Featured Post

WIZARA YA MAMBO YA NDANI YAOMBA BAJETI YA SHS. BILIONI 946


HOTUBA YA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI
MHE. DKT. MWIGULU LAMECK NCHEMBA (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI
KWA MWAKA 2018/19
A.  UTANGULIZI

1.     Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu, baada ya kuzingatia taarifa iliyowasilishwa hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, likubali kupokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2018/19.


2.   Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na kuniwezesha kuwasilisha Hotuba ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambayo itajadiliwa na Bunge hili.

3.   Mheshimiwa Spika, pia natumia fursa hii kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Kwa kuongoza vema Taifa letu Na kuendelea kusimamia amani, utulivu na usalama nchini. Ni dhahiri kuwa hali ya usalama ni nguzo muhimu katika kuleta maendeleo ya uchumi wa viwanda ambayo ni azma ya Serikali ya Awamu ya Tano.

4.   Mheshimiwa Spika, vilevile, napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru Viongozi Wote Wakuu wa Serikali na Bunge kwa kuendelea kusimamia shughuli mbalimbali za Taifa. Aidha, nawashukuru wajumbe wote wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama chini ya Mwenyekiti wake, Mhe. Mussa Azzan Zungu, Mbunge wa Jimbo la Ilala, kwa kuyachambua Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2018/19. Ushauri uliotolewa na Kamati utasaidia katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara hii.

5.    Mheshimiwa Spika, naomba kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza ndugu zao kutokana na maafa, majanga na ajali mbalimbali zilizotokea katika kipindi cha mwezi Julai, 2017 mpaka sasa.

B.       UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA WIZARA KWA MWAKA 2017/18 NA MALENGO YA MPANGO NA BAJETI KWA
MWAKA 2018/19

Mapato na Matumizi

6.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Wizara iliendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia vipaumbele vilivyopangwa. Wizara iliidhinishiwa bajeti ya jumla ya Shilingi 930,396,817,000 ambapo Shilingi 367,706,884,000 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo, Shilingi 522,681,568,000 ni Mishahara na Shilingi 40,008,365,000 ni fedha za Miradi ya Maendeleo.

7.     Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Machi, 2018 Wizara ilipokea jumla ya Shilingi 725,328,535,604 sawa na asilimia 78 ya bajeti yote. Kati ya fedha hizo, Shilingi 21,800,000,000 zilikuwa ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo, sawa na asilimia 54 ya bajeti ya maendeleo, Shilingi 367,055,054,909 zilikuwa ni Mishahara na Shilingi 336,473,480,695 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo. Pia, Wizara ilikusanya mapato ya Shilingi 187,075,690,821 sawa na asilimia 63 ya lengo la kukusanya Shilingi 293,822,132,859. Katika mwaka 2018/19 Wizara inatarajia kukusanya jumla ya Shilingi 297,014,614,300.

Mafanikio ya Wizara

8.   Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu na shughuli za Wizara kwa kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2018 mafanikio mbalimbali yamepatikana ikiwa ni pamoja na: kukamilika kwa ujenzi wa nyumba za kuishi familia 32 za askari wa Jeshi la Polisi Mkoani Arusha; kukamilika kwa ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Rungwe; kukamilika kwa asilimia 97 kwa ujenzi wa Vituo vya Polisi Daraja A Mburahati na Daraja B Mbweni – Dar es Salaam; kuhuishwa kwa mfumo wa ufuatiliaji wa mienendo ya kesi za jinai ili kuharakisha upelelezi wa kesi; na kuanzishwa kwa Mkoa Mpya wa Kipolisi Rufiji.

9.   Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine ni pamoja na kuzinduliwa kwa Mradi wa Uhamiaji Mtandao (e- immigration) mwezi Januari, 2018 kwa kuanza na utoaji wa pasipoti za Tanzania za kielektroni za Afrika Mashariki; kukamilika kwa Kituo cha Kutunzia Kumbukumbu (Data Centre) na Kituo cha Uokozi wakati wa Majanga (Data Recovery Centre) kwa ajili ya utambuzi na usajili wa watu; na kukamilika kwa ofisi 13 za usajili za wilaya Tanzania Bara na Zanzibar.

10.     Mheshimiwa Spika, Mpango na Bajeti ya Wizara kwa Mwaka 2018/19 umezingatia: Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/17 –2020/21; Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 - 2020; Mpango Mkakati wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi 2016/17 – 2020/21; Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kudhibiti na Kuzuia Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto 2017/18 – 2021/22; Maagizo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Viongozi wa Juu wa Taifa yaliyotolewa kwa nyakati tofauti; na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti wa Mwaka 2018/19. Utekelezaji wa shughuli za Wizara kwa mwaka 2017/18 na Malengo ya Mpango na Bajeti kwa mwaka 2018/19 ni kama ifuatavyo:

JESHI LA POLISI

 Hali ya Usalama Nchini

11.       Mheshimiwa Spika, amani na utulivu ni muhimu katika maendeleo ya nchi yetu kiuchumi, kijamii na kisiasa. Jeshi la Polisi limeendelea kuchukua hatua stahiki za kubaini, kuzuia na kudhibiti uhalifu wa aina zote ili kuendelea kuwa na nchi yenye utulivu utakaowezesha shughuli za kiuchumi na kijamii kufanyika kwa ufanisi.

12.      Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwepo kwa hali ya amani na utulivu nchini yamejitokeza matukio kadhaa ya uhalifu. Katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2018 jumla ya makosa makubwa ya jinai 47,236 yaliripotiwa ikilinganishwa na makosa 56,913 yaliyoripotiwa kipindi kama hicho mwaka 2016/17. Kwa jumla makosa hayo yamepungua kwa asilimia 17. Kati ya makosa hayo, 44,866 yaliripotiwa Tanzania Bara na 2,370 Tanzania Zanzibar ambapo makosa 9,252 yalikuwa dhidi ya binadamu, 23,278 ya kuwania mali na 14,706 ya maadili ya jamii. Kutokana na matukio hayo ya uhalifu jumla ya watuhumiwa 42,702 walikamatwa na kufikishwa mahakamani. Katika mwaka 2018/19 Wizara kupitia Jeshi la Polisi itaendelea kuimarisha mbinu za kubaini, kuzuia na kupambana na uhalifu pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kushirikiana na Jeshi la Polisi kudhibiti vitendo vya uhalifu nchini.

13.      Mheshimiwa Spika, kati ya mwezi Julai, 2017 hadi Machi, 2018 Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata silaha haramu 358 na risasi 1,970 kwa mchanganuo ufuatao: gobore 224 na risasi 127; shortgun 43 na risasi 654; bastola 36 na risasi 208; SMG 19 na risasi 423; SAR mbili (2); Mark iv mbili (2) na risasi 85, Riffle 23 na risasi 410; Uzi Gun tano (5) na risasi moja (1); AK 47 nne (4) na risasi 55; na risasi saba (7) za G3. Watuhumiwa 333 waliopatikana na silaha hizo wamekamatwa na kufikishwa mahakamani ambapo kesi zipo katika hatua mbalimbali. Katika mwaka 2018/19 Jeshi la Polisi litaendelea kutoa elimu ya kuhamasisha umma kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu pamoja na zile za watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria.

Hali ya Usalama Barabarani

14.      Mheshimiwa Spika, hali ya usalama barabarani imeendelea kuimarika kutokana na hatua za kisheria zinazoendelea kuchukuliwa kwa madereva na wamiliki wa vyombo vya moto. Katika kipindi cha mwezi Julai, 2017 hadi Machi, 2018 jumla ya ajali 4,180 za barabarani ziliripotiwa. Aidha, ajali 1,613 zilisababisha vifo vya watu 1,985 na watu 4,447 kujeruhiwa. Takwimu zinaonyesha kupungua kwa ajali hizo kwa asilimia 35.7 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2016/17. Ajali nyingi kati ya hizo zimesababishwa na madereva kutozingatia Sheria za Usalama Barabarani na ubovu wa miundombinu katika baadhi ya maeneo. Aidha, katika kipindi hicho jumla ya madereva 5,185 walikamatwa kwa makosa mbalimbali ya usalama barabarani kwa kukiuka Sheria na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria. Kati ya hao madereva wa magari walikuwa 4,102 na waendesha pikipiki 1,083.

15.      Mheshimiwa Spika, ili kupunguza ajali za barabarani, Wizara kwa kushirikiana na wadau imeandaa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani Sura, 168, ambayo pamoja na mambo mengine inapendekeza kuzuia matumizi mabaya ya simu wakati dereva anapoendesha gari, kuondoa nukta kwenye leseni za madereva wanaokiuka Sheria za Usalama Barabarani na kufanya maboresho ya Baraza la Taifa la Usalama Barabarani kulifanya kuwa tendaji na taasisi kiongozi (Leading Agency) katika masuala ya usalama barabarani.

