Featured Post

MPINA AOMBA RADHI BUNGE SAKATA LA SAMAKI



WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, ameliomba radhi Bunge kwa kitendo cha maofisa wake kuingia ndani ya mgahawa wa kisha kupima samaki waliopikwa kwa ajili ya wabunge bila kuzingatia taratibu na kanuni za afya.
Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya maofisa hao kuingia kwenye mgahawa wa Bunge bila utaratibu na kupima samaki waliopikwa, hali ambayo ilizua kizaazaa na ksuababisha wabunge kulijadili kwa nusu saa.

Hatua hiyo imetokana na Naibu Spika, Dkt. Tulia Ackson, kuiagiza serikali kutoa kauli bungeni kabla ya kuchukua uamuzi kama jambo hilo lipelekwe kwenye Kamati ya Kinga, Hadhi na Madaraka ya Bunge ama la.
Akitoa kauli hiyo ya radhi jana, Mpina alisema, Juni 19, 2018 alipokuwa kwenye mgahawa huo alibaini uwepo wa samaki aina ya Sato wanaouzwa wasiokidhi viwango vya kisheria.
Alisema baada ya kuona hivyo alimuagiza Katibu wake kwenda kujiridhisha kama ni kweli ama la ambapo baada ya kufanya hivyo waligundua kuwa samaki hao walikuwa na urefu wa chini ya sentimeta 25.
"Nikamuagiza katibu wangu katika uhakiki unaoendelea wakaguzi wajiridhishe katika mgahawa wa Bunge ambapo walibaini baadhi ya samaki ni wachanga waliokuwa na urefu chini ya sentimeta 25.
"Baada ya kukiri kosa mmiliki wa mgahawa huo alitozwa faini ya Shs. 300,000 na samaki hao wasioruhusiwa waliondolewa kwenye mgahawa huo," alisema Mpina.
Mpina alikiri kuwa, watumishi hao katika kutekeleza wajibu huo waliingia eneo la Bunge bila kibali cha kuwawezesha kufanya kazi hiyo na kupima chakula kilichopikwa.
"Kwa sababu hiyo, wizara inaliomba radhi Bunge lako tukufu na ninasisitiza kuwa wizara yangu haikuwa na lengo lolote la dharau kwa Bunge lako tukufu na Ofisi ya Spika.
"Pia naliomba Bunge lako tukufu liendelee kuunga mkono jitihada za wizara yangu katika kuendelea kulinda rasilimali za nchi," alieleza.
Baada ya kuomba radhi, Spika Job Ndugai, alisema licha ya maelezo mazuri ya waziri, alimueleza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa namna ambavyo Bunge lilisikitishwa na kitendo hicho.
Alisema, endapo mabunge mengine yakisikia waziri amefanya kitendo hicho ni dharau ya hali ya juu.
"Hata panapokuwa na kosa la jinai linafanyika katika eneo la Bunge, RPC anapaswa kunifahamisha na sisi si kazi yetu kulinda jinai, sisi hatulindi wahalifu, lakini lazima tutaarifiane,” alisema.
Spika aliongeza: "Mtu anaponunua samaki kilo 100, kwa akili ya kawaida watu wananunua samaki kwa kilo si kwa futi. Halafu samaki mwenyewe ameshakuwa kitoweo. Sasa hii sheria ya kupima vitoweo itabidi tuzisome vizuri.
"Hivi tunataka watu wafunge milango ndiyo wale samaki? Yani samaki mbichi aliyevuliwa atafika Dodoma kwa muda gani, afanyiwe process (matayarisho) bado urefu wake huo huo wakati ameshapikwa?
"Halafu wapimaji wenyewe wanapima mikono haina hata groves (mipira ya kuvaa mikononi), wanashikashika samaki na wamealika waandishi wa habari, wamejaa zaidi ya 20 kwenye chumba kimoja na baada ya pale wamerusha kwenye mitandao kama kuliweka Bunge mahali pasipostahili.
"Kwa kawaida ukikasirishwa sana na jambo lazima usamehe kwa hiyo naomba waheshimiwa wabunge, tusamehe," alihitimisha.

Comments