Featured Post

BAJETI YA NISHATI 2018/2019: WIZARA YAOMBA TRILIONI 1.69/-


HOTUBA YA WAZIRI WA NISHATI MHE. DKT. MEDARD MATOGOLO CHANANJA KALEMANI (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA NISHATI KWA MWAKA 2018/19

UTANGULIZI

1.      Mheshimiwa   Spika,  kufuatia taarifa  iliyowasilishwa  leo  hapa  Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji ya Mwaka 2017/18 na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Taasisi zilizo chini yake kwa Mwaka 2018/19.

2.      Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kutekeleza majukumu yangu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu. Vilevile, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwawezesha Waheshimiwa Wabunge wenzangu kutekeleza kazi zao za Kibunge na kushiriki Mkutano huu wa 11 wa Bunge lako Tukufu.
3.      Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee nitumie fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miongozo makini wanayonipatia ili kuhakikisha kuwa azma ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda inafikiwa. Ni wazi kuwa viongozi wetu hawa wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa maelekezo yenye lengo la kuhakikisha kuwa umeme wa kutosha, wa uhakika, unaotabirika na wa gharama nafuu unazalishwa ili kuchochea ukuaji wa viwanda hapa nchini. Nampongeza Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuiongoza vyema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
4.   Mheshimiwa Spika, nampongeza pia Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa usimamizi thabiti wa shughuli za Serikali ndani na nje ya Bunge lako Tukufu. Ni imani yangu kuwa kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, Viongozi wetu hawa wa Kitaifa wataendelea kuwa chachu ya uhamasishaji wa shughuli za maendeleo nchini.
5.   Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kumshukuru Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kuniteua kuiongoza Wizara ya Nishati. Uteuzi huo umenipa fursa ya kutoa mchango wangu katika kuisimamia Sekta hii muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu. Napenda kumhakikishia Mhe. Rais na Watanzania kuwa nitasimamia shughuli za Wizara hii kwa nguvu zangu zote, akili zangu zote, ubunifu na weledi mkubwa ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Nishati inadhihirisha kuwa ndiyo injini kuu katika kujenga uchumi wa viwanda wa Taifa letu. Vilevile, nampongeza Mhe. Subira Khamis Mgalu, Mbunge wa Viti Maalum kwa kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati.
6.      Mheshimiwa Spika, napenda nikupongeze wewe binafsi, Naibu Spika, Wenyeviti wa Bunge, Wenyeviti wote wa Kamati mbalimbali za Kudumu pamoja na watendaji wote wa Ofisi ya Bunge lako Tukufu kwa uongozi wenu mahiri katika kuliongoza Bunge hili na Kamati zake. Kwa namna ya pekee nampongeza Mhe. Dustan Luka Kitandula (Mb.), kwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na Mhe. Mariam Ditopile Mzuzuri (Mb.), kwa kuteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo. Aidha, nawapongeza na kuwashukuru Wajumbe wote wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa kupokea Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara kwa Mwaka 2017/18 na Makadirio ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2018/19.
7.      Mheshimiwa Spika, pamoja na upya wa Kamati hiyo, imekuwa ikitoa michango na ushauri unaolenga kuboresha utendaji wa Wizara kwa maslahi ya Taifa, hususan katika kuhakikisha kuwa umeme wa uhakika unazalishwa na wananchi wengi zaidi wanafikiwa na huduma hiyo hapa nchini. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa Wizara ya Nishati itaendelea kupokea ushauri na mapendekezo ya Kamati hiyo na Kamati nyingine za Bunge katika kuhakikisha kuwa Wizara inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
8.      Mheshimiwa Spika, naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuwapongeza, Mhe. Dkt. Damas Daniel Ndumbaro, Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini; Mhe. Justin Joseph Monko, Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini; Mhe. Dkt. Stephen Lemono Kisurwa, Mbunge wa Jimbo la Longido; Mhe. Maulid Mtulia, Mbunge wa Jimbo la Kinondoni; na Mhe. Dkt. Godwin Mollel, Mbunge wa Jimbo la Siha kwa kuchaguliwa kwao kwa kishindo kuwa Wawakilishi wa wananchi katika Majimbo yao. Hakika ni heshima kubwa waliyopewa na wananchi na nawaombea kila la heri katika kutekeleza jukumu lao hilo la uwakilishi katika Bunge letu Tukufu.
9.      Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kuungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kutoa pole kwako wewe binafsi, Naibu Spika, Bunge lako Tukufu na kwa familia ya aliyekuwa Mbunge wa Songea Mjini, Mheshimiwa Leonidas Gama kwa kuondokewa na mpendwa wetu huyo. Tunamwomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi, Amina.
10.       Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, naomba sasa kuwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Shughuli za Wizara ya Nishati kwa Mwaka 2017/18 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2018/19.

A.   TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA WIZARA YA NISHATI KWA MWAKA 2017/18

11.     Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara kwa Mwaka 2017/18 ulijielekeza katika maeneo yafuatayo: kuimarisha uzalishaji, usafirishaji na kuongeza kasi ya usambazaji wa umeme nchini; kufanikisha utekelezaji wa Mradi mkubwa wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta ghafi kutoka Kabaale (Uganda) hadi Bandari ya Tanga (Tanzania); kuendeleza miradi ya nishati jadidifu kama vile umeme-jua,  maporomoko ya maji, jotoardhi na tungamotaka; kuwezesha uwekaji wa miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia katika viwanda mbalimbali na matumizi ya majumbani pamoja na kufanikisha utekelezaji wa Mradi wa kusindika gesi asilia (Liquefied Natural Gas - LNG); kuvutia uwekezaji katika Sekta ya Nishati, hususan katika uzalishaji wa umeme kupitia vyanzo mbalimbali vilivyopo; utafutaji wa mafuta na gesi asilia; na kuwezesha Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Nishati kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
12.     Mheshimiwa Spika, maeneo mengine ni: kuendelea kutekeleza agizo la Serikali la kuhamia Dodoma; kuwajengea uwezo Watumishi wa Wizara katika fani za umeme, mafuta, gesi asilia na nishati jadidifu; kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kunufaika na rasilimali za mafuta na gesi asilia; kuelimisha umma na kuboresha mawasiliano kati ya Wizara na wadau mbalimbali kuhusu masuala ya Nishati. Wizara ilijielekeza pia katika kusimamia, kufuatilia na kuboresha Sera, Sheria, Mikakati na Miongozo mbalimbali ili kuboresha ufanisi na tija katika Sekta ya  Nishati.
13.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini (Fungu 58) iliidhinishiwa na Bunge Jumla ya Shilingi bilioni 998.34. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 945.89 sawa na asilimia 94.7 ya bajeti yote zilitengwa kwa ajili ya Sekta ya Nishati. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 916.84 sawa na asilimia 96.9 ni fedha za Maendeleo na Shilingi bilioni 29.04 sawa na asilimia 3.1 ni fedha za Matumizi ya Kawaida. Kati ya fedha za Maendeleo zilizotengwa, Shilingi bilioni 748.60 sawa na asilimia 81.7 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 168.24 sawa na asilimia 18.3 ni fedha za nje. Kwa upande wa Bajeti ya Matumizi ya Kawaida, Shilingi bilioni 14.92 sawa na asilimia 1.6 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (O.C) na Shilingi bilioni 14.12 sawa na asilimia 1.5 ya bajeti yote ni Mishahara ya Watumishi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake.
14.     Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Aprili, 2018 Wizara ya Nishati kupitia (Fungu 58) ilikuwa imepokea Jumla ya Shilingi bilioni 446.50 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za Sekta ya Nishati. Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 424.91 sawa na asilimia 95.2 zilikuwa ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ambapo fedha za ndani ni Shilingi bilioni 413.09 sawa na asilimia 97.2 na Shilingi bilioni 11.82 sawa na asilimia 2.8 ni fedha za nje. Aidha, kiasi kilichobaki cha Shilingi bilioni 21.58 sawa na asilimia 4.8 zilikuwa kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida.
15.     Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha mwaka 2017/18 iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini ilipanga kukusanya Jumla ya Shilingi bilioni 532.83 kutokana na mapato yanayohusu Sekta ya Nishati. Mapato hayo yanatokana na vyanzo mbalimbali vikiwemo: Shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asillia; Mauzo ya gesi asilia; Mauzo ya Nyaraka za Zabuni; Tozo ya umeme na Stakabadhi nyinginezo. Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Aprili, 2018 Wizara ilikuwa imekusanya Jumla ya Shilingi bilioni 280.27 sawa na asilimia 53. Wizara itaendelea na juhudi za kukusanya mapato ili kufikia lengo lililowekwa kwa kipindi cha mwaka 2017/18.