16.      Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Jeshi la Polisi (Kikosi cha Usalama Barabarani) itaendelea kudhibiti mwendokasi kwa kutumia vifaa vya kudhibiti mwendo huo (Speed Radar) na kufanya operesheni na doria za magari barabarani wakati wote. Aidha, Wizara itaendelea kufuta leseni za madereva wanaofanya makosa hatarishi barabarani, kutoa elimu ya Usalama Barabarani kwa umma na mashuleni, kufanya ukaguzi wa mabasi ya abiria kabla hayajaanza safari, kusimamia mfumo wa kielektroniki wa udhibiti mwenendo  wa mabasi barabarani (Vehicle Tracking System – VTS) kwa  kushirikiana na SUMATRA na kupima kiwango cha ulevi wa madereva.

17.      Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha usimamizi wa usalama barabarani, masuala yote yanayohusu vyombo vya moto na madereva, hususan katika mafunzo ya udereva na utoaji wa leseni yatafanywa na Jeshi la Polisi kwa mujibu wa Sheria. Aidha, nasisitiza kuwa vifaa vyote vinavyofungwa kwenye vyombo vya moto, vinavyohusu usalama barabarani (kama vile ving’ora na taa za vimulimuli) wahusika wawasiliane na Jeshi la Polisi.

18.     Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa mamlaka zote zinazofanya operesheni na kazi mbalimbali zinazohusu shughuli zote za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na ukamataji wa vyombo vya moto, ufungaji wa minyororo kwenye matairi hasa kwenye maeneo ya maegesho, kugeuza maeneo ya pembezoni mwa barabara kuwa maegesho ya magari na kutoza fedha za maegesho, kutoza fedha kwa magari yanayofika katika maeneo ya huduma za kijamii, hususan hospitali ni vyema mamlaka husika ziwasiliane na Jeshi la Polisi ili kuondoa kero na malalamiko yanayotokana na operesheni hizo.

Miradi ya Ujenzi wa Makazi na Vituo vya Polisi

19.      Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na sekta binafsi limekamilisha ujenzi wa nyumba za kuishi familia 31 za askari Mkoani Arusha. Mradi wa nyumba hizo ulizinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli tarehe 07 Aprili, 2018. Katika uzinduzi huo Mhe. Rais alitoa ahadi ya Shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya askari wa ngazi za chini. Jeshi la Polisi linatarajia kutumia fedha hizo kujenga nyumba 400 katika mikoa yote nchini. Nachukua nafasi hii kumshukuru kwa dhati Mhe. Rais kwa kusaidia kuboresha makazi ya askari. Aidha, napenda kutoa rai kwa Wakuu wa Mikoa wote nchini kutekeleza agizo la Mhe. Rais la kushirikiana na mashirika ya Umma na sekta binafsi katika kufanikisha ujenzi wa makazi ya askari na vituo vya Polisi katika mikoa yote nchini.

20.    Mheshimiwa Spika, vilevile, Jeshi la Polisi limekamilisha ukarabati wa iliyokuwa Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya Ofisi ya Makao Makuu ya muda ya Jeshi la Polisi. Aidha, ujenzi wa ofisi mpya ya Jeshi la Polisi katika eneo hilo umefikia asilimia 40. Vilevile, ujenzi wa nyumba za kuishi familia 48 za askari katika eneo la  Mabatini – Mwanza na Musoma – Mara zenye uwezo wa kuishi familia 24 kwa kila mkoa unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni, 2018.

21.      Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali limekamilisha ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Rungwe. Aidha, ujenzi wa Vituo vya Polisi Daraja A Mburahati na Daraja B Mbweni – Dar es Salaam umefikia asilimia 97 na Kituo cha Polisi Mbweni kimeanza kutumika.

22.    Mheshimiwa Spika, hatua za ujenzi katika maeneo mengine ni kama ifuatavyo: ujenzi wa Vituo vya Polisi daraja C Mkoani Lindi katika maeneo ya Mtama, Londo, Mchinga, Nanjilinji na Ikokoto vyote vimefikia wastani wa asilimia 50; ujenzi wa nyumba nane (8) za makazi ya askari Mkoani Kigoma umefikia asilimia 40; ujenzi wa Kituo cha Polisi daraja C  Mkinga Madebe - Handeni pamoja na nyumba tatu (3) za makazi ya askari zinazofadhiliwa na Kampuni ya Tanga Cement zote zimefikia asilimia 55; ujenzi wa Vituo vya Polisi daraja C katika maeneo ya Kombeni na Amani Zanzibar umefikia asilimia 40; ujenzi wa Kituo cha Polisi daraja C Kinyasini Zanzibar umefikia asilimia 10; ujenzi wa nyumba mbili (2) za makazi na Vituo vya Polisi daraja C katika maeneo ya Kamogi, Kakese na Karema Mkoani Katavi umefikia asilimia 55. Kazi hizo za ujenzi zitaendelea na kukamilika katika mwaka 2018/19.

23.    Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kuwapongeza wananchi wote waliochangia katika miradi hiyo kwa lengo la kuimarisha ulinzi katika maeneo yao.  Hiki ni kielelezo kuwa tukiamua tunaweza, hivyo natoa wito kwa wananchi kuendeleza jitihada hizi katika maeneo mengine nchini.

24.    Mheshimiwa Spika, kazi ya upanuzi wa Chuo cha Polisi Moshi kwa ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China inaendelea. Ujenzi wa mabweni yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 662 na madarasa ya wanafunzi 320 umefikia asilimia 50. Kazi hiyo inatarajiwa kukamilika  katika mwaka 2018/19.

Udhibiti wa Dawa za Kulevya Nchini

25.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2018 Jeshi la Polisi lilikamata jumla ya kilogramu 8.44 za dawa za viwandani. Watuhumiwa 833 wamefikishwa mahakamani, ambapo kesi zipo katika hatua mbalimbali. Aidha, kilogramu 37,786.8 za bhangi na kilogramu 6,956.6 za mirungi zilikamatwa na watuhumiwa 9,005 walifikishwa mahakamani. Vilevile, mashamba ya bhangi 59 yenye takribani ekari 206.6 yaliteketezwa na watuhumiwa 39 walikamatwa na kufikishwa mahakamani.

Kuboresha Mfumo wa Upelelezi wa Kesi za Jinai

26.    Mheshimiwa Spika, mfumo wa ufuatiliaji wa mienendo ya kesi za jinai umehuishwa ili kuhakikisha upelelezi wa kesi unakamilika kwa wakati na hivyo kupunguza malalamiko kwa wananchi. Mfumo huo unaofahamika kama Dossier Management Sytem unaimarisha ufuatiliaji wa kesi kuanzia jalada linapofunguliwa Kituo cha Polisi hadi linapofikishwa mahakamani.  Mfumo huo pia hutumia taarifa kutoka Maabara ya Uchunguzi wa Kisayansi ambayo imeimarishwa kwa kukamilisha ufungaji wa mfumo wa uchunguzi wa vinasaba vya binadamu.

27.     Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi linaendelea kuimarisha ushirikiano na wadau wa Haki Jinai katika hatua mbalimbali za mashauri ya jinai na kuimarisha vitengo vya ukaguzi kuanzia ngazi ya Makao Makuu ya Polisi, Mikoa, Wilaya na Vituo ili kutatua mlundikano wa kesi.

Hatua za Utatuzi kwa Wananchi Kubambikiwa Kesi

28.    Mheshimiwa Spika, tatizo la kubambikiwa kesi kwa wananchi limepungua baada ya Jeshi la Polisi kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na: kuimarisha mfumo wa kusimamia mashauri ya jinai na kuyapitia kabla ya kupelekwa kwa Mwanasheria wa Serikali; kuimarisha ushirikiano kati ya wapelelezi na waendesha mashtaka kuanzia hatua za awali za upelelezi mpaka hatua ya mwisho wa kesi mahakamani; na ukaguzi wa mahabusu/wafungwa unaofanywa na wadau wa Haki Jinai katika Vituo vya Polisi na magerezani.
Usalama wa Makundi Maalum

29.    Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai, 2017 hadi Machi, 2018 jumla ya watu 117 (wazee/vikongwe) waliuawa, kati ya hao wanawake 26 na wanaume 91. Matukio hayo yalitokea katika Mikoa ya  Arusha 6, Dodoma 1, Geita 9, Iringa 1, Kagera 10, Katavi 3, Kigoma 1, Mara 2, Mbeya 7, Morogoro 2, Mwanza 9, Njombe 5, Rukwa 10, Shinyanga 3, Simiyu 5, Singida 6, Songwe 12 na Tabora 25. Aidha, katika kipindi hicho matukio mawili (2) ya kujeruhiwa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi yaliripotiwa katika Mikoa ya Morogoro na Tabora.

