Featured Post

YUSSUF POULSEN: MTANZANIA WA KWANZA KUCHEZA KOMBE LA DUNIA


Poulsen (wa pili kushoto) akiwa na wachezaji wenzake timu ya taifa

MCHEZAJI ambaye baba yake ni Mtanzania ameteuliwa kwenye kikosi kamili cha wachezaji watakaoiwakilisha Denmark katika Kombe la Dunia nchini Urusi.

Iwapo atachezeshwa, basi Yussuf Yurary Poulsen huenda akawa mchezaji wa kwanza wa asili ya Tanzania kucheza katika fainali za Kombe la Dunia.
Denmark wamepangwa Kundi C na Ufaransa, Australia na Peru.
Poulsen amekuwa akicheza soka ya kulipwa katika klabu ya RB Leipzig inayocheza ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga.
Baba yake mzazi alitokea Tanga na alifariki kutokana na kansa mchezaji huyo alipokuwa na umri wa miaka sita.
Baba yake alikuwa akifanya kazi katika meli ya makontena iliyokuwa inatoka nchi za Afrika kwenda Denmark. Ni katika moja ya safari hizo ambapo alikutana na mama yake mchezaji huyo, Lene.
Poulsen alizaliwa mwaka 1994 Copenhagen, Denmark na msimu uliopita 2017/2018 alicheza katika michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya ambapo alicheza mechi nne na kusaidia ufungaji wa bao moja.
Ni mchezaji wa safu ya mashambulizi lakini hufahamika sana kutokana na kasi yake na ukabaji na kusaidia kuvuruga mchezo wa wapinzani.
Alijiunga na Leipzig wakiwa bado ligi ya daraja ya tatu Ujerumani, Julai 2013 na akapanda nao hadi daraja la pili na mwishowe Ligi Kuu 2016.
Alifunga bao lake la kwanza Bundesliga msimu wa 2016/2017 mechi ya nyumbani dhidi ya FC Augsburg.
Kwa kawaida yeye huvalia jezi nambari tisa, na amewachezea Leipzig jumla ya mechi 156 na kuwafungia mabao 37.

Shabiki wa Liverpool
Poulsen amekuwa akiashiria kwamba yeye ni shabiki wa Liverpool na ana ndoto ya kujiunga na Ligi ya Premia. Yeye pia ni shabiki wa Barcelona.
"Ligi ya Premia inaweza kunivutia sana. Inaweza kuingiana vyema na mchezo wangu," alinukuliwa na gazeti la Bild la Ujerumani mapema mwaka huu.
"Nilipokuwa mdogo, nilikuwa Liverpool. Rafiki yangu mkuu alikuwa shabiki wa klabu hiyo - na we pia unakuwa hapo, pia."
Mchezaji huyo alizuru Tanzania mwaka jana na kutembelea bibi yake Tannga.
Aliwahi kuzuru taifa hilo la Afrika Mashariki miaka ya 1996, 2002, 2008 na tena 2011.
Kutokana na babake kuwa Mtanzania, Poulsen alikuwa amehitimu kuchezea timu ya taifa ya Tanzania.
Lakini anasema hakupata ofa yoyote ya kumwalika kuichezea nchi hiyo.
"Kwanza ilikuwa faraja kwangu kucheza timu iliyokuwa daraja la kwanza Denmark mwanzoni na kucheza kwa msimu mzima, kuhusu kwani nini sikucheza timu ya taifa ya Tanzania? ni swali zuri lakini kiukweli sikupokea ofa kutoka Tanzania ya kucheza timu ya taifa lakini pia sijui ingekuwaje kama ofa ingekuja," alisema alipohojiwa na Ayo TV Julai 2017.
Hata hivyo, alikiri kwamba hawezi kusema iwapo angelipokea ofa kama hiyo, uamuzi wake ungekuwa gani.
"Nimecheza timu zote za vijana za taifa za Denmark na sasa timu ya wakubwa lakini sikuwahi kufikiria kama ningepata nafasi ya kucheza timu ya taifa ya wakubwa ya Denmark hadi nilivyoitwa lakini nimezaliwa na kukulia Denmark kama nilivyosema awali kama ofa ya Tanzania ingekuja sijui ningechagua kucheza timu gani".
Klabu ya Red Bull Leipzig anayoichezea Bundesliga ilimaliza msimu ikiwa nafasi ya sita, nyuma ya Bayern, Schalke 04, Hoffenheim, Dortmund na Bayer leverkusen.
Mkataba wake katika klabu hiyo unamalizika mwaka 2021.
Alikuwa akichezea klabu ya Lyngby BK, ambapo alikuwa amekua kutoka kwenye timu ya vijana tangu ajiunge nao akiwa na miaka 14, kabla ya kuhamia Ujerumani, uhamisho uliogharimu £1.17.
Alikuwa ameanza uchezaji wake akiwa angali mdogo katika klabu ya BK Skjold.
Mchezaji huyo ambaye kimo chake ni futi 6 inchi 4 anatumai kwamba kucheza katika Kombe la Dunia kutamfanya kufahamika zaidi Ulaya.
Wolfsburg na Borussia Monchengladbach ni miongoni mwa klabu ambazo zimeonesha nia ya kumnunua.

