Featured Post

CROATIA YAMTIMUA MSHAMBULIAJI WAKE KUTOKA KOMBE LA DUNIA



MOSCOW, RUSSIA
MSHAMBULIAJI wa Croatia, Nikola Kalinic, amefukuzwa katika fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi baada ya kukataa kuingia uwanjani wakati wa mabadiliko ambapo Croatia ilishinda Nigeria 2-0.

Nafasi ya mchezaji huyo wa miaka 30 haitachukuliwa na mtu mwingine ikimaanisha kuwa kikosi kitabaki na wachezaji 22 kwenye Kombe la Dunia.
Kalinic, mchezaji wa AC Milan, anasema ana jereha la mgongo baada ya kulalamikia tatizo hilo wakati wa mechi ya kirafiki na Brazil.
Kocha Zlatko Dalic alisema: "Ninataka wachezaji wangu wawe sawa na tayari kucheza."
Kalinic ambaye aliichezea Blackburn Rovers kati ya mwaka 2009 na 2011 amefunga mabao 15 katika mechi 41 alizoichezea Croata.
"Wakati wa mechi na Nigeria, Kalinic alikuwa akifanya mazoezi na alistahili kucheza kipindi cha pili," Dalic alisema.
Lakini akasema kuwa, hakuwa tayari kutokana na matatizo ya mgongo.
Croatia watacheza na Argentina siku ya Alhamisi na kumalizia kundi lao la D dhidi ya Iceland Jumanne tarehe 26.
Wachezaji wengine watano waliohama Kombe la Dunia mapema:

Willie Johnston (Scotland)
Mchezaji huyo wa West Brom alifukuzwa kutoka fainali za Kombe la Dunia 1978 huko Argentina na Shirikisho la Kandanda la Scotland baada ya kupatikana na hatia ya kutumia madawa ya kuongeza nguvu za mwili.

Roy Keane (Jamhuri ya Ireland)
Kuondoka kwa kiungo huyo wa kati wa Manchester United kutoka kambi ya mazoezi ya Jamhuri ya Ireland ilikuwa moja ya nyakati zinazokumbukwa sana wakati wa Kombe la Dunia la mwaka 2002.
Hakufurahishwa na jinsi Ireland ilivyofanya maandalizi yake hali iliyosababisha kuwepo majibizano na kocha Mick McCarthy mbele ya wachezaji wengine.
Licha ya kujiandaa kucheza mechi ya ufunguzi na Cameroon, Keane alibaki akitembea na mbwa wake kwenye mitaa ya Cheshire.

Diego Maradona (Argentina)
Nyota huyo wa Argentina alitimuliwa kutoka kwa Kombe la Dunia la mwaka 1994 nchini Marekani kabla ya mechi ya mwisho ya makundi na Bulgaria.
Alikuwa awali ameiongoza Argentina kwenda Kombe la Dunia la mwaka 1986 alipoipatia taji na mwaka 1990 ambapo walipoteza dhidi ya Ujerumani kwenye fainali.
Maradona alifunga wakati wa ushindi wa mabao 4-0 kabla ya kupatikana na kosa la kutumia madawa ya kuongeza nguvu za mwili na kufikisha kikomo cha taaluma yake.

Nicolas Anelka (Ufaransa)
Mshambuliaji huyo wa Ufaransa aliondolewa kutoka kikosi cha taifa nchini Afrika Kusini baada ya kutofautiana na kocha.
Mshambuliaji huyo ambaye wakati huo alikuwa akiichezea Chelsea alimshambulia kwa maneno meneja wakati wa kipindi cha mapumziko wakati wa mechi ya na Mexico mwaka 2010 walipofungwa mabao 2-0.
Alikataa kuomba msamaha na licha ya wachezaji wengine kulamika jinsi alivyotendwa, aliamrishwa kurudi nyumbani na Shirikisho la Soka Ufaransa na kupigwa marufuku ya mechi 18.

Zlatko Zahovic (Slovenia)
Roy Keane hakuwa mchezaji pekee kuondoka Kombe la Dunia la mwaka 2002 baada ya mchezaji wa Slovenia, Zahovic kumfuata nyuma.
Kiungo huyo wa Benfica wakati huo alikuwa na tofauti na kocha Srecko Katanec baada ya kumuondoa uwanjani wakati wa mechi waliyofungwa 3-1 na Hispania ambapo shirikisho la kandanda liliamua kumtimua mapema.

Comments