- Get link
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- Other Apps
HOTUBA YA
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO,
MHESHIMIWA DKT. PHILIP I. MPANGO (MB),
AKIWASILISHA BUNGENI
MAPENDEKEZO
YA SERIKALI KUHUSU MAKADIRIO
YA
MAPATO NA MATUMIZI KWA
MWAKA 2018/19
I.
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa
hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kupitisha Makadirio ya
Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2018/19. Bajeti hii inawasilishwa kwa
kuzingatia matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,
Ibara ya 137 ikisomwa pamoja na Sheria ya Bajeti namba 11 ya mwaka 2015 kifungu
cha 26.
2.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na
hotuba hii, ninawasilisha vitabu vinne vya bajeti. Kitabu cha Kwanza ni
Makadirio ya Mapato; Kitabu cha Pili ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa
Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali; Kitabu cha Tatu
ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za
Serikali za Mitaa; na Kitabu cha Nne ni Makadirio ya Matumizi ya Maendeleo kwa
Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na
Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka
2018 pamoja na Muswada wa Sheria ya Matumizi ya Serikali wa mwaka 2018 ambayo
ni sehemu ya bajeti hii.
3.
Mheshimiwa
Spika, ni
heshima kubwa na upendeleo wa hali ya juu kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu
kuwasilisha bajeti ya tatu ya Serikali ya awamu ya tano. Hivyo, namshukuru
kwanza Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuijalia nchi yetu neema nyingi, utulivu na
amani na kwa kuniwezesha kuwasilisha bajeti kuu ya Serikali kwa wananchi wa
Tanzania kwa mara ya tatu. Pili napenda kumpongeza kwa dhati Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kiongozi wetu
shupavu; kiongozi anayeaminiwa na kutumainiwa na wananchi, hasa wanyonge; kiongozi
anayechukia na kupiga vita rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma kwa
vitendo; na Rais anayejipambanua kwa kufanya maamuzi magumu ya kulinda
rasilimali za Taifa. Ninampongeza kwa kazi kubwa ambazo ameendelea kuzifanya
tangu aliposhika hatamu za uongozi wa Taifa letu, ambazo zimepelekea kupatikana
kwa mafanikio makubwa sana katika kipindi kifupi cha miaka miwili na nusu tu ya
utawala wake. Napenda niyataje mambo kumi tu aliyothubutu kutenda na kuiletea
nchi mafanikio makubwa:
(i)
Kuhamishia makao makuu
ya Serikali Dodoma:
Ametekeleza ndoto ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na uamuzi
wa Chama Tawala wa mwaka 1972 wa kuhamishia makao makuu ya Serikali Dodoma.
Aidha, kwa mamlaka aliyo nayo amepandisha hadhi ya iliyokuwa Manispaa ya Dodoma
kuwa Jiji kuanzia tarehe 26/4/2018;
(ii)
Kujenga ukuta kuzunguka
mgodi wa Tanzanite Mirerani: Amejenga ukuta wenye mzingo wa kilomita 24.5
kuzunguka machimbo ya madini ya Tanzanite Mirerani, Wilaya ya Simanjiro
uliogharimu shilingi bilioni 5.42. Lengo likiwa ni kudhibiti uchimbaji na
uuzaji holela wa madini hayo yanayopatikana Tanzania pekee na kuliingizia Taifa
mapato. Katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi, 2018
Serikali imefanikiwa kukusanya mrabaha wa shilingi milioni 714.6. Kati ya kiasi
hicho, shilingi milioni 614.6 kilitokana na makusanyo kutoka kwa wachimbaji
wadogo. Kiasi hicho kilichokusanywa kutoka kwa wachimbaji wadogo kinazidi jumla
ya makusanyo ya mrabaha wa miaka mitatu iliyopita. Kiasi kilichokusanywa na Serikali
kilikuwa shilingi milioni 116.8 (2015), shilingi milioni 71.8 (2016), na
shilingi milioni 147.1 (2017);
(iii) Kudhibiti uuzaji wa makinikia nje ya nchi na kutunga sheria
kuwezesha nchi kunufaika na rasilimali zake: Amezuia usafirishaji wa makontena 277 ya
makinikia nje ya nchi yenye thamani ya kati ya shilingi bilioni 829.4 na
shilingi bilioni 1,438.8 na kuagiza kutungwa kwa sheria mpya za mfano katika
Afrika kuwezesha nchi zenye maliasili kunufaika na rasilimali hizo. Sheria hizo
ambazo zilipitishwa na Bunge lako Tukufu ni:
(a) Sheria ya Mamlaka ya nchi kuhusu Umiliki wa Maliasili ya
mwaka 2017 (The Natural Wealth and
Resources - Permanent Sovereignity Act, 2017);
(b)
Sheria ya
Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za
Nchi ya Mwaka 2017 (The Natural Wealth
and Resources Contracts (Review and
Re- Negotiation of Unconscionable Terms) Act, 2017; na
(c) Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali ya mwaka 2017 (The Written Laws - Miscellaneous Ammendments
) Act, 2017.
(iv)
Kutoa elimu msingi bila ada na kuongeza bajeti ya dawa, vifaa tiba na
vitendanishi kwa zaidi ya mara nane: Ametoa elimu msingi
bila ada ambapo kila mwezi Serikali inalipa shilingi bilioni 20.8. Kutokana na
hatua hiyo, uandikishwaji wanafunzi wa darasa la kwanza umeongezeka kutoka
watoto 1,568,378 mwaka 2015 hadi watoto 2,078,379 mwaka 2018. Aidha, uandikishaji wa wanafunzi wa kidato cha
kwanza nao umeongezeka kutoka wanafunzi 448,826 mwaka 2015 hadi wanafunzi
562,695 mwaka 2017. Kadhalika, ameongeza fedha za mikopo ya wanafunzi wa elimu
ya juu ambapo mgao uliotolewa mwaka 2017/18 ni shilingi bilioni 409.9
ikilinganishwa na matumizi halisi ya shilingi bilioni 367.4 mwaka 2015/16. Idadi
ya wanafunzi wanaopata mikopo hiyo imeongeza kutoka wanafunzi 96,589 mwaka 2015
hadi 122,623 mwaka 2017. Katika sekta ya afya, amethubutu kuongeza bajeti kwa
ajili ya kugharamia ununuzi wa dawa, chanjo, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi
kufikia shilingi bilioni 269 mwaka
2017/18 kutoka shilingi bilioni 31 mwaka
2015/16, hivyo kuimarisha huduma za afya;
(v)
Ununuzi wa
ndege mpya kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL): Amefufua
Shirika la Ndege la Tanzania kwa kufanya maamuzi magumu ya kununua ndege mpya
tatu aina ya Bombardier Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja ambazo
tayari ziko nchini na zinafanya safari za ndani. Aidha,
ndege kubwa nyingine tatu (3), moja aina ya Boeing 787-8 Dreamliner yenye uwezo
wa kubeba abiria 262 na ndege mbili aina
ya Bombardier CS 300 zenye uwezo wa kubeba abiria 132 kila moja zitawasili
nchini baadae mwaka huu. Kadhalika, Serikali imekamilisha taratibu za kupata
ndege ya pili kubwa aina ya Boeing 787-8 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba
abiria 262 na malipo ya awali yamekamilika;
(vi)
Kudhibiti
matumizi yasiyo ya lazima, kuondoa watumishi hewa na wenye vyeti vya kughushi: Amedhibiti
matumizi yasiyo ya lazima hususan safari za watumishi wa Serikali nje ya nchi,
kuondoa watumishi hewa 19,708 waliokuwa wanalipwa mshahara wa jumla ya shilingi
bilioni 19.8 kwa mwezi, na watumishi 14,404 wenye vyeti vya kughushi waliokuwa wanalipwa
mshahara wa jumla ya shilingi bilioni 15.5 kwa mwezi, ambazo zote hizo
zimeokolewa. Aidha, chini ya utawala wake, nidhamu katika utumishi wa umma
imeimarika na ameanzisha Mahakama ya mafisadi ili kupambana na mafisadi
wanaonyonya uchumi wa nchi;
(vii)
Ujenzi wa
reli ya kati ya kisasa kwa kiwango cha kimataifa (Standard Gauge Railway – SGR): Ameanza
ujenzi wa reli ya kati ya kisasa kwa kiwango cha kimataifa (Standard Gauge Railway – SGR). Awamu ya kwanza kutoka Dar es
Salaam hadi Morogoro (km 205) na awamu ya pili kutoka Morogoro hadi Makutupora
Dodoma (km 422) tayari zinatekelezwa. Awamu zote mbili zitagharimu takriban
Dola za Marekani bilioni 3.14;
(viii)
Ujenzi wa
mradi wa umeme katika bonde la mto Rufiji: Amefanya
uamuzi wa kuanza ujenzi wa mradi mkubwa wa umeme katika mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) ambao nao ulikuwa
ndoto ya Baba wa Taifa utakaozalisha MW 2,100 utakapokamilika nao umeanza
katika hatua za awali;
(ix)
Kuimarisha
usimamizi wa mapato ya ndani: Ametekeleza ahadi yake kwa
Watanzania kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kudhibiti ukwepaji kodi, hatua
ambazo zimewezesha Serikali kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka wastani wa
shilingi bilioni 850 kwa mwezi hadi wastani wa shilingi tirioni 1.3 kwa mwezi;
(x)
Kuendeleza
umeme vijijini na kusitisha miradi ya wazalishaji binafsi wa umeme (IPPs): Ameendeleza
utekelezaji wa mradi kabambe wa kupeleka umeme vijijini kupitia REA Awamu ya
Tatu kwa ufanisi mkubwa, ambapo ndani ya miaka miwili na nusu ya utawala wake jumla
ya vijiji 557 vimeunganishwa umeme. Vijiji hivyo vimetokana na utekelezaji wa
miradi ya REA II na REA III ya kuongeza msongamano (densification), mkongo (backbone) na ule wa kusafirisha umeme Makambako
- Songea. Aidha, amesitisha miradi ya wazalishaji binafsi wa umeme (Independent Power Producers – IPPs) ambayo
ilikuwa inaigharimu Serikali fedha nyingi. Vile vile, bila yeye mradi wa Bomba
la Mafuta kutoka Hoima (Uganda) hadi bandari ya Tanga usingepatikana na tayari
ujenzi unaendelea;
4.
Mheshimiwa Spika, yapo mambo mengi
sana makubwa (barabara, meli, madaraja, maji, usimamizi wa sekta ya fedha n.k.)
ambayo Jemadari huyu ametekeleza, lakini kwa uchache wa muda siwezi kuyataja
yote. Haya yote ni ushahidi usio na mashaka kwamba Tanzania chini ya Rais
Magufuli imeshika kasi ya maendeleo. Hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania
kuchangia katika jitihada hizi za Mheshimiwa Rais kujenga Tanzania mpya. Maeneo
matatu ya msingi sana kwa kila mwananchi kuwajibika ni: (i) uzalendo kwa nchi
yetu; (ii) kupiga vita wizi, ubadhirifu na ufisadi; na (iii) kufanya kazi kwa
bidii na kulipa kodi.
5.
Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo za dhati kwa Rais wetu,
napenda kumshukuru kwa moyo wangu wote kwa kuendelea kuniamini na kuniongoza katika
kazi zangu za Waziri wa Fedha na Mipango. Hata pale nilipoelemewa na kazi na kulaumiwa
kwamba waziri huyu ni bahili mno katika kutoa fedha na baadhi wakinipaka tope
la kiburi, alinitia moyo. Niliwahi kumuuliza Mheshimiwa Rais kwa nini
alinitwika mimi kazi hii nzito kama msalaba wa zege, tena bila matumaini ya
kutokea mtu mfano wa Simon wa Kirene katika Biblia wa kuja kunipokea mzigo
huu!. Yeye alinijibu kwamba “Mungu
atawatuma malaika wake watakusaidia!” na akaongeza kwamba “lazima watu wachache tuwe tayari kuumia kwa
faida ya Watanzania wengi maskini”. Naomba nikiri kuwa, majibu hayo
yalinichoma na kunikumbusha sala ya wana “Opus
Dei” katika mateso isemayo “Mapenzi
ya Mungu, yenye haki na yanayopendeza sana, yafanyike, yatimizwe, yasifiwe na
kutukuzwa kuliko vitu vyote milele. Amina. Amina.” Baada ya hapo, nilipata amani
ya kuendelea katika utumishi huu. Asante sana Mheshimiwa Rais. Najua unasikiliza!.
6.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Mama Samia Suluhu
Hassan Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kumsaidia Rais
kuongoza Taifa letu kwa hekima na uadilifu. Kadhalika, ninatoa pongezi kwa Mheshimiwa
Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi kwa kuiongoza Zanzibar kwa busara, jambo ambalo
limepelekea wananchi wa Zanzibar kuishi katika hali ya amani na utulivu mkubwa
kwa kipindi cha miaka saba na nusu sasa. Aidha, ninampongeza sana Mheshimiwa
Kassim M. Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia
ni Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, kwa kuwa kapteni hodari wa timu ya Serikali hapa
Bungeni na kwa kumsaidia Rais kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Chama Tawala
CCM ya mwaka 2015 – 2020. Vile vile, ninawapongeza wakuu wa mihimili mingine ya
dola, nikianza na wewe Mheshimiwa Job Yustino Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Kongwa kwa kuliongoza Bunge kwa umahiri;
na Mheshimiwa Profesa
Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa
Tanzania kwa kazi nzuri ya kuongoza chombo cha utoaji haki. Napenda vile vile
kumpongeza Mheshimiwa Balozi Mhandisi John Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi ambaye pia
ni mkuu wa Utumishi wa Umma na Katibu wa Baraza la Mawaziri kwa utumishi
uliotukuka.
7.
Mheshimiwa Spika, ni vema pia niwapongeze waheshimiwa
wenza wa viongozi wakuu wa kitaifa kwa umuhimu wao wa kipekee. Niruhusu niwataje kwa majina yao Mwalimu Janet Magufuli, Bwana Ameir Hafidh Ameir,
Mama Mwanamwema Shein, Mwalimu Mary Majaliwa, Dkt. Fatuma Ramadhani Mganga, na
Mama Marina Papadopoulos Juma. Tunawapongeza na kuwashukuru kwa kuwawezesha
viongozi wetu wakuu wa kitaifa kutekeleza vizuri majukumu yao kwa utulivu,
hamasa na tabasamu kutokana na mapenzi makubwa wanayopata nyumbani.
8.
Mheshimiwa Spika, napenda niwapongeze na
kuwashukuru wakuu wote wa vyombo vya ulinzi na usalama ambao ni Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo; Inspekta
Jenerali wa Polisi, Simon Sirro; Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Ali
Malewa; Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala; Mkurugenzi wa Usalama
wa Taifa, Dkt. Modestus Kipilimba; Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa, Kamishna wa Polisi, Valentino Mlowola; Kamishna Jenerali wa Mamlaka
ya Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Bw. Rogers William Sianga; na Kamishna
Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji Bw. Thobias Andengenye. Mimi na Watanzania wenzangu
tunawapongeza kwa dhati kabisa viongozi hawa, pamoja na makamanda, askari na
watumishi wote wa vyombo hivi nyeti kwa kuendelea kuilinda nchi yetu kwa ushupavu, kudumisha amani na usalama na
kuwawezesha wananchi wote wa Tanzania kufanya shughuli za maendeleo kwa
utulivu. Aidha, ninampongeza Mheshimiwa
Dkt Adelardus Lubango Kilangi kwa kuteuliwa na Rais kuwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, na ninamshukuru kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa Sheria ya Fedha
wa mwaka 2018 na Muswada wa Sheria ya Matumizi wa mwaka 2018.
9.
Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii pia kutoa shukrani mahsusi
kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti inayoongozwa na Mheshimwa Hawa
Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini na Makamu wake Mheshimiwa Jitu V.