Mafanikio yaliyopatikana kwa Mwaka 2017/18
16.       Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyopatikana katika Sekta ya Nishati kwa kipindi cha mwaka 2017/18 ni pamoja na:
            (i)         Kuendelea na utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Kupeleka Umeme Vijijini kupitia REA Awamu ya Tatu ambapo hadi mwezi Mei, 2018 kazi zilizokamilika ni pamoja na ujenzi wa kilomita 985 za njia ya msongo wa kV 33, ujenzi wa kilomita 1,870.37 za njia ya usambazaji umeme wa msongo wa kV 0.4 na ufungaji wa transfoma 751 zenye ukubwa tofauti. Jumla ya vijiji 518 vimeunganishwa na kuwashwa umeme na wateja 14,817 wameunganishiwa umeme na Jumla ya vijiji 420 vimejengwa miundombinu ya umeme na vinatarajiwa kuwashwa hivi karibuni;
         (ii)         Kukamilika kwa upelekaji umeme katika Makao Makuu ya Wilaya ya Tanganyika na Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli na kufanya Makao Makuu ya Wilaya zote nchini kuwa yamepelekewa umeme;
       (iii)         Kukamilika kwa asilimia 100 kwa Mradi wa ORIO katika Miji ya Ngara, Biharamulo na Mpanda ambapo kwa sasa miji hiyo inapata umeme wa uhakika;
        (iv)         Kusitisha matumizi ya mitambo ya kukodi ya binafsi ya kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta mazito katika kuzalisha umeme ikiwemo ya Aggreko na IPTL na kuokoa wastani wa jumla ya Shilingi bilioni 11.46 kwa mwezi;
          (v)         Kukamilisha ujenzi wa Mradi mpya wa Kinyerezi II na kuingiza katika Gridi ya Taifa umeme wa MW 168 mwezi Aprili, 2018;
        (vi)         Kukamilika kwa Mradi mpya wa Kinyerezi II na ukarabati wa mitambo ya kuzalisha umeme ya Kihansi, Kidatu, Mtera, New Pangani Falls na Ubungo II kumeongeza uhakika wa upatikanaji umeme katika Gridi ya Taifa na kuwa na ziada ya umeme wa wastani wa MW 280 kwa siku na kuondokana na mgao wa umeme;
     (vii)         Kukamilika kwa ukarabati wa mitambo ya kuzalisha umeme Mtwara pamoja na kuongeza mitambo mipya miwili (2) yenye uwezo wa MW 4 na hivyo kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme katika Mikoa ya Lindi na Mtwara;
   (viii)         Kukamilika kwa asilimia 100 kwa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kV 132 yenye urefu wa kilomita 80 kutoka Mtwara hadi Mahumbika (Lindi) pamoja na vituo vya kupoza umeme vya Mtwara na Mahumbika;
       (ix)         Kukamilika kwa asilimia 95 kwa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kV 220 kutoka Makambako hadi Songea;
          (x)         Kukamilika kwa ujenzi wa vituo vipya vya kupoza umeme vya Mbagala, Kipawa, Gongolamboto na Mburahati Mkoani Dar es Salaam;
       (xi)         Kukamilika kwa ujenzi wa vituo vya kupoza umeme vya Njiro B, Mount Meru, Sakina, Unga Ltd, Kiltex na Themi Mkoani Arusha;
     (xii)         Kukamilika kwa ujenzi wa vituo vya kupoza umeme vya Bomambuzi na Trade School Mkoani Kilimanjaro;
  (xiii)         Kukamilika kwa ukarabati wa vituo vya kupoza umeme vya Mikocheni, Oysterbay, City Centre, Gongolamboto, Kariakoo, Mbagala, Chang’ombe, Kipawa na Ubungo Mkoani Dar es Salaam;
   (xiv)         Kuunganishwa kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara katika Gridi ya Taifa kutokana na kukamilisha ujenzi wa njia ya msongo wa kV 33 kutoka Mbagala kupitia Mkuranga, Ikwiriri, Somanga Fungu, Lindi hadi Mtwara yenye urefu wa kilomita 451;
      (xv)         Kuunganishwa kwa Wilaya za Ngara na Biharamulo katika Gridi ya Taifa kutokana na kukamilika kwa ujenzi wa njia ya msongo wa kV 33 yenye urefu wa kilomita 70 na hivyo kupunguza gharama za matumizi ya mafuta kwa wastani wa Shilingi bilioni 3.5 kwa mwaka. Kukamilika kwa ujenzi wa njia hizi kumewezesha kuunganisha nchi yetu katika Gridi ya Taifa kutoka Mtwara mpakani mwa Msumbiji hadi Ngara mpakani mwa Rwanda na Burundi;
   (xvi)         Kusitisha uingizaji wa vifaa vya ujenzi wa miundombinu ya umeme ikiwemo nguzo, transfoma, nyaya na mita za LUKU ndani ya nchi na hivyo kulipunguzia gharama kubwa Shirika la Umeme Nchini, TANESCO na kuokoa  wastani wa Shilingi bilioni 162.57 kwa mwaka;
 (xvii)         Kuanza maandalizi ya ujenzi na utekelezaji wa Mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa maji wa maporomoko ya Mto Rufiji MW 2100;
 (xviii)         Kuunganishiwa umeme wateja wapya 201,046 na kufanya jumla ya wateja waliounganishiwa umeme hadi mwezi Mei, 2018 kufikia 2,226,036;
 (xix)            Kukamilika maandalizi ya utekelezaji wa Mradi wa Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania);
     (xx)         Kukamilika kwa ujenzi na kuanza kutumika kwa Bandari ya Mtwara kupokea mafuta hivyo kufanya Tanzania kuwa na Bandari tatu (3) za kupokea mafuta zikiwemo Dar es Salaam na Tanga;
   (xxi)         Kuanza utekelezwaji wa Mpango wa Kusambaza Gesi Asilia Majumbani katika Mikoa ya Dar es Salaam na Mtwara; na
 (xxii)         Kuongezeka kwa gesi asilia iliyogunduliwa kutoka Futi za Ujazo Trilioni  57.25 mwaka 2016/17 na kufikia Futi za Ujazo Trilioni 57.54 mwaka 2017/18 kutokana na ugunduzi wa kitalu cha Ruvuma cha Futi za Ujazo Bilioni 466 kutoka Futi za Ujazo Bilioni 178.

17.       Mheshimiwa Spika, mafanikio hayo yametokana na utekelezaji thabiti wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 - 2020 chini ya Uongozi makini wa Serikali ya Awamu ya Tano. Ilani hiyo imejielekeza katika kufikia uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2020 ambao Sekta ya Nishati ndiyo injini.

B.   MPANGO NA BAJETI YA WIZARA YA NISHATI KWA MWAKA 2018/19

18.     Mheshimiwa Spika, maeneo ya kipaumbele ya Wizara ya Nishati kwa kipindi cha mwaka 2018/19 ni pamoja na: kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo: Mradi wa kuzalisha umeme katika Mto Rufiji MW 2,100 uliopo wilayani Rufiji na miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia ya Kinyerezi I - Extension MW 185; Kinyerezi II MW 240; Somanga Fungu MW 330 Mkoani Lindi; pamoja na MW 300 Mkoani Mtwara; kuimarisha mifumo ya usafirishaji wa umeme mkubwa nchini; kuendelea na utekelezaji wa Awamu ya Tatu ya Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini (REA III); kuendelea na utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Bomba la kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania); kuimarisha shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia; na kuendeleza miradi ya nishati jadidifu (jotoardhi, upepo na umeme-jua). Wizara imejielekeza katika kutekeleza maeneo mengine ya kipaumbele yakiwemo: kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wa Wizara na Taasisi zilizo chini yake katika kusimamia Sekta ya Nishati; kuboresha mazingira ya ofisi kwa watumishi wa Wizara na Taasisi zake ili kutoa huduma bora zaidi; na kuendelea kuelimisha umma na kuboresha mawasiliano na wadau mbalimbali kuhusu masuala ya nishati.
19.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara imepangiwa kukusanya Jumla ya Shilingi bilioni 394.45. Kati ya makusanyo hayo, Shilingi bilioni 394.44 zitakusanywa kupitia shughuli za mafuta na gesi asilia na Shilingi milioni 10.00 zitakusanywa kupitia shughuli za utawala.

