Featured Post

MWANAMUZIKI XXXTENTACION AUAWA KWA KUPIGWA RISASI FLORIDA, MAREKANI



FLORIDA, MAREKANI
MWANAMUZIKI wa nyimbo za rap Marekani XXXTentacion, ambaye alipata umaarufu kwa haraka kupitia albamu zake mbili ameuawa kwa kupigwa risasi akiwa na miaka 20.
Alikuwa anaondoka kwenye duka la kuuza pikipiki kusini mwa Florida Jumatatu pale mtu mwenye bunduki alipomfyatulia risasi.

Polisi katika tarafa ya Broward wanasema XXXTentacion, ambaye jina lake Janseh Onfroy, alikimbizwa hospitalini lakini akathibitishwa kufariki.
Alikuwa mara nyingi akielezwa kama mmoja wa wanamuziki wa rap wenye matata zaidi.
Alikuwa pia amekabiliwa na mashtaka ya kumshambulia mpenzi wake.
Rapa huyo, ambaye alipata umaarufu kwa kupakia nyimbo zake katika mtandao wa SoundCloud, alikuwa anatazamwa na wengi kama kielelezo cha mtu kufanikiwa kupitia kipaji chake.
Wapenzi wa muziki wake na wanamuziki nyota wa hip-hop wamekuwa wakituma salamu za rambirambi kuomboleza kifo chake.
Liwali wa tarafa hiyo amesema Onfroy alikuwa anaondoka kwenye duka hilo muda mfupi kabla ya saa kumi alasiri pale washukiwa wawili waliokuwa na silaha walipofika kwake.
Mmoja wao anadaiwa kumpiga risasi kabla ya wote wawili kukimbia eneo la tukio Deerfield Beach, takriban 69km kaskazini mwa Miami wakitumia gari aina ya SUV la rangi nyeusi.
Wachunguzi wanasema huenda kilikuwa kisa cha wizi wa mabavu.
Video iliyopakiwa kwenye mitandao ya kijamii ilimuonyesha mwanamuziki huyo akiwa amelala ndani ya gari lake baada ya kupigwa risasi.
Mmoja wa walioshuhudia ameambia tovuti ya TMZ kwamba milio kadhaa ya risasi ilisikika nje ya duka hilo.
Rapa huyo, ambaye nyimbo zake ni pamoja na SAD! na Moonlight, zilipata umaarufu sana baada yake kutoa albamu yake ya kwanza kwa jina 17 Agosti mwaka jana.
Alitoa albamu nyingine kwa jina ? ambayo ilianza ikiwa kwenye chati ya nyimbo 200 maarufu mwezi Machi na nyimbo za albamu hiyo zilikuwa zimesikilizwa mara milioni mia kadhaa mtandaoni.
Alizungumzia mambo kama vile mfadhaiko na msongo wa mawazo na alisifiwa na baadhi ya wanamuziki nyota wa rap.
Lakini uimbaji wake ulikumbwa na utata, huku akituhumiwa kwa makosa ya kuwashambulia na kuwapiga watu.
Alikuwa anakabiliwa na mashtaka 15 ya kuwashambulia watu kufikia wakati wa kifo chake, shtaka moja likiwa la kumpiga mjamzito.
XXXTentacion alikulia katika maisha ya dhiki na alifukuzwa shuleni kwa sababu ya kupigana, lakini alielekeza nguvu zake na ghadhabu kwenye muziki.
Kufikia Oktoba 2017, alikuwa ametia saini mkataba wa muziki uliodaiwa kuwa wa thamani ya Dola milioni 6.
Kanye West amesema: "Sikukwambia jinsi ulivyonihamasisha ulipokuwa hapa nasi."
Mchezaji soka wa Liverpool na England Daniel Sturridge amesema leo ni "siku ya huzuni kwa muziki."
Rapa J Cole pia ametuma salamu zake za rambirambi.


Comments