Soni, Mbunge wa Babati Vijijini. Maoni na ushauri uliotolewa na Kamati ya
Bajeti wakati wa kuchambua mapendekezo ya bajeti ninayoiwasilisha mbele ya
Bunge lako Tukufu, ulikuwa wa kizalendo na wenye tija. Aidha, ninawapongeza
Wenyeviti, Makamu wenyeviti na wajumbe wa Kamati zote za Kudumu za Bunge kwa
michango yao waliyoitoa kupitia vikao vya kamati za kisekta katika kuboresha
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2018/19 ili kuwapatia
wananchi wa Tanzania huduma bora zaidi.
10. Mheshimiwa
Spika, kama ilivyokuwa mwaka
2017/18, dhima ya bajeti ya mwaka 2018/19 kwa nchi zote wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki itakuwa ni “kujenga uchumi wa viwanda utakao chochea ajira
na ustawi endelevu wa jamii”. Bajeti hii imeandaliwa kwa kuzingatia uhalisia
wa nchi yetu ambao sisi wote tunaufahamu, kwa maana ya changamoto kuu za
kiuchumi na kijamii zinazotukabili, fursa tulizo nazo, mafanikio hadi sasa na
malengo yetu kama Taifa. Naomba nifafanue haya kwa kifupi:
a) Changamoto
(i)
Bado tuna kiwango kikubwa cha umaskini ambapo taarifa kutoka Ofisi ya Taifa
ya Takwimu zinaonesha kiwango cha umaskini kimepungua kidogo kutoka asilimia
28.2 (2011/12) hadi asilimia 26.4 (2015/16). Matarajio ni kuwa Utafiti wa
Matumizi ya Kaya unaoendelea hivi sasa utatupatia taarifa nzuri zaidi ya
kuendelea kupungua kwa umaskini kwa kuzingatia kuwa uchumi wa Taifa umeendelea
kukua kwa kasi ya wastani wa asilimia 7.0 kwa mwaka katika miongo miwili sasa;
(ii)
Ukosefu wa
fursa za ajira hasa kwa vijana, ambapo takwimu zinaonesha kuwa
asilimia 10.4 ya Watanzania hawana ajira. Vile vile kati ya vijana wanaohitimu
masomo yao wapatao 800,000 kila mwaka, uwezo wa Serikali kuajiri ni wastani wa
watu 40,000 tu;
(iii)
Sekta ya
kilimo (inayojumuisha mazao, mifugo na uvuvi) ambayo inaajiri asilimia 66 ya
Watanzania na inachangia asilimia 30 ya Pato la Taifa inaendelea kukua kwa kasi
ndogo ya wastani wa asilimia 3.7 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita
kutokana na uwekezaji mdogo, tija ndogo na kutegemea mvua, sambamba na mchango
mdogo wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa wa asilimia 5.5;
(iv)
Mahitaji makubwa
ya upatikanaji wa huduma muhimu za jamii (hasa maji, afya na elimu bora) na
yanaongezeka kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu (asilimia 3.1 kwa mwaka).
Aidha, hali ya miundombinu ya umeme, usafiri na usafirishaji (barabara, reli,
usafiri wa anga na majini) bado haikidhi mahitaji ya uchumi kukua kwa kasi
zaidi na kugusa wananchi wengi. Mathalani, mtandao wa barabara nchini ni
kilomita 86,472 ambapo ni asilimia 9.7 tu ndiyo za kiwango cha lami. Aidha,
mahitaji ya umeme kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na viwandani bado ni
makubwa ikilinganishwa na uwezo wa uzalishaji. Mitambo iliyopo kwa sasa ina
uwezo wa kuzalisha Megawati 1,424.6 ikilinganishwa na mahitaji ya zaidi ya
Megawati 3,000 ili kuweza kuhimili mahitaji ya uchumi wa viwanda; na
(v)
Wigo mdogo
wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ambapo uwiano wa mapato ya
ndani na Pato la Taifa ni takriban asilimia 15.0 ikilinganishwa na wastani wa
asilimia 17.0 kwa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
b) Fursa
11. Mheshimiwa
Spika, maandalizi ya bajeti hii pia
yamezingatia fursa mbalimbali tulizo nazo katika Taifa letu hususan nguvukazi
kubwa ya Taifa ambao ni vijana; rasilimali na fursa nyingi tulizonazo katika
kilimo (mazao, mifugo, na uvuvi); madini; gesi; vivutio vya utalii; viwanda vya
huduma za kilimo (agri-business); vyanzo mbalimbali vya uzalishaji wa umeme;
biashara na huduma za usafirishaji wa mizigo kwenda nchi jirani.
c) Mafanikio
12. Mheshimiwa
Spika, bajeti hii pia imezingatia
mafanikio tuliyopata hadi hivi sasa ambayo hatuna budi tuyaimarishe na
nitayaeleza kwa muhtasari katika sehemu ya mapitio ya utekelezaji wa bajeti.
d) Malengo
13. Mheshimiwa
Spika, bajeti hii vile vile imeandaliwa
kwa kuzingatia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Mpango wa Pili wa
Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21) na Ilani ya CCM ya mwaka
2015 – 2020. Malengo makuu ni kuondokana na umaskini na kuibadilisha Tanzania kuwa
nchi ya uchumi wa viwanda na kuingia kwenye kundi la nchi zenye kipato cha kati
(Middle Income Countries) ifikapo mwaka 2025.
14. Mheshimiwa
Spika, changamoto, fursa mafanikio
na malengo niliyoyaeleza sasa hivi lazima yaende pamoja na wajibu upande wa
Serikali, sekta binafsi, wadau wengine na mwananchi mmoja mmoja, wa kuzipatia
majibu changamoto hizo na kuchangia ipasavyo katika jitihada za kulipeleka
Taifa letu mbele. Tutafanya hivyo ikiwa kila mwananchi atafanya kazi na kutumia
uwezo wake wote kwa ajili ya maendeleo yake na ya Taifa. Aidha, ni muhimu pia
tuendelee kujenga na kutumia ubia wa kimkakati (harness strategic partnerships). Ujumbe wangu kwa Watanzania
kupitia bajeti hii ni kuwa, lazima tuendelee kufanya chaguo gumu (tough choices) katika kuelekeza
rasilimali kidogo tunazokusanya ili tuweze kuzishinda changamoto hizo zilizoko
mbele yetu. Ukweli ni kuwa, mabadiliko ni magumu na mara nyingi yanapingwa!.
Hivyo, lazima tuwe imara, tukusudie kufanikiwa na tutumie vizuri fursa na uwezo
wa Watanzania, sekta binafsi na Serikali ili kufikia azma yetu.
15. Mheshimiwa Spika,
katika hotuba niliyosoma leo asubuhi, nilieleza kwa kirefu hali ya uchumi wetu
ilivyokuwa katika mwaka 2017, utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa
mwaka 2017/18, mafanikio yetu na changamoto tulizokumbana nazo na niliainisha
pia maeneo ya vipaumbele kwa mwaka 2018/19. Katika hotuba hii nitajikita zaidi
katika masuala ya kibajeti, nikianza na utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2017/18,
hatua muhimu zitakazopewa msukumo zaidi upande wa matumizi katika mwaka ujao wa
fedha, maboresho ya mfumo wa kodi na tozo mbalimbali na mapendekezo ya bajeti
ya mwaka 2018/19.
II.
TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2017/18
Mwenendo wa Mapato
16. Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Aprili, 2018 mapato kutoka vyanzo vyote
yalifikia shilingi trilioni 21.89 sawa na asilimia 69 ya lengo la mwaka la
kukusanya shilingi trilioni 31.71 Mchanganuo wa mapato hayo ni kama ifuatavyo:
A. Mapato ya Ndani
17. Mheshimiwa Spika,
Mapato ya ndani yakijumuisha mapato ya Halmashauri yalifikia shilingi trilioni
14.84 ikilinganishwa na lengo la kukusanya shilingi trilioni 19.98 kwa mwaka sawa
na asilimia 74.3. Kati ya kiasi hicho, makusanyo ya kodi yalikuwa shilingi trilioni
12.61; makusanyo yasiyo ya kodi ni shilingi trilioni 1.79; na makusanyo ya Halmashauri
ni shilingi bilioni 437.6. Kutofikiwa kwa malengo ya ukusanyaji kumetokana na changamoto mbalimbali ikiwa ni
pamoja na:
(i)
Ukwepaji wa kodi;
(ii)
Ugumu wa kutoza kodi wafanya
biashara walioko katika sekta isiyo rasmi kwa vile hawana sehemu rasmi na za
kudumu za kufanyia biashara na hawatunzi kumbukumbu;
(iii)
Mazingira yasiyo rafiki ya
ulipaji kodi na mlolongo wa kodi na tozo, hasa huduma zinazotolewa na mamlaka za udhibiti na
usimamizi (zikiwemo TBS, TFDA, EWURA, TCRA,
OSHA, Zimamoto), viwango vikubwa vya kodi; urasimu katika taratibu za
kulipa kodi, na ugumu na gharama kubwa za kulipa kodi;
(iv)
Matumizi hafifu ya mashine za
kielektroniki za kutolea risiti (EFD);
(v)
Udhaifu katika usimamizi wa
uvunaji wa rasilimali za nchi hasa madini, gesi asilia, misitu, rasilimali
bahari, utalii na ardhi; na
(vi)
Mchango mdogo na utegemezi wa
mashirika ya umma katika bajeti ya Serikali.
B. Mikopo ya Ndani na Nje yenye
Masharti ya Kibiashara
18.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
ilikopa jumla ya shilingi trilioni 4.96 kutoka soko la ndani sawa na asilimia 80 ya
shilingi trilioni
6.17 zilizotarajiwa kukopwa kwa mwaka 2017/18. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 4.13 zilikopwa kwa ajili ya kulipia dhamana na
hati fungani za Serikali zilizoiva (rollover), na shilingi bilioni 832.3
zilikopwa ili kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo. Aidha, Serikali
ilikopa kutoka soko la nje shilingi bilioni 224 sawa na asilimia 14 ya lengo la
kukopa shilingi trilioni 1.6. Fedha hizi zimeelekezwa kwenye utekelekelezaji wa
miradi mbalimbali ya kimkakati. Aidha, mwezi Mei, 2018, Serikali ilipokea mkopo
wa kibiashara kiasi cha shilingi trilioni 1.13.
C. Misaada na Mikopo Nafuu kutoka kwa
Washirika wa Maendeleo
19.
Mheshimiwa Spika, misaada na mikopo nafuu
iliyopokelewa kutoka kwa Washirika wa Maendeleo ilikuwa shilingi trilioni 1.87
sawa na asilimia 47 ya makadirio ya mwaka ya shilingi trilioni 3.97. Kati ya kiasi
hicho, shilingi bilioni 70.2 ni misaada na mikopo nafuu ya kibajeti sawa na
asilimia 7.5 ya makadirio ya shilingi bilioni 941.3, shilingi bilioni 182.9 ni
misaada na mikopo nafuu ya Mifuko ya Kisekta sawa na asilimia 33 ya makadirio
ya shilingi bilioni 556.1, na shilingi trilioni 1.61 ni misaada na mikopo
nafuu ya Miradi ya Maendeleo sawa na asilimia 65 ya makadirio ya shilingi trilioni 2.47.
Mwenendo wa Matumizi
20.
Mheshimiwa
Spika, katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Aprili 2018, Serikali imetoa
jumla shilingi trilioni 21.68 sawa na asilimia 68.4 ya lengo la mwaka la shilingi
trilioni 31.71. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 16.56 zilikuwa kwa ajili
ya matumizi ya kawaida ambazo zinajumuisha shilingi trilioni 5.63 kwa ajili ya
mishahara ya watumishi wa umma na shilingi trilioni 8.42 kwa ajili ya
kugharamia Deni la Serikali na mahitaji mengine ya Mfuko Mkuu.
21.
Mheshimiwa
Spika, hadi kufikia Aprili, 2018 Serikali imetoa jumla ya shilingi trilioni 5.12 kwa ajili
utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo shilingi trilioni 4.35 ni fedha za
ndani na shilingi bilioni 775.8 ni fedha za nje. Hata hivyo, kiasi hiki
hakijumuishi fedha kutoka kwa Washirika wa Maendeleo zilizopelekwa moja kwa
moja kwenye utekelezaji wa miradi ambazo hazikupita kwenye mfumo wa malipo wa
Serikali. Fedha hizi zitajumuishwa pindi taratibu ya kiuhasibu
zitakapokamilika.
22. Mheshimiwa Spika,
naomba nieleze mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka
2017/18 katika kipindi cha Julai 2017 hadi Aprili 2018 kama ifuatavyo:
(i)
Jumla ya shilingi bilioni 59.0
zimetolewa katika Halmashauri za Wilaya 110 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa
vituo vya afya, na shilingi bilioni 24.1 kwa ajili ya ukarabati wa hospitali za
mikoa 24. Aidha, jumla ya shilingi bilioni 125.7 zimetolewa kwa ajili ya
ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi;
(ii)
Kiasi cha shilingi bilioni
156.1 kimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji mijini na vijijini;
(iii)
Kiasi cha shilingi bilioni
409.9 kimetolewa kwa ajili ya miradi ya nishati vijijini, umeme wa jotoardhi,
uzalishaji wa umeme katika vyanzo mbalimbali na usambazaji wa gesi asilia;
(iv)
Katika kutekeleza azma ya
kutoa elimumsingi bila ada na kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu,
Serikali imetoa shilingi bilioni 618.0;
(v)
Serikali imeendelea kutekeleza
ujenzi wa miundombinu ili kupanua fursa za uchumi, kilimo, biashara na viwanda
ikiwemo barabara zinazounganisha mikoa na nchi jirani, barabara zinazopunguza
msongamano katika majiji, barabara za vijijini, reli, viwanja vya ndege, na
bandari. Katika eneo hili kiasi cha shilingi trilioni 1.87 kimetolewa;
na
(vi)
Serikali imeendelea kulipa
malimbikizo ya madai ya watumishi umma, wazabuni, wakandarasi na watoa huduma
ambapo kiasi cha shilingi trilioni 1.17
kimelipwa.
23. Mheshimiwa Spika,
Serikali pia imeendelea kuchukua hatua nyingine zenye lengo la kuimarisha
usimamizi wa bajeti ya Serikali kama ifuatavyo:
a) Deni la Serikali
24. Mheshimiwa Spika,
katika kuhakikisha Deni la Serikali linadhibitiwa na linaendelea kuwa himilivu,
Serikali inaendelea kuzingatia Sheria ya Mikopo, Dhamana, na Misaada SURA 134.
Aidha, Serikali inatekeleza Mkakati wa Muda wa Kati wa Kusimamia Deni unaotoa
dira ya namna bora ya ukopaji ili kuepuka gharama na athari mbalimbali
zinazoweza kujitokeza katika kusimamia deni la Serikali. Katika kudhibiti
kuongezeka kwa gharama za mikopo, Serikali ilijikita zaidi kukopa kwenye mikopo
yenye masharti ya kati (Semi Concessional
Loans) hasa mikopo inayowezesha uagizaji wa vifaa na mitambo kutoka nchi inayokopesha
(Export Credit Agency - ECA) na pale
ilipolazimu, mikopo ya masharti ya kibiashara ilikopwa kwa uangalifu mkubwa
ikiwemo kuhakikisha kwamba mikopo hiyo inatumika kwenye maeneo ambayo
yanachochea ukuaji wa uchumi.
25. Mheshimiwa Spika,
hadi kufikia Aprili 2018, deni la Serikali lilifikia shilingi trilioni 49.65 ikiwa ni sawa na
ongezeko la asilimia 13.4 ikilinganishwa na shilingi trilioni 43.79 Aprili
2017. Kati ya kiasi hicho, deni la ndani
lilikuwa shilingi trilioni 14.05 na deni la nje shilingi trilioni 35.60 sawa na asilimia
71.71 ya deni lote. Ongezeko la deni
hilo limetokana na mikopo ya zamani na inayoendelea kupokelewa yenye masharti
nafuu au kibiashara na malimbikizo ya riba ya Deni la Nje hasa kwenye nchi zisizo wanachama wa kundi la
Paris ambazo Serikali bado inajadiliana nazo kuhusu msamaha wa madeni kulingana na makubaliano na kundi hilo.
