Featured Post

KOMBE LA DUNIA 2018: RUSSIA YAIKUNYUGA SAUDI ARABIA 5-0


MOSCOW, RUSSIA
WENYEJI wa fainali za Kombe la Dunia 2018, Russia, jana walianza ufunguzi wa mashindano hayo kwa ushindi mnono baada ya kuichakaza Saudi Arabia kwa jumla ya mabao 5-0.

Licha ya sherehe za ufunguzi kukosa shamra shamra nyingi kwenye Uwanja wa Luchniki jijini Moscow, lakini kikosi cha kocha Dimitry Cherchesov kilionyesha nia ya dhahiri ya kutaka kufuzu kutoka kwenye Kundi A kutokana na mabao ya Yuri Gazinskiy, Denis Cheryshev aliyepachika mawili, Artem Dzyuba na Aleksandr Golovin.
Hata hivyo, wenyeji walimpoteza Alan Dzagoev ambaye aliumia vibaya kwenye mechi hiyo.
Gazinskiy alifunga bao la kwanza - la kwake katika kikosi hicho na kwanza kwa mashindano hayo - katika dakika ya 12, akiruka juu kuunganisha krosi kutoka wingi ya kushoto na kumwacha Abdullah al-Mayouf akiwa hana namna ya kumzuia.
Cheryshev baadaye aliingia baada ya Dzagoev kuumia msuli, na katika dakika ya 43 Cheryshev akapachika bao la pili na kuwafanya wenyeji waende mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-0.
Katika kipindi cha pili, Artem Dzyuba akapachika bao la tatu katika dakika ya 71 akipachika kwa kichwa muda mfupi tu baada ya kuingia uwanjani.
Wakati mpira ukielekea mwisho, Cheryshev akapachika bao la nne kwa guu lake la kushoto kunako dakika ya 90, lakini katika dakika za nyongeza, Aleksandr Golovin akafunga la tano kwa mpira wa adhabu uliokwenda moja kwa moja nyavuni bila kuguswa.
Timu nyingine zinaanza kampeni zao leo Ijumaa, ambapo Misri itapambana na Uruguay jijini Ekaterinburg katika mechi ya kwanza.
Russia itarejea uwanjani Jumanne kucheza na Misri jijini St Petersburg, kabla ya kukamilisha mechi zao na makundi mjini Samara dhidi ya Uruguay Juni 25.
 

Comments