Featured Post

'SPIDERMAN' ALIYEMUOKOA MTOTO UFARANSA AREJEA KWAO MALI


BAMAKO, MALI
MHAMIAJI raia wa Mali, Mamoudou Gassama, ambaye alipata umaarufu kote duniani mwezi uliopita wakati alikwea jengo mjini Paris, Ufaransa kumukoa mtoto, amesema amefurahishwa sana kurudi kwao Mali kutembea.
"Nina furaha sana. Nina furaha sana sana kwa sababu kila mtu alikuja uwanja wa ndege na kisha nikamuona baba yangu na watu wote wa familia yangu. Sikuwa nimemuona baba yangu kwa miaka tisa," aliiambia BBC.

Video ya Mamoudou Gassama akimuokoa mtoto ilisambaa sana kwenye mitandao ya kijamii.
Alivuka kutoka kwenye ubaraza mmoja hadi mwingine kwa muda wa chini ya dakika moja akamvuta mtoto huyo aliyekuwa amekwama na kumsalimisha.
Gassama, 22, alivuka bahari ya Mediterranean kwa mashua ya wahamiaji mwezi Septemba 2014.
Alijiunga na ndugu yake nchini Ufaransa na kufanya kazi sehemu ya ujenzi kama kibarua.
Tarehe 26 mwezi Mei, alimuona mtoto mdogo akining'inia kutoka ghorofa ya nne kwenye jengo moja mjini Paris.
Alichukua hatua na kukwea jengo hilo na kumuokoa mtoto huyo kwa miaka mine. Alinaswa kwenye video na watu waliokuwa chini na kupewa jina "Spiderman".
"Sikuogopa. mimi ni kama mtu yeyote yule. Nililipata ujasiri. Ulitoka kwa Mungu. Mungu aliniokoa," alisema.
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, binafsi alimshukuru Gassama na kumuahidi kuwa atapa uraia wa Ufaransa.
Wiki ijayo anatarajiwa kuanza mafunzo kwenye idara ya zima moto mjini Paris.
"Nimefanya uchunguzi wa kiafya. Nitasaini mkataba wangu tarehe 28. Kisha nitaanza mafunzo ya miezi 10," Gassama aliiambia BBC.
Gassama anayetoka kijiji karibu na Kayes magharibi mwa Mali, atakaa nchini Mali kwa muda wa siku tatu na atakutana na Rais Ibrahim Boubakar Keita.
Meya wa Paris, Anne Hidalgo, pia alisifu sana ushujaa wa mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 22, na akasema alimpigia simu kumshukuru.
Alimuelezea kama "Spiderman wa 18", akimaanisha wilaya nambari 18 ambako uokoaji huo ulifanyika mjini Paris.
"Hongera kwa Mamoudou Gassama kwa tendo lake la ujasiri la kumuokoa mtoto," ulisema ujumbe wa Twitter wa Hidalgo.
"Alinielezea kwamba alikuwa amewasili kutoka nchini Mali miezi michache iliyopita akiwa na ndoto ya kujenga maisha yake hapa.
"Nilimjibu kwamba ishara yake hii ya ushujaa ni mfano kwa raia wote na kwamba Jiji la Paris bila shaka litakuwa tayari kumuunga mkono katika juhudi zake za kuishi Ufaransa.


Comments