26. Mheshimiwa Spika,
Mikopo nafuu kutoka Mashirika ya Fedha ya Kimataifa imeendelea kuwa chanzo
kikubwa cha mikopo kutoka nje ambayo imechangia asilimia 59.6 ya deni lote la
nje. Mikopo yenye masharti ya kibiashara imechangia asilimia 28.5, wakati mikopo
kutoka nchi wahisani imechangia asilimia 11.9. Mikopo hii imetumika kugharamia
miradi mbalimbali ya maendeleo.
27. Mheshimiwa Spika,
Deni la Serikali limekuwa likiongezeka. Hata hivyo deni hilo limeendelea kuwa
himilivu na ukuaji wake unawiana na kasi ya ukuaji wa uchumi wetu. Tathmini ya
uhimilivu wa deni iliyofanyika Novemba 2017 inaonesha kuwa deni ni himilivu kwa
kipindi cha muda wa kati na muda mrefu. Uwiano wa deni kwa thamani ya sasa
(present value) kwa Pato la Taifa ni asilimia 34.4 ikilinganishwa na ukomo wa
asilimia 56; thamani ya deni la nje kwa mauzo ya nje ilikuwa asilimia 81.8
ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 150; thamani ya deni la nje kwa mapato ya
ndani asilimia 117.1 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 250; ulipaji wa deni
la nje kwa mapato yatokanayo na mauzo nje asilimia 9.3 ikilinganishwa na ukomo
wa asilimia 20; na ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mapato ya ndani ulifikia
asilimia 13.3 ikilinganishwa na ukomo wa
asilimia 20. Napenda kusisitiza tena kwamba hakuna dhambi kwa nchi kukopa kwa
busara (prudently). Mambo ya muhimu ya kujiridhisha nayo ni kuwa mikopo hiyo
inatumika kujenga uwezo zaidi wa kuzalisha mali (productive capacity) na
kurejesha mikopo hiyo kwa kuzingatia uwezo wa uchumi kuhimili mzigo wa madeni
(debt sustainability).
b) Kudhibiti Malimbikizo ya Madai
ya Serikali
28. Mheshimiwa Spika,
Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za kupunguza malimbikizo ya madai
ikiwa ni pamoja na kutenga fedha kila mwaka kwenye bajeti kwa ajili ya kulipa
madai yaliyohakikiwa; kuhimiza uzingatiaji wa sheria na kanuni zake kama vile,
Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015; Sheria ya Ununuzi wa Umma SURA 410;
Sheria ya Fedha za Umma SURA 348 na kanuni zake na kutoa miongozo na maelekezo
mbalimbali yakiwemo Waraka Na. 1 wa Mlipaji Mkuu wa Serikali unaotolewa kila
mwaka kuhusu utekelezaji wa bajeti na Mwongozo wa Mpango na Bajeti unaotolewa
kila mwaka.
29. Mheshimiwa Spika,
Katika kukabiliana na changamoto hiyo ya malimbikizo ya madai, Serikali
imeandaa Mkakati wa Kulipa Madeni na Kuzuia
ulimbikizaji wa Madeni. Madai yanayohusika kwenye Mkakati huo ni yale
yaliyozalishwa na Wizara, Idara Zinazojitegemea (MDAs) na Sekretarieti za Mikoa (RSs)
yakiwemo madeni ya Watumishi, Wazabuni na Watoa Huduma, pamoja na madai ya
Wakandarasi. Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kulipa madai
yaliyohakikiwa kwa kuzingatia mpango (roadmap) ulioandaliwa kulipa
madeni hayo hadi yatakapofikia kiwango himilivu. Katika ulipaji wa madeni,
kipaumbele kitatolewa kwa madeni yanayogusa watoa huduma wengi na yale ambayo yanaongezeka
kutokana na riba.
30. Mheshimiwa Spika,
Mkakati huo unamtaka kila Afisa Masuuli kushiriki kikamilifu katika utekelezaji
wake ili kuiwezesha Serikali kufikia malengo yake ya kudhibiti malimbikizo ya
madai na kutoa huduma kwa wananchi kwa wakati. Hivyo, katika kuhakikisha kwamba
hakuna madeni mapya yanayozalishwa, kila Afisa Masuuli atapaswa kuzingatia
yafuatayo:
(i)
Mikataba yote ya ujenzi wa
miundombinu inazingatia viwango vya bajeti vilivyowekwa katika kila Fungu.
Aidha, Fungu husika lisiingie mikataba nje ya viwango hivyo bila kibali cha
Mlipaji Mkuu wa Serikali; vile vile Kifungu cha 51(1) na (2) cha Sheria ya Bajeti
ya 2015 kinaelekeza kwamba miadi yote ya miaka zaidi ya mmoja (Multi-year Commitments) lazima ipate
idhini ya Waziri wa Fedha ikiwa imezingatia viwango vya bajeti, malipo ya miadi
hii isizidi viwango/bajeti iliyoidhinishwa na Bunge, pamoja na kulipa madai baada
ya uhakiki;
(ii)
Kutoa kipaumbele kwa
ukamilishaji wa miradi inayoendelea kabla ya kuanzisha miradi mipya, sambamba
na kuhakikisha kwamba miradi inayoanzishwa inatengewa fedha katika bajeti;
(iii)
Maafisa Masuuli kutoingia
makubaliano ya kupatiwa huduma au bidhaa bila ya kuwa na fedha au kibali cha
maandishi kutoka kwa Mlipaji Mkuu wa Serikali; na miadi yoyote ni lazima
iingizwe kwenye mtandao wa IFMS;
(iv)
Madai ya watoa huduma wote na Wakandarasi
lazima yafanyike baada ya kupata hati za ununuzi (LPO) kutoka kwenye mfumo wa IFMS
iliyozingatia bajeti iliyoidhinishwa na Bunge, pamoja na kuwepo kwa ridhaa ya
matumizi (Exchequer Issue Notification)
kwa vifungu husika vya matumizi. Hivyo, Serikali inasisitiza kwamba, LPO
zilizotoka kwenye mfumo wa Malipo ya Serikali (IFMIS) ndiyo zitumike kama msingi wa malipo kwa Watoa Huduma; na
(v)
Kuzingatia matumizi ya Sheria
ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015 na Sheria
ya Fedha za Umma SURA 348 na waraka wa Mlipaji Mkuu wa Serikali kuhusu
utekelezaji wa bajeti.
III.
SERA ZA BAJETI KWA MWAKA 2018/19
Shabaha za Uchumi Jumla na
Bajeti
31. Mheshimiwa Spika, Shabaha
za uchumi jumla na bajeti katika kipindi cha mwaka 2018/19 ni kama ifuatavyo:-
(i)
Pato la Taifa kukua kwa
asilimia 7.2 mwaka 2018 kutoka ukuaji halisi wa asilimia 7.1 mwaka 2017;
(ii)
Mfumuko wa bei kuendelea
kubaki katika wigo wa tarakimu moja;
(iii)
Mapato ya ndani kufikia
asilimia 15.8 ya Pato la Taifa mwaka 2018/19 kutoka matarajio ya asilimia 15.3
mwaka 2017/18 na uwiano halisi wa asilimia 15.6 mwaka 2016/17;
(iv)
Mapato ya kodi kufikia
asilimia 13.6 ya Pato la Taifa mwaka 2018/19 kutoka matarajio ya asilimia 13.0
mwaka 2017/18 na uwiano halisi wa asilimia 13.3 mwaka 2016/17;
(v)
Matumizi ya Serikali kufikia
asilimia 24.5 ya Pato la Taifa mwaka
2018/19 kutoka matarajio ya asilimia 23.0 mwaka 2017/18 na matumizi halisi ya asilimia 22.2 mwaka
2016/17; na
(vi)
Nakisi ya bajeti kufikia
asilimia 3.2 ya Pato la Taifa mwaka 2018/19 kutoka matarajio ya asilimia 2.1
mwaka 2017/18 na uwiano halisi wa asilimia 1.5 mwaka 2016/17.
Sera na Mikakati ya Kuongeza Mapato
32.
Mheshimiwa
Spika, ili kuongeza na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, sera
za mapato kwa mwaka 2018/19 zitalenga katika kuongeza wigo wa kodi, kuimarisha
usimamizi wa vyanzo vilivyopo hususan katika matumizi ya mifumo ya
kielektroniki na hatua nyingine za kiutawala.
33. Mheshimiwa Spika,
katika kuongeza wigo wa kodi, yapo
maeneo makuu mawili yatakayozingatiwa na Serikali ambayo ni kurasimisha sekta
isiyo rasmi na kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kupata vyanzo vipya vya
mapato vitokanavyo na uwekezaji huo. Zipo hatua za urasimishaji zilizoanza
kufanyika mfano uthaminishaji wa majengo, na upimaji wa viwanja, zoezi ambalo
linaendelea nchi nzima. Serikali itaongeza kasi ya urasimishaji ikiwa ni pamoja
na kuwepo na mbinu bunifu, rafiki, shirikishi na za kimkakati.
34. Mheshimiwa Spika,
mazingira bora ndio msingi mkuu wa kuvutia biashara na uwekezaji ikiwemo
kuboresha miundombinu msingi, vivutio vya kikodi, sera zisizobadilika (policy consistency and predictability),
upatikanaji wa ardhi na taratibu za kisheria na usimamizi. Pale mazingira yanapokuwa
mazuri, uwekezaji, uzalishaji, ajira na miamala ya kibiashara inaongezeka na
hivyo kupelekea kuongezeka kwa vyanzo vipya vya mapato.
35. Mheshimiwa Spika,
uchambuzi uliofanywa na Serikali mwaka 2017/18 ulibaini changamoto zifuatazo
kuhusiana na mazingira ya biashara na uwekezaji :
(i)
Migongano ya sheria, kanuni na
taratibu zinazotumiwa na mamlaka mbalimbali;
(ii)
Gharama kubwa za
kuanzisha na kuendesha biashara kutokana
na wingi wa kodi, ada na tozo zinazoambatana na taratibu ngumu na nyingi zenye
urasimu usio na tija na hivyo kutoa mianya na mazingira ya rushwa;
na
(iii)
Muingiliano wa majukumu na
wingi wa mamlaka za udhibiti katika kuidhinisha na kutoa hati, vibali na vyeti
kwenye shughuli za uwekezaji na biashara.
36. Mheshimiwa Spika,
kutokana na uchambuzi huo, Serikali imeandaa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa
Udhibiti wa Biashara (Blueprint for
Regulatory Reforms to Improve Business Environment for Tanzania). Miongoni
mwa mapendekezo ya Mpango huo ambayo yatatekelezwa kwa nguvu zaidi kuanzia mwaka
ujao wa fedha (2018/19) ni kurahisisha
taratibu za kulipa kodi, tozo na ada mbalimbali, na kupunguza muda na mlolongo
mrefu wa kusajili makampuni na biashara. Serikali ya Awamu ya Tano inaamini
kuwa maendeleo endelevu yatapatikana kwa haraka zaidi katika mazingira yenye
ushirikiano wa kweli na wa dhati kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.
37.
Mheshimiwa
Spika, katika kuimarisha
usimamizi wa vyanzo vya mapato vilivyopo, Serikali itaendelea na zoezi la uunganishaji
wa Wizara, Idara, Wakala, taasisi na mashirika ya umma kwenye Mfumo wa Serikali
wa Kielektroniki wa ukusanyaji wa mapato (Government electronic Payment Gateway -GePG) ili kuboresha ukusanyaji na kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali. Mfumo huu ulianzishwa mwaka 2017 na kupitishwa na Bunge kupitia
marekebisho ya Sheria ya Fedha za Umma SURA 348 ambayo iliziagiza taasisi zote
za Serikali kukusanya mapato kwa kutumia Mfumo wa GePG. Hadi mwezi Mei, 2018, jumla ya taasisi 234 zinazokusanya
maduhuli zikijumuisha Halmashauri zote 185 zimeunganishwa kwenye Mfumo huu.
Nachukua fursa hii kuagiza Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wizara, Idara
na Taasisi zote za Serikali zilizobaki zihakikishe kwamba zimeunganishwa na
kuanza kutumia mfumo wa GePG kabla ya
Juni, 2019. Mbali na Mfumo huu, ninawakumbusha Maafisa Masuuli wote kuhakikisha
kuwa ukusanyaji wa maduhuli unafanyika kwa kutumia mashine za kielektroniki
(EFDs) pamoja na benki na siyo risiti za kuandikwa kwa mkono.
38. Mheshimiwa Spika,
kuhusu hatua nyingine za kiutawala
za kuongeza mapato ya Serikali, ninaelekeza yafuatayo:
(i)
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
ichukue hatua za makusudi za kuboresha mahusiano kati yake na walipa
kodi kwa lengo la kuondoa dhana
iliojengeka miongoni mwa walipa kodi kuwa TRA inatumia nguvu na vitisho
kudai kodi;
(ii)
Ofisi ya Msajili wa Hazina
iimarishe usimamizi na ukaguzi kwenye kampuni ambazo Serikali ina hisa ili
kuhakikisha kuwa Serikali inapata gawio stahiki katika uwekezaji wake; na
(iii)
Mamlaka za Serikali za Mitaa
zijielekeze kwenye miradi itakayochochea upatikanaji wa mapato katika mamlaka
hizo hususan viwanda, masoko na machinjio ya kisasa, stendi za mabasi, stendi
za maegesho ya malori kwenye mipaka na nchi jirani na maghala ya kuhifadhi
nafaka.
Kuimarisha Ushirikiano na Washirika wa Maendeleo
39.
Mheshimiwa Spika, misaada na mikopo nafuu
imekuwa ikipungua kutoka wastani wa asilimia 26.3 ya bajeti halisi ya mwaka
2010/11 hadi asilimia 10.4 mwaka 2016/17. Kutokana na umuhimu wa kuwa na
maendeleo endelevu na kuhakikisha kuwa misaada na mikopo nafuu inapatikana kama ilivyoahidiwa na kwa wakati, Serikali
kwa kushirikiana na Washirika wa Maendelo na wadau wengine imekamilisha
Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo (Development
Cooperation Framework - DCF). Mwongozo huo uliidhinishwa na Serikali mwezi
Agosti 2017 na umebainisha:
(i)
Misingi ya jumla ya kuongoza ushirikiano
ambayo ni pamoja na Serikali kuongoza michakato ya kuibua vipaumbele vya miradi
ya maendeleo; na
(ii)
Mfumo wa majadiliano ambao uko
katika ngazi tatu; Majadiliano ya Kitaifa ya Kimkakati, Majadiliano ya Kisekta
na Majadiliano yenye Mwelekeo wa Kisiasa.
Sera za Matumizi
40.
Mheshimiwa
Spika, sera za matumizi katika mwaka 2018/19 zitajumuisha:
(i)
Kudhibiti nakisi ya bajeti isizidi asilimia 3.2 ya
Pato la Taifa;
(ii)
Kuelekeza fedha kwenye maeneo ya kipaumbele na yenye
tija ili kuchochea ukuaji wa kilimo na viwanda, kupanua fursa za ajira, kujenga
na kuboresha miundombnu ya uchumi na kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za
jamii;
(iii)
Kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma na
kuendelea kupunguza matumizi yasiyo ya lazima; na
(iv)
Kudhibiti ulimbikizaji wa madai.
41.
Mheshimiwa
Spika, Katika kusimamia sera hizi, Serikali itachukua hatua
zifuatazo:
(i)
Kuwachukulia hatua za
kisheria, kinidhamu na kiutawala wote watakaothibitika kwenda kinyume na sheria
na kanuni zinazoongoza utendaji katika nafasi zao.
Napenda niwakumbushe tena kuwa kula fedha za miradi ya wananchi ni sawa na kula
sumu – wasijaribu!!
