Featured Post

WIZARA YA KILIMO YANG'ARA TUZO ZA UTEKELEZAJI WA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI 2017/2018

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba Tuzo ya Uwezeshaji Kiuchumi, baada ya Wizara ya kilimo kuibuka mshindi wa pili katika kundi la Wizara, Wakala na Idara za Serikali kwenye  Kongamano la Tatu la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi lililofunguliwa na Waziri Mkuu katika ukumbi wa LAPF Jijini Dodoma Juni 18, 2018. (Picha Na Mathias Canal Wizara ya Kilimo)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionesha Taarifa ya Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya Mei 2017 Mpaka Mei 2018  baada ya kuizindua katika Kongamano la Tatu la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi lililofanyika kwenye ukumbi wa LAPF jijini Dodoma Juni 18, 2018. Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama na kulia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Dkt. John Jingu.
Baadhi ya washiriki wa Kongamano la Tatu la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua Kongamano hilo kwenye ukumbi wa LAPF jijini Dodoma Juni 18, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na baadhi ya viongozi walioshiriki katika Ufunguzi wa Kongamano la Tatu la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi wakipiga makofi baada ya Waziri Mkuu kufungua Kongamano hilo kwenye ukumbi wa LAPF Jijini Dodoma Juni 18, 2018. kutoka kushoto ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu  Profesa, Faustine Kamuzora, Meya wa jiji la Dodoma Profesa Davis Mwamfupe, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Anthony Mtaka, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi  Dkt. John Jingu, Mkuu wa mkoa wa Dodoma,  Dkt. Binilith Mahenge na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Beng'i Issa.

Na Mathias Canal-WK, Dodoma 

Wizara ya kilimo imeipuka Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwa wizara iliyoshika nafasi ya pili kama wizara iliyofanya vizuri dhidi ya taasisi nyingine za serikali zikiwemo wizara katika utekelezaji wa shughuli na programu mbalimbali za uwezeshaji wananchi kiuchumi, kuongeza ujuzi na kuimarisha uratibu wa shughuli za uwezeshaji katika kipindi cha mwaka 2017/2018.

Kwa niaba ya wizara ya kilimo tuzo hiyo imepokelewa na Waziri wa kilimo Dkt Charles Tizeba ambaye amesema kuwa wizara yake ilistahili kushika nafasi ya kwanza kwani imefanya majukumu makubwa kupitia nafasi yake ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Tuzo hiyo dhidi ya Wizara zilizofanya vizuri, Taasisi za serikali, na wajasiriamali zimetolewa leo (Jumatatu, Juni 18, 2018) na waziri Mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa  wakati akifunguaKongamano la Tatu la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa LAPF, Jijini Dodoma.
Katika hafla hiyo WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema taarifa ya Kongamano la Uchumi la Dunia la mwaka 2018 inaonesha kuwa Tanzania inaongoza kwa kuwa na uchumi jumuishi miongoni mwa nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Amesema hali hiyo, imetokana na Tanzania kufungua fursa za ujasiriamali ambapo kuna zaidi ya biashara milioni tatu zinazokuwepo kila mwaka, lengo la nchi ni kuhakikisha kuwa uchumi unakua na unamgusa kila Mtanzania hususan mwananchi wa kawaida. 
Waziri Mkuu ameongeza kwamba Serikali inaamini kuwa uchumi wa viwanda ukiimarika uchumi utakuwa kwa kasi kubwa na matokeo yake yataonekana wazi kwa kupanua wigo wa ajira, soko la huduma na shughuli nyingine za kiuchumi. 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema suala la uchumi wa viwanda kuelekea uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 ni moja ya ajenda muhimu ya Serikali ya Awamu ya Tano, hivyo amezitaka sekta zote zihakikishe zinatoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa viwanda.

Wakala wa barabara nchini ndio umeongoza kwa kushika nafasi ya kwanzailiyofanya vizuri dhidi ya taasisi nyingine za serikali huku vigezi vilivyotumika kuwapata washindi ikiwa ni pamoja na kutengeneza mazingira wezeshi kwa watanzania kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi katika mwaka wa fedha 2017/2018 kwa mabadiliko ya sera, sheria, kutengeneza kanuni, mikataba, kujenga uwezo n.k

Kongamano hilo lililoandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bibi Jenista Mhagama, Waziri wa Kilimo Dkt Charles Tizeba, Waziri Viwanda, Biashara na Uwekezaji Bw. Charles Mwijage na Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Bw. Suleiman Jafo.

Wengine ni Wakuu wa Mikoa mbalimbali, Makatibu Wakuu wa Wizara, Wakuu wa Wilaya ya Mkoa wa Dodoma, Makatibu Tawala wa Mikoa, Mwenyekiti na Wajumbe wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi,Wakurugenzi wa Halmashauri za Mamlaka za Serikali za Mitaa,

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bibi Beng’ Issa, wadhamini wa Kongamano hilo na Wawakilishi kutoka katika taasisi mbalimbali za Serikali na Sekta binafsi.

Comments