Featured Post

TUKIFUATA MAADILI NA MIIKO YA UONGOZI TUTAMSAIDIA MAGUFULI



Na Daniel Mbega
YEHU mwana wa Yehoshafati, mwana wa Nimshi alikuwa miongoni mwa wafalme wa Israel na alitawala baada ya Ahabu katika Samaria.
Kabla ya kuwa mfalme, yeye ndiye aliyekuwa jemedari wa jeshi la Israel.
Katika kipindi hicho wafalme waliotangulia walikuwa wamemuasi Bwana, Mungu wao ambaye aliwakomboa kutoka utumwani Misri, wakaabudu miungu ya kigeni ambayo Mungu, kwa kinywa cha Nabii Musa, aliwakataza.

Siku alipoingia tu madarakani, Yehu akaamua kuuondoa uovu wote ndani ya Israel ambao ulikuwa umemkasirisha Mungu na kulitia taifa hilo mikononi mwa adui zake.
Aliwafyeka manabii wote wa Baali na Ashera, miungu ya kigeni iliyokuwa ikiabudiwa, na akawaua manabii na wale wote waliokuwa wakimwinamia na kumtolea sadaka Baali. Baada ya hapo Mungu akaibariki Israel tena.
Naam. Hiyo ilikuwa ni miaka mingi nyuma, na Yehu alitekeleza maagizo ambayo Bwana, Mungu wa Israel alikuwa ameagiza, siyo kwa makusudi yake.
Leo hii dunia inaendeshwa kwa utawala wa sheria, wala hawezi kutokea mtawala yeyote akawafyeka watu wake, hata wakosefu, kwa upanga, bali atawabana kwa sheria zile zilizowekwa.
Tanzania ni taifa ambalo kwa kipindi kirefu sasa wananchi wake wamekuwa wakiilalamikia serikali yao kwa matendo mengi maovu, ukiwemo ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.
Wananchi wanaishi maisha duni wakati viongozi wenye dhamana wakijilimbikizia mali za umma kwa kutumia nyadhifa zao, kero ambazo zimesababisha Chama cha Mapinduzi kipate wakati mgumu katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inafafanua vyema kuhusu maadili na miiko ya uongozi, lakini kwa makusudi kabisa viongozi wetu wamekuwa kama wanaomwinamia Baali na kumtolea sadaka za kuteketezwa.
Wameiacha hata misingi imara iliyosimika taifa hili na kuleta heshima, kwa sababu ingawa tuko kwenye mfumo wa vyama vingi, lakini sidhani kama zile ahadi 10 za mwana Tanu, chama kilichoikomboa nchi yetu kutoka kwenye makucha ya wakoloni, eti zinaweza zisiwe na maana.
Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja; Nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote; Nitajitolea nafsi yangu kuondoa umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma; Rushwa ni adui wa haki. Sitapokea wala kutoa rushwa; Cheo ni dhamana. Sitakitumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu; Nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu na kutumia elimu yangu kwa faida ya wote; Nitashirikiana na wenzangu wote kuijenga nchi yetu; Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko; Nitakuwa mwanachama mwaminifu wa Tanu na raia mwema wa Tanganyika na Afrika; na Nitakuwa mtiifu na mwaminifu kwa Rais wa Serikali ya Tanganyika ndizo ahadi yakini za mwana Tanu ambazo kipindi kile cha awamu ya kwanza zilijenga nidhamu na kudumisha uzalendo.
Kwa tafsiri nyingine, ahadi hizi ni kiapo, na kwenda kinyume chake ni sawa na kuifuata miungu ya kigeni kama walivyofanya Waisraeli kabla Yehu hajatwaa ufalme mikononi mwa Ahabu na mkewe Yezebeli.
Taifa lilikuwa linaelekea kubaya na haikushangaza hata baadhi ya watu, kabla ya kumwelewa Dk. Magufuli wakati wa kampeni, walitamani eti ‘hata kama wangewekewa mbuzi wangeweza kumchagua, lakini siyo CCM’ ambayo watendaji wachache walikuwa wamekiuka misingi yake.
Kutokana na hali hiyo, Watanzania walihitaji mabadiliko, na zaidi mtu ambaye angeweza kuleta mabadiliko hayo kwa kuvaa uso wa Yehu na kuwakamata manabii wote wa Baali ili awakatilie mbali.