(ii)
Kuhakikisha kuwa Maafisa
Masuuli hawaingii mikataba bila kuwa na uhakika wa upatikanaji wa fedha au
ridhaa ya Mlipaji Mkuu wa Serikali na kuzuia matumizi na ahadi (commitments) za matumizi nje ya mfumo wa
“IFMS”. Lengo ni kudhibiti ulimbikizaji wa madai;
(iii)
Kuwianisha matumizi na mapato
halisi yatakayopatikana kwa kila mwezi;
(iv)
Kulipa madai mbalimbali
yaliyohakikiwa;
(v)
Kuhakikisha kuwa ununuzi wa
umma unawiana na thamani ya fedha itakayotumika; na
(vi)
Kuimarisha ufuatiliaji wa
matumizi ya fedha za umma ili zitumike kama ilivyokusudiwa.
Maeneo ya
vipaumbele kwa mwaka 2018/19
42. Mheshimiwa Spika,
kama ilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2018/19 ambao
niliuwasilisha leo asubuhi, bajeti ya matumizi katika mwaka 2018/19 itaweka
mkazo zaidi katika uendelezaji wa miradi ya kielelezo; kufungamanisha maendeleo
ya watu; na ujenzi wa mazingira wezeshi kwa ajili ya uwekezaji na uendeshaji
biashara.
43. Mheshimiwa Spika, maeneo
ya kipaumbele katika bajeti hii ni yafuatayo:
(i)
Kilimo: Fedha zitaelekezwa
zaidi kuboresha miundombinu ya umwagiliaji, maghala na masoko, kuimarisha
upatikanaji wa pembejeo na zana za
kilimo, kupanua huduma za ugani, kuboresha mfumo wa utafiti na utoaji wa
matokeo ya utafiti kwa wananchi, na uendelezaji wa sekta ndogo za uvuvi na
mifugo. Mkazo umewekwa katika sekta hii kwa kuzingatia kuwa inategemewa na
wananchi wengi na ndiyo itakayotupatia malighafi kwa ajili ya viwanda, kutuhakikishia
usalama wa chakula na kuongezeka kwa kipato cha wananchi;
(ii)
Viwanda: Katika kuchochea
ukuaji wa viwanda nchini, Serikali itaelekeza nguvu zake kwa kutekeleza Mpango
wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara ili kuvutia uwekezaji
wa sekta binafsi hususan viwanda vya nguo, ngozi na nyama, samaki, mafuta ya
kula, madawa na vifaa tiba, vyakula vya binadamu na mifugo, na katika sekta ya
madini. Aidha, uendelezaji wa viwanda na kilimo utapaswa kuzingatia uendelevu
wa mazingira;
(iii)
Huduma za Jamii: Maji: Eneo lingine muhimu
ni kuongeza upatikanaji na usambazaji wa maji safi hasa vijijini na uondoshaji
wa majitaka, uchimbaji wa visima katika maeneo kame nchini na ujenzi wa mabwawa
makubwa ya kimkakati. Elimu: Serikali itaendelea kugharamia
elimu msingi bila ada, kuongeza
idadi ya wataalam katika fani adimu kwenye maeneo ya madini, mafuta na gesi,
madaktari bingwa (moyo na figo) pamoja na utoaji wa mikopo kwa
wanafunzi wa elimu ya juu. Afya:
rasilimali fedha zitaelekezwa kuongeza
usambazaji wa dawa, vifaa tiba, vitendanishi na uboreshaji wa huduma
katika vituo vya afya, zahanati na hospitali za rufaa. Vile vile katika mwaka
ujao wa fedha, Serikali itaelekeza fedha zaidi za LGCD kwenye miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri
hususan miradi ya elimu na afya. Aidha, Serikali itaweka msukumo kuimarisha
upatikanaji wa lishe bora kwa mama
na mtoto hususan katika siku 1,000 za mtoto tangu kutungwa kwa mimba ili kuondokana
na changamoto ya kuwa na watoto wenye udumavu na hivyo kukua vema kimwili na
kiakili. Aidha, mahitaji ya makundi
maalum katika jamii yetu (wanawake, vijana, watoto, watu wenye ulemavu na
wazee) yataendelea kuangaliwa kipekee;
(iv)
Kujenga na kukarabati miundombinu wezeshi hususan kuongeza uzalishaji wa umeme kwa
kutumia vyanzo mbalimbali, kuendelea na ujenzi wa reli mpya ya kati kwa kiwango
cha kimataifa (standard gauge),
ujenzi wa barabara za kuunganisha mikoa na zile za vijijini, na kuimarisha
usafiri wa anga na majini; na
(v)
Maeneo mengine ya kipaumbele ni: kurahisisha umiliki wa
ardhi, kuimarisha huduma za mawasiliano,
kifedha na utalii na kuimarisha ulinzi,
usalama, utawala bora, na utoaji haki.
IV.
HATUA ZA MAPATO NA MABORESHO YA MFUMO WA KODI, ADA NA TOZO MBALIMBALI
Maboresho
ya Mfumo wa Kodi, Ada na Tozo Mbalimbali
44.
Mheshimiwa
Spika, napenda kuwasilisha mapendekezo ya kufanya
marekebisho ya mfumo wa kodi ikiwemo kurekebisha baadhi ya viwango vya kodi,
tozo na ada zinazotozwa chini ya Sheria mbalimbali na pia taratibu za
ukusanyaji na usimamiaji wa mapato ya Serikali. Marekebisho haya yanalenga
pamoja na mambo mengine, kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi hususan katika
sekta ya Viwanda, Utalii, kukuza ajira, na kuongeza mapato ya Serikali. Aidha, marekebisho
haya yamezingatia dhamira ya Serikali ya kuwa na mfumo wa kodi ambao ni tulivu
na wenye kutabirika. Marekebisho hayo yanahusu Sheria zifuatazo:-
a.
Sheria
ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148;
b. Sheria ya Kodi ya
Mapato, SURA 332;
c.
Sheria
ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147;
d.
Sheria
ya Fedha za Serikali za Mitaa, SURA 290;
e.
Sheria
ya Usimamizi wa Kodi, SURA 438;
f.
Sheria
ya Fedha za Serikali za Mitaa, SURA 290; Sheria ya Fedha za Umma, Sura 348; na Sheria ya Benki Kuu, SURA 197;
g.
Sheria
ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004;
h. Sheria zinazosimamia
Bodi za Mazao;
i.
Sheria
ya Michezo ya Kubahatisha SURA 41;
j.
Marekebisho
madogo madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi na Sheria nyingine mbalimbali; na
k.
Marekebisho
ya Ada na Tozo mbalimbali zinazotozwa na Wizara, Mikoa na Idara
zinazojitegemea.
a)
Sheria ya Kodi ya
Ongezeko la Thamani, SURA 148
45.
Mheshimiwa
Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi
ya Ongezeko la Thamani,Sura 148 kama ifuatavyo:-
(i)
Kusamehe
Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye vifungashio vya madawa ya binadamu
vitakavyotengenezwa mahsusi kwa ajili ya viwanda vinavyozalisha dawa hapa
nchini. Aidha, vifungashio hivyo vitakuwa na machapisho ya majina ya kiwanda
husika cha utengenezaji madawa ili kuhakikisha kwamba vinatumiwa na viwanda
hivyo na siyo vinginevyo. Lengo la hatua hii nikupunguza gharama za uzalishaji
na kuvilinda viwanda vinavyotengeneza madawa hapa nchini ili viweze kumudu
ushindani na kuongeza uzalishaji;
(ii)
Kusamehe
Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye virutubisho vinavyotumika kutengenezea
vyakula vya mifugo (animal and poultry
feeds additives) vinavyoagizwa kutoka nje. Lengo la hatua hii ni kupunguza
gharama kwa wafugaji na kuhamasisha ufugaji bora ili kuongeza mchango wa Sekta
hiyo katika Uchumi;
(iii) Kufanya marekebisho
kwenye kifungu cha 6(2)(a) cha Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili kumpa
mamlaka Waziri mwenye dhamana na maswala ya fedha kutoa msamaha wa kodi kwa miradi ya Serikali
inayotekelezwa kwa mikopo ya kibiashara. Hivi sasa Sheria ya Kodi ya Ongezeko
la Thamani inakataza kusamehe kodi kwenye mikopo ya kibiashara hali ambayo
imesababisha kukwama kwa utekelezaji wa miradi muhimu ya Serikali kama vile
miradi ya Maji, barabara n.k. Hivyo, marekebisho yanayopendekezwa yatawezesha
utekelezaji wa miradi ya Serikali kwa wakati uliopangwa;
(iv) Kufanya marekebisho
kwenye kifungu cha 6(2)(a) cha Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili kumpa
mamlaka Waziri mwenye dhamana na masuala ya fedha kusamehe kodi hiyo pale
ambapo kuna mkataba uliosainiwa baina ya Serikali ya Tanzania na Taasisi ya
Fedha au Benki ambayo ni “mwakilishi” wa Serikali nyingine aliyepewa dhamana na
Serikali hiyo kuingia mikataba na kusimamia utekelezaji wa miradi husika. Hivi
sasa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani inampa mamlaka Waziri huyo kusamehe
kodi pale ambapo kuna mkataba baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya nchi
nyingine unaotoa msamaha wa kodi. Hivyo miradi mingi inayohusisha mikataba ya
misaada au mikopo kupitia mabenki na Taasisi za fedha imekwama utekelezaji
wake. Kwa msingi huo, marekebisho haya yanalenga katika kuondoa ukwamishaji na
ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi mingi ya Serikali inayotekelezwa kwa
fedha za Washirika wa Maendeleo kupitia mikataba inayosainiwa na Serikali yetu
na Benki au Taasisi za Fedha za Serikali za nchi nyingine; na
(v)
Kusamehe
Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye taulo za kike (sanitary pads) HS Code 9619.00.10. Lengo la hatua hii ni kuwezesha
upatikanaji wa bidhaa hii muhimu kwa bei nafuu kwa ajili ya kulinda afya ya
mama na mtoto wa kike hasa watoto walio shuleni na vijijini. Ni matarajio ya
Serikali kuwa wazalishaji na wauzaji wa taulo za kike wataziuza kwa bei nafuu
baada ya kusamehewa kodi hii.
Hatua hizi zote za Kodi
ya Ongezeko la Thamani kwa ujumla wake zinatarajiwa kupunguza mapato ya
Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni
219.1
b)
Sheria ya Kodi ya
Mapato, SURA 332
46.
Mheshimiwa
Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332 kama ifuatavyo:-
(i)
Kufanya
marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato ili kupunguza kiwango cha Kodi ya
Mapato ya Makampuni (Corporate Income Tax)
kutoka asilimia 30 mpaka asilimia 20 kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2018/19
hadi mwaka 2022/23 kwa wawekezaji wapya wa viwanda vya madawa ya binadamu na
viwanda vinavyotengeneza bidhaa za
ngozi. Aidha, Serikali itaingia mkataba wa makubaliano (performance agreement) na kila mwekezaji
ambao utaainisha wajibu wa kila upande. Lengo la hatua hii ni kuongeza
uwekezaji katika sekta ya madawa ya binadamu na usindikaji wa ngozi ambao kwa
sasa haufanyiki nchini na pia kuongeza ajira na mapato ya Serikali. Aidha,
hatua hii itapunguza matumizi ya fedha za kigeni zinazotumika kuagiza dawa hizo
kutoka nje na kuhamasisha uzalishaji wa madawa mengi zaidi hapa nchini;
(ii)
Kufuta
kifungu cha 10A cha Sheria ya Kodi ya Mapato kinachomkataza Waziri mwenye
dhamana ya masuala ya fedha kutoa msamaha wa kodi kwenye miradi ya Serikali
inayotekelezwa kwa fedha za mikopo ya kibiashara (non concessional loans). Lengo la hatua hii ni kumpa mamlaka
Waziri huyo kutoa msamaha wa kodi ya mapato kwa miradi hiyo ambayo imekuwa na
changamoto katika utekelezaji wakati Serikali inapopata mikopo ya aina hiyo; na
(iii) Kurekebisha Sheria ya
Kodi ya Mapato ili kutoa msamaha wa Kodi ya zuio inayotozwa kwenye riba kwa
mikopo inayotolewa kwa Serikali na Benki, Taasisi za Fedha na wahisani kwa
ajili ya utekelezaji wa miradi ya Serikali.
Hatua hizi za Kodi ya
Mapato kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 220.5.
c)
Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147
47.
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Ushuru wa Bidhaa Kifungu cha
124(2), marekebisho ya viwango maalum vya Ushuru wa Bidhaa (specific duty rates) zisizo za petroli yanaweza kufanyika kila
mwaka ili kuviwianisha na mfumuko wa bei na viashiria vingine vya uchumi jumla.
Hata hivyo, ili kutekeleza azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi
wa viwanda, napendekeza kutofanya mabadiliko ya viwango maalum vya Ushuru wa
Bidhaa zisizo za petroli zinazozalishwa hapa nchini na kuongeza viwango vya
Ushuru wa Bidhaa zisizo za petroli zinazoagizwa kutoka nje ya nchi kama ifuatavyo:-
(i)
Ushuru
wa Bidhaa kwenye vinywaji baridi utaendelea kutozwa kwa kiwango cha shilingi 61
kwa lita;
(ii)
Ushuru
wa Bidhaa kwenye maji ya kunywa yaliyosindikwa kwenye chupa yaliyoagizwa kutoka
nje utaongezeka kutoka shilingi 61 kwa lita hadi shilingi 64.05 kwa lita ikiwa
ni ongezeko la shilingi 3.05 kwa lita. Aidha, Ushuru wa Bidhaa kwenye maji
yanayozalishwa hapa nchini utaendelea kutozwa kwa kiwango cha sasa cha shilingi 58 kwa lita;
(iii) Ushuru wa Bidhaa kwenye
maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda yanayozalishwa hapa nchini (local juices) hautaongezeka na
utaendelea kutozwa kwa kiwango cha shilingi 9 kwa lita;
(iv) Ushuru wa Bidhaa kwenye
maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda ambayo hayazalishwi hapa
nchini (imported juices) utaongezeka
kutoka shilingi 221 kwa lita hadi shilingi 232 kwa lita ikiwa ni ongezeko la
shilingi 11 kwa lita;
(v)
Ushuru
wa Bidhaa kwenye bia inayotengenezwa kwa nafaka ya hapa nchini na ambayo
haijaoteshwa (Beer from Local Unmalted
Cereals) hautaongezeka na utaendelea kutozwa kwa kiwango cha shilingi 450
kwa lita;
(vi) Ushuru wa Bidhaa kwenye
bia zinazoagizwa kutoka nje ya nchi utaongezeka kutoka shilingi 765 kwa lita
hadi shilingi 803.25 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 38.25 kwa lita;
(vii) Ushuru wa Bidhaa kwenye
bia zisizo za kilevi, ikijumuisha vinywaji vya kuongeza nguvu vinavyoagizwa
kutoka nje ya nchi utaongezeka kutoka shilingi 561 kwa lita hadi shilingi
589.05 kwa lita ikiwa ni ongezeko la shilingi 28.05 kwa lita. Aidha, Ushuru wa
Bidhaa kwenye bia zisizo za kilevi, ikijumuisha vinywaji vya kuongeza nguvu
vinavyozalishwa hapa nchini utaendelea kutozwa kwa kiwango cha sasa cha
shilingi 561 kwa lita;
(viii) Kuanzisha Ushuru wa
Bidhaa wa shilingi 200 kwa lita kwenye mvinyo uliotengenezwa kutokana na
usindikaji wa matunda (kama ndizi, rozela/choya, nyanya, nk) yanayozalishwa
hapa nchini tofauti na zabibu kwa kiwango kinachozidi asilimia 75;
(ix) Ushuru wa Bidhaa kwenye
mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa ndani ya nchi kwa kiwango
kinachozidi asilimia 75 hautaongezeka na utaendelea kutozwa kwa kiwango cha
shilingi 200 kwa lita;
(x)
Ushuru
wa Bidhaa kwenye mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa
kiwango kinachozidi asilimia 25, utaongezeka kutoka shilingi 2,349 kwa lita
hadi shilingi 2,466 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la shilingi 117 kwa lita;
(xi) Ushuru wa Bidhaa kwenye
vinywaji vikali vinavyoagizwa kutoka nje utaongezeka kutoka shilingi 3,481 kwa
lita hadi shilingi 3,655.05 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la shilingi 174.05 kwa
lita. Aidha, Ushuru wa Bidhaa kwenye vinywaji vikali vinavyozalishwa nchini
hautaongezeka na utaendelea kutozwa kwa kiwango cha shilingi 3,315 kwa lita;
(xii) Ushuru wa Bidhaa kwenye
sigara zisizo na kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa
hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, hautaongezeka na utaendelea
kutozwa kwa kiwango cha shilingi 12,447 kwa kila sigara elfu moja;
(xiii) Ushuru wa Bidhaa kwenye
sigara zenye kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa
nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, hautaongezeka na utaendelea kutozwa
kwa kiwango cha shilingi 29,425 kwa kila sigara elfu moja;
(xiv)
Ushuru
wa Bidhaa kwenye sigara zenye sifa tofauti na (xii) na (xiii) utaongezeka kutoka shilingi 53,235 hadi shilingi
55,896.75 kwa kila sigara elfu moja ikiwa ni ongezeko la shilingi 2,661.75 kwa
kila sigara elfu moja;
(xv) Ushuru wa Bidhaa kwenye
tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara (cut filler) inayoagizwa kutoka nje utaongezeka kutoka shilingi
26,888 hadi shilingi 28,232.4 kwa kilo, ikiwa ni ongezeko la shilingi 1,344.4
kwa kilo; na
(xvi)
Ushuru
wa Bidhaa wa ‘cigar’ unabaki kuwa asilimia 30.
