Featured Post

JAFO AITABIRIA SERENGETI BOYS UBINGWA WA AFRIKA



NA SELINA MATHEW, DODOMA
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, amesema kama Serengeti Boys waliweza kushinda kwenye mashindano yaliyopita na kuleta ushindi nyumbani basi ana uhakika watashinda hata kwenye Kombe la Bara la Afrika.

Aidha, amewapongeza vijana hao kwa heshima kubwa waliyoipa nchi baada ya kutwaa ubingwa wa Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) nchini Burundi na kuomba malezi ya vijana hao yasimamiwe ili yasiende kupotea mitaani baadaye.
Jafo aliyasema hayo jana wakati akizindua matangazo ya moja kwa moja ya Umoja wa Michezo ya Shule za Sekondari (Umisseta) na ya Umoja wa Michezo wa Shule za Msingi Tanzania (Umitashumta) yatakayorushwa na kituo cha Televisheni cha Azam kuanzia Juni 4 hadi 29 mwaka huu katika viwanja vya Butimba vilivyopo jijini Mwanza.
“Taifa letu limepata heshima kubwa kupitia vijana hawa juzi juzi waziri aliweza kuwapokea pale uwanja wa ndege, vipaji vya vijana wale walioweza kucheza mpira na kuzifunga timu zote tokea mwanzo mpaka wamemaliza ubora wao ni ubora wa hali ya juu.
"Waziri Mwakyembe tuwaatamie vizuri tusiwapoteze vijana wale, mimi naamini kama tuliweza kuzishinda timu zote tukiwalea vizuri mpaka mwisho vijana wale nina uhakika tunaenda kushinda kombe la bara la afrika sina mashaka na nyinyi,” aliongeza Jafo.
Waziri Jafo aliwataka maofisa elimu wa mikoa hasa wanaosimamia michezo nchini  kuhakikisha wanawapeleka walimu wa michezo waliofundishwa katika shule za michezo ili wafundishe shule maalum zilizotengwa kuandaa vijana kimichezo.
“Waziri Ndalichako unasimamia sera na umetoa maelekezo kwa mujibu wa sera na hivi sasa kila mkoa tuna shule zipatazo mbili za michezo, na bahati nzuri kwa taarifa za wataalam wangu shule zile zimeanza kusimamiwa vizuri kwa kuinua vipaji vya vijana wetu ndani ya nchi yetu, hivyo naomba mlisimamie,” alisisitiza.
Aidha, alisema kitendo cha Televisheni ya Azam  kurusha matangazo hayo moja kwa moja kitatoa hamasa kwa vijana wenyewe na wazazi kuona umuhimu wa michezo hiyo na kuruhusu watoto wao kuweza kushiriki lakini huku akiwataka wadau kuunga mkono jitihada hizo.
Awali, akizungumza katika uzinduzi huo waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisisitiza kila mkoa kuhakikisha wanakuwa na shule mbili mahsusi kwa ajili ya michezo ili kuinua kiwango cha michezo kwa vijana.


Comments