C.         SEKTA NDOGO YA UMEME

   HALI YA UPATIKANAJI  WA UMEME NCHINI
20.     Mheshimiwa Spika, katika kutimiza azma ya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda na kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025, Serikali kupitia Wizara ya Nishati imelenga kuzalisha umeme MW 5,000 ifikapo mwaka 2020 na kufikisha MW 10,000 ifikapo mwaka 2025. Aidha, mahitaji ya umeme nchini yameendelea kuongezeka kutokana na kukua na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi zinazohitaji nishati ya umeme wa kutosha, wa uhakika, unaotabirika na wa gharama nafuu katika uzalishaji.
21.     Mheshimiwa Spika, umeme uliozalishwa nchini uliongezeka kutoka GWh 7,092 mwaka 2016 na kufikia GWh 7,114 mwaka 2017 sawa na ongezeko la asilimia 0.3. Aidha, katika mwaka 2017/18 uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme (installed capacity) iliyopo nchini umeongezeka kutoka MW 1,450 mwaka 2016/17 na kufikia MW 1,517.47 mwezi Mei, 2018 sawa na ongezeko la asilimia 4.7. Ongezeko hilo limetokana na kukamilika kwa mitambo sita (6) ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi II ambayo hadi sasa inazalisha Jumla ya MW 168. Kati ya MW 1,517.47 zilizounganishwa katika Gridi ya Taifa ni MW 1,435.56 na zilizopo nje ya Gridi ya Taifa ni MW 81.91 (Kielelezo Na.1 na Na.2). Ongezeko hili limewezesha kuwa na umeme wa ziada wa wastani wa MW 280 ambapo matumizi ya juu ya umeme yamefikia wastani wa MW 1,051 kwa siku.

MIRADI YA KUZALISHA UMEME
Ujenzi wa Mradi wa Rufiji (Rufiji Hydro Power Project) – MW 2,100
22.     Mheshimiwa Spika, lengo la kutekeleza Mradi huu ni kuzalisha umeme wa Jumla ya MW 2,100 kwa kutumia maji (Hydro Power Plant) katika Bonde la Mto Rufiji. Utekelezwaji wa Mradi huu mkubwa nchini ni kichocheo muhimu katika kuwezesha Tanzania kufikia azma yake ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Katika kipindi cha mwaka 2017/18 hatua iliyofikiwa ni pamoja na kufanya uchambuzi wa zabuni (tender evaluation) zilizowasilishwa na Wakandarasi walioonesha nia ya kutekeleza Mradi huu. Aidha, ujenzi wa njia ya msongo wa kV 33 kutoka eneo la Dakawa kwa ajili ya kupeleka umeme utakaotumiwa na Mkandarasi wakati wa ujenzi wa Mradi ulianza mwezi Novemba, 2017 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Julai, 2018.
23.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2018/19 Serikali itaendelea na utekelezaji wa Mradi huu ambapo kazi zitakazofanyika ni pamoja na: ujenzi wa kambi na ofisi za wafanyakazi; ujenzi wa bwawa (main dam and spillways); na ujenzi wa njia kuu za kupitisha maji (tunnels). Fedha za maendeleo za ndani Shilingi bilioni 700 zimetengwa katika mwaka  2018/19 kwa ajili ya kuanza kutekeleza kazi hizo. Utekelezaji wa shughuli za ujenzi wa Mradi unatarajiwa kuanza mwezi Julai, 2018 kwa Mkandarasi kuanza kazi za awali kwa miezi mitatu (3) na kufuatiwa na ujenzi wa miundombinu ya Mradi unaotarajiwa  kukamilika katika kipindi cha miezi 36.

Mradi wa Kinyerezi I Extension - MW 185
24.     Mheshimiwa Spika, Mradi huu unahusu upanuzi wa kituo cha kuzalisha umeme cha Kinyerezi I kwa kuongeza mitambo itakayozalisha MW 185 na kufanya kituo hicho ambacho kwa sasa kinazalisha umeme wa MW 150 kuzalisha jumla ya MW 335. Mradi huu unagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 188 sawa na takriban Shilingi bilioni 434. Katika mwaka 2017/18 kazi zilizokamilika ni pamoja na: ujenzi wa misingi ya kusimika mitambo ya kuzalisha umeme na transfoma; ujenzi wa misingi ya kituo cha kupoza umeme; na ujenzi wa njia ya msongo wa kV 220 inayounganisha mtambo wa Kinyerezi I Extension na Kinyerezi II na kuunganishwa katika Gridi ya Taifa.
25.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2018/19 kazi ya usimikaji wa mitambo pamoja na ukamilishaji wa ujenzi wa kituo cha kupoza umeme zitafanyika kwa gharama ya Shilingi bilioni 164 zikiwa ni fedha za ndani. Ujenzi wa Mradi ulianza mwezi Novemba, 2016 na unatarajiwa kukamilika mwezi Januari, 2019.

Mradi wa Kinyerezi II - MW 240
26.     Mheshimiwa Spika, Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia wa Kinyerezi II unatarajiwa kuongeza Jumla ya MW 240 katika Gridi ya Taifa. Uzalishaji umeme katika Mradi huu ulizinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli tarehe 03 Aprili, 2018. Hadi sasa mitambo sita (6) ya gas turbines imefungwa na inazalisha umeme wa jumla ya MW 168 zilizoingizwa katika Gridi ya Taifa. Ufungaji wa mitambo miwili (2) yenye uwezo wa kuzalisha Jumla ya MW 80.4 kwa kutumia mvuke (steam turbines) unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2018. Gharama za kutekeleza Mradi huu ni Dola za Marekani milioni 344 sawa na takriban Shilingi bilioni 794.12. Asilimia 15 ya gharama za Mradi huu ni fedha za ndani na asilimia 85 ni mkopo wa masharti nafuu kutoka benki za Japan Bank for International Cooperation (JBIC) na Sumitomo Mitsui Banking Corporation (SMBC) za Japan.

Mradi wa Somanga Fungu - MW 330

27.     Mheshimiwa Spika, Mradi huu unahusu ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme wa MW 330 kwa kutumia gesi asilia. Aidha, Mradi unahusu ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kV 400 umbali wa kilomita 198.2 kutoka Somanga Fungu hadi Kinyerezi. Mradi huu utamilikiwa na Serikali kupitia TANESCO kwa asilimia 100. Gharama za Mradi zinakadiriwa kuwa Dola za Marekani milioni 396 sawa na takriban Shilingi bilioni 914.16. Upembuzi Yakinifu wa Mradi umekamilika na taratibu za kumpata Mkandarasi mwenye uwezo wa kitaalam na fedha kwa kushindanishwa chini ya utaratibu wa EPC plus Financing zinaendelea.
28.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2018/19 kazi zilizopangwa kufanyika ni pamoja na: kukamilisha taratibu za kumpata Mkandarasi na fedha za kutekeleza Mradi; kumpata Mshauri Mwelekezi wa usimamizi wa Mradi; na kuanza utekelezaji wa Mradi. Shilingi bilioni 4.5 fedha za nje zimetengwa ili kutekeleza kazi hizo. Ujenzi wa Mradi huu unatarajiwa kuanza mwezi Septemba, 2018 na kukamilika ifikapo mwezi Septemba, 2021.

Mradi wa Mtwara MW 300
29.     Mheshimiwa Spika, Mradi wa Mtwara unahusu ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme wa MW 300 kwa kutumia gesi asilia na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme. Mradi utahusu pia ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kV 400 umbali wa kilomita 253 kutoka Mtwara hadi Somanga Fungu. Utekelezaji wa Mradi huu utaimarisha upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara. Mradi huu unatarajiwa kugharimu Dola za Marekani milioni 360 sawa na takriban Shilingi bilioni 831 na utamilikiwa na Serikali kupitia TANESCO kwa asilimia 100. Katika mwaka 2017/18 kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kuanza Upembuzi Yakinifu chini ya ufadhili wa JICA mwezi Julai, 2017 ambao unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti, 2018.
30.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 kazi zilizopangwa kufanyika ni pamoja na: kukamilisha Upembuzi Yakinifu wa Mradi; kumtafuta Mshauri Mwelekezi; na kuandaa nyaraka za zabuni kwa ajili ya kumpata Mkandarasi. Jumla ya Shilingi bilioni 3.7 zinakadiriwa kutumika kuwalipa fidia wananchi watakaopisha Mradi. Katika mwaka 2018/19 fedha za nje Shilingi bilioni 4 zimetengwa ili kutekeleza shughuli za Mradi huu. Ujenzi wa Mradi unatarajiwa kuanza mwezi Novemba, 2018 na kukamilika mwezi Juni, 2021.