48. Mheshimiwa Spika,
napendekeza kuanzisha Mfumo Mpya wa Stempu za Kodi za kielektroniki utakaoanza
kutumika tarehe 1 Septemba 2018. Mfumo mpya wa Stempu za Kodi za kielektroniki
utaiwezesha Serikali kutumia teknolojia ya kisasa kupata taarifa sahihi za
uzalishaji viwandani na kwa wakati (real time) zinazotumika kupanga mipango ya
maendeleo ya Taifa. Pia mfumo huu mpya utaiwezesha Serikali kudhibiti uvujaji
wa mapato na kutambua mapema kiasi cha Kodi ya Ushuru wa Bidhaa, Kodi ya Mapato
na ile ya Ongezeko la Thamani itakayolipwa. Aidha, mfumo wa Stempu za Kodi za
kielektroniki utadhibiti tatizo la uwepo wa stempu za karatasi za kugushi
ambalo linachangia uwepo wa bidhaa zisizokidhi viwango vya ubora na zinazoweza
kuathiri afya za binadamu. Mfumo huu mpya unatumika katika nchi nyingine ikiwa
pamoja na Kenya, Morocco, Uturuki, Malaysia na Switzerland na umekuwa na
mafanikio makubwa.
Hatua za Ushuru wa
Bidhaa kwenye bidhaa zisizo za petroli kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza
mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi
milioni 119,456.6
d)
Sheria ya Fedha za
Serikali za Mitaa, SURA 290.
49.
Mheshimiwa Spika napendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali
za Mitaa Sura 290 kama ifutavyo:-
(i)
Kuongeza
kifungu cha 37A kwenye Sheria ya Serikali za Mitaa ili kumpa Mamlaka Waziri
mwenye dhamana na Serikali za Mitaa Kuzitaka Serikali za Mitaa kutenga asilimia
10 ya fedha wanazokusanya kutoka kwenye vyanzo vyao vya mapato kwa ajili ya
kuwezesha vikundi vya vijana na wanawake. Aidha asilimia 50 ya fedha hizo
zitatengwa kwa ajili ya vikundi vya vijana na asilimia 50 kwa vikundi vya
wanawake. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- TAMISEMI ataandaa Kanuni ambazo
zitaweka utaratibu wa kusimamia utoaji wa fedha hizo kwa vikundi vya vijana na
wanawake vilivyosajiliwa. Pia, fedha zitatolewa kwa kuwakopesha bila kutoza
riba yoyote; na
(ii)
Kurekebisha
kifungu cha 16(6) cha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290, ambacho
kinatoa mwanya kwa Taasisi/Makampuni yanayolipa Ushuru wa Huduma kutolipa
Ushuru wa Mazao. Mfano, Makampuni mengi yanayochakata zao la mkonge ili
kuzalisha nyuzi za katani yanamiliki pia mashamba ya mkonge. Hivyo siyo busara
kuwalipisha ushuru wa mazao na ushuru wa huduma. Hata hivyo, yapo makampuni
yenye mashamba ya mkonge ambayo hayachakati mkonge, haya yanapaswa kulipa
ushuru wa mazao badala ya ushuru wa huduma. Napendekeza kiongezwe kifungu cha
16(7) kwenye Sheria hiyo kuyataka Makampuni yanayozalisha mazao na hayachakati
kwa ajili ya kuyaongezea thamani yawajibike kulipa Ushuru wa Mazao.
e)
Sheria ya Usimamizi wa
Kodi, SURA 438
50.
Mheshimiwa Spika, napendekeza Kurekebisha
Sheria ya Usimamizi wa Kodi SURA 438, ili kuanzisha utaratibu maalum wa
kusamehe kodi (Tax Amnesty) ambao unalenga kusamehe malimbikizo ya nyuma ya
riba na adhabu (Interest and Penalties) kwa kiwango cha asilimia 100. Msamaha
huo utatolewa kwa kipindi cha miezi sita (6) kinachoanzia tarehe 1 Julai 2018
mpaka tarehe 31 Desemba 2018. Aidha kwa kufanya hivyo, Serikali inatarajia
kukusanya malimbikizo ya madeni ya nyuma ya kodi (Principal Tax) pamoja na
kuinua kiwango cha ulipaji kodi kwa hiyari kwa zaidi ya asilimia 10.
Hatua hiyo ya marekebisho
ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa
kiasi cha shilingi milioni 500,000.
f)
Sheria ya Fedha za
Serikali za Mitaa, SURA 290, Sheria ya Fedha za Umma, SURA 348 na Sheria ya
Benki Kuu, SURA 197.
51.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kurekebisha
Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura 290, Sheria ya Fedha za Umma Sura
348, na Sheria ya Benki Kuu, Sura 197 ili kuanzisha Akaunti Jumuifu ya Hazina (Treasury
Single Account) ambapo akaunti hii itatumika kupokea fedha zote za Serikali na
kufanya malipo yote ya Serikali. Msingi wa kuanzishwa kwa akaunti hii ni
kutekeleza makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
yaliyozitaka nchi wanachama kuanzisha akaunti jumuifu ili kuimarisha usimamizi
wa fedha za Serikali. Uwepo wa akaunti hii pamoja na mambo mengine utarahisisha
usimamizi wa fedha za Serikali kwa kupunguza idadi ya akaunti kwenye benki za
biashara na Benki Kuu, kupunguza gharama za kibenki zinazolipwa hivi sasa na
Serikali kufuatia huduma zinazotolewa kwa Serikali na Benki za Biashara,
kupunguza nakisi kwenye mfuko Mkuu wa Serikali ambapo akaunti maalum
zitajumuishwa kwenye ukokotoaji wa bakaa katika Mfuko Mkuu wa Serikali tofauti
na utaratibu wa hivi sasa ambapo akaunti hizi hazijumuishwi katika ukokotoaji
huo.
g)
Sheria ya Forodha ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka
2004
52.
Mheshimiwa Spika, kikao cha Mawaziri wa
Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki cha Maandalizi ya Bajeti (Pre-Budget
consultations of Ministers of Finance) kilichofanyika tarehe 4 Mei, 2018 mjini
Arusha, Tanzania kilipendekeza kufanya marekebisho ya Viwango vya Ushuru wa
Pamoja wa Forodha (EAC – Common External Tariff “CET”) na Sheria ya Forodha ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Customs Management Act, 2004) kwa Mwaka
2018/19. Mapendekezo hayo yanalenga kwa kiwango kikubwa katika kuchochea
maendeleo ya viwanda ili kukuza ajira na ustawi wa jamii (Industrialization for
Job Creation and Shared Prosperity).
53.
Mheshimiwa Spika, mapendekezo ya kufanya
marekebisho kwenye Viwango vya Pamoja Ushuru wa Forodha ni kama ifuatavyo:-
(i)
Kuendelea
kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala ya asilimia 35 kwenye ngano (HS
Code 1001.99.00 na HS Code 1001.99.90) kwa mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni
kuendelea kutoa unafuu kwa viwanda vya wazalishaji wa bidhaa na vyakula
vinavyotumia ngano na kuimarisha utulivu wa bei kwa bidhaa zinazozalishwa kwa
kutumia ngano hiyo. Aidha, hatua hii inazingatia kwamba bado kiwango cha
uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu ni kidogo katika nchi za Jumuiya ya Afrika
Mashariki na hivyo hautoshelezi mahitaji. Ili kudhibiti uagizaji wa bidhaa hii,
utaratibu wa “Duty Remission”
utatumika ambapo viwanda vinavyotumia ngano ya aina hii katika uzalishaji
ndivyo vitakavyohusika na kutumia kiwango hicho cha msamaha wa Ushuru wa
Forodha;
(ii)
Kuendelea
kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 10
kwenye mashine za Kielektroniki zinazotumika kukusanya mapato ya Serikali
(Electronic Fiscal Devices) zinazotambulika katika HS Code 8470.50.00 kwa mwaka
mmoja. Hatua hii inatarajiwa kuendelea kutoa unafuu na kuhamasisha
wafanyabiashara na walipa kodi kutumia mashine hizo katika kufanya mauzo na
kuongeza ufanisi katika Usimamizi na Udhibiti wa kodi;
(iii) Kutoza Ushuru wa Forodha
wa asilimia 15 badala ya asilimia 25
kwenye karatasi zinazotambulika katika HS Codes 4804.11.00; 4804.21.00;
4804.31.00; na 4804.41.00. Utaratibu wa “Duty
Remission” utatumika ambapo wazalishaji wanaotumia karatasi hizo katika
kutengeneza madaftari na vitabu ndio watakaofaidika. Lengo la hatua hii ni kupunguza
gharama kwa wazalishaji hao. Ni matarajio ya Serikali kwamba wazalishaji
watauza bidhaa hizi kwa bei nafuu na hivyo kuwezesha watumiaji, hususan
wanafunzi, kuzipata kwa gharama nafuu;
(iv) Kutoza Ushuru wa forodha
wa asilimia 0 badala ya asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye karatasi
zinazoingizwa kutoka nje kwa ajili ya utengenezaji wa gypsum board (Gypsum
paper for manufacturing of gypsum board) zinazotambulika katika HS Code
4805.92.00;
(v)
Kutoza
Ushuru wa forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 100 kwenye sukari ya
matumizi ya kawaida (consumption sugar) inayoagizwa kutoka nje ya nchi kwa
vibali maalum kwa lengo la kuziba pengo (gap sugar) la uzalishaji hapa nchini.
Hivi sasa sukari hiyo inatozwa Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya
asilimia 100;
(vi) Kuendelea kutoza Ushuru
wa Forodha wa asilimia 10 badala ya asilimia 0 kwenye "Gypsum Powder" inayotambuliwa kwa HS Code 2520.20.00 kwa
mwaka mmoja. Marekebisho haya yanalenga katika kulinda viwanda vinavyozalisha
bidhaa hiyo hapa nchini na kuhamasisha wawekezaji watumie "gypsum" inayopatikana hapa nchini kuzalisha "gypsum" powder. Aidha, hatua
hii inatarajiwa kuongeza ajira na mapato ya Serikali;
(vii) Kutoza Ushuru wa Forodha
wa asilimia 10 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye bidhaa ijulikanayo
kama "Self-adhesive label"
(HS Code 4821.10.90) ambayo hutumika kama alama ya kutambulisha aina ya bidhaa
kwa watengenezaji wa dawa za meno. Hatua hii inalenga katika kupunguza gharama
ya uzalishaji kwenye viwanda vya dawa za meno kwa kuwa self-adhesive labels
hazizalishwi hapa nchini;
(viii) Kutoza Ushuru wa Forodha
wa asilimia 0 badala ya asilimia 25 kwenye bidhaa ijulikanayo kama “Printed Alluminium Barrier Laminates"
(ABL) HS Code 3920.10.90 kwa mwaka mmoja. Aidha utaratibu wa “duty remission” utatumika ambapo hatua
hii itawahusu wenye viwanda vinavyoagiza bidhaa hiyo kwa matumizi ya kiwandani.
Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama ya uzalishaji kwa viwanda vya dawa za
meno. Aidha, ina lengo la kuvilinda viwanda hivi kutokana na ushindani na
ajira;
(ix) Kutoza Ushuru wa Forodha
wa asilimia 25 badala ya asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye mafuta ghafi ya kula
ya mawese (Crude Palm Oil) yanayotambulika katika HS Code 1511.10.00 kwa mwaka
mmoja. Hatua hii inalenga katika kulinda na kuhamasisha uzalishaji wa mbegu za
mafuta na mafuta ya kula hapa nchini kwa kuzingatia kuwa nchi yetu ina fursa
kubwa ya kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo. Aidha,
lengo ni kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kuchakata mafuta ghafi kwa
kutumia mbegu zinazozalishwa hapa nchini. Pia inatarajiwa kwamba uzalishaji wa
mbegu utaongezeka na kuongeza ajira viwandani na mashambani pamoja na kuongeza
kipato cha wakulima;
(x)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya asilimia 0 au asilimia 10 kwa mwaka
mmoja kwenye mafuta ghafi ya kula (mfano alizeti, mawese, soya, mzaituni, nazi,
karanga, mahindi n.k). Lengo la hatua hii ni kuhamasisha uzalishaji wa mbegu na
mafuta ya kula hapa nchini kwa kutumia mbegu zinazozalishwa nchini. Aidha,
inatarajiwa kwamba hatua hii italinda viwanda na ajira katika sekta ndogo ya
mafuta ya kula, na kuongeza mapato ya serikali na wakulima;
(xi) Kutoza Ushuru wa Forodha
wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye mafuta ya kula
yaliyochakatwa kwa kiwango cha kati na cha mwisho (semi-refined, refined/double refined oil) mfano alizeti, mawese,
soya, mzaituni, nazi, karanga, mahindi n.k. Ongezeko hilo la Ushuru wa Forodha
linatarajiwa kulinda uzalishaji wa mafuta ya kula na kuhamasisha uchakataji wa
mbegu za mafuta zinazozalishwa nchini badala ya kuagiza mafuta ya kula kutoka
nje ya nchi. Aidha, hatua hii inatarajiwa kupunguza fedha za kigeni
zinazotumika kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi;
(xii) Kutoza Ushuru wa Forodha
wa asilimia 25 au dola za Kimarekani 350 kwa kila tani moja ya ujazo (Metric
ton) kwa mwaka mmoja kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwenye bidhaa za chuma
za misumari zinazotambulika katika HS Code 7317.00.00 (nails, tacks, drawing
pins, corrugated nails, staples other than those of heading 83.05). Hatua ya
kuweka kiwango hicho cha Ushuru wa Forodha inalenga katika kulinda viwanda vya
bidhaa hizo hapa nchini kutokana na uingizaji wa bidhaa kama hizo kutoka nje ya
nchi;
(xiii) Kutoza Ushuru wa Forodha
wa asilimia 25 au dola za kimarekani 1.35 kwa kilo moja ya viberiti (safety matches)
vinavyotambuliwa kwenye HS Code 3605.00.00 kutegemea kiwango kipi ni kikubwa.
