA BADO LIKO HATARINI



NA CONGES MRAMBA, MWANZA
JIJI la Mwanza, Juni 5, liliadhimisha siku ya Mazingira Duniani huku  likiendelea kuacha kiasi kikubwa cha plastiki kuingia Ziwa Victoria.
Plastiki hizi zinaharibu ubora wa maji na kuhatarisha uhai wa rasilimali za ziwa hili, wakiwemo samaki.

Kwa mujibu wa Ofsisi ya Uhusiano, Halmashauri ya Jiji miaka michache iliyopita, ilikuwa ikizalisha kiasi cha tani 357 za taka ngumu kila siku, na  walikuwa wakihifadhi tani 265 tu za taka kila siku, kiasi ambacho ni takriban asilimia 80 ya taka zote.
Asilimia 20 ya taka hizi zilikuwa hazihifadhiwi, zingine huingia ziwa Victoria, ambamo hutishia uhai wa viumbe hai wakiwemo samaki.
Jiji la Mwanza lina Halmashauri mbili,  Halmashauri ya Jiji na Manispaa ya Ilemela, ambayo pia inasemwa kushindwa kukusanya taka zote zinazozalishwa kila siku.
Halmashauri ya jiji la Mwanza imesema imekuwa ikizalisha tani  nyingi za taka za plastiki, huku tani 30 zikiachwa kuingia Ziwa Victoria kila mwezi, kitu ambacho ni hatari kwa mazingira.
Afisa Uhusiano wa Jiji la Mwanza, Martin Sawema, amesema juzi kwamba hivi sasa Halmashauri yake imepata wabia ambao hurejereza kiasi kikubwa cha taka za plastiki, lengo likiwa kuondoa uwezekano wa taka hizo kuathiri ziwa Victoria na rasilimali zilizomo.
Tayari baadhi ya nchi zimepiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki, ikiwemo  Rwanda na Kenya ambazo zilipiga marufuku matumizi ya plastiki mwaka 2014.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Uhusiano ya Jiji, kabla ya wabia hawa kuja, zaidi ya tani 300 za plastiki zilikuwa zikiingia ziwa Victoria kila mwaka, na kwamba wanafanya jitihada kurejereza plastikiili zitengeneze bidhaa nyingine na kupunguza uzalishaji wa plastiki katika maji ya ziwa Victoria.
Sawema anasema, Mwanza ni Jiji ambalo idadi ya watu huongezeka maradufu kila mwaka, na mwingiliano wa wageni ni mikubwa unaosababisha biashara kuongezeka huku zikisababisha pia uharibifu wa kutisha wa mazingira hususan ziwa Victoria ambalo ni chanzo kikubwa cha pato na  chakula cha takriban watu milioni 10 wanaoishi kuzunguka ziwa hili muhimu.
Kulingana na Afisa Uhusiano huyo, jijini Mwanza wakati wa mchana,kuna kuwa na jumla ya watu milioni moja ambao Ofisa Uhusiano huyo, Sawema, anasema wanasababisha uharibifu wa mazingira, lakini hadi sasa kuna kila juhudi kuhakikisha taka za plastiki zinasombwa na kuhifadhiwa ili zitengeneza mbolea na bidhaa nyingine.
Ziwa Victoria  pia huzungukwa na idadi kubwa ya migodi ambayo uchenjuaji wa madini katika miji na vijiji huhatarisha usalama wa ziwa hili.
Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) liliwahi kusema, asilimia 86 ya miradi iliyokuwa inayotekelezwa miaka ya nyuma, ikiwemo  migodi ya madini, Kanda ya Ziwa, ilitekelezwa kinyume cha Sheria, mingi  ilikuwa haina hata vyeti vya ithibati ya  mazingira.
Miaka michache iliyopita, Taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Ulinzi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), Injinia Bonaventure Baya, iliyotolewa kwa Wakuu wa Mikoa  sita ya Kanda ya Ziwa mwaka jana,  ilisema licha ya miradi mingi kuendeshwa kwa ukiukwaji mkubwa wa sheria za Ulinzi na Uhifadhi wa Mazingira, asilimia 12 ya miradi hiyo huendeshwa pasipo kuzingatia sheria, licha ya kuahidi kila mara kwamba kuna mipango ya utunzaji wa mazingira.
Kulingana na Mkurugenzi huyo wa NEMC, Taarifa yake imetokana na zoezi la Ukaguzi uliofanywa na Baraza hilo tangu mwezi Mei hadi Julai mwaka juzi 2016 nchi nzima ikiwemo  mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera, Geita, Simiyu na Shinyanga.
Wakaguzi wa NEMC pia walizunguka katika mikoa hiyo ya Kanda ya Ziwa yenye idadi kubwa ya migodi ya madini, Ujenzi wa Mahoteli makubwa yanayotiririsha maji taka yenye kemikali, na yenye kuhatarisha usalama wa maji na viumbe hai katika Ziwa Victoria.
NEMC walisema zoezi la ukaguzi lilifanyika kwa umakini mkubwa  kwa siku 80, wakabaini kwamba asilimia 86 ya miradi mikubwa hapa nchini, huchafua mazingira.
Zoezi la ukaguzi la NEMC liliendeshwa na Timu ya wataalam walioongozwa na Dkt. Yohana Mtoni, ndilo Mkurugenzi huyo wa NEMC analosema lilibaini miradi mingi ukanda wa Ziwa Victoria inakiuka sheria ya Mazingira Sura 191 EMA, ya mwaka 2004, iliyoanza kutekelezwa rasmi hapa nchini Julai Mosi mwaka 2005.
Kulingana na Mkurugenzi huyo wa NEMC, Injinia Bonaventure Baya, zaidi ya miaka 10 imepita tangu sheria hiyo itungwe na Bunge na kuanza kutumika hapa nchini, lakini hadi sasa miradi inayoendeshwa kwa kuitii, ni asilima mbili tu.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘PAMBANA NA TAKA ZA PLASTIKI’ kuokoa mazingira.
CHANZO: TANZANITE

Comments