30.    Mheshimiwa Spika, kufuatia matukio hayo jumla ya watuhumiwa 100 walikamatwa na kufikishwa mahakamani. Natoa rai kwa wananchi kuacha kujihusisha na vitendo hivyo viovu vinavyokiuka haki za binadamu. Jeshi la Polisi litaendelea kudhibiti na kuzuia mauaji ikiwemo ya makundi maalum na kuendelea kushirikiana na wadau katika kutoa elimu kwa umma ili kuacha mila na imani potofu kama ilivyoelekezwa katika Ibara ya 146 (v) ya Ilani ya CCM ya Mwaka 2015 – 2020.

Kuanzishwa kwa Mkoa Mpya wa Kipolisi Rufiji

31.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Serikali iliahidi kuanzisha Mkoa Mpya wa Kipolisi wa Rufiji ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi. Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa ahadi hiyo imetimizwa na hatua hii imeleta utulivu na udhibiti wa viashiria vya uhalifu katika eneo hilo. Nachukua nafasi hii kuvipongeza vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama kwa juhudi na bidii kubwa waliyoifanya na wanayoendelea kuifanya ya kuhakikisha eneo hilo na maeneo mengine nchini yanakuwa salama. Pia, naomba na kuwasisitiza wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo hivi kwa ajili ya kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu. Aidha, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla kuwa Serikali itaendelea kuwahifadhi na kuwalinda wanaotoa taarifa za wahalifu na uhalifu.

Udhibiti wa Uhalifu Nchini

32.    Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi limefanya operesheni maalum na za kawaida (misako na doria) kwa lengo la kuendelea kupambana na kudhibiti uhalifu wa aina zote ikiwemo makosa ya ndani ya nchi (kama vile mauaji, ubakaji na unyang’anyi) na makosa yanayovuka mipaka (kama vile uingizaji wa bidhaa bandia nchini, uharamia, wizi wa vyombo vya moto na utakatishaji wa fedha). Katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2018 operesheni maalumu saba (7) zilifanyika katika maeneo ya Kibiti, Rufiji, Mkuranga – mkoani Pwani, mapango ya Amboni mkoani Tanga, Mwanza, Morogoro, Mtwara na Lindi pamoja na operesheni za kawaida ikiwa ni misako na doria zilikuwa 3,628. Kwa sasa hali ya usalama katika maeneo hayo na kwingineko nchini ni tulivu.

Kushiriki katika Kuimarisha Amani na Usalama katika Nchi Mbalimbali

33.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 jumla ya askari 74 wa Jeshi la Polisi walipelekwa kushiriki kulinda amani na usalama katika nchi mbalimbali. Kati ya askari hao 48 walipelekwa katika jimbo la Darfur-Sudan (UNAMID), 10 Abyei - Sudan (UNISFA), 15 Sudani Kusini (UNMISS) na mmoja nchini Marekani – New York (DPKO). Lengo ni kuendelea kupata uzoefu na mbinu mpya za kiutendaji, kama ilivyoelekezwa katika Ibara ya 146 (iv) ya Ilani ya CCM ya Mwaka 2015 – 2020.

Kushiriki katika Operesheni za Kimataifa na Kikanda

34.    Mheshimiwa Spika, kuanzia tarehe 4 hadi 5 Oktoba, 2017 Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Ofisi za INTERPOL Kanda ya Kusini mwa Afrika limefanya operesheni za pamoja katika Jumuiya ya SARPCCO na EAPCCO.  Kufuatia operesheni hizo, magari 2 kutoka Uingereza na Malaysia yalikamatwa pamoja na dawa za kulevya kwa mchanganuo ufuatao: Heroine gramu 51.41; Cocaine gramu 20.87; bhangi kilogramu 870.16 na mirungi kilogramu 13. Pia, silaha 8 (SMG 1 na Gobore 7) na risasi 31 zilikamatwa. Jumla ya watuhumiwa 265 walikamatwa kwa makosa hayo na kufikishwa mahakamani. Vilevile, wahamiaji haramu 31 kutoka katika nchi za Burundi (12), China watano (5), India mmoja (1), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) watano (5), Kenya mmoja (1), Malawi wawili (2), Pakistan mmoja (1), Uganda mmoja (1), Yemen mmoja (1) na Zambia wawili (2) walikamatwa na kufikishwa mahakamani. Jeshi la Polisi litaendelea kufanya operesheni kwa kuzingatia Ibara ya 146 (vi) ya Ilani ya CCM ya Mwaka 2015 – 2020.



Kudhibiti Uvunjifu wa Amani unaotokana na Migogoro ya Wakulima na Wafugaji

35.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2018 jumla ya matukio ya migogoro ya wakulima na wafugaji 86 yalitokea na kusababisha vifo vya watu 44 (wanaume 34 na wanawake 10) na majeruhi 75 (wanaume 71 na wanawake 4). Watuhumiwa 129 walikamatwa na kufikishwa mahakamani. Katika mwaka 2018/19, Jeshi la Polisi litaendelea kudhibiti matukio hayo kwa kushirikisha mamlaka husika.

Upandishwaji Vyeo na Ajira Mpya kwa Askari

36.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Jeshi la Polisi limeomba kibali cha kupandisha vyeo maafisa 300 na askari 3,071 wa vyeo mbalimbali. Aidha, katika kutekeleza agizo la Mhe. Rais, Jeshi la Polisi limepata kibali cha kuajiri vijana 1,500 waliopo katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU). Nafasi hizo zimeshatangazwa kupitia vyombo vya habari ikiwemo radio, televisheni na magazeti.

Kuboresha Maslahi ya Askari

37.     Mheshimiwa Spika, kati ya mwezi Julai, 2017 hadi Machi, 2018 Serikali imelipa madeni ya askari na watumishi jumla ya Shilingi bilioni 17.94 ikiwa ni utekelezaji wa Ibara ya 146 (ii) ya Ilani ya CCM ya Mwaka 2015 – 2020. Madeni hayo yalitokana na madai ya posho za likizo na stahili mbalimbali kwa mwaka 2014/15 na 2015/16. Vilevile, Serikali imelipa madeni ya wazabuni na watoa huduma ya jumla ya Shilingi bilioni 5.69. Aidha, katika kipindi hicho askari 347 walioumia/kufariki wakiwa kazini wamelipwa fidia ya jumla ya Shilingi bilioni 2.09.

Ununuzi wa Sare za Jeshi la Polisi

38.    Mheshimiwa Spika, taratibu za ununuzi wa sare na vifaa vingine vya kijeshi kwa kutumia viwanda vya ndani zinaendelea baada ya Kiwanda cha 21st Century kilichopo Mkoani Morogoro kuthibithisha uwezo wa kutengeneza vitambaa bora vya kushona sare zinazotakiwa na majeshi yetu. Aidha, Jeshi la Polisi linakamilisha mkataba wa ununuzi wa jozi 15,000 za viatu (buti jozi 10,000, viatu vya kawaida (staff shoes) jozi 5,000) kutoka Kiwanda cha Viatu cha Jeshi la Magereza Karanga - Moshi.
Upatikanaji wa Vitendea Kazi

39.    Mheshimiwa Spika, ili kuendelea kuimarisha na kuboresha doria, misako na operesheni maalum na za kawaida Jeshi la Polisi limepokea magari 172 aina ya Ashok Leyland yakiwa ni sehemu ya ununuzi wa magari 777 kutoka Kampuni ya Ashok Leyland ya nchini India. Magari hayo yatagawiwa katika Mikoa, Vikosi na Wilaya za Kipolisi. Pia, Jeshi la Polisi limepokea pikipiki 10 aina ya Tongba kutoka kwa wadau wa usalama wa mkoa wa Dar es Salaam. Pikipiki hizo zimesambazwa katika Vituo vya Polisi katika kanda maalumu ya Dar es Salaam kwa kazi za doria za kuzuia makosa ya usalama barabarani.

40.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 Jeshi la Polisi la Polisi litaendeleza juhudi za kupata vitendea muhimu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa lengo la kuimarisha hali ya ulinzi na usalama nchini.

Mafunzo kwa Askari/Watumishi wa Jeshi la Polisi

41.      Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2018 mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji maafisa 736, wakaguzi 395, askari wa vyeo mbalimbali 4,943 na watumishi raia 10 yamefanyika. Katika mwaka 2018/19 Jeshi la Polisi litaendelea kutoa mafunzo kwa maafisa, wakaguzi, askari wa vyeo mbalimbali pamoja na watumishi raia ili kukabiliana na mbinu mpya za kiuhalifu pamoja na kuongeza ufanisi.

