Featured Post

DKT. KIJAJI AITAKA BENKI YA ABC KUPELEKA HUDUMA VIJIJINI KUCHOCHEA SEKTA YA KILIMO NA VIWANDA

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (wa pili kulia), akikata utepe kuashilia kufunguliwa rasmi kwa tawi jipya la Benki ya ABC Jijini Dodoma huku akishuhudiwa na Naibu Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Walemavu, Mhe. Anthony Mavunde (kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Bilinith Mahenge (kulia) na Kaimu Mkurugenzi wa Benki hiyo Bw. Imani John, Jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Bilinith Mahenge, wakizungumza jambo kabla ya kufungua rasmi tawi la Benki ya ABC Jijini Dodoma.

Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
SERIKALI imelipa madeni ya wakandarasi na watoa huduma mbalimbali yanayofikia zaidi ya shilingi trilioni 1.2 katika mwaka huu wa fedha hatua iliyochangia kuongeza ukwasi wa fedha katika jamii ikiwa ni hatua ya Serikali ya kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi unakua kwa haraka.
Hayo yamesemwa Jijini Dodoma, na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, wakati akifungua rasmi tawi la benki ya ABC, lililoanzisha huduma zake za kibenki mkoani humo tangu Januari mwaka huu.
Alisema kuwa hatua hiyo imechukuliwa ili kuwaongezea uwezo wajasiriamali na wafanyabiashara waliotoa huduma Serikalini ili waongeze mzunguko wa fedha katika uchumi.
Ametoa rai kwa wakazi wa mkoa wa Dodoma kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na Benki hiyo ambayo riba yake haizidi asilimia 17 ili waweze   kuendeleza shughuli  za uzalishaji mali na huduma za jamii kwa kuwekeza katika miradi inayochochea kasi ya ukuaji wa uchumi.
"Ni matarajio yangu kuwa sehemu kubwa ya mikopo itakayotolewa na Benki yetu ya ABC, itaelekezwa kwenye sekta ya kilimo na ujenzi wa viwanda vidogo vidogo, vya kati, mifugo, uvuvi na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na misitu" alisema Dkt. Kijaji
Dkt. Kijaji alisisitiza umuhimu wa uwepo wa sekta imara ya fedha itakayochochea ujenzi wa viwanda vitakavyo saidia kuongeza thamani ya bidhaa za kilimo pamoja na kukuza ajira kwa vijana.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo ya ABC Bw. Imani John, alieleza kuwa Benki yake yenye mtaji wa zaidi ya shilingi bilioni 67 imeendelea na jitihada zake za kupanua huduma zake ili kukidhi mahitaji ya kibenki ya wananchi.
Alisema kuwa benki yake imeanzisha huduma zake katika Jiji la Dodoma kufuatia utafiti uliofanyika hivi karibuni unaoonesha kuwa asilimia 13 pekee ya wakazi wa mkoa huo wanafikiwa na huduma za kipenki, pamoja na uamuzi wa benki hiyo wa kuunga mkono hatua ya Serikali ya kuufanya mkoa wa Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi.
Kwa upande wake Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Walemavu, Mhe. Anthony Mavunde, ameishukuru Benki ya ABC kwa kupeleka huduma za kibenki karibu na wananchi wa Jiji la Dodoma na kuwataka wananchi wa mkoa huo kuchangamkia fursa za mikopo ili waweze kujikwamua kiuchumi na kujiletea maendeleo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge, pamoja na kuipongeza Benki ya ABC kwa hatua yake ya kusogeza huduma za kibenki kwa wakazi wa Jiji la Dodoma, amezitaka taasisi nyingine kuwekeza katika sekta hiyo pamoja na huduma nyingine kama vile ujenzi wa Hoteli za kisasa kwa kuwa mkoa huo una fursa nyingi ikiwemo ardhi yenye rutuba.
Benki ya ABC inafanya huduma zake hapa nchini kwa zaidi ya miaka 20 na inamilikiwa na wanahisa  akiwemo TDFC ambaye ni mbia wa ABC Holding Ltd, anayemiliki asilimia 14.7, kati ya asilimia hizo 14.7, asilimia 68 zinamilikiwa na ABC Holding ltd, na asilimia 32 zinamilikiwa na Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Comments