Hatua hii inazingatia kuwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zina uwezo wa
kuzalisha viberiti na kutosheleza mahitaji katika soko hivyo kuwepo na umuhimu
wa kulinda viwanda vinavyozalisha bidhaa hiyo;
(xiv)
Nchi
za Jumuiya zimekubaliana kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 10 hadi
asilimia 0 kwenye malighafi ya kutengeneza bidhaa za rangi za kupaka nyumba
ijulikanayo kama “polyvinyl Alcohol”
(HS Code 3905.30.00). Lengo la hatua hii ni kuhamasisha uwekezaji katika uzalishaji
wa bidhaa hizo;
(xv) Kutoza Ushuru wa Forodha
wa asilimia 0 kwa utaratibu wa “duty
remission” kwenye malighafi (inputs)
zinazotumika katika kutengeneza dawa za kuua wadudu (pesticides, fungicides, insecticides na acaricides). Hatua hii
itahusisha viwanda vinavyotumia malighafi hizo kutengeneza dawa za kuua wadudu.
Aidha, viwanda vitakavyoagiza malighafi hizo vitatakiwa kupata kibali cha
Wizara ya Kilimo. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za uzalishaji na
kuhamasisha uwekezaji kwenye viwanda hivyo;
(xvi)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 0 badala ya asilimia 10 kwa utaratibu wa duty
remission kwenye bidhaa ya kutengeneza sabuni ijulikanayo kama “RBD Palm Stearin” inayotambulika katika
HS Code 1511.90.40. Hatua hii inahusisha viwanda vinavyotumia bidhaa hiyo
katika kutengeneza sabuni. Aidha, hatua ya kupunguza ushuru huo imezingatia
kwamba Serikali imeongeza ushuru wa forodha katika mafuta ghafi ya mawese;
(xvii) Kutoza Ushuru wa Forodha
wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye viazi (potatoes fresh or chilled, other than seeds) vinavyotambulika
katika HS Code 0701.90.00. Lengo la hatua hii ni kulinda uzalishaji wa viazi
hapa nchini;
(xviii) Kutoza Ushuru wa Forodha
wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye Chingamu (Chewing Gum) zinazotambulilka katika HS Code 1704.10.00. Lengo la
hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani kwa kuwa kuna uwezo wa kuzalisha chewing
gum katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki;
(xix)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye peremende HS Code
1704.90.00. Hatua hii inachukuliwa kwa lengo la kulinda viwanda vya ndani na
ajira;
(xx) Kutoza Ushuru wa Forodha
wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye Chokoleti (chocolates) HS Code 18.06. Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki
zinazalisha bidhaa hizi na zina uwezo wa kutosheleza mahitaji ya soko;
(xxi) Kutoza Ushuru wa Forodha
wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye Biskuti (Biscuits) zinazotambullika kwa HS Code 1905. Hatua hii inazingatia
kuwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zina uwezo wa kuzalisha bidhaa hiyo na
kutosheleza mahitaji ya soko;
(xxii) Kutoza Ushuru wa Forodha
wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye nyanya zilizosindikwa (tomato sauce) zinazotambulika katika HS
Code 2103.20.00. Lengo la hatua hii ni kulinda uzalishaji wa bidhaa hiyo katika
viwanda vya ndani na mashambani. Aidha, imezingatia kwamba nchi yetu inazalisha
nyanya za kukidhi mahitaji na pia kuna umuhimu wa kusindika nyanya hizo hapa
nchini ili kuongeza thamani na kuongeza ajira katika kilimo cha nyanya;
(xxiii) Kutoza Ushuru wa Forodha
wa asilimia 60 badala ya asilimia 25 kwenye maji (mineral water) yanayotambulika katika HS Code 2201.10.00. Hatua hii
ni muhimu katika kuhamasisha uzalishaji na kulinda viwanda vya hapa nchini
vinavyozalisha bidhaa hiyo;
(xxiv) Kutoza Ushuru wa Forodha
wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye nyama (meat and edible meat offal in chapter 12) kwa mwaka mmoja. Lengo la
hatua hii ni kuhamasisha uanzishaji wa viwanda vya uchakataji wa nyama hapa
nchini na hivyo kuongeza thamani yake. Aidha, itaongeza fursa za ajira na
kipato katika sekta ya ufugaji na viwandani; na
(xxv)Kutoza Ushuru wa Forodha
wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye Soseji (sausages) na bidhaa za aina hiyo (HS Code 1601.00.00). Hatua hii
ina lengo la kulinda na kuhamasisha Viwanda vinavyozalisha bidhaa hiyo katika
Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
54.
Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha wa
Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya pia marekebisho kwenye
Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Customs Management Act, 2004) kama ifuatavyo:-
(i)
Kufanya
marekebisho katika Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki linalotoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye magari yanayotumika
kwenye mashindano ya mbio za magari (rally
cars) na kuingiza pikipiki (motorcycles)
ili nazo ziweze kupata msamaha huo. Aidha, magari na pikipiki husika
hutengenezwa mahsusi kwa ajili ya mashindano hayo. Hatua hiyo inatarajiwa
kuhamasisha mashindano hayo na kukuza sekta ya utalii;
(ii)
Kufanya
marekebisho kwenye Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki ili kutoa msamaha kwa boti inayotumika mahsusi kwa ajili ya kutoa
huduma kwa wagonjwa kwenye maji (Motor
Boat Ambulance) inayotambulika katika HS Code 8903.99.10 kama vile
yanavyosamehewa magari ya kutoa huduma kwa wagonjwa (Motor Vehicle Ambulance). Hatua hii ina lengo la kupunguza gharama
na kuwezesha utoaji wa huduma za matibabu katika usafiri wa majini; na
(iii) Kufanya Marekebisho
katika Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili
kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye magari ya kubebea watalii (Motor vehicle for Transport of Tourists).
Magari haya yanajumuisha magari ya aina mbalimbali ambayo yametengenezwa
mahsusi kwa ajili ya kubebea watalii (Motor
sightseeing buses, overland trucks). Lengo la kutoa msamaha huo ni
kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya utalii, kuboresha huduma ya usafiri kwa
watalii na kuongeza ajira na mapato ya Serikali.
55.
Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki tumekubaliana kupunguza Viwango vya Ushuru wa
Forodha (duty remission) kwenye malighafi
na vipuri vinavyohitajika katika kutengeneza nguo na viatu katika Jumuiya ya
Afrika Mashariki. Aidha, tayari nchi hizi zimewasilisha orodha ya malighafi na
vifaa vitakavyopunguziwa Ushuru wa Forodha. Uamuzi huo utaanza kutekelezwa
mwaka 2018/19.
Hatua hizi za Ushuru wa
Forodha kwa pamoja zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 1,630.2
h)
Sheria zinazosimamia
Bodi za Mazao.
56.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya
marekebisho kwenye sheria zote zinazosimamia Bodi za mazao mbalimbali kwa lengo
la kuwezesha ushuru wote unaokusanywa na bodi hizo kuingizwa kwenye Mfuko Mkuu
wa Serikali. Lengo la hatua hii ni kuhakikisha kwamba mapato yatokanayo na
ushuru unaotozwa kwenye mazao mbalimbali yanasimamiwa ipasavyo na kutumika kwa
ajili ya shughuli zilizokusudiwa. Aidha,
shughuli za kuendeleza mazao pamoja na gharama za uendeshaji wa Bodi
zitagharamiwa kupitia Bajeti ya Serikali.
i)
Sheria ya Michezo ya
kubahatisha, SURA 41
57.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya
mabadiliko ya kiwango cha kodi katika michezo ya kubahatisha ya ubashiri wa
matokeo ya michezo (sports betting)
kutoka asilimia 6 ya mauzo ghafi hadi asilimia 10. Lengo ni kuongeza mapato ya
Serikali kutoka kwenye sekta ndogo ya michezo hiyo ya kubahatisha.
58.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya
marekebisho ya kiwango cha kodi kinachotozwa kwenye mashine za michezo ya
kubahatisha (slot machines) kutoka
shilingi 32,000 hadi shilingi 100,000 kwa kila mashine kwa mwezi. Lengo ni
kuongeza mapato ya Serikali.
59.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kuongeza
kiwango cha kodi kinachotozwa kwenye michezo ya kubahatisha (Casino) kutoka asilimia 15 hadi asilimia
18 ya mapato halisi ambayo hupatikana baada ya kutoa zawadi (Gross Gaming Revenue -GGR). Lengo ni
kuongeza mapato ya Serikali kwa sababu kiwango cha asilimia 15 kimedumu kwa
muda mrefu kuanzia mwaka 2012.
60.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya
marekebisho ya kiwango cha kodi kinachotozwa kwenye mashine arubaini (Forty Machines Site) za michezo ya
kubahatisha kutoka asilimia 15 hadi asilimia 20 ya mapato halisi ambayo
hupatikana baada ya kutoa zawadi (Gross
Gaming Revenue -GGR). Lengo ni kuongeza mapato ya Serikali.
Hatua hizi za
marekebisho ya michezo ya kubahatisha zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali
kwa kiasi cha shilingi milioni 21,198.8.
j)
Marekebisho madogo
madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi na
Sheria nyingine mbalimbali.
61.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya
marekebisho mengine madogo madogo yasiyo ya kisera katika sheria mbalimbali za
kodi pamoja na sheria nyingine mbalimbali ili ziwe sanjari na azma ya
kurahisisha utekelezaji wake. Marekebisho hayo yataainishwa katika Muswada wa
Sheria ya Fedha ya mwaka 2018 na Matangazo ya Serikali (Government Notices).
k)
Marekebisho ya Ada na
Tozo mbalimbali zinazotozwa na Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea.
62.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya
marekebisho ya viwango vya ada na tozo mbalimbali zinazotozwa na Wizara, Mikoa
na Idara zinazojitegemea ili kuvihuisha kulingana na hali halisi ya ukuaji wa
uchumi. Aidha, marekebisho hayo yataainishwa katika Muswada wa Sheria ya Fedha
ya mwaka 2018 na Matangazo ya Serikali (Government
Notices). Marekebisho hayo yatajumuisha:-
(i)
Kusamehe
Kodi ya Ardhi kwa Taasisi za Serikali kwa sababu taasisi hizi ni za umma
hazitengenezi faida. Aidha, marekebisho mengine ya ada na tozo mbalimbali
yanayohusu sekta ya ardhi yalitangazwa na Waziri mwenye dhamana ya ardhi kwenye
hotuba yake;
(ii)
Kufuta
na kupunguza baadhi ya viwango vya tozo na ada zinazotozwa kwenye sekta ya
uzalishaji wa Chumvi. Hatua hii imetokana na kuwepo kwa utitiri wa tozo na ada
zinazotozwa kwenye Madini ya Chumvi hali ambayo inasababisha gharama za
uzalishaji kuwa juu na kuwakatisha tamaa wazalishaji kuendelea na uzalishaji wa
chumvi. Hivyo napendekeza kufanya marekebisho ya tozo na ada kwenye sekta ya
uzalishaji chumvi kama ifuatavyo:-
a)
Kufuta
ushuru wa mazao ya chumvi unaotozwa na Halmashauri;
b)
Kufuta
ada ya ukaguzi wa madini ya chumvi (Inspection
and Clearance fee) inayotozwa kwa kiwango cha asilimia moja (1%) ya thamani
ya madini;
c)
Kufuta
ushuru wa Mikoko (Mangrove Levy)
unaotozwa kwenye maeneo ya uzalishaji wa chumvi kwa kiwango cha shillingi
100,000 kwa eka moja kwa mwaka;
d)
Kufuta
ada ya kupitia andiko la mradi kwenye sekta ya uzalishaji chumvi inayotozwa na
Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira;
e)
Kufuta
ada ya usajili wa Jangwa la Chumvi (Solar
Salt Panel);
f)
Kufuta
ada ya Usimamizi kwenye eneo la Chumvi (Supervision
fee) inayotozwa na Wakala wa Misitu
Tanzania;
g)
Kufuta
ada ya usajili wa mradi wa uzalishaji chumvi inayotozwa na Baraza la Taifa la
Usimamizi wa Mazingira;
h)
Kufuta
ada ya Ukaguzi wa Mazingira (Environmental
Impact Assesment) inayotozwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira
kwenye sekta ya uzalishaji chumvi;
i)
Kupunguza
ada ya gharama za ukaguzi wa usalama mahala pa kazi inayotozwa kwenye sekta ya
uzalishaji chumvi kutoka shilingi millioni 2 hadi shilingi millioni 1 kwa
mwaka; na
j)
Kupunguza
ada ya kibali cha kusafirisha madini ya chumvi nje ya nchi kutoka Dola za
Kimarekani 100 hadi shilingi 20,000 kwa mwaka.
(iii) Napendekeza kufanya
marekebisho ya ada na tozo zinazotozwa na Mamlaka ya Afya na Usalama (OSHA)
mahali pa kazi kama ifuatavyo:-
a)
Kufuta
ada inayotozwa kwenye fomu ya usajili sehemu za kazi;
b)
Kufuta
tozo ya usajili sehemu za kazi;
c)
Kufuta
faini zinazohusiana na vifaa vya kuzimia moto inayotozwa kwa kiwango cha
shilingi 500,000;
d)
Kufuta
Leseni ya kukidhi matakwa ya Sheria ya afya na usalama; na
e)
Kufuta
tozo ya ushauri wa kitaalam ya usalama wa afya.
63.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea
kufanya uchambuzi na tathmini ya tozo na ada zinazotozwa na mashirika, taasisi
na wakala mbalimbali ili kuendelea kuweka mazingira bora ya kufanya biashara na
kuwekeza na kuondoa kero kwa wananchi. Hii itajumuisha kupitia upya na
kuvisawazisha viwango vya tozo na ada hizo na pia kuondoa tozo na ada za
usumbufu.
l)
Tarehe ya Kuanza
Kutekeleza Hatua Mpya za Kodi
64.
Mheshimiwa Spika, hatua hizi za kodi
zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2018, isipokuwa pale
ilipoelezwa vinginevyo.
V.
SURA YA BAJETI KWA MWAKA 2018/19
65.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia shabaha na sera za bajeti kwa mwaka
2018/19, Sura ya Bajeti inaonesha kuwa jumla ya shilingi trilioni 32.48 zinatarajiwa kukusanywa na
kutumika katika kipindi hicho. Jumla ya mapato ya ndani (ikijumuisha mapato ya
Halmashauri) yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 20.89, sawa na asilimia 64.3
ya bajeti yote. Kati ya mapato hayo, Serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi
ya jumla ya shilingi trilioni 18.0 sawa na asilimia 13.6 ya Pato la Taifa.
Aidha, mapato yasiyo ya kodi yanakadiriwa kuwa shilingi trilioni 2.16 na mapato
kutoka vyanzo vya Halmashauri shilingi bilioni 735.6.
66.
Mheshimiwa Spika, Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuchangia
shilingi trilioni 2.68 ambayo ni asilimia 8.2 ya bajeti yote. Misaada na mikopo
hii inajumuisha misaada na mikopo nafuu ya miradi ya maendeleo shilingi trilioni
2.0; mifuko ya pamoja ya kisekta shilingi bilioni 125.9; na misaada na mikopo
nafuu ya kibajeti (GBS) shilingi
bilioni 545.8.
67.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inatarajia kukopa
shilingi trilioni 8.90 kutoka soko la ndani na nje kwa masharti ya kibiashara.
Mikopo ya ndani inatarajiwa kuwa shilingi trilioni 5.79, ambapo shilingi trilioni
4.6 ni kwa ajili ya kulipia dhamana za Serikali zinazoiva (rollover) na shilingi trilioni 1.19 ni mikopo mipya kwa ajili ya
kugharamia miradi ya maendeleo. Ili kuongeza kasi katika ujenzi wa miundombinu,
Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 3.11 kutoka soko la nje.
68.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Serikali inapanga kutumia jumla
ya shilingi trilioni 32.48. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 20.47
zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ikijumuisha shilingi trilioni 7.41
za mishahara na shilingi trilioni 10.00 kwa ajili ya kulipia deni la Serikali,
michango ya Serikali kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na huduma nyinginezo.