JESHI LA MAGEREZA

Uhifadhi wa Wafungwa na Program za Urekebishaji Magereza

42.    Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Machi, 2018 Jeshi la Magereza lilihifadhi jumla ya wafungwa na mahabusu 39,763 (wafungwa ni 20,312 na mahabusu ni 19,451) ikilingwanishwa na uwezo wa kuhifadhi wafungwa na mahabusu 29,902. Hali hiyo inaashiria kuendelea kuwepo msongamano magerezani kwa asilimia 33. Hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa ili kukabiliana na hali hiyo zikiwemo: kutumia utaratibu wa huduma kwa jamii; utaratibu wa Parole; kutumia Kamati za Kusukuma Kesi; ujenzi wa magereza mapya; na ukarabati wa mabweni ya wafungwa. Aidha, Jeshi la Magereza liliendelea kutekeleza jukumu la kuwasindikiza mahabusu kwenda mahakamani na kurudi Gerezani katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Wilaya ya Arusha mjini na Wilaya ya Dodoma mjini.

Uboreshaji wa Makazi ya Askari wa Jeshi la Magereza

43.    Mheshimiwa Spika, ujenzi wa maghorofa 12 yenye uwezo wa kuishi familia 320 za maafisa na askari eneo la Gereza Ukonga unaendelea kwa fedha Shilingi billion 10 zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Pia, ujenzi wa nyumba za askari zenye uwezo wa kuishi familia 24 unaendelea katika Gereza Chato. Nachukua nafasi hii kumshukuru Mhe. Rais kwa nia yake ya dhati ya kuendelea kusaidia kuboresha makazi ya askari.

44.    Mheshimiwa Spika, vilevile, ujenzi wa nyumba 323 za kuishi maafisa na askari kwa njia ya kujitolea katika maeneo mbalimbali ya magereza nchini unaendelea. Ujenzi huo upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Aidha, Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza limetoa Shilingi milioni 246 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa nyumba za askari katika Magereza ya Bukoba, Muleba, Biharamulo, Kigongoni, Mkuza, Kibiti, Arusha, Rombo, Karanga, Mwanga, Isanga na Gereza Mahabusu Morogoro.

45.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Jeshi la Magereza litaendelea na ujenzi wa nyumba za kuishi askari kwenye Magereza ya Ukonga na Chato pamoja na kukamilisha ujenzi wa nyumba 323 zinazojengwa katika magereza mbalimbali nchini.

Utekelezaji wa Sera ya Uchumi wa Viwanda

46.    Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Uchumi wa Viwanda, Jeshi la Magereza kwa ubia na Kampuni ya Mkulazi Holding Ltd inayoundwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii NSSF na PPF limewekeza katika kilimo cha miwa na ufufuaji wa Kiwanda cha Sukari Gereza Mbigiri - Morogoro. Kiwanda hicho kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 50,000 za sukari kwa mwaka. Mpaka sasa hekta 800 zimeshalimwa na kupandwa miwa, sambamba na hilo ununuzi wa mitambo kwa ajili ya kiwanda unaendelea.

47.     Mheshimiwa Spika, vilevile, Jeshi la Magereza limeingia ubia na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PPF ili kuboresha Kiwanda cha Viatu Gereza Karanga na ujenzi wa kiwanda kipya katika eneo hilo. Ubia huo umeunda kampuni inayoitwa Karanga Leather Industries. Uboreshaji wa kiwanda unaendelea, ambapo mashine mpya zinategemea kuwasili katika mwaka 2018. Hivyo, kiwanda kitakuwa na uwezo wa kuzalisha jozi za viatu 400 kwa siku badala ya 150 zinazozalishwa sasa. Kiwanda kipya kitakachojengwa kitakuwa na uwezo wa kuzalisha jozi 4,000 za viatu, kuchakata ngozi sq. ft 12,500 na  kutengeneza soli jozi 3,000 kwa siku pamoja na kutengeneza bidhaa mbalimbali za ngozi (mikanda, mikoba na pochi) 4,000 kwa mwaka. Katika mwaka 2018/19 Jeshi la Magereza litaimarisha viwanda vya kati vya Useremala Mkoani Dodoma na Mtwara pamoja na mradi wa kuzalisha kokoto Msalato.

Programu za Urekebishaji wa Wafungwa

48.    Mheshimiwa Spika, programu za urekebishaji wa wafungwa zinaendelea kupitia shughuli za kilimo na mifugo. Jumla ya hekari 7,000 za mazao kama vile mahindi, mpunga, maharage, alizeti, chai, pamba, migazi/michikichi na mikorosho zimelimwa. Aidha, Jeshi la Magereza kwa kushirikiana na Wakala wa Mbegu za Kilimo (Agricultural Seed Agency - ASA) limeendelea kuzalisha mbegu bora katika Magereza ya: Wami Kuu, Mbigiri, Idete (Morogoro), Isupilo (Iringa), Songwe (Mbeya), Mollo (Rukwa), Kitai (Ruvuma) na Karanga (Kilimanjaro).

49.    Mheshimiwa Spika, vilevile, Jeshi la Magereza linaendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo katika uzalishaji wa vipando vya mihogo yenye ukinzani dhidi ya ugonjwa wa batobato kali (cassava mosaic - Uganda variant). Jumla ya hekta 170 zililimwa katika Magereza 23 yaliyopo katika Mikoa ya Dodoma, Kagera, Lindi, Mara, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Pwani, Shinyanga, Singida, Tabora na Tanga.

50.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 Jeshi la Magereza linatarajia kulima jumla ya hekta 349 za mbegu bora za alizeti, mpunga, mahindi na nyanya katika Magereza ya Wami, Mbigiri na Idete (Morogoro), Isupilo (Iringa), Songwe (Mbeya), Mollo (Rukwa), Kitai (Ruvuma) na Karanga (Kilimanjaro) na kuuzwa kwa wadau mbalimbali. Jeshi pia, litalima ekari 7,000 za mazao ya chakula ikiwemo mahindi, maharage, mtama na mpunga.

51.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 urekebishaji wa wafungwa kupitia ufugaji uliendelea, ambapo jumla ya mifugo 18,588 ya aina mbalimbali ilihudumiwa kama ifuatavyo: ng’ombe wa maziwa (691), Ng’ombe wa nyama (5,497) Mbuzi (2,405), Kondoo (134), Nguruwe (60), Sungura (175), Kuku na Bata (9,626). Jeshi la Magereza litaendelea kuhudumia mifugo 26,632 ya aina mbalimbali katika mwaka 2018/19.

Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza

52.     Mheshimiwa Spika, Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza limefanya kazi mbalimbali za ujenzi kwa Taasisi za Serikali na watu binafsi ikiwa ni pamoja na ukarabati wa jengo la Utawala la Bunge ambalo limekamilika na kukabidhiwa mwezi Disemba, 2017. Katika mwaka 2018/19 Shirika litaendelea na shughuli mbalimbali ikiwemo kupokea zabuni za ujenzi na kufanya ukarabati wa majengo.  

Upimaji wa Maeneo ya Magereza

53.     Mheshimiwa Spika, upimaji wa maeneo mbalimbali ya Magereza nchini unaendelea kwa lengo la kupunguza migogoro iliyopo katika maeneo yanayomilikiwa na Jeshi la Magereza. Hadi kufikia mwezi Machi, 2018 Jeshi limeweza kupima na kupata Hati za umiliki wa maeneo ya Gereza Karanga, Hati tatu (3) za mashamba ya Mbigiri na eneo la Gereza Isupilo.

Utunzaji na Hifadhi ya Mazingira

54.     Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza limeendelea na juhudi za utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti, kuendeleza misitu ya asili na ufugaji wa nyuki kwenye eneo la hekta 14,698.5. Aidha, kwa sasa miti ya aina mbalimbali inaendelea kutunzwa kwenye magereza kote nchini kwa ufadhili wa Mfuko wa Misitu (Tanzania Forest Fund - TFF). Aidha, Gereza Isupilo – Iringa limeanzisha kitalu cha miti kwa ajili ya kuendeleza juhudi za utunzaji wa mazingira.

Ajira na Maslahi kwa Askari Magereza

55.     Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza litaajiri askari wapya 2,750 kati ya hao askari 750 wataajiriwa katika mwaka 2017/18 na askari 2,000 katika mwaka 2018/19. Aidha, katika kuimarisha uongozi wa ngazi za juu wa Jeshi la Magereza jumla ya maafisa 29 wamepandishwa vyeo katika ngazi mbalimbali.