Mradi wa Kakono – MW 87
31.     Mheshimiwa Spika, Mradi huu unahusu ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme wa MW 87 kwa kutumia maji ya Mto Kagera na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kV 132 yenye urefu wa kilomita 38.8 kutoka Kakono hadi Kyaka. Gharama za ujenzi wa Mradi ni Dola za Marekani milioni 379.4 sawa na takriban Shilingi bilioni 875.84. Kazi iliyofanyika katika mwaka 2017/18 ni kupima na kutathmini eneo la Mradi ambapo taarifa kuhusu alama za mipaka na tathmini ya eneo la ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme pamoja na njia ya kusafirisha umeme imekamilika. Aidha, Mshauri Mwelekezi (Kampuni ya Studio Pietrangeli kutoka Italia) kwa ajili ya  kusimamia utekelezaji wa Mradi ameshapatikana.
32.     Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2018/19, kazi zitakazofanyika ni pamoja na: kuwalipa fidia wananchi watakaopisha Mradi; kumpata Mtaalam Mshauri kwa ajili ya kufanya utafiti zaidi wa kijiolojia na haidrolojia; na kutayarisha zabuni kwa ajili ya Mkandarasi wa ujenzi wa kituo na miundombinu ya kusafirisha umeme. Jumla ya Shilingi bilioni 4.05 zimetengwa kwa ajili ya shughuli hizo. Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 2 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 2.05 ni fedha za nje. Mradi huu unatarajiwa kuanza mwezi Machi, 2019 na kukamilika ifikapo mwezi Novemba, 2021.

Mradi wa Rusumo - MW 80
33.     Mheshimiwa Spika, Mradi huu unahusu ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme wa MW 80 kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Kagera ambapo umeme huo utagawanywa kwa usawa kati ya nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi. Mradi unahusisha pia ujenzi wa njia za kusafirisha umeme wa msongo wa kV 220 kutoka Rusumo hadi kituo cha kusafirishia umeme kwa kila nchi. Kwa upande wa Tanzania umeme utasafirishwa hadi Nyakanazi. Katika kipindi cha mwaka 2017/18, kazi zilizofanyika ni kuanza ujenzi wa: bwawa la kuhifadhia maji; njia za kupitisha maji (intake tunnel); eneo la kusimika mitambo (power house); barabara za kuingia eneo la Mradi; pamoja na ofisi na nyumba za wafanyakazi.
34.     Mheshimiwa Spika, kazi zilizopangwa kufanyika mwaka 2018/19 ni: kukamilisha ujenzi wa kambi ya kudumu ya wafanyakazi; kukamilisha miundombinu ya barabara za kuingia eneo la Mradi; na kuendelea na ujenzi wa bwawa la kuhifadhia maji; njia za kupitisha maji (intake tunnel); na eneo la kusimika mitambo (power house). Fedha za nje Shilingi  bilioni 3 zimetengwa katika mwaka  2018/19 kwa ajili ya Mradi huu. Utekelezaji wa Mradi ulianza mwezi Machi, 2017 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Februari, 2021.

Mradi wa Murongo/Kikagati - MW 14
35.     Mheshimiwa Spika, Mradi huu unahusu ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme wa MW 14 kwa kutumia maji ya Mto Kagera zitakazogawanywa kwa usawa kati ya nchi ya Tanzania na Uganda. Mradi pia utahusisha ujenzi wa njia za kusafirisha umeme wa msongo wa kV 33 yenye urefu wa kilomita 0.7 kutoka Kikagati (Uganda) hadi Murongo (Tanzania). Mradi huu unatekelezwa na mwekezaji binafsi, Kampuni ya Kikagati Power Company Ltd (KPCL) iliyosajiliwa nchini Uganda ambapo umeme utakaozalishwa utauzwa kwa Kampuni za Uganda Electricity Transmission Company Ltd (UETCL) na Tanzania Electricity Supply Company Ltd (TANESCO). Mradi utagharimu Dola za Marekani milioni 58 sawa na takriban Shilingi bilioni 133.89.
36.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2017/18 kazi zilizofanyika ni pamoja na: kusainiwa kwa Mkataba wa Ugawanaji wa Umeme kwa Usawa (Power Sharing and Sales Agreement) kati ya UETCL na TANESCO; kusainiwa kwa Mkataba wa Kuuziana Umeme (Power Purchase Agreement) kati ya kampuni ya KPCL na UETCL; kukamilika kwa malipo ya fidia kwa wananchi wanaopisha Mradi; na kuanza kutekelezwa kwa kazi za awali za ujenzi ikiwemo kambi ya wafanyakazi na barabara za kuingia kwenye eneo la Mradi (access road). Kazi zitakazotekelezwa kwa mwaka 2018/19 ni pamoja na: kukamilisha ujenzi wa kambi ya kudumu ya wafanyakazi na miundombinu ya barabara za kuingia eneo la Mradi; na kuanza ujenzi wa bwawa (main dam and spillways) na njia kuu za kupitisha maji (tunnels). Mradi huu ulianza mwezi Novemba, 2017 na unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, 2020.

Mradi wa Malagarasi – MW 45
37.     Mheshimiwa Spika, Mradi huu unahusu ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme wa MW 45 kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Malagarasi Mkoani Kigoma na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kV 132 yenye urefu wa kilomita 53 kutoka Malagarasi hadi Kidahwe-Kigoma. Gharama za utekelezaji wa Mradi ni Dola za Marekani milioni 149.5 sawa na takriban Shilingi bilioni 345.12. Katika mwaka 2017/18 kazi zilizofanyika ni pamoja na: uboreshaji wa tathmini ya athari za jamii na mazingira (ESIA) na tathmini ya fidia kwa wananchi watakaopisha Mradi; upimaji na uthamini wa eneo la Mradi wa njia ya kusafirisha umeme umeanza; na Mshauri Mwelekezi (Kampuni ya Studio Pietrangeli kutoka Italia) kwa ajili ya  kusimamia utekelezaji wa Mradi amepatikana.
38.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, kazi zilizopangwa kufanyika ni pamoja na: kukamilisha Upembuzi Yakinifu wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kV 132; kumpata Mkandarasi; na kukamilisha upimaji na uthamini wa eneo la Mradi na njia ya kusafirisha umeme. Jumla ya Shilingi bilioni 7.8 zinakadiriwa kutumika kuwalipa fidia wananchi watakaopisha Mradi. Katika mwaka 2018/19 Shilingi bilioni 4.3 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za Mradi. Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 1.5 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 2.8 ni fedha za nje. Shughuli za ujenzi wa Mradi huu zinatarajiwa kuanza mwezi Machi, 2019 na kukamilika ifikapo mwezi Juni, 2021.

Mradi wa Ruhudji - MW 358
39.     Mheshimiwa Spika, Mradi huu unahusu ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme wa MW 358 kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Ruhudji. Mradi utahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kV 400 yenye urefu wa kilomita 170 kutoka Ruhudji Mkoani Njombe hadi kituo cha kupoza umeme cha Kisada Mkoani Iringa. Kazi zilizofanyika hadi sasa ni pamoja na Serikali kuwasilisha maombi ya ufadhili wa Mradi kwa Benki ya Dunia na kufanyika kwa zoezi la uhakiki wa kiwango cha maji katika Mto Ruhudji ili kujua kiwango halisi cha umeme kinachoweza kuzalishwa. Utekelezaji wa Mradi huu unakadiriwa kugharimu Dola za Marekani milioni 460.6 sawa na takriban Shilingi trilioni 1.06. Katika kipindi cha mwaka 2018/19 Serikali itaendelea na majadiliano na wafadhili ili kuwezesha upatikanaji wa fedha za kutekeleza Mradi. Mradi huu unatarajiwa kuanza kujengwa  katika kipindi cha mwaka 2018/19 baada ya fedha kupatikana na unatarajiwa kukamilika mwaka 2020/21.

Miradi ya Kinyerezi III - MW 600
40.     Mheshimiwa Spika, Mradi huu utahusisha  ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia MW 600 katika  awamu mbili (2) za MW 300 kwa kila awamu katika eneo la Kinyerezi - Dar es salaam. Kazi zilizopangwa kutekelezwa katika mwaka 2018/19 ni pamoja na: kukamilisha Upembuzi Yakinifu; na kumpata Mkandarasi mwenye uwezo wa kitaalam na fedha kwa kushindanishwa chini ya utaratibu wa EPC plus Financing. Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kuanza mwezi Novemba, 2018 na kukamilika mwezi Desemba, 2021.

Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa kutumia Makaa ya Mawe Kiwira – MW 200
41.     Mheshimiwa Spika, Mradi huu unahusu ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe chenye uwezo wa MW 200 katika eneo la Kiwira na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kV 220 yenye urefu wa kilomita 100 kutoka Kiwira hadi Uyole-Mbeya. Gharama za kutekeleza Mradi zinakadiriwa kuwa Dola za Marekani milioni 320 sawa na takriban Shilingi bilioni 738.72. Katika mwaka 2018/19 TANESCO na STAMICO watakamilisha Makubaliano ya Awali (Memorandum of Understanding - MoU) ya kuuziana makaa ya mawe na taratibu za kumpata Mkandarasi mwenye teknolojia na uwezo wa kutekeleza Mradi na kuanza shughuli za ujenzi baada ya kukamilisha Upembuzi Yakinifu. Mradi huu unatarajiwa kuanza mwezi Oktoba, 2019 na kukamilika mwezi Aprili, 2022.

Ukarabati wa Mitambo katika Kituo cha Kufua Umeme cha Hale (Hale Hydro Power Plant)
42.     Mheshimiwa Spika, Mradi huu unahusu ukarabati wa mitambo na ujenzi wa miundombinu ya kuzalisha umeme katika Kituo cha Hale ili kuwezesha kituo hicho kuzalisha umeme kwa kiwango cha uwezo wake wa MW 21 kutoka MW 10.5 zinazozalishwa sasa. Makadirio ya gharama za Mradi huu ni SEK milioni 200 sawa na takriban Shilingi bilioni 50.98 ambapo asilimia 60 ya gharama hizo ni msaada kutoka Serikali ya Sweden kupitia Shirika lake la Maendeleo la Kimataifa (Sida) na asilimia 40 ni mchango wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika kipindi cha mwaka 2017/18 kazi zilizofanyika ni pamoja na kukamilika kwa: usanifu (design) wa Mradi; uandaaji wa Mpango Kazi; pre-qualification ya Wakandarasi. Zabuni zitafunguliwa mwezi  Juni, 2018. Kwa mwaka 2018/19 Mkandarasi ataanza kazi ya ukarabati wa mitambo ambapo jumla ya Shilingi bilioni 6.7 fedha za nje zimetengwa. Mradi unatarajiwa kuanza mwezi Oktoba, 2018 na kukamilika mwezi Novemba, 2021.

Mradi wa Umeme Unaotokana na Nishati ya Jua katika Mkoa wa Shinyanga – MW 150
43.             Mheshimiwa Spika, Mradi huu unahusu ujenzi wa kituo cha kufua umeme-jua MW 150 katika eneo la Ibadakuli Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga. Mradi huu unatarajiwa kutekelezwa na Serikali kupitia TANESCO kwa ufadhili wa Taasisi ya Maendeleo ya Ufaransa (AFD). Katika kuendeleza Mradi huu AFD imetoa msaada wa Euro 520,130 sawa na takriban Shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya kuwezesha na kukamilisha zoezi la Upembuzi Yakinifu utakaojumuisha tathmini ya kitaalam, kiuchumi na mazingira. Kazi zilizofanyika katika mwaka 2017/18 ni pamoja na: kukamilisha tathmini ya fidia kwa wananchi watakaopisha Mradi pamoja na kupatikana kwa Mshauri Mwelekezi ambaye ameanza kazi ya Upembuzi Yakinifu unaotarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2018. Jumla ya Shilingi bilioni 1.3 zinakadiriwa kutumika kuwalipa fidia wananchi watakaopisha Mradi. Katika mwaka 2018/19 kazi zilizopangwa kufanyika ni pamoja na: kulipa fidia wananchi watakaopisha Mradi;  kukamilisha taratibu za ufadhili wa Mradi; na kuanza utekelezaji wa Mradi. Mradi huu unatarajiwa kuanza mwezi Januari, 2019 na kukamilika mwezi Desemba, 2020.

Mradi wa Umeme wa Upepo SingidaWind East Africa (WEA) MW 100
44.     Mheshimiwa Spika, Mradi huu ni wa kuzalisha umeme wa MW 100 unaotokana na nishati ya upepo katika eneo la Kisaki na Utaho  Mkoani Singida. Mradi utatekelezwa kwa ubia kati ya Kampuni ya Six Telecoms (Tanzania), International Finance Corporation - IFC (Marekani) na Aldwych International (Uingereza). Gharama za Mradi huu zinakadiriwa kuwa  Dola za Marekani milioni 285 sawa na takriban Shilingi bilioni 657.92. Kwa mwaka 2017/18 majadiliano ya Mkataba wa Kibiashara (PPA) kati ya TANESCO na Kampuni ya Wind East Africa (WEA) yako katika hatua za mwisho. Katika mwaka 2018/19 kazi zilizopangwa kufanyika ni pamoja na kukamilisha majadiliano ya PPA na kuanza utekelezaji wa Mradi. Ujenzi wa Mradi huu unatarajiwa kuanza mwezi Oktoba, 2018 na kukamilika mwezi Desemba, 2020.


UJENZI WA NJIA ZA KUSAFIRISHA UMEME
Mradi wa njia ya Umeme wa Msongo wa kV 220 kutoka Makambako hadi Songea na Usambazaji wa Umeme Vijijini kwa Mikoa ya Njombe na Ruvuma
45.     Mheshimiwa Spika, lengo la Mradi ni kujenga njia ya umeme wa msongo wa kV 220 yenye urefu wa kilomita 250 kutoka Makambako hadi Songea kupitia Madaba. Kazi nyingine zinazohusu Mradi ni: ujenzi wa vituo vipya viwili (2) vya kupoza umeme vya Madaba na Songea mjini; upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Makambako; utandazaji wa nyaya za mawasiliano; ujenzi wa njia za kusambaza umeme wa msongo wa kV 33 wenye urefu wa kilomita 900; na kuunganisha wateja wa awali 22,700 katika Vijiji 120 vya Wilaya za Makambako, Njombe na Ludewa katika Mkoa wa Njombe; na Songea Vijijini, Songea Mjini, Namtumbo na Mbinga katika Mkoa wa Ruvuma.
46.     Mheshimiwa Spika,  kazi zilizotekelezwa kwa mwaka 2017/18 kwa upande wa njia ya kusafirisha umeme kV 220 Makambako hadi Songea ni kukamilika kwa usanifu, utengenezaji, usafirishaji wa vifaa na ujenzi wa misingi ya nguzo.  Kwa upande wa ujenzi wa vituo vya kupoza umeme vyenye uwezo wa kV 220/33 vya Makambako, Madaba na Songea, usafirishaji wa vifaa na ujenzi wa misingi umekamilika. Hadi kufikia mwezi Mei, 2018 ujenzi wa miundombinu ya usambazaji umeme kwenye vijiji 32 kati ya 120 umekamilika na jumla ya wateja 1,500 kati ya 22,000 wameunganishiwa umeme.
47.     Mheshimiwa Spika, kwa ujumla hadi kufikia mwezi Mei, 2018 ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kV 220 kutoka Makambako – Songea umefikia asilimia 95; Ujenzi wa vituo viwili (2) vipya vya kupoza umeme vya Madaba na Songea umefikia asilimia 76; na usambazaji umeme umefika asilimia 68.5 kwa Mikoa ya Ruvuma na Njombe. Kazi zilizopangwa kufanyika mwaka 2018/19 ni kukamilisha: ujenzi wa vituo vya kupoza umeme; ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kV 220; na uunganishaji wa wateja. Jumla ya Shilingi bilioni 13 zimetengwa katika mwaka  2018/19 ili kutekeleza kazi hizo. Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 7 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 6 ni fedha za nje. Mradi huu ulianza mwezi Desemba, 2016 na unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2018.

Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 400 kutoka Iringa - Shinyanga (Backbone – Awamu ya Pili)
48.     Mheshimiwa Spika, Mradi huu unahusu kuongeza uwezo (upgrade) wa vituo vya kupoza umeme kutoka kV 220 hadi kV 400 katika miji ya Iringa, Dodoma, Singida na Shinyanga. Gharama ya Mradi ni Dola za Marekani Milioni 120 sawa na takriban Shilingi bilioni 277.02 zinazotokana na mikopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Benki ya Jumuiya ya Ulaya (EIB) na Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo la Kimataifa (JICA). Katika kipindi cha mwaka 2017/18 Mkandarasi atakayefanya kazi katika vituo vya kupoza umeme vya Dodoma na Singida amepatikana na tayari ameanza kazi. Katika mwaka 2018/19 kazi zilizopangwa kufanyika ni: kumpata Mkandarasi  kwa ajili ya vituo vya Iringa na Shinyanga na kuendelea na utekelezaji wa Mradi. Mradi huu unatarajiwa kuanza mwezi Septemba, 2018 na kukamilika mwezi Juni, 2020.

Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 400 kutoka Masaka - Mwanza 
49.     Mheshimiwa Spika, Mradi huu unahusu ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kV 400 kutoka Masaka nchini Uganda hadi Mwanza - Tanzania na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme wa kV 400/220 katika maeneo ya Kyaka na Rusumo/Nyakanazi. Kazi zilizofanyika kwa mwaka 2017/18 ni kukamilika kwa majadiliano ya Mkataba kati ya TANESCO na Mshauri Mwelekezi Kampuni ya Norconsult kutoka Norway atakayedurusu Upembuzi Yakinifu wa Mradi. Upembuzi Yakinifu huo unatarajiwa kuanza mwezi Oktoba, 2018 na kukamilika mwezi Novemba, 2019. Katika mwaka 2018/19 Shilingi bilioni 2.5 fedha za nje zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo.

Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 400, Iringa - Mbeya – Tunduma - Sumbawanga – Mpanda - Kigoma – Nyakanazi (North West Grid)
50.       Mheshimiwa Spika, Mradi unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kV 400 kutoka Iringa - Mbeya – Tunduma - Sumbawanga – Mpanda - Kigoma – Nyakanazi yenye urefu wa kilomita 1,372. Mradi huu utawezesha kuunganisha umeme maeneo ya Magharibi na Kaskazini-Magharibi mwa Tanzania katika Gridi ya Taifa na kuondoa matumizi ya mitambo ya mafuta (diesel) katika maeneo hayo na kuwafikishia umeme wananchi wengi.
51.     Mheshimiwa Spika, Benki ya Dunia imeonesha nia ya kufadhili ujenzi wa vituo vya kupoza umeme na njia ya kusafirisha umeme kutoka Iringa – Mbeya – Tunduma – Sumbawanga – Kigoma yenye urefu wa kilomita 612 inayounganisha Zambia na Tanzania. Mradi utagharimu Dola za Marekani milioni 455 sawa na takriban Shilingi trilioni 1.05. Sehemu hii ya Mradi itaunganisha Mradi wa North-West grid kV 400 unaoanzia Sumbawanga – Mpanda – Kigoma – Nyakanazi yenye urefu wa kilomita 760. Serikali ya Korea Kusini kupitia Mfuko wake wa Maendeleo (EDCF) imeonesha nia ya kufadhili ujenzi wa vituo vya kupoza umeme katika maeneo ya Kigoma na Nyakanazi kwa Dola za Marekani  milioni 40.5 sawa na takriban Shilingi bilioni 93.49 na AfDB imeonesha nia ya kufadhili ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Nyakanazi hadi Kigoma yenye urefu wa kilomita 280 kwa Dola za Marekani milioni 93.5 sawa na takriban Shilingi bilioni 215.84.
52.     Mheshimiwa Spika, kazi zilizofanyika katika kipindi cha mwaka 2017/18 ni pamoja na: kupima na kufanya tathmini ya maeneo kwa ajili ya kujenga vituo vya kupoza umeme vya Kigoma, Mpanda, Sumbawanga na Tunduma; kukamilisha uandaaji wa taarifa za fidia kwa wananchi watakaopisha Mradi  kutoka Kigoma hadi Nyakanazi; na kuendelea na majadiliano na wafadhili wa Mradi ambao ni Benki ya Dunia, AfDB na EDCF. Jumla ya Shilingi bilioni 25.5 zinakadiriwa kuwa zitatumika kulipa fidia wananchi watakaopisha Mradi katika maeneo ya Iringa - Mbeya; Mbeya – Tunduma - Sumbawanga; na Kigoma - Nyakanazi.
53.  Mheshimiwa Spika, kazi zilizopangwa kufanyika mwaka 2018/19 ni: ulipaji wa fidia kwa wananchi watakaopisha Mradi; kukamilisha majadiliano na wafadhili wa Mradi; kuwapata wakandarasi wa ujenzi; na kuanza utekelezaji wa Mradi. Jumla ya Shilingi bilioni 33.2 zimetengwa kwa ajili ya kazi hizo. Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 31 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 2.2 ni fedha za nje. Mradi huu unatarajiwa kuanza mwezi Desemba, 2018 na kukamilika mwezi Agosti, 2021.

Mradi wa Njia za Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 400 na kV 220, North – East Grid
54.     Mheshimiwa Spika, lengo la Mradi huu ni kusafirisha umeme utakaozalishwa katika kituo cha Kinyerezi, Dar es Salaam kwenda katika Mikoa ya Arusha na Tanga ambapo njia zilizopo kwa sasa zimezidiwa na mahitaji makubwa ya  umeme. Mradi huu utagharimu  Dola za Marekani milioni 692.7 sawa na takriban Shilingi trilioni 1.59. Kati ya gharama hiyo, asilimia 85 ni mkopo kutoka Benki ya Exim ya China na asilimia 15 ni mchango wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Katika kipindi cha mwaka 2017/18 kazi zilizofanyika ni pamoja na: kukamilisha upimaji na tathmini ya mali za wananchi watakaopisha Mradi kwa kipande cha kutoka Kinyerezi - Kiluvya - Chalinze hadi Segera. Fidia kwa kipande cha Kinyerezi – Chalinze inatarajiwa kulipwa wakati wowote kuanzia sasa na maandalizi ya ulipaji fidia kwa kipande cha kuanzia Chalinze hadi Segera yanaendelea. Kwa mwaka 2018/19 jumla ya Shilingi bilioni 47.8 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi. Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 34.8 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 13 fedha za nje.

Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 400 kutoka Somanga Fungu - Kinyerezi
55.       Mheshimiwa Spika, Mradi huu unahusu ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kV 400 kutoka Somanga Fungu Mkoani Lindi hadi Kinyerezi, Dar es Salaam wenye urefu wa kilomita 198 na kujenga kituo cha kupoza umeme cha Somanga Fungu. Mradi huu utaunganisha na kusafirisha umeme unaotarajiwa kuzalishwa katika maeneo ya Somanga Fungu na Mtwara hadi Kinyerezi Dar es Salaam. Gharama za Mradi ni Dola za Marekani milioni 150 sawa na takriban Shilingi bilioni 346.27.
56.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2017/18 kazi zilizofanyika ni pamoja na: kuendelea na ulipaji wa fidia kwa wananchi wanaopisha Mradi ambapo hadi kufikia mwezi Aprili, 2018 jumla ya Shilingi bilioni 49.5 zimelipwa kwa wananchi 2,487 kati ya 3,901. Aidha, Mshauri Mwelekezi (Kampuni ya Byucksan Power Limited ya Korea Kusini) kwa ajili ya kudurusu Upembuzi Yakinifu ameanza kazi mwezi Desemba, 2017 na anatarajia kukamilisha mwezi Julai, 2018. Kazi zilizopangwa kufanyika kwa mwaka 2018/19 ni: kukamilisha malipo ya fidia kwa wananchi waliobaki na kudurusu Upembuzi Yakinifu. Jumla ya Shilingi bilioni 23.5 zimetengwa kutekeleza kazi hizo. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 22 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 1.5 ni fedha za nje. Shughuli za ujenzi zinatarajiwa kuanza mwezi Agosti, 2019 na kukamilika mwezi Machi, 2020.

Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 400 kutoka Rufiji – Chalinze – Dodoma
57.     Mheshimiwa Spika, Mradi huu unahusu ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kV 400 yenye urefu wa kilomita 512 kutoka Rufiji kupitia Chalinze Mkoani Pwani hadi Dodoma na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme wa kV 400/220 katika Mji wa Chalinze na Jiji la Dodoma. Gharama za Mradi zinakadiriwa kuwa Dola za Marekani milioni 276.36 sawa na takriban Shilingi bilioni 637.97.
58.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2017/18 kazi zilizofanyika ni: Upembuzi Yakinifu kwa kipande cha kutoka Chalinze hadi Dodoma; na Upembuzi Yakinifu wa Awali (Pre-feasibility Study) kutoka Rufiji hadi Chalinze. Pia, maandalizi ya kumpata Mshauri Mwelekezi kwa ajili ya kufanya mapitio ya Upembuzi Yakinifu kwa eneo la Rufiji hadi Chalinze yameanza. Kazi zilizopangwa kufanyika kwa mwaka 2018/19 ni: kufanya Upembuzi Yakinifu; kuweka mipaka na kufanya tathmini ya njia ya kusafirishia umeme kutoka Rufiji hadi Chalinze; na kukamilisha malipo ya fidia kwa wananchi watakaopisha Mradi. Fedha za ndani Shilingi bilioni 39 zimetengwa kwa ajili ya kazi hizo. Mradi huu unatarajiwa kuanza mwezi Desemba, 2018 na kukamilika mwezi Desemba, 2020.

Mradi wa Njia ya Umeme wa Msongo wa kV 220 kutoka Bulyanhulu – Geita
59.     Mheshimiwa Spika, Mradi huu unahusu ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kV 220 yenye urefu wa kilomita 55 kutoka Bulyanhulu hadi Geita; ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Geita; upanuzi wa Kituo cha kupoza umeme cha Bulyanhulu; usambazaji wa umeme katika vijiji nane (8) vitakavyopitiwa na Mradi (kilomita 115) ambapo wateja wapya 1,500 wataunganishiwa umeme. Gharama za Mradi huu ni Dola za Marekani milioni 23 sawa na takriban Shilingi bilioni 53.09.
60.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2017/18 kazi zilizofanyika ni pamoja na: kukamilika uhakiki wa fidia kwa wananchi watakaopisha Mradi pamoja na kuwapata Wakandarasi watakaotekeleza Mradi. Jumla ya Shilingi bilioni 2 zinakadiriwa kutumika kuwalipa fidia wananchi watakaopisha Mradi. Kwa mwaka 2018/19  Shilingi bilioni 5 fedha za nje zimetengwa kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa Mradi. Mradi unatarajiwa kuanza mwezi Agosti, 2018 na kukamilika mwezi Aprili, 2020.

Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 220 ya Geita – Nyakanazi na Usambazaji wa Umeme katika Vijiji vitakavyopitiwa na Mradi
61.     Mheshimiwa Spika, Mradi huu unahusu ujenzi wa njia ya kV 220 (km 133), kituo cha kupoza umeme Nyakanazi na kusambaza umeme katika vijiji 32 vinavyopitiwa na Mradi. Gharama za utekelezaji wa Mradi huu ni EURO milioni 45 sawa na takriban Shilingi bilioni 113.31. Mradi huu unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW), Taasisi ya Maendeleo ya Ufaransa (AFD), Umoja wa Ulaya (EU) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
62.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2017/18 kazi zilizofanyika ni: kufanya tathmini na uhakiki wa mali zitakazoathiriwa na Mradi; kumpata Mkandarasi atakayejenga njia ya kusafirisha  umeme; kujenga vituo vya kupoza umeme; na usambazaji wa umeme vijijini. Jumla ya Shilingi bilioni 5.79 zinakadiriwa kutumika kuwalipa fidia wananchi watakaopisha Mradi. Kazi zilizopangwa kufanyika katika kipindi cha mwaka 2018/19 ni kuwalipa fidia wananchi na kuanza utekelezaji wa Mradi. Fedha za nje Shilingi bilioni 1.6 zimetengwa kwa ajili ya shughuli za Mradi. Mradi huu unatarajiwa kuanza mwezi Julai, 2018 na kukamilika mwezi Desemba, 2019.

Mradi wa Njia ya  Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 400 kutoka Singida  - Arusha – Namanga
63.     Mheshimiwa Spika, Mradi huu unahusu ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kV 400 kutoka Singida hadi Namanga kupitia Arusha yenye urefu wa kilomita 414. Mradi umegawanyika katika maeneo matano (5) ya utekelezaji ambayo ni: Singida - Babati (km150); Babati - Arusha (km150); Arusha – Namanga (km114); ujenzi na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme (Substations) na usambazaji wa umeme katika vijiji 21 vitakavyopitiwa na Mradi. Gharama za Mradi huu ni Dola za Marekani milioni 258.82 sawa na takriban Shilingi bilioni 597.48 ambapo asilimia 83 ya fedha hizo zitatolewa na wafadhili (AfDB na JICA). Aidha, Serikali ya Tanzania itachangia Dola za Marekani milioni 43.89 sawa na takriban Shilingi bilioni 101.32 ambazo ni asilimia 17 ya gharama za Mradi.
64.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2017/18 kazi zilizofanyika ni pamoja na: Mkandarasi kufanya detailed survey ya njia ya umeme wa msongo wa kV 400 kutoka Singida hadi Namanga; kusanifu na kufanya majaribio ya nguzo na vifaa vingine vitakavyotumika katika ujenzi; kufanya utafiti wa udongo katika njia ya umeme; na Serikali kukamilisha uhakiki wa malipo ya fidia kwa wananchi watakaopisha Mradi. Jumla ya Shilingi bilioni 68.31 zinakadiriwa kutumika kuwalipa fidia wananchi. Kazi nyingine zilizotekelezwa ni kufanya malipo ya awali (advance payment) kwa Wakandarasi wote wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme na kumpata Mkandarasi wa kujenga kituo kipya cha kupoza umeme cha Kisongo Mkoani Arusha. Vilevile, taratibu za kumpata Mkandarasi atakayesambaza umeme katika vijiji 21 vinavyopitiwa na Mradi zinaendelea.
65.     Mheshimiwa Spika, kazi zilizopangwa kufanyika mwaka 2018/19 ni Serikali kuwalipa fidia wananchi watakaopisha ujenzi wa Mradi na Wakandarasi kuendelea na shughuli za ujenzi wa Mradi. Shilingi bilioni 15 fedha za nje zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza kazi hizo. Utekelezaji wa Mradi huu ulianza mwezi Machi, 2017 na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2019.

Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 400 kutoka Mtwara - Somanga Fungu
66.     Mheshimiwa Spika, Mradi huu unahusu ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kV 400 yenye urefu wa kilomita 253 kutoka Mtwara hadi Somanga Fungu na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme katika Manispaa ya Mtwara. Katika kipindi cha mwaka 2017/18 kazi zilizotekelezwa ni kufanya Upembuzi Yakinifu ulioanza mwezi Julai, 2017 na unatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2018 pamoja na tathmini ya athari za mazingira.
67.     Mheshimiwa Spika, kazi zilizopangwa kutekelezwa kwa mwaka 2018/19 ni kukamilisha: Upembuzi Yakinifu; Taarifa ya Athari za Mazingira; taratibu za ufadhili wa Mradi; uwekaji wa  alama za mipaka na kutathmini mali za wananchi watakaopisha eneo la Mradi; utafutaji wa Mshauri Mwelekezi kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa Mradi; na upatikanaji wa  Mkandarasi wa ujenzi. Mradi huu utafadhiliwa na Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la JICA na unakadiriwa kugharimu Dola za Marekani milioni 231.1 sawa na  takriban Shilingi bilioni 533.49. Fedha za nje Shilingi bilioni 2 zimetengwa katika mwaka 2018/19 kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi. Mradi huu unatarajiwa kuanza mwezi Desemba, 2018 na kukamilika mwezi Machi, 2021.

Mradi wa Rusumo – Nyakanazi kV 220
68.     Mheshimiwa Spika, Mradi unahusu ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kV 220 yenye urefu wa kilomita 98.2  kutoka Rusumo hadi Nyakanazi. Gharama za Mradi ni Dola za Marekani milioni 35 sawa na takriban Shilingi bilioni 80.79. Katika kipindi cha mwaka 2017/18 kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kukamilisha: usanifu wa Mradi; uandaaji wa taarifa ya mpango wa mazingira; utangazaji wa zabuni kwa ajili ya kumpata Mkandarasi; na uhakiki wa fidia kwa wananchi watakaopisha Mradi. Jumla ya Shilingi bilioni 5.19 zinakadiriwa kutumika kuwalipa fidia wananchi watakaopisha Mradi. Kwa mwaka 2018/19 kazi zilizopangwa kufanyika ni: kukamilisha maandalizi ya mkataba wa ujenzi na kumpata Mkandarasi wa Mradi; kuwalipa fidia wananchi; na kuanza ujenzi wa Mradi. Fedha za nje Shilingi bilioni 5 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi. Mradi huu unatarajiwa kuanza mwezi Julai, 2018 na kukamilika mwezi Julai, 2019.

MIRADI YA KUBORESHA NJIA ZA KUSAMBAZA UMEME

Mradi wa Kuboresha Vituo 10 vya Kupoza Umeme
69.     Mheshimiwa Spika, Mradi huu unahusu ujenzi na uboreshaji wa vituo 10 vya kupoza umeme ambavyo ni Mlandizi, Chalinze, Mufindi, Mwakibete, Zuzu, Tabora, Nyakato, Musoma, Kibeta na Same. Vilevile, Mradi unalenga kuboresha Mfumo wa Usimamizi na Upatikanaji wa Data (Supervisory Control and Data Acquisition - SCADA/Energy Management System –EMS) pamoja na kuunga waya wa mawasiliano (optic fiber) wenye urefu wa jumla ya kilomita 1,345 kwa vituo vya Kanda ya Kusini Magharibi, Kanda ya Ziwa na maeneo ya Kondoa, Babati, Mbulu na Karatu ambayo hayana optic fiber.  Gharama za Mradi zinakadiriwa kuwa Euro milioni 53 sawa na takriban Shilingi bilioni 133.45 na unafadhiliwa na Taasisi ya Maendeleo ya Ufaransa (AFD). Katika kipindi cha mwaka 2017/18 kazi iliyofanyika ni kumpata Mshauri Mwelekezi kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa Mradi na anatarajiwa kuanza kazi mwezi Julai, 2018.
70.     Mheshimiwa Spika, kazi zilizopangwa kufanyika mwaka 2018/19 ni pamoja na: kukamilisha durusu ya wigo wa kazi (Scope of Work); kufanya tathmini ya athari kwa jamii na mazingira (ESIA); kuandaa michoro (Conceptual Design); kuwapata Wakandarasi; na kuanza utekelezaji wa Mradi. Mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2020.

Mradi wa TEDAP wa kuboresha njia za usambazaji umeme (Distribution) katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Kilimanjaro
71.             Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha mwaka 2017/18 ufungaji wa vifaa vya kuongozea na kulinda mitambo (control and protection) pamoja na transfoma umekamilika katika vituo vyote 19 na vituo 18 vimewashwa na vinatumika. Aidha, ujenzi wa njia za msongo wa kV 33 na 11 katika Mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Kilimanjaro umekamilika kwa asilimia 100. Kazi zilizopangwa kutekelezwa kwa mwaka 2018/19 ni: kukamilisha kazi zilizobaki katika njia ya msongo wa kV 132 ya Mbagala kwenda Kurasini pamoja na kituo cha kupoza umeme cha Kurasini. Fedha za nje Shilingi bilioni 6.4 zimetengwa katika mwaka 2018/19 kwa ajili ya malipo ya Mkandarasi. Kazi hizo zinatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2018.

Mradi wa Kuboresha Mfumo  wa Usambazaji Umeme katika Jiji la Dodoma chini ya Ufadhili wa JICA
72.     Mheshimiwa Spika, Mradi huu utahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kV 132 kutoka Zuzu kwenda Msalato na kutoka Zuzu kwenda Kikombo pamoja na ujenzi wa vituo viwili (2) vipya vya kupoza umeme katika maeneo ya Msalato na Kikombo Mkoani Dodoma. Kazi nyingine ni ujenzi wa njia za kusambaza umeme wa msongo wa kV 33 katika Jiji la Dodoma. Lengo la mradi huu ni kujiandaa na ongezeko la mahitaji ya umeme yanayokadiriwa kufikia MW 2OO ifikapo mwaka 2020 kutoka mahitaji ya juu ya sasa ya MW 28 kutokana na Serikali kuhamishia shughuli zake Makao Makuu Jijini Dodoma. Katika kipindi cha mwaka 2017/18 kazi zilizofanyika ni pamoja na Serikali kuwasilisha maombi ya ufadhili wa Mradi kwa Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo la JICA. Kazi zilizopangwa kwa mwaka 2018/19 ni kukamilisha taratibu za ufadhili wa Mradi na kuanza utekelezaji. Mradi unatarajiwa kukamilika mwaka 2020/21.

Mradi wa Usambazaji Umeme kwa Maeneo ya Mijini (Urban Electrification Program)
73.     Mheshimiwa Spika, Mradi huu unahusu kuongeza kasi ya kuunganisha wateja mijini na kupanua miundombinu ya usambazaji umeme ili kuhamasisha ujenzi wa viwanda na kufikisha umeme katika makazi na maeneo ya huduma za jamii. Kwa mwaka 2017/18 Serikali iliwasilisha maombi katika Benki ya AfDB kwa ajili ya ufadhili wa Mradi ambapo Benki hiyo imempata Mshauri Mwelekezi kwa ajili ya kuandaa Mpango Kabambe wa Usambazaji Umeme (Distribution Master Plan) katika mikoa minne (4) ya Dodoma, Mbeya, Arusha na Mwanza. Kazi hiyo itakapokamilika itaiwezesha AfDB kupata makadirio ya fedha zinazohitajika kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi katika mikoa husika. Kazi ya kuandaa Mpango huo inatarajiwa kufanyika katika mwaka 2018/19.
74.     Mheshimiwa Spika, Serikali pia imewasilisha maombi Benki ya Dunia kwa ajili ya ufadhili wa Mradi katika mikoa mingine iliyobaki ya Tanzania. Bara Katika mwaka 2018/19 Benki ya Dunia itamtafuta Mshauri Mwelekezi atakayefanya Upembuzi Yakinifu ili kuainisha maeneo ya mijini yanayohitaji umeme katika mikoa hiyo. Upembuzi Yakinifu unatarajiwa kuanza mwezi Septemba, 2018 na kukamilika mwezi Septemba, 2019 ambapo fedha za nje Shilingi bilioni 7 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo.

MIRADI YA KUSAMBAZA UMEME VIJIJINI

Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Pili (Turnkey Phase II)
75.     Mheshimiwa Spika, Mradi huu ulihusisha ujenzi wa vituo sita (6) vya kuongeza msongo wa umeme (kV 11/33) katika miji ya Kigoma, Kasulu, Kibondo, Ngara, Mbinga na Tunduru; ujenzi wa kilomita 17,740 za njia ya msongo wa kV 33; ujenzi wa kilomita 10,970 za njia za usambazaji umeme wa msongo wa kV 0.4/0.23; ufungaji wa transfoma 4,100 za ukubwa tofauti; na uunganishaji wa wateja wa awali 250,000.
76.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeendelea  kukamilisha utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Pili (REA II) kwa kumalizia kazi za nyongeza (additional scope) na kuunganisha wateja. Hadi kufikia mwezi Desemba, 2017 Mradi huo ulikuwa umekamilika kwa asilimia 99 kwa kufikisha miundombinu ya umeme katika vijiji 2,598 kati ya 2,697  sawa na asilimia 96.3 na hivyo kuwezesha kuwaunganishia umeme jumla ya wateja 178,641 ambao ni sawa na asilimia 71.46 ya matarajio ya awali ya wateja 250,000. Zoezi la kuunganisha wateja ni endelevu kulingana na wateja wanavyolipia na kazi hiyo itaendelea kufanywa na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO). Uunganishwaji wa wateja hao umechangia ongezeko la upatikanaji wa huduma za umeme vijijini (access) kufikia asilimia 49.5.
77.      Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mradi huu uliokuwa umesimama katika Mikoa ya Kilimanjaro na Singida kutokana na Mkandarasi wa awali Kampuni ya Spencon Services Ltd kushindwa kuukamilisha kwa sasa unaendelea. Mradi huo unatekelezwa na Kampuni za Kitanzania za Njarita Contractors na Octopus Engineering kwa Mkoa wa Kilimanjaro na JV EMEC Engineering Dynamic and Systems na East African Fossil Co & CMG Construction Co Ltd JV kwa Mkoa wa Singida. Kazi zitakazofanyika katika mwaka 2018/19 ni: ukamilishaji wa Mradi katika Mikoa ya Kilimanjaro na Singida; kumalizia marekebisho madogo-madogo (snags) yaliyojitokeza katika miundombinu iliyojengwa; na TANESCO kuendelea kuwaunganisha wateja wanaolipia. Mradi katika Mikoa hii ya Kilimanjaro na Singida unatarajiwa kukamilika Mwezi Agosti 2018.

78.     Mheshimiwa Spika, Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) unalenga: kufikisha umeme katika vijiji 7,873 ambavyo hadi kufikia mwezi Juni, 2016 vilikuwa havijafikiwa na miundombinu ya umeme. Aidha, katika kipindi cha kuanzia mwezi  Februari hadi Mei, 2018 jumla ya vijiji 518 kati 7,873 vilivyobaki tayari vimeunganishiwa umeme na hivyo kubaki vijiji 7,355 vinavyoendelea kuunganishiwa umeme. Kazi zinazofanyika ni pamoja na: kujenga miundombinu ya kusambaza umeme na kufunga transfoma katika maeneo mbalimbali ikiwemo Taasisi za Umma, miradi ya maji na shughuli nyingine za kiuchumi, vitongoji na vijiji ambavyo havijafikiwa na umeme (Turnkey III - Round One); vijiji vilivyopitiwa na miundombinu ya usafirishaji wa umeme kupitia Mradi wa Densification; vijiji vilivyopo pembezoni mwa Mkuza wa njia kuu ya kusafirisha umeme wa msongo wa kV 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga. Kazi nyingine zinazofanyika ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya usambazaji na ufungaji wa mifumo ya nishati jadidifu katika maeneo yaliyo mbali na Gridi ya Taifa ambayo yanahusisha visiwa vilivyomo ndani ya Maziwa na Bahari (Off-Grid Renewable Energy Project).

79.     Mheshimiwa Spika; utekelezaji wa miradi iliyopo katika Mpango wa REA III ni kama ifuatavyo:-

(i)    Mradi wa Usambazaji Umeme katika Maeneo ambayo yameshