- Get link
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- Other Apps
John Bocco, Erasto Nyoni na Emmanuel Okwi wote wanawania tuzo ya Mchezaji Bora 2017/2018.
NA MWANDISHI WETU
NYOTA watatu wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba, ndio walioteuliwa
na Kamati ya Tuzo za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), kuwania tuzo ya mchezaji bora msimu
wa 2017/2018.
Taarifa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imesema kwamba,
wachezaji watatu waliobaki katika kinyang'anyiro hicho ni Emmanuel Okwi, John
Bocco na Erasto Nyoni wote wa Simba.
Msemaji wa TFF, Cliford Ndimbo, alisema katika taarifa hiyo
kwamba, Kamati ya Tuzo hiyo ya Mchezaji Bora imeandaa utaratibu wa kupiga kura
kuwashirikisha Wahariri wa Habari za Michezo, manahodha wa timu za Ligi Kuu ya
Vodacom na makocha wa timu za Ligi Kuu.
"Kamati imekamilisha uteuzi wa wachezaji watakaowania
tuzo katika kategori mbalimbali kwenye sherehe hizo za Tuzo ya Mchezaji Bora wa
VPL itakayofanyika ukumbi wa Mlimani City, Dares Salaam Juni 23, mwaka huu,"
ilisema taarifa hiyo.
Tuzo 16 zinatarajiwa kutolewa siku hiyo, ambapo baadhi ni za
kikanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara, ambazo tayari washindi wake wamefahamika,
ambazo ni bingwa, mshindi wa pili, mshindi wa tatu, mshindi wa nne na mfungaji
bora.
"Ukiacha tuzo hizo tano za kikanuni, zipo tuzo 10
ambazo zimefanyiwa kazi na Kamati ya Tuzo kulingana na takwimu mbalimbali za
ligi hiyo, ambapo tuzo moja nyingine ya Mchezaji Bora chini ya umri wa miaka 20
(Tuzo ya Ismail Khalfan), inayohusisha vikosi vya vijana vya timu za Ligi Kuu
yenyewe inaendelea kufanyiwa kazi kwa vile mashindano yanaendelea mkoani Dodoma
na itakapokamilika watatangazwa wateule watatu," ilisema taarifa hiyo.
Tuzo nyingine zitakazotolewa siku hiyo ni Timu yenye Nidhamu
inayowaniwa na Kagera Sugar, Simba na Mtibwa Sugar, wakati Mchezaji Bora
Chipukizi inawaniwa na Shaaban Idd Chilunda, Yahya Zayd (Azam) na Habibu
Kiyombo (Mbao).
Mwamuzi Msaidizi Bora inawaniwa na Helen Mduma, Mohammed
Mkono na Ferdinand Chacha, wakati Mwamuzi Bora wateule ni Elly Sasii, Jonesia
Rukyaa na Hans Mabena.
Tuzo ya Kipa Bora wanaowania ni Aron Kalambo (Prisons),
Aishi Manula (Simba) na Razack Abalora (Azam), huku Kocha Bora wateule ni
Abdallah Mohamed (Prisons), Zuberi Katwila (Mtibwa) na Pierre Lechantre
(Simba).
Goli Bora ni Seif Karihe (Lipuli) na Shaaban Idd Chilunda
(Azam) ambaye ameingiza mabao mawili.
Tuzo nyingine ambazo zitatolewa Juni 23 ni Mchezaji wa
Heshima ambayo licha ya kuwa kamati ina majina ya wachezaji mbalimbali inaoona
wanastahili tuzo kwa mwaka husika, lakini haitangazi majina hayo, isipokuwa
hutaja jina la aliyepewa tuzo siku ya sherehe.
Pia kutakuwa na kikosi bora (VPL Best Eleven), ambacho
kitatangazwa siku ya sherehe.
Comments
Post a Comment