56.     Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imeendelea kuboresha maslahi ya Watumishi kwa kuwalipa posho ya chakula kwa wakati na fedha za msamaha wa kodi ya bidhaa kwa maafisa na askari nchini. Serikali pia imelipa baadhi ya madeni ya askari na watumishi ya Shilingi bilioni 5.55 katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba, 2017.

Mafunzo kwa Askari wa Jeshi la Magereza

57.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Jeshi la Magereza limeendelea kuwawezesha watumishi kupata mafunzo mbalimbali ndani na nje ya nchi. Jumla ya watumishi 306 wanaendelea na mafunzo ya kitaaluma katika vyuo mbalimbali kwa mchanganuo ufuatao: Astashahada 98, Stashahada 86, shahada 85, Stashahada ya Uzamili 08, Shahada ya Uzamili 26 na Shahada za uzamivu 02. Jeshi pia limeendelea kutoa mafunzo ndani ya Jeshi ambapo askari 37 walihitimu mafunzo ya Astashahada ya ufundi bomba na useremala na askari 24 walipata cheti cha Sayansi ya Urekebishaji wa Wafungwa. Aidha, askari 17 wanaendelea na mafunzo ya cheti cha urekebishaji katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Ukonga.

58.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 Jeshi la Magereza linatarajia kutoa mafunzo ya ndani katika fani na ngazi mbalimbali kwa maafisa na askari 3,270. Vilevile, litaendelea kutoa vibali kwa maafisa na askari kusoma vyuo vya nje ya Jeshi kwa kuzingatia mahitaji kwa taaluma zenye upungufu Jeshini. Aidha, mafunzo ya ufundi katika Chuo cha Ruanda kwa askari, pamoja na wafungwa kama sehemu ya urekebishaji yataendelea kutolewa.

PROGARAMU YA ADHABU MBADALA YA KIFUNGO CHA GEREZANI

59.     Mheshimiwa Spika, Wizara inasimamia utekelezaji wa Programu ya Adhabu Mbadala wa Kifungo Gerezani ili kupunguza msongamano magerezani na gharama za kuhudumia wafungwa na mahabusu. Katika kipindi cha mwezi Julai, 2017 hadi Machi, 2018 jumla ya wafungwa 2,781 walinufaika na Programu hiyo. Uwepo wa wafungwa hao nje ya magereza umesaidia Serikali kuokoa jumla ya Shilingi bilioni 1.31 ambazo zingetumika kuwahudumia wafungwa hawa kama wangetumikia adhabu zao magerezani ikizingatiwa kuwa gharama za kumhudumia mfungwa mmoja kwa siku ni Shilingi 1,300. Serikali pia imeweza kuokoa jumla ya Shilingi billion 4.03 ambazo zingetumika kuajiri vibarua kwenye Taasisi za Umma kwani kibarua mmoja hulipwa wastani wa Shilingi 4,000 kwa siku.

60.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Wizara imefanikiwa kupanuwa wigo wa utekelezaji wa adhabu mbadala kwa kuongeza Mikoa ya Kigoma na Simiyu na hivyo kufanya jumla ya mikoa 23 ya Tanzania Bara inayotekeleza programu hiyo. Katika mwaka, 2018/19 Wizara inatarajia kuongeza Mikoa ya Katavi, Rukwa na Lindi kwa ajili ya utekelezaji wa programu hiyo.

JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI

Ukaguzi wa Tahadhari na Kinga Dhidi ya Moto na Majanga

61.      Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2018, Jeshi limekagua jumla ya maeneo 60,366 sawa na asilimia 74 ya lengo la ukaguzi kwa kipindi husika. Katika mwaka 2018/19 Jeshi litaendelea na ukaguzi wa tahadhari na kinga dhidi ya moto katika maeneo mbalimbali nchini ili kuzuia na kupunguza matukio ya moto.

Matukio ya Moto na Majanga Mengine

62.    Mheshimiwa Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeendelea kupambana na majanga ya moto pamoja na kufanya maokozi katika maeneo mbalimbali nchini. Hadi kufikia mwezi Machi, 2018, Jeshi limefanikiwa kuzima moto katika matukio 1,217 Tanzania Bara ikiwemo tukio la moto katika soko la SIDO, mkoani Mbeya, moto katika nyumba za makazi ya Polisi mkoani Arusha, kuungua kwa kiwanda cha Superdoll, kupasuka kwa bomba la gesi Buguruni – Mnyamani na moto katika Kituo cha Utangazaji cha Clouds Media. Aidha, katika kukabiliana na majanga mengine, jumla ya maokozi 335 yalifanyika katika matukio mbalimbali ikiwemo mafuriko, kuangukiwa vifusi, ajali za barabarani, kutumbukia chooni na kuzama kwa vyombo vya usafiri ziwani/baharini.

Hali ya Vituo vya Zimamoto Nchini na Vitendea Kazi

63.    Mheshimiwa Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lina jumla ya vituo vya zimamoto 82 Tanzania Bara wakati mahitaji halisi ya vituo ni 162. Jeshi pia lina magari 72 ya kuzimia moto na maokozi, ikilinganishwa na mahitaji halisi ya magari 324. Hata hivyo, Jeshi linaendelea na jitihada mbalimbali za kuimarisha hali ya vitendea kazi ili kuendana na kasi ya ukuaji wa miji pamoja na maendeleo ya viwanda nchini ikiwemo kukamilisha taratibu husika ili kununua magari manne (4) ya kuzimia moto kupitia bajeti ya mwaka 2017/18; kuimarisha uhusiano na nchi wahisani na wadau wa maendeleo ili kuendelea kupata misaada mbalimbali ikiwemo vitendea kazi na mafunzo; na kuendelea kutafuta mikopo yenye masharti nafuu kutoka kwa wadau wa maendeleo. Katika mwaka wa 2018/19 Jeshi limepanga kununua magari matano (5) ya kuzimia moto pamoja na vifaa vya kuzimia moto.

64.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Jeshi limepata msaada wa magari matano (5) ambapo matatu (3) ni ya kuzimia moto na maokozi, moja la kubebea wagonjwa na moja la utawala kutoka nchi za Ujerumani na Italia. Pia, Jeshi limepata msaada wa vifaa mbalimbali vya kuzimia moto na maokozi zikiwemo mashine za kujazia mitungi ya kusaidia hewa ya ziada wakati wa maokozi ambayo imepelekwa katika Mikoa ya Mbeya, Ruvuma na Lindi.

Elimu kwa Umma kuhusu namna ya Kukabiliana na Majanga ya Moto

65.     Mheshimiwa Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeendelea kutoa elimu kwa umma juu ya namna ya kukabiliana na majanga mbalimbali ya moto kupitia vyombo vya habari ikiwemo vipindi vya luninga 37, vipindi vya redio 754 na makala za magazeti 20 na katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu ikiwemo shule, masoko, vivuko na vituo vya mabasi. Katika kukabiliana na matukio ya moto katika shule za bweni nchini, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limetoa elimu ya namna ya kuzuia na kukabiliana na matukio ya moto katika shule za bweni 256 katika mikoa mbalimbali.  Jeshi la Zimamoto litaendelea kutoa elimu kwa umma kwa lengo la kupunguza majanga ya moto nchini.

Mafunzo kwa Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji

66.    Mheshimiwa Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeendelea kuwapatia maafisa na askari wake mafunzo kwa lengo la kuboresha utendaji katika majukumu yake. Katika mwaka 2017/18 askari 64 walipatiwa mafunzo mbalimbali ndani ya nchi ikiwemo mafunzo ya kuzima moto na maokozi. Aidha, maafisa na askari 10 wamehitimu mafunzo ya kuzima moto na maokozi nchini Morocco na maafisa 11 wamepatiwa mafunzo ya kukabiliana na majanga mbalimbali nchini China. Katika mwaka 2018/19 Jeshi la Zimamoto na Uokoaji litaendelea kutoa mafunzo mbalimbali kwa askari na watumishi ili kuwaongezea ujuzi.


IDARA YA UHAMIAJI

Kuanzishwa kwa Mfumo wa Uhamiaji Mtandao

67.     Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mradi wa Uhamiaji Mtandao (e-immigration) ambao ulizinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli tarehe 31 Januari, 2018 unaendelea. Mradi huo umeanza kwa kutoa pasipoti za kielektroniki za Tanzania na Afrika Mashariki katika Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji Dar es Salaam na Zanzibar. Pasipoti mpya za kielektroniki zimetengenezwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa yenye uwezo wa kubeba taarifa mbalimbali pamoja na alama nyingi za kiusalama. Aidha, pasipoti hiyo inamwezesha mtumiaji kuwa na nakala yake ya pasipoti kwenye simu yake ya kiganjani baada ya kupakua ‘app’ ya pasipoti yake kwenye simu.