Rais Dk. John Magufuli ameingia kwa kasi kama alivyofanya Yehu, mwana wa Yehoshafati, zamani zile, lakini yeye hatumii upanga kwa watu ambao wamekwenda kinyume na sheria za nchi na kukiuka maadili na miiko ya uongozi.
Kitendo cha kuwafurumusha vigogo takriban 100 ndani ya siku 50 tu alizokaa Ikulu kinadhihirisha kwamba Dk. Magufuli siyo tu amekuja kulikomboa taifa hili kutoka katika makucha ya mafisadi wachache, bali pia amerudisha imani kwa wananchi kwamba anaweza kusimamia sera za CCM ambazo zilibaki kwenye makaratasi tu.
Kauli mbiu yake ya ‘Hapa Kazi Tu!’ imesaidia kurudisha heshima ya kazi kwa sababu huko nyuma watumishi wa umma walikuwa wakifanya kazi kwa mazowea bila kujali wanazalisha nini almuradi tu wanapata mishahara yao.
Mwalimu Julius Nyerere alipata kusema: "...Binadamu hao unaotuona hapa, na hao waliosambaa dunia nzima wanaishi kwa kazi. Hawana namna nyingine ya kuishi. Wakiacha kufanya kazi watakufa; hawana namna nyingine; kuishi kwao, na kuendelea kuishi, lazima wafanye kazi... Lakini binadamu haishi kama farasi. Binadamu haridhiki kuishi kama farasi au punda; binadamu ana kitu anakiita maendeleo; lazima aendelee... Wakati mwingine ili kusudi maendeleo haya yaje wana shughuli za kupigana misasa akili, wanapanuana mawazo tu, nayo ni kazi... nendeni mkaulizane... kama kazi si kitu cha lazima, kama binadamu anaweza kujikalia tu hafanyi kazi, akaishi, na maendeleo yakaja bila kazi. Na huyo anayepinga ujamaa naye ajiulize kama hilo analipinga? Na hilo la kufanya kazi analipinga au kuna jingine analopinga?"
Wakati wa kampeni Dk. Magufuli aliahidi kutowafumbia macho mafisadi na wala rushwa, huku akiahidi kuanzisha mahakama maalum ya kuwashughukilia ‘majizi’ wote.
Suala la kupambana na ufisadi halihitaji sera wa ilani ya chama, bali uwezo wa kiongozi katika kutoa uamuzi wenye kuzingatia utawala bora na maadili ya uongozi, ambayo yamemomonyoka kwa kiasi kikubwa.
“Nawaombeni mnichague kwa sababu mimi ni maji moto, nipeni urais muone nitakavyowaunguza mafisadi,” alisikika akisema kwenye kampeni zake. Tayari amekwishawaunguza na kuwababua mafisadi ndani ya serikali na kasi yake bado inaendelea.
Watanzania walikuwa wanahitaji mabadiliko, lakini Dk. Magufuli kwa kipindi kifupi amedhihirisha siyo tu mabadiliko, bali hata maendeleo ya kweli yatapatikana.
Alisema wakati wa kampeni: “Natambua kuwa Watanzania mnataka maisha mazuri, naahidi kukomesha wizi na rushwa haraka kwa sababu palipo na rushwa hakuna maendeleo. Haiwezekani mwananchi anaumwa, anapokwenda hospitali anaambiwa akanunue dawa kwenye duka binafsi lililo jirani na hospitali… kwa nini duka binafsi liwe na dawa na hospitali ikose dawa, nimejiandaa kulishughulikia hilo.”
Leo hii anapowabana hao mafisadi na viongozi wazembe na wabadhilifu, ni dhahiri wapo watu wanaochukia kwa sababu wananyang’anywa tonge mdomoni.
Kupambana na mafisadi wakubwa siyo jambo dogo, ndiyo maana hata viongozi wa dini wamesikika wakisema ni lazima Rais Magufuli aombewe ulinzi – kwa Mungu, kwa sababu kazi anayoifanya ‘imebarikiwa’.
Lakini kwa nini tusubiri mpaka tufuatwe na ‘Yehu’ ndipo tutimize wajibu wetu? Kwa nini tusubiri kuadhiriwa eti tunamwabudu Baali na Ashera?
Ninaamini kwamba, kila mtu akichapa kazi na kuzingatia maadili na miiko ya viongozi, tutalijenga taifa letu kuwa lenye nidhamu ya juu na tutakuwa tumemsaidia Dk. Magufuli.
Kwa kufanya hivyo pia tutaimarisha uzalendo hata kwa vizazi vyetu, maana Mungu humlaani mtu hata kizazi chake cha nne, vivyo humbariki mtu hata kizazi chake cha nne!
Wasalaam!

0656-331974

Comments