Aidha, matumizi ya maendeleo yatakuwa shilingi trilioni 12.01 sawa na asilimia
37 ya bajeti yote, ambapo shilingi trilioni 9.88 ni fedha za ndani na shilingi trilioni
2.13 ni fedha za nje. Kiwango hiki cha bajeti ya maendeleo kimezingatia matakwa
ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 wa kutenga bajeti ya
maendeleo kati ya asilimia 30 na 40 ya bajeti yote.
69.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mfumo wa bajeti kama
nilivyoeleza, sura ya bajeti kwa mwaka 2018/19 ni kama inavyooneshwa katika Jedwali A.
Jedwali
A: Mfumo wa Bajeti ya Mwaka 2018/19
Chanzo: Wizara
ya Fedha na Mipango
VI.
HITIMISHO
70.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia
kusema hapo awali, dhima ya bajeti ya mwaka 2018/19 ni kuendelea “kujenga uchumi wa viwanda utakaochochea
ajira na ustawi endelevu wa jamii”. Mageuzi haya ya uchumi wa viwanda
yatajengwa kupitia ushiriki wetu katika shughuli za kiuchumi, ubia na
kuunganisha juhudi zetu pamoja. Ili kufikia malengo tunayoyakusudia, maamuzi
magumu ni lazima yafanyike katika kuelekeza rasilimali chache tulizonazo katika
maeneo ya kimkakati. Mabadiliko yoyote ni vigumu kuyakubali na mara nyingi
mabadiliko hupingwa. Naomba Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla
tuunganishe nguvu zetu, vipaji vya wananchi wetu na biashara zetu ili kufikia
malengo tunayoyakusudia. Hivyo, tunahitaji uzalendo na nidhamu ya kazi ya hali
ya juu tukikusudia kuondoa umasikini, kuongeza ajira na kuwa na uchumi
jumuishi.
71.
Mheshimiwa Spika, ili kufikia malengo hayo,
Serikali itaendelea kuchukua hatua zaidi kuongeza uzalishaji katika sekta za
viwanda na kilimo na ukusanyaji wa mapato ya ndani yatakayowezesha ugharamiaji wa
miradi ya maendeleo na matumizi ya kawaida na hivyo kupunguza utegemezi. Hatua
hizo ni pamoja na: kuvutia uwekezaji; kuelekeza rasilimali kwenye maeneo
machache yenye tija; kusimamia utekelezaji wa sheria za kodi; kurasimisha sekta
isiyo rasmi ikiwemo usajili wa wamiliki wa ardhi na majengo katika mfumo wa
walipa kodi; na kuhimiza matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika miamala
mbalimbali ikiwemo matumizi ya EFD na
kadi za kielectroniki za benki (Debt/credit
cards) katika maeneo yanayotoa huduma kama vile katika maduka makubwa,
hoteli na vituo vya mafuta. Hivyo, napenda kuwahimiza Watanzania tuwajibike
kulipa kodi na kuhakikisha tunatoa na kudai risiti kulingana na muamala uliofanyika. Aidha,
Serikali inawashukuru kwa dhati wananchi wote ambao wameonesha uzalendo kwa
kuendelea kulipa kodi kwa hiari.
72.
Mheshimiwa Spika, kipaumbele kikuu cha
Serikali ni kujenga uchumi wa viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana
nchini hususan zinazotokana na kilimo, mifugo na uvuvi ili kupanua fursa za
ajira, kuboresha upatikanaji na ubora wa huduma za jamii (maji, afya, elimu) na
kupunguza umaskini. Aidha, Serikali itaendeleza mapambano dhidi ya rushwa,
kuimarisha ulinzi wa rasilimali za umma na kudhibiti matumizi ya fedha za umma.
Serikali pia itaongeza msukumo katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji
kwa kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara (Blueprint for Regulatory Reforms to Improve
the Business Environment). Mpango huu, pamoja na mambo mengine unakusudia
kuhuisha na kurahisisha taratibu za kulipa kodi, tozo na ada mbalimbali.
73.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya awamu ya tano
inalenga kujenga utamaduni na nidhamu ya
kukubali maoteo halisia ya ukusanyaji wa mapato ambayo yanapaswa kuwa ukomo wa
matumizi (expenditure ceiling)
badala ya utarabu uliozoeleka wa kuanza kupanga au kuorodhesha mahitaji kwanza.
Hivyo, Serikali itajielekeza katika utekelezaji wa miradi michache ya kimkakati
kwa namna ambayo itashirikisha sekta zote zinazotegemeana na kuhakikisha kuwa
miradi hiyo inakamilika kabla ya kuanza miradi mipya.
74.
Mheshimiwa Spika, mimi ni mpenzi sana wa
kujisomea kuhusu maisha na sifa za viongozi mashuhuri, viongozi bora na wa
kipekee wa nchi mbalimbali waliofanikiwa kuongoza mabadiliko makubwa ya
kijamii, kisiasa na kiuchumi katika nchi zao kama vile Deng Tsiaoping –Jamhuri
ya Watu wa China; Dkt. Mahithir Mohamed – Malaysia; Lee Kuan Yew – Singapore;
Park Chung Hee – Korea, Nelson Mandela –Afrika ya Kusini, Baba wa Taifa Mwl.
Julius Nyerere, Quett Masire – Botswana nk. Nilichojifunza na nilieleza katika
hotuba ya bajeti kuu ya Serikali mwaka
jana kuwa viongozi wa aina hiyo wana sifa muhimu zifuatazo:
(i)
Dira au maono dhahiri kuhusu maendeleo ya nchi zao;
(ii)
Hawasiti kutekeleza dira hizo kwa dhamira kubwa tena bila
kusita au kubadili msimamo;
(iii)
Ni jasiri, shupavu na wenye kuthubutu kutekeleza jambo
wanaloliamini bila kigugumizi;
(iv)
Wana kipaji cha kujali maumivu ya wanyonge;
(v)
Ni waadilifu, wanachukia rushwa na ufisadi na ni wenye
nidhamu ya kazi ya hali ya juu;
(vi)
Wanaongoza kwa vitendo; na
(vii) Huvumilia magumu ili kuiletea nchi
mabadiliko chanya.
75.
Mheshimiwa Spika, ninapenda niwaambie tena
Watanzania kwamba Mwenyezi Mungu ametutunukia kiongozi Mkuu wa nchi Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli mwenye sifa hizo zote nilizotaja. Nilieleza mwanzoni mambo machache ambayo amethubutu
kutenda kwa kipindi kifupi kuthibitisha sifa hizo. Rai yangu kwa Watanzania
wenzangu ni kuwa tutumie fursa hii adimu kwa kufanya kazi kama njia bora ya kumuunga
mkono Rais wetu katika jitihada zake za kuijenga Tanzania mpya, Tanzania ya
Viwanda. Jambo hili ni muhimu kwa sababu kama Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere
alivyotabiri, katika safari ya maendeleo – ya kuelekea kujenga uchumi wa
viwanda – kiongozi wetu atakumbana na vikwazo na kelele nyingi za kuzomea
kutoka kwa wale wasiotutakia mema ili kutukatisha tamaa tusifikie malengo. Hivyo,
Watanzania wote tunao wajibu wa kumtia nguvu Rais wetu ili asirudi nyuma katika
safari aliyoianza na aweze kutuvusha kuifikia Tanzania ya viwanda. Niruhusu
nimalizie rai yangu kwa nukuu ya mazungumzo ya Mwalimu Nyerere kwa “TANU study Group” tarehe 13 Juni, 1967:
“Maendeleo na kazi
ni kitu kile kile, hakuna namna nyingine sisi ya kuendelea, hatukupewa namna
nyingine sisi ya kuendelea….. Huwezi kutenganisha vitu viwili hivi, kuendelea na kazi, kwani kazi ndiyo shughuli ya ….. kuondoa matatizo yanayomzuia binadamu hali
yake kukamilika…. Hakuna njia nyingine lazima kufanya kazi…… na kila unavyozidi
kufanya kazi kwa akili zaidi ndivyo mnavyozidi kwenda, ndivyo mnavyozidi
kuendelea,….. Kazi ndio utu …kazi ndio maendeleo…kazi ndio maisha, ni uhai,
kazi ndio civilization, ndio uungwana, ndio kula vizuri, ndio kuvaa vizuri,
ndio kuishi katika nyumba nzuri,…. ndio kushinda matatizo yote tuliyo nayo duniani
– namna ya kuyashinda ni kazi….”[1]
76.
Mheshimiwa Spika, ninapoelekea mwisho wa
hotuba hii, napenda kuwashukuru Washirika wa Maendeleo kwa misaada na mikopo wanayoendelea
kutupatia katika kutekeleza miradi na programu mbalimbali za maendeleo
nchini. Wahisani hao wanatarajiwa
kuchangia jumla ya shilingi bilioni 2,676.6 katika bajeti ya mwaka 2018/19 kama
ifuatavyo: Benki ya Dunia/IDA shilingi bilioni 863.13; Benki ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB) shilingi bilioni 358.63; Global Fund shilingi bilioni 313.90;
Sweden shilingi bilioni 179.80; Jumuiya ya Umoja wa Ulaya shilingi bilioni
158.40; India shilingi bilioni 104.57; Ujerumani (Kfw & GIZ) shilingi
bilioni 81.31; Japan/JICA shilingi bilioni 76.96; Uingereza/DFID shilingi
bilioni 71.21; Denmark shilingi bilioni 69.57; French/AFD shilingi bilioni
61.06; Canada shilingi bilioni 48.84; BADEA shilingi bilioni 40.01; Korea ya
Kusini/EDCH shilingi bilioni 39.05; UNICEF shilingi bilioni 36.53; Finland
shilingi bilioni 28.08; IFAD shilingi bilioni 26.82; Italy shilingi bilioni
22.05; Norway shilingi bilioni 20.04; Benki ya Uwekezaji ya Ulaya shilingi
bilioni 17.88; Uswisi shilingi bilioni 15.74; UNDP shilingi bilioni 12.34 ; Ubelgiji
shilingi bilioni 11.08; Saudi Arabia/Saud Fund shilingi bilioni 4.81; USAID
shilingi bilioni 4.20; OPEC/OFID shilingi bilioni 2.75; na UNFPA shilingi
bilioni 2.56. Ni matarajio yetu kuwa fedha zilizoahidiwa na marafiki zetu hawa
zitatolewa kama nilivyozisoma na kwa wakati muafaka. Sisi kama Serikali tunaahidi
kuwa fedha watakazotupatia zitatumika kama ilivyokusudiwa.
77.
Mheshimiwa Spika, ninakiri kuwa bajeti
niliyowasilisha isingekuwa hivi ilivyo bila kupata michango mizuri ya kuboresha
kutoka kwa Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu
Wakuu, Sekretariaeti ya Baraza la Mawaziri na wataalam wa wizara zote na
taasisi za Serikali. Ninatoa shukrani kwa kila mmoja wenu kwa michango mliyotoa
katika mchakato mzima wa maandalizi ya bajeti hii.
78.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kuwashukuru
viongozi wenzangu wa Wizara ya Fedha na Mipango, nikianza na Mheshimiwa Dkt.
Ashatu K. Kijaji, Mbunge wa Kondoa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, pia
Bwana Doto M. James, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu
wa Serikali, na Naibu Makatibu Wakuu, Bibi Amina Kh. Shaaban, Dkt. Khatibu M.
Kazungu, na Bibi Susan B. Mkapa. Wote hawa kwa pamoja wamenipatia ushirikiano
na msaada wa hali ya juu katika kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Wizara na
wameratibu vizuri maandalizi ya bajeti hii. Aidha, ninampongeza Profesa Florens
Dominick Makinyika Luoga kwa kuteuliwa na Rais kuwa Gavana mpya wa Benki Kuu ya
Tanzania na kwa kusimamia vema majukumu makubwa ya mhimili huo wa sekta ya
fedha akisaidiwa na Naibu Gavana watatu, Wakurugenzi na watumishi wote wa Benki
Kuu ya Tanzania. Vivyo hivyo, napenda kutambua kazi nzuri ya viongozi na watumishi
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania katika kukusanya mapato ya Serikali wakiongozwa
na Bw. Charles E. Kichere, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Profesa
Musa Assad, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Dkt. Albina
Chuwa, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu. Aidha, nampongeza Bwana
Athumani Selemani Mbuttuka aliyeteuliwa na Mheshimiwa Rais hivi karibuni kuwa
Msajili wa Hazina (Treasury Registrar).
79.
Mheshimiwa Spika, vile vile, ninawashukuru
Wakuu wengine wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango ikijumuisha
Mabenki (TADB, TIB-DFI, TIB-CBL,TPB Bank); Mifuko ya hifadhi ya jamii (PSPF,
GEPF, PPF); Rufani za kodi (TRAB, TRAT); Huduma za bima (TIRA,NIC); Mitaji na
dhamana (CMSA, TCEM, DSE); Dhamana za uwekezaji (UTT-MFI, UTT-AMIS,UTT-PID);
Bodi ya michezo ya kubahatisha; Taasisi za mafunzo (IFM, IRDP, IAA, TIA,
EASTC); na Mfuko wa huduma ndogo za fedha (SELF
Microfinance Fund). Nawashukuru pia Wakuu wa Idara na Vitengo, bila kuwasahau
wataalam, makatibu muhtasi, watunza kumbukumbu, madereva, wahudumu na walinzi
wa Wizara yetu na taasisi zake kwa kazi kubwa walizofanya katika mwaka 2017/18
na katika kukamilisha Bajeti hii.
80.
Mheshimiwa Spika, nashindwa kumaliza hotuba
hii bila kumtaja mke wangu na rafiki yangu mpenzi Mbonimpaye. Moyo wake wa
ibada kwa Mungu na uaminifu wake vimekuwa ndiyo nguzo yangu kuu katika utumishi
wangu. Ninamshukuru sana yeye pamoja na watoto na wajukuu wetu wote tuliopewa
na Mungu na familia nzima. Aidha, ninawiwa kuwashukuru wananchi wote wa
Tanzania (wakulima, wafanyakazi, na wafanyabiashara). Ninawashukuru sana kwa
uzalendo wao wa kufanya kazi kwa bidii na kulipa kodi kwa mujibu wa sheria kwa
ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Ninawashukuru pia wanafunzi wote wa shule za awali,
msingi, sekondari na vyuo wanaosoma kwa bidii maana miongoni mwao tutapata
viongozi na nguvukazi bora ya Taifa. Ninawashukuru pia Wazee wetu ambao walitoa
mchango mkubwa kwa Taifa letu katika umri wao wa kufanya kazi. Aidha, siwezi
kuwasahau wananchi wa wilaya za Buhigwe na Kasulu, na mkoa wetu wa Kigoma kwa
ujumla. Ninyi ni fahari yangu maana mlinikuza. Ninawapenda! Vile vile ninawashukuru
wananchi wenzangu wa Nzinje hapa Dodoma (Zuzu kwa jina la zamani), kwa
kunipokea vizuri mimi na familia yangu.
81.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa inatarajiwa leo
itakuwa siku ya mwisho wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan, naomba nihitimishe hotuba
hii kwa kuwatakia Waislamu wote Eid Mubarak.
82.
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema
ASANTE SANA MUNGU” kwa baraka zako zilizoniwezesha kukamilisha kusoma hotuba
hii. Na kwenu Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote …….
(i)
“SANDENYI SANA”!