68.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 Idara ya Uhamiaji itaendelea kukamilisha ufungaji wa mfumo wa pasipoti za kielektroniki katika mikoa yote hapa nchini. Vilevile, itaendelea kufunga mifumo ya viza za kielektroniki (e-visa), Hati za Ukaazi za kielektroniki (e-permit) na kufunga mifumo ya kudhibiti watu wanaoingia na kutoka nchini (e-border management Control System) pamoja na miundombinu ya uwekaji wa mtandao wa mawasiliano ya mifumo (wide area network) katika ofisi na vituo vya uhamiaji vya mipakani. Kukamilika kwa mradi huu kutasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka yetu pamoja na kuongeza udhibiti wa ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali.

Hali ya Ulinzi na Usalama Mipakani

69.    Mheshimiwa Spika, jumla ya wageni 1,021,071 waliingia nchini kuanzia mwezi Julai 2017 hadi Machi, 2018 ikilinganishwa na wageni 1,032,978 waliongia katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2016/17. Aidha, jumla ya wageni 954,926 walitoka nchini ikilinganishwa wageni 881,478 waliotoka kwa mwaka 2016/17. Katika mwaka 2018/19 Idara ya Uhamiaji itaendelea kutoa huduma kwa kufuata Sheria na Kanuni za Uhamiaji kwenye mipaka kwa wageni wanaoingia na kutoka nchini.

Misako, Doria na Ukaguzi

70.    Mheshimiwa Spika, Idara ya Uhamiaji iliendelea kufanya misako, doria na ukaguzi katika sehemu mbalimbali kama vile mipakani, migodini, viwandani, mahotelini na kwenye mashamba makubwa kwa lengo la kudhibiti wahamiaji haramu pamoja na biashara haramu ya usafirishaji binadamu nchini. Katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2018 jumla ya watuhumiwa wa uhamiaji haramu 13,393 walikamatwa na kuchukuliwa hatua mbalimbali za kisheria, ikiwa ni ongezeko la asilimia 40 ya wahamiaji haramu 9,581 waliokamatwa katika kipindi kama hiki mwaka 2016/17. Vilevile, jumla ya Watanzania 211 waliokwenda nje ya nchi kinyume na taratibu za uhamiaji walirudishwa nchini.  Wizara kupitia Idara ya Uhamiaji itaendelea kufanya misako na doria ili kuwabaini na kuwaondoa wahamiaji haramu nchini na kuhakikisha watu wote wanaoingia na kutoka nchini wanatumia njia zilizo rasmi.

Vibali Vilivyotolewa kwa Wageni Wakaazi

71.      Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2018, jumla ya vibali vya ukaazi 13,151 (daraja “A” 1,407; daraja “B” 8,551; na daraja “C” 3,193) vilitolewa kwa wageni walioingia nchini kwa madhumuni mbalimbali kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za kiuhamiaji  ikilinganishwa na vibali 11,259 (daraja A 2,474, daraja B 6,736, daraja C 2,049) vilivyotolewa kwa mwaka 2016/17. Aidha, katika kipindi husika jumla ya Hati za Mfuasi 1,335 zilitolewa ikilinganishwa na Hati 650 zilizotolewa katika kipindi kama hiki mwaka 2016/17. Vilevile, Hati za Msamaha 2,393 zilitolewa ikilinganishwa na Hati 1,427 zilizotolewa katika kipindi kama hiki mwaka 2016/17.

Pasipoti na Hati Nyingine za Safari

72.     Mheshimiwa Spika, jumla Pasipoti 45,965 zilitolewa kwa Watanzania waliotaka kusafiri nje ya nchi kwa madhumuni mbalimbali katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2018 kwa mchanganuo ufuatao: Pasipoti za Kawaida ni 45,697; Pasipoti za Kibalozi ni 220; Pasipoti za Kiutumishi ni 48. Katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2016/17 jumla ya Pasipoti 55,573 zilitolewa kama ifuatavyo: Pasipoti za Kawaida ni 54,503, Pasipoti za Kibalozi 229, Pasipoti za Kiutumishi 56, Pasipoti za Afrika Mashariki 785.  Aidha, Idara ya Uhamiaji ilitoa Hati za Dharura za safari 109,726 ikilinganishwa na Hati za Dharura za Safari 80, 445 zilizotolewa katika kipindi kama hiki mwaka 2016/17.

73.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 Idara ya Uhamiaji itaendelea kuboresha na kukamilisha huduma za kiuhamiaji kwa kutumia mfumo wa Uhamiaji Mtandao (e- passport, e-visa, e-permit na e-border management control).

Wageni Walioomba na Kupewa Uraia wa Tanzania

74.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2018 jumla ya wageni 135 walipewa uraia, idadi hii ni ongezeko la asilimia 10 ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka 2016/17 ambapo wageni 110 walipewa uraia. Wageni waliopewa uraia kwa kipindi hiki ni kutoka Burundi (4), Cameroon (2), China (1), Greece (1), India (83), Jordan (1), Kenya (1), Korea (1), Lebanon (2), Rwanda (2), Sierra Leone (1), Somalia (4), Uganda (2), Umoja wa nchi za Falme za Kiarabu (6), Yemen (23) na Zambia (1).

Watanzania Waliopatiwa Uraia wa Mataifa Mengine

75.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2018 Watanzania  60  waliukana uraia baada ya kujipatia Uraia wa mataifa mengine kama ifuatavyo: Australia (2), Botswana (4), Canada (3), India (4), Kenya (4), Lesotho (1), Norway (9), Sweden (1), Uganda (2), Uingereza (1), Ujerumani (19) na Zimbabwe (3) hivyo kupoteza hadhi ya kuwa raia wa Tanzania kwa mujibu wa Sheria ya Uraia Sura ya 357 Rejeo la 2002. Katika kipindi kama hiki kwa mwaka 2016/17 Watanzania 35 waliukana uraia wa Tanzania.

76.     Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa marekebisho ya Kanuni za Sheria ya Tanzania ya Uraia, Tangazo la Serikali Na. 427/2017 imetoa punguzo la ada ya uraia kutoka Dola za Marekani 5,000 hadi Shilingi 2,000,000. Punguzo hilo la ada linawahusu watu waliozaliwa Tanganyika kabla na baada ya uhuru ambao wazazi wao hawakutambulika kuwa raia wa Tanganyika kwa mujibu wa Sheria ya uraia ya Tanganyika Sura Na. 512 ya mwaka 1961. Vilevile, Kanuni imejumuisha watu waliongia nchini Tanganyika kabla na baada ya uhuru na kuendelea kuishi nchini kwa kipindi chote pamoja na watu waliozaliwa nje ya Tanzania kwa wazazi ambao ni raia kwa Tanzania kwa kuridhi. Hivyo, natoa rai kwa watu hao kurekebisha hadhi yao ya uraia ili kukidhi matakwa ya Sheria.

Mafunzo katika Idara ya Uhamiaji

77.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 askari wapatao 23 wamehudhuria mafunzo ya muda mfupi nchini China na wawili (2) nchini Botswana kwa ufadhili wa Serikali hizo. Aidha, askari 47 wamepatiwa mafunzo mbalimbali ndani ya nchi.

Vitendea Kazi, Majengo ya Ofisi na Makazi ya Askari wa Uhamiaji

78.    Mheshimiwa Spika, Idara ya Uhamiaji imenunua nyumba 103 katika eneo la Iyumbu mjini Dodoma kwa ajili ya makazi ya askari. Hadi sasa Idara imekabidhiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) jumla ya nyumba 63 na ujenzi wa nyumba 40 unaendelea.Aidha, ujenzi wa majengo ya ofisi unaendelea katika Mikoa ya Geita (asilimia 50), Manyara (asilimia 40), Mtwara (asilimia 11) na Lindi (asilimia 53). Ujenzi wa nyumba ya makazi ya Kamishna Jenerali wa Uhamiaji umefikia asilimia 65. Namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kutoa ahadi ya Shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji Mjini Dodoma ambao utaanza mwaka 2018/19.

MAMLAKA YA VITAMBULISHO VYA TAIFA (NIDA)

Utambuzi, Usajili na Utoaji wa Vitambulisho vya Taifa

79.     Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutekeleza lengo la Ibara 145 (f) ya Ilani ya CCM ya mwaka 2015 - 2020 kwa kuandikisha na kutoa Vitambulisho vya Taifa kwa Watanzania kuanzia miaka 18 na zaidi, wageni wakaazi na wakimbizi. Hadi kufikia Machi, 2018 Mamlaka imesajili jumla ya wananchi 14,048,493, wageni wakazi 13,254 na wakimbizi 6,289 katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar. Zoezi la uchukuaji picha na alama za kibaiolojia linaendelea katika mikoa yote ili kutengeneza vitambulisho na kuvigawa kwa walengwa.