Kikosi cha Denmark

Walinda lango: Kasper Schmeichel (Leicester), Frederik Ronnow (Brondby), Jonas Lossl (Huddersfield).
Mabeki: Simon Kjaer (Sevilla), Mathias Jorgensen (Huddersfield), Andreas Christensen (Chelsea), Henrik Dalsgaard (Brentford), Jannik Vestergaard (Borussia Monchengladbach), Jens Stryger Larsen (Udinese), Jonas Knudsen (Ipswich).
Viungo wa kati: Christian Eriksen (Tottenham), Lasse Schone (Ajax), Michael Krohn-Dehli (Deportivo La Coruna), Thomas Delaney (Werder Bremen), William Kvist (FC Copenhagen), Lukas Lerager (Bordeaux).
Washambuliaji: Andreas Cornelius (Atalanta), Kasper Dolberg (Ajax), Martin Braithwaite (Middlesbrough), Nicolai Jorgensen (Feyenoord), Pione Sisto (Celta Vigo), Viktor Fischer (FC Copenhagen), Yussuf Poulsen (RB Leipzig).

Kusaidia Denmark kufuzu kwa Kombe la Dunia
Poulsen alisaidia Denmark kufuzu kwa Kombe la Dunia kupitia mechi za muondoano za baada ya makundi dhidi ya Jamhuri ya Ireland.
Denmark walishinda kwa jumla ya 5-1, ambapo wachambuzi wanasema kasi yake ilichangia kuwatatiza wachezaji wa Jamhuri ya Ireland.

Ndoto ya Patrick Mtiliga Kombe la Dunia
Kwa sasa Yussuf Poulsen amefikia ufanizi wa mchezaji mwingine mwenye asili kama yake, Patrick Jan Mtiliga ambaye kwa sasa amestaafu soka.
Mtiliga alizaliwa 28 Januari 1981 ambapo baba yake alikuwa Mtanzania.
Alikuwa beki na alichezea timu ya taifa ya Denmark mechi sita na alikuwa ameteuliwa kikosi cha wachezaji 23 wa kucheza Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini. Hata hivyo hakufanikiwa kucheza. Denmark waliondolewa kwenye michuano hiyo hatua ya makundi baada ya kumaliza nafasi ya tatu kundi lao.
Katika soka ya kulipwa, alichezea klabu kadha za Denmark na Uholanzi kabla ya kuhamia Malaga ya Uhispania mwaka 2009. Mwanzoni mwa mwaka 2010, aliumizwa kwneye pua na Cristiano Ronaldo wa Real Madrid jambo lililomfanyakutocheza wiki tatu.
Aliondoka Malaga Juni 2011 baada ya mkataba wake kumalizika na kujiunga na FC Nordsjælland ya Denmark ambapo alimalizia uchezaji wake mwaka 2015 baada ya kuwachezea mechi 150 na kufunga mabao 5.

Comments