(ii)
“NGW’ABHEJA SANA”
(iii)
“WAITU MWAKORA”
(iv)
“OKORREE BHUYA”
(v)
“HAIKENI SANA”
(vi)
“MSENGWILE”
(vii) “NDAGHA FIJO”
(viii)
“HEWELA”
(ix)
“KAJEKAJE”
(x)
“MURAKOZE CHANE”
(xi)
“ASANTENI SANA”
83.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja
Jedwali Na 1:
Mwenendo wa Makusanyo ya Mapato ya Serikali: 2011/12 -2018/19 Shilingi Milioni
|
||||||||||||||||||||||||||||||||
2012/13
|
2013/14
|
2014/15
|
2015/16
|
2016/17
|
2017/18
|
2017/18
|
2018/19
|
|||||||||||||||||||||||||
Halisi
|
Halisi
|
Halisi
|
Halisi
|
Halisi
|
Bajeti
|
Matarajio
|
Bajeti
|
|||||||||||||||||||||||||
Jumla ya Mapato (Yakijumuisha
Halmashauri)
|
8,442,611
|
11,537,523
|
10,957,765
|
14,139,230
|
16,639,933
|
19,977,001
|
18,692,251
|
20,894,578
|
||||||||||||||||||||||||
A. Mapato yanayotokana na
Kodi
|
7,729,986
|
10,395,440
|
9,908,996
|
12,525,378
|
14,126,590
|
17,106,336
|
15,312,632
|
18,000,219
|
||||||||||||||||||||||||
1. Ushuru wa Forodha
|
584,137
|
852,199
|
748,961
|
880,296
|
998,164
|
1,231,135
|
1,077,034
|
1,204,090
|
||||||||||||||||||||||||
2. Ushuru wa Bidhaa
|
1,258,242
|
1,908,857
|
1,742,721
|
2,144,395
|
2,106,442
|
2,776,302
|
2,248,954
|
2,541,287
|
||||||||||||||||||||||||
3. Kodi ya Ongezeko la Thamani
|
2,146,337
|
2,590,291
|
2,488,066
|
2,992,835
|
3,912,674
|
4,767,853
|
4,390,218
|
5,463,990
|
||||||||||||||||||||||||
4. Kodi ya Mapato
|
3,034,360
|
3,656,506
|
3,716,685
|
4,594,971
|
5,117,862
|
5,997,039
|
5,556,523
|
6,540,038
|
||||||||||||||||||||||||
5. Kodi Nyingine
|
706,910
|
1,387,587
|
1,212,563
|
1,912,880
|
1,991,449
|
2,334,006
|
2,039,904
|
2,250,814
|
||||||||||||||||||||||||
B. Mapato yasiyotokana na
Kodi
|
683,362
|
869,936
|
1,048,769
|
1,613,852
|
2,513,343
|
2,870,665
|
3,379,619
|
2,894,358
|
||||||||||||||||||||||||
1.
Michango na Gawio la Mashirika
|
47,602
|
110,014
|
161,234
|
388,551
|
893,935
|
529,583
|
646,415
|
597,770
|
||||||||||||||||||||||||
2. Wizara Nyingine na Mikoa
|
414,925
|
444,694
|
527,451
|
799,449
|
1,107,690
|
1,653,776
|
2,183,359
|
1,561,000
|
||||||||||||||||||||||||
3. Mapato ya Halmasahuri
|
220,835
|
315,228
|
360,084
|
425,852
|
511,718
|
687,306
|
549,845
|
735,589
|
||||||||||||||||||||||||
Chanzo: Wizara ya Fedha na Mipango
Jedwali 2a: Mfumo wa Bajeti
2011/12-2018/19 Shilingi Milioni
2010/11
|
2011/12
|
2012/13
|
2013/14
|
2014/15
|
2015/16
|
2016/17
|
2017/18
|
2017/18
|
2018/19
|
|
Halisi
|
Halisi
|
Halisi
|
Halisi
|
Halisi
|
Halisi
|
Halisi
|
Bajeti
|
Matarajio
|
Matarajio
|
|
I.
Mapato Yote
|
10,202,603
|
12,171,877
|
15,404,216
|
15,667,535
|
17,488,626
|
22,543,664
|
25,417,791
|
31,711,986
|
28,619,612
|
32,475,949
|
Mapato ya Ndani
|
5,577,986
|
7,025,884
|
8,221,776
|
9,867,227
|
10,597,681
|
13,622,182
|
16,128,215
|
19,289,695
|
17,639,052
|
20,158,989
|
Mapato ya Halmashauri
|
158,280
|
195,525
|
220,835
|
315,228
|
360,084
|
425,852
|
511,718
|
687,306
|
549,845
|
735,589
|
Misaada na Mikopo ya Bajeti
|
900,825
|
967,163
|
894,955
|
1,040,659
|
757,016
|
291,381
|
342,785
|
941,258
|
684,227
|
545,765
|
Misaada na Mikopo ya Miradi
|
1,013,078
|
1,207,445
|
1,423,579
|
1,194,930
|
1,154,909
|
1,186,982
|
1,857,399
|
2,473,770
|
1,804,663
|
2,005,016
|
Mikopo ya Kisekta (Basket Loans)
|
220,681
|
172,212
|
186,336
|
207,665
|
163,177
|
161,842
|
104,991
|
355,454
|
355,454
|
33,701
|
Misaada ya Kisekta (Basket Grants)
|
334,609
|
301,152
|
280,936
|
188,623
|
127,637
|
86,199
|
168,984
|
200,621
|
177,799
|
92,163
|
MCA (T) USA
|
196,114
|
221,601
|
220,350
|
213,612
|
0
|
0
|
0
|
0
|
0
|
0
|
Mikopo ya Ndani (Rollover)
|
720,249
|
1,326,852
|
1,734,535
|
1,528,153
|
2,064,756
|
3,005,789
|
4,615,670
|
4,948,229
|
4,835,199
|
4,600,000
|
Mikopo ya
Ndani (Financing)
|
1,244,330
|
334,864
|
1,069,321
|
976,712
|
799,776
|
2,299,151
|
1,300,000
|
1,220,668
|
1,199,373
|
1,193,669
|
Marekebisho
|
-317,498
|
-382,101
|
88,588
|
-1,059,790
|
408,786
|
1,010,781
|
-838,731
|
0
|
0
|
0
|
Mikopo ya kibiashara
|
153,948
|
801,282
|
1,063,006
|
1,194,516
|
1,054,803
|
453,504
|
1,226,760
|
1,594,985
|
1,374,000
|
3,111,058
|
II.
Matumizi Yote
|
10,202,602
|
12,171,877
|
15,404,216
|
15,667,535
|
17,488,626
|
22,543,664
|
25,417,791
|
31,711,986
|
28,619,612
|
32,475,950
|
Matumizi ya Kawaida
|
7,453,565
|
8,397,155
|
10,904,521
|
11,741,493
|
13,778,397
|
18,204,111
|
18,144,967
|
19,712,394
|
19,302,746
|
20,468,676
|
CFS
|
1,625,883
|
2,518,207
|
3,383,124
|
3,666,799
|
4,724,910
|
6,480,906
|
8,643,560
|
9,461,433
|
9,892,197
|
10,004,480
|
Kulipa Madeni
|
1,116,572
|
1,843,666
|
2,627,946
|
2,686,455
|
3,552,426
|
5,047,764
|
7,234,530
|
7,829,918
|
8,260,682
|
8,372,951
|
Malipo Mengine
|
509,311
|
674,541
|
755,178
|
980,344
|
1,172,484
|
1,433,142
|
1,409,030
|
1,631,515
|
1,631,515
|
1,631,529
|
Matumizi ya Kawaida (Bila CFS)
|
5,827,682
|
5,878,949
|
7,521,397
|
8,074,693
|
9,053,487
|
11,723,205
|
9,501,407
|
10,250,961
|
9,410,549
|
10,464,196
|
o/w
Malipo ya Mishahara
|
2,346,378
|
2,722,084
|
3,349,959
|
3,969,108
|
4,617,648
|
5,627,497
|
5,599,246
|
6,276,267
|
5,962,454
|
6,386,265
|
Mishahara
ya Mashirika
|
457,665
|
455,006
|
518,755
|
568,708
|
637,711
|
925,760
|
767,901
|
929,501
|
883,026
|
1,023,687
|
Fedha ya
Halmashauri
|
158,280
|
195,525
|
362,206
|
315,228
|
170,627
|
170,340
|
251,484
|
274,922
|
274,922
|
389,862
|
Matumizi Mengine
|
3,628,554
|
2,506,333
|
3,290,477
|
3,221,649
|
3,627,501
|
4,999,607
|
2,882,775
|
2,770,270
|
2,290,147
|
2,664,382
|
Matumizi ya Maendeleo
|
2,749,037
|
3,774,722
|
4,499,695
|
3,926,042
|
3,710,228
|
4,339,553
|
7,272,824
|
11,999,592
|
9,316,866
|
12,007,273
|
Fedha za Ndani
|
984,555
|
1,872,312
|
2,314,718
|
2,121,212
|
2,264,506
|
2,904,530
|
5,141,451
|
8,969,747
|
6,978,950
|
9,876,393
|
Fedha za Nje
|
1,764,482
|
1,902,410
|
2,184,977
|
1,804,831
|
1,445,722
|
1,435,023
|
2,131,374
|
3,029,845
|
2,337,916
|
2,130,880
|
Pato la
Taifa
|
48,607,221
|
57,098,397
|
66,193,721
|
75,197,863
|
85,153,090
|
97,304,216
|
106,589,234
|
120,866,799
|
118,737,328
|
132,629,849
|
Chanzo: Wizara ya Fedha na Mipango
Jedwali
2b: Mfumo wa Bajeti 2010/11 - 2018/19
|
|||||||||
Asilimia
ya Pato la Taifa
|
|||||||||
2011/12
|
2012/13
|
2013/14
|
2014/15
|
2015/16
|
2016/17
|
2017/18
|
2017/18
|
2018/19
|
|
Halisi
|
Halisi
|
Halisi
|
Halisi
|
Halisi
|
Halisi
|
Bajeti
|
Matarajio
|
Bajeti
|
|
Mapato Yote
|
21.3%
|
23.3%
|
20.8%
|
20.5%
|
23.2%
|
23.8%
|
26.2%
|
24.1%
|
24.5%
|
Mapato ya Ndani
|
12.3%
|
12.4%
|
13.1%
|
12.4%
|
14.0%
|
15.1%
|
16.0%
|
14.9%
|
15.2%
|
LGAs own source
|
0.3%
|
0.3%
|
0.4%
|
0.4%
|
0.4%
|
0.5%
|
0.6%
|
0.5%
|
0.6%
|
Misaada na Mikopo ya Bajeti
|
1.7%
|
1.4%
|
1.4%
|
0.9%
|
0.3%
|
0.3%
|
0.8%
|
0.6%
|
0.4%
|
Misaada na Mikopo ya Miradi
|
2.1%
|
2.2%
|
1.6%
|
1.4%
|
1.2%
|
1.7%
|
2.0%
|
1.5%
|
1.5%
|
Mikopo ya Kisekta (Basket Loans)
|
0.3%
|
0.3%
|
0.3%
|
0.2%
|
0.2%
|
0.1%
|
0.3%
|
0.3%
|
0.0%
|
Misaada ya Kisekta (Basket Grants)
|
0.5%
|
0.4%
|
0.3%
|
0.1%
|
0.1%
|
0.2%
|
0.2%
|
0.1%
|
0.1%
|
MCA (T) USA
|
0.4%
|
0.3%
|
0.3%
|
0.0%
|
0.0%
|
0.0%
|
0.0%
|
0.0%
|
0.0%
|
Mikopo ya Ndani (Rollover)
|
2.3%
|
2.6%
|
2.0%
|
2.4%
|
3.1%
|
4.3%
|
4.1%
|
4.1%
|
3.5%
|
Mikopo ya
Ndani (Financing)
|
0.6%
|
1.6%
|
1.3%
|
0.9%
|
2.4%
|
1.2%
|
1.0%
|
1.0%
|
0.9%
|
Marekebisho
|
-0.7%
|
0.1%
|
-1.4%
|
0.5%
|
1.0%
|
-0.8%
|
0.0%
|
0.0%
|
0.0%
|
Mikopo yenye masharti ya kibiashara
|
1.4%
|
1.6%
|
1.6%
|
1.2%
|
0.5%
|
1.2%
|
1.3%
|
1.2%
|
2.3%
|
II. Matumizi Yote
|
21.3%
|
23.3%
|
20.8%
|
20.5%
|
23.2%
|
23.8%
|
26.2%
|
24.1%
|
24.5%
|
Matumizi ya Kawaida
|
14.7%
|
16.5%
|
15.6%
|
16.2%
|
18.7%
|
17.0%
|
16.3%
|
16.3%
|
15.4%
|
CFS
|
4.4%
|
5.1%
|
4.9%
|
5.5%
|
6.7%
|
8.1%
|
7.8%
|
8.3%
|
7.5%
|
Kulipa Madeni
|
3.2%
|
4.0%
|
3.6%
|
4.2%
|
5.2%
|
6.8%
|
6.5%
|
7.0%
|
6.3%
|
Malipo Mengine
|
1.2%
|
1.1%
|
1.3%
|
1.4%
|
1.5%
|
1.3%
|
1.3%
|
1.4%
|
1.2%
|
Matumizi ya Kawaida (Bila CFS)
|
10.3%
|
11.4%
|
10.7%
|
10.6%
|
12.0%
|
8.9%
|
8.5%
|
7.9%
|
7.9%
|
o/w Malipo ya Mishahara
|
4.8%
|
5.1%
|
5.3%
|
5.4%
|
5.8%
|
5.3%
|
5.2%
|
5.0%
|
4.8%
|
Mishahara ya Mashirika
|
0.8%
|
0.8%
|
0.8%
|
0.7%
|
1.0%
|
0.7%
|
0.8%
|
0.7%
|
0.8%
|
Fedha za Halmashauri
|
0.3%
|
0.5%
|
0.4%
|
0.2%
|
0.2%
|
0.2%
|
0.2%
|
0.2%
|
0.3%
|
Matumizi Mengine
|
4.4%
|
5.0%
|
4.3%
|
4.3%
|
5.1%
|
2.7%
|
2.3%
|
1.9%
|
2.0%
|
Matumizi ya Maendeleo
|
6.6%
|
6.8%
|
5.2%
|
4.4%
|
4.5%
|
6.8%
|
9.9%
|
7.8%
|
9.1%
|
Fedha za Ndani
|
3.3%
|
3.5%
|
2.8%
|
2.7%
|
3.0%
|
4.8%
|
7.4%
|
5.9%
|
7.4%
|
Fedha za Nje
|
3.3%
|
3.3%
|
2.4%
|
1.7%
|
1.5%
|
2.0%
|
2.5%
|
2.0%
|
1.6%
|
Chanzo: Wizara ya Fedha na Mipango
|
Jedwali Na. 3 Misaada na Mikopo Nafuu kutoka Nje 2014/15 - 2018/19
|
|||||||
Shilingi Milioni
|
|||||||
2014/15
|
2015/16
|
2016/17
|
2017/18
|
2017/18
|
2018/19
|
||
Halisi
|
Halisi
|
Halisi
|
Bajeti
|
Matarajio
|
Bajeti
|
||
Misaada ya Kibajeti
|
Misaada
|
546,709
|
0
|
190,303
|
190,023
|
190,613
|
236,264
|
Mikopo yenye Masharti
Nafuu
|
375,459
|
291,381
|
152,482
|
751,235
|
493,614
|
309,501
|
|
Jumla
|
922,168
|
291,381
|
342,785
|
941,258
|
684,227
|
545,765
|
|
Mifuko ya Kisekta
|
Misaada
|
189,112
|
86,199
|
168,984
|
200,621
|
177,799
|
92,163
|
Mikopo yenye Masharti
Nafuu
|
84,975
|
161,842
|
104,991
|
355,454
|
355,454
|
33,701
|
|
Jumla
|
274,087
|
248,041
|
273,975
|
556,075
|
533,253
|
125,864
|
|
Miradi ya Maendeleo
|
Misaada
|
745,344
|
409,157
|
733,208
|
853,815
|
607,101
|
752,982
|
Mikopo yenye Masharti
Nafuu
|
1,000,000
|
777,825
|
1,124,190
|
1,820,576
|
1,197,563
|
1,252,035
|
|
Jumla
|
1,745,344
|
1,186,982
|
1,857,399
|
2,674,391
|
1,804,663
|
2,005,016
|
|
Jumla Kuu
|
2,941,599
|
1,726,404
|
2,474,159
|
4,171,723
|
3,022,143
|
2,676,645
|
|
Chanzo: Wizara ya Fedha na Mipango
Chanzo: Wizara ya Fedha na Mipango
Comments
Post a Comment