80.   Mheshimiwa Spika, Mamlaka imeunganisha (interface) mfumo wake wa utambuzi na taasisi nyingine 35 ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa jamii na kuboresha hali ya ulinzi na usalama nchini. Aidha, Mamlaka imekamilisha ujenzi wa kituo cha kutunzia kumbukumbu (Data Centre) huko Kibaha Mkoa wa Pwani na kituo cha uokozi wakati wa majanga (Data Recovery Centre) Kihonda Mkoa wa Morogoro pamoja na ofisi 13 za usajili za Wilaya Tanzania Bara na Zanzibar. Vilevile, NIDA imeweka mtandao wa mawasiliano (fibre optic) kati ya Makao Makuu na ofisi 117 za usajili za wilaya ili kusaidia kusafirisha taarifa kutoka wilayani kwenda kituo kikuu cha kutengeneza vitambulisho na kutunza taarifa.

81.     Mheshimiwa Spika, uelewa kuhusu umuhimu wa Kitambulisho cha Taifa umeongezeka miongoni mwa wananchi na kusababisha ongezeko kubwa la wananchi wanaojitokeza kusajiliwa kwa ajili ya Vitambulisho vya Taifa. Hali hii imetokana na juhudi za Serikali kupitia vyombo mbalimbali vya habari kutoa elimu ya umuhimu wa Vitambulisho vya Taifa kwa uchumi na maendeleo ya mwananchi na nchi yetu kwa ujumla. Mamlaka inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa Kitambulisho cha Taifa na jinsi kinavyoweza kuwasaidia katika kupata huduma mbalimbali mfano huduma za kibenki, pasi ya kusafiria, fidia wakati wa majanga na kubaini vitendo vya kihalifu.

82.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 Wizara itaendelea na zoezi la utambuzi na usajili wa watu nchi nzima pamoja na kuunganisha mtandao wa mawasiliano kati ya ofisi za usajili za wilaya 33 na Makao Makuu. Aidha, Wizara kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Korea inatarajia kuanza ujenzi wa Makao Makuu ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa katika Mkoa wa Dodoma pamoja na ujenzi wa ofisi katika wilaya 42 Tanzania Bara na Zanzibar. Mamlaka pia itaendelea na ukarabati kwa baadhi ya ofisi za usajili za wilaya na kuungunisha mfumo wa utambuzi na mifumo ya taasisi nyingine ili iweze kusomana na hatimaye kubadilishana taarifa.

83.    Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa lengo la utambuzi na usajili imebainika kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuanza kutekeleza jukumu la utambuzi na usajili mara tu mtoto anapozaliwa na kupewa namba ya pekee ya utambuzi na usajili. Suala la utambuzi wa watoto ni muhimu katika kuimarisha hali ya usalama katika nchi yetu. Mtakumbuka kuwa katika siku za hivi karibuni kumeibuka makundi mbalimbali ya kihalifu yanayowahusisha vijana chini ya miaka 18. Tumeshuhudia makundi kama Panya Road na Wakorea weusi wakijihusisha na vitendo vya kihalifu katika Jiji la Dar es Salaam na Mbeya. Athari za kutokuwatambua vijana hawa wanapozaliwa mpaka wafikie umri wa miaka 18 umeathiri upelelezi wa kupata taarifa sahihi za kuwatambua uasili wao, wazazi au walezi na makazi ili kuwadhibiti kutojihusisha katika vitendo vya uhalifu.


HUDUMA KWA WAKIMBIZI

84.    Mheshimiwa Spika, nchi yetu imeendelea kutekeleza jukumu lake la kimataifa la kuhifadhi wakimbizi na waomba hifadhi kutoka nchi mbalimbali. Katika kipindi cha mwaka 2017/18, Tanzania imeshuhudia kwa mara nyingine ongezeko la waomba hifadhi wanaopokelewa, hususan kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Hadi kufikia mwezi Machi, 2018 Tanzania ilikuwa na jumla ya wakimbizi na waomba hifadhi 356,548. Kati ya hao 276,047 kutoka Burundi, 79,950 Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, 150 Somalia na 401 kutoka mataifa mengine.

85.    Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwezi Julai, 2017 hadi Machi, 2018 Kamati ndogo ya Kitaifa ya Kuhoji Waomba Hifadhi (Ad hoc Committee), iliwahoji waomba hifadhi 1,342 kutoka nchi ya Burundi ambapo waomba hifadhi 198 walipendekezwa kupewa hadhi ya ukimbizi nchini baada ya kukidhi vigezo kwa mujibu wa Sheria ya Wakimbizi ya mwaka 1998 na waomba hifadhi 1,144 walikosa sifa za kupewa hadhi ya ukimbizi.

86.    Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kati ya Julai, 2017 hadi Machi, 2018 jumla ya wakimbizi na waomba hifadhi 50,437 kutoka Burundi walijiandikisha ili wasaidiwe kurejea kwa hiari kwenye nchi yao ya asili. Zoezi la kuwarejesha kwa hiari linaendelea na mpaka kufikia mwezi Machi, 2018 jumla ya wakimbizi 21,008 wamerejea Burundi. Ili kuongeza kasi ya kuwarejesha wakimbizi katika nchi zao, Serikali ya Tanzania ilishiriki katika Mkutano wa ishirini (20) wa Pande Tatu uliofanyika nchini Burundi tarehe 28 Machi, 2018 ambapo iliazimiwa kuwa ifikapo mwezi Desemba, 2018 zaidi ya wakimbizi 72,000 wawe wamerejeshwa katika nchi ya asili. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2019, wakimbizi wote wa Burundi waliopo kwenye makambi ya Kigoma wawe wamerejea nchini kwao.

87.    Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) inatekeleza mpango wa kuwapeleka wakimbizi katika nchi ya tatu ikiwa ni moja ya suluhisho la kudumu linalotolewa kwa wakimbizi.Katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2018 jumla ya wakimbizi 926 walihamishiwa nchi ya tatu katika mataifa ya Australia 25, Canada 137, Finland 4, Marekani 756 na Uingereza 4.

88.   Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Mikoa ya Katavi, Kigoma na Tabora ilifanya zoezi la uhakiki na usajili wa wakimbizi wa Burundi walioingia nchini mwaka 1972. Katika zoezi hilo kwenye Mikoa ya Tabora na Katavi wakimbizi 19,187 walihakikiwa katika kipindi cha mwezi Julai hadi Oktoba, 2017. Katika Mkoa wa Kigoma, zoezi la uhakiki lilifanyika mwezi Januari na Februari, 2018 ambapo jumla ya wakimbizi 15,791 walihakikiwa.  Lengo la zoezi hili ni kuiwezesha Serikali kuwa na takwimu sahihi za wakimbizi wote wa kundi hilo.

89.    Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na UNHCR imeendelea kuhamasisha na kusimamia shughuli za hifadhi ya mazingira kwenye kambi za wakimbizi na vijiji jirani.  Katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2018, shughuli za mazingira zilizotekelezwa ni pamoja na: Upandaji wa miti 1,988,028; ujenzi wa majiko banifu 84,590; na nyumba za tofali na bati 2,274.  Aidha, mradi wa matumizi ya gesi umeendelea kutekelezwa ambapo jumla ya mitungi 26,450 ya gesi imegawiwa kwa wakimbizi. Vilevile, Wizara kwa kushirikiana na UNHCR inaendelea na zoezi la kufanya tathmini ya athari za mazingira kutokana na shughuli za wakimbizi ndani ya kambi na maeneo ya vijiji jirani ili kuwa na mikakati endelevu ya kukabiliana na athari hizo.

90.    Mheshimiwa Spika, kwa ujumla hali ya ulinzi na usalama imeendelea kuwa shwari ndani na nje ya kambi za wakimbizi. Wizara kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama katika mikoa inayohifadhi wakimbizi, imeendelea kuimarisha ulinzi na usalama kwa kufanya doria za mara kwa mara. Aidha, wakimbizi wanaobainika kujihusisha na vitendo vya kihalifu wamekuwa wakichukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi.

VITA DHIDI YA BIASHARA HARAMU YA USAFIRISHAJI WA BINADAMU

91.      Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2018 Wizara kupitia Sekretarieti ya Kupambana na Kuzuia Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) imewaokoa wahanga 20 (Watanzania 18, Afrika Kusini (1) na Mrundi (1)) wa biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu waliokuwa wakitumikishwa katika maeneo mbalimbali nchini na kuwaunganisha na familia zao. Katika kipindi hicho jumla ya kesi 24 zimefunguliwa ambapo kesi 23 zinaendelea katika mahakama mbalimbali nchini na kesi moja (1) watuhumiwa wawili (2) wote Wanawake walihukumiwa kifungo cha miaka saba (7) gerezani.

92.    Mheshimiwa Spika, Sekretariati ilifanya ukaguzi katika maeneo hatarishi ya utumikishwaji wa wahanga wa biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu katika wilaya zote Jijini Dar es Salaam. Maeneo yaliyokaguliwa ni pamoja na viwanda, massage parlor, gereji za Wachina, kampuni kubwa na klabu za usiku. Lengo la ukaguzi huo ni kujiridhisha kuwa watumishi wanajua haki zao za msingi na kuwaelimisha juu ya biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu.

93.    Mheshimiwa Spika, vilevile, Sekretarieti kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Lawyers Without Borders imetoa elimu juu ya biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu kwa wadau muhimu katika mikoa saba ambayo ni Arusha, Geita, Kagera, Mara, Mwanza, Shinyanga na Simiyu. Wadau hao ni pamoja na Mahakimu, Waendesha Mashtaka, Askari wa Jeshi la Polisi, Maafisa Uhamiaji, Maafisa Ustawi wa Jamii, Viongozi wa Serikali za Mitaa na wawakilishi kutoka mashirika mbalimbali yasiyo ya Serikali.Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wa namna ya kupeleleza, kuchunguza na kuendesha mashtaka na kusikiliza kesi dhidi ya biashara haramu ya usafirishaji binadamu. Sekretarieti pia imetoa elimu kwa Watanzania hususan wasichana wanaoomba hati za kusafiria kwenda nje ya nchi kufanya kazi kufuatia taarifa mbalimbali zinazohusu manyanyaso kwa wasichana wanaopelekwa kwenda kufanya kazi nje ya nchi. Aidha, kutokana na taarifa hizo, mnamo mwezi Januari, 2018 nilitoa tamko la kuzuia utoaji wa pasipoti za mafungu kwa wasichana wanaoenda kufanya kazi za ndani nchi za nje, hususan nchi za Uarabuni.

94.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 Sekretarietiitaendelea kupambana na biashara haramu ya usafirishaji binadamu ikiwemo kutoa elimu kwa umma pamoja na kuratibu mafunzo kwa wadau/vyombo vinavyosimamia sheria ya Kuzuia na Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu.

UTARATIBU WA KUSHUGHULIKIA MALALAMIKO

95.      Mheshimiwa Spika, jumla ya Malalamiko 175 kutoka kwa wananchi dhidi ya utendaji wa Wizara yalipokelewa katika kipindi cha mwezi Julai, 2017 hadi Machi, 2018. Kati ya malalamiko hayo 121 yalihusu Jeshi la Polisi, 26 Jeshi la Magereza, 19 Uhamiaji, matatu (3) Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, matatu (3) Idara ya Huduma kwa Wakimbizi, mawili (2) Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa na moja (1) Idara ya Huduma ya Sheria. Aidha, malalamiko 100 yalishughulikiwa na kukamilika na mengine 75 yanaendelea kushughulikiwa yakiwa kwenye hatua mbalimbali. Wizara itaendelea kupokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi katika mwaka 2018/19 ili kuimarisha utoaji wa huduma.

USAJILI WA VYAMA VYA KIJAMII NA KIDINI

96.    Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2018 jumla ya maombi 252 ya kusajili vyama yalipokelewa ambapo maombi 178 ni vyama vya kijamii na 74 ni vyama vya kidini. Kati ya maombi hayo vyama 136 vilisajiliwa na maombi 5 yalikataliwa kutokana na kutotimiza matakwa ya kisheria na sababu nyingine za kiusalama na maombi 111 ya usajili wa vyama yapo katika hatua mbalimbali za kushughulikiwa.Wizara itaendelea na zoezi la usajili na uhakiki wa vyama vya kijamii na kidini katika mwaka 2018/19.

97.     Mheshimiwa Spika, hata hivyo kuna malimbikizo mengi ya maombi ya usajili ya vyama vya kidini kutokana na maombi yote kutakiwa kufikia ofisi ya Msajili Makao Makuu ya Wizara. Wakati Serikali inaelekea kuwa na ofisi za msajili kwa kila kanda, naelekeza wote wenye Taasisi za Kidini mikoani wafike ofisi za wilaya na kuwasilisha maombi yao kwa Katibu Tawala wa Wilaya. Na wote waliofikisha maombi katika wilaya husika, wapate utambuzi wa awali ili taasisi hizo zifanye kazi zikifahamika wakati taratibu za kupata usajili wa kudumu ukiendelea. Narudia wapatiwe utambuzi wa awali wakati wanasubiri usajili wa kudumu.

Maendeleo ya Rasilimali Watu na Ajira Makao Makuu ya Wizara

98.    Mheshimiwa Spika, Makao Makuu ya Wizara imepanga kuajiri watumishi 74 ili kuziba nafasi zilizoachwa wazi kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufariki, kustaafu na kuacha kazi. Wizara pia itawapandisha vyeo watumishi 106 wa kada mbalimbali na nafasi 11 za watumshi watabadilishwa vyeo.

Mapambano Dhidi ya Maambukizi ya VVU/UKIMWI

99.    Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia miongozo husika Wizara iliendelea kuwapatia fedha za kila mwezi watumishi wanaoishi na virusi vya UKIMWI na UKIMWI kwa ajili ya kuimarisha afya zao dhidi ya magonjwa nyemelezi.  Aidha, Wizara ilitoa elimu ya jinsi ya kujikinga na magonjwa sugu yasiyoambukizwa kwa watumishi 200. Katika mwaka 2018/19 Wizara itaendelea kutoa elimu ili kuwahamasisha watumishi kufuata taratibu za afya ili kujikinga na maambukizi dhidi ya virusi vya UKIMWI na UKIMWI pamoja na magonjwa sugu yasiyoambukizwa.

C.  SHUKRANI

100.    Mheshimiwa Spika, natoa shukurani zangu za dhati kwa Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mhandisi Hamad Masauni kwa msaada wake anaonipa katika kutekeleza majukumu ya Wizara. Pia, nawashukuru kwa dhati Katibu Mkuu Meja Jenerali (Mstaafu) Projest A. Rwegasira na Naibu Katibu Mkuu Balozi Hassan S. Yahya kwa juhudi zao kubwa za kusimamia utendaji kazi wa Wizara.

101.      Mheshimiwa Spika, vilevile, nawashukuru Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi, Bw. Simon N. Sirro; Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Dkt. Juma A. Malewa; Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Bw. Thobias E. Andengenye; Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna P. Makakala; na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Bw. Andrew W. Massawe. Natoa shukurani zangu pia kwa Makamishna; Makamishna Wasaidizi; Wakuu wa Idara, Vitengo na Sehemu; askari na watumishi wote kwa kuendelea kutekeleza vema kazi na majukumu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

102.    Mheshimiwa Spika, vilevile, ninatoa shukrani zangu kwa nchi    wahisani zikiwemo Austarlia, Botswana, Canada, China, Finland, India, Italia, Jamhuri ya Watu wa Korea, Marekani, Morocco, Uingereza na Ujerumani pamoja na Taasisi na Mashirika ya Kimataifa ya DFID, FSDT, IOM, UNDP, UNHCR, Vyombo vya Habari, Taasisi za kijamii, kidini na zisizo za Serikali na wananchi kwa kuendelea kutoa misaada na taarifa mbalimbali ambazo zimesaidia utendaji kazi wa Wizara.

103.    Mheshimiwa Spika, kipekee naishukuru familia yangu, ndugu, marafiki na wananchi, hususan wa Jimbo langu la Iramba Magharibi kwa ushirikiano wao katika kuchangia maendeleo ya jimbo letu.

D. HITIMISHO

104.    Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kudhibiti matukio ya uhalifu ili kuhakikisha amani na usalama unaendelea kuwepo nchini. Katika kutekeleza jukumu hilo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itashirikiana na vyombo vingine vya dola nchini pamoja na wadau mbalimbali.

105.     Mheshimiwa Spika, naomba sasa Bunge lako Tukufu liidhinishe Bajeti ya jumla ya Shilingi 945,555,651,000 kwa ajili ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2018/19. Kati ya fedha hizo, Shilingi 907,269,969,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida, ambapo Shilingi 385,725,478,187 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Shilingi 521,544,490,813 ni Mishahara. Fedha za Miradi ya Maendeleo ni Shilingi 38,285,682,000 kati ya fedha hizo Shilingi 37,500,000,000 ni fedha za ndani na Shilingi 785,682,000 ni fedha za nje.

106.    Mheshimiwa Spika, naomba kutoa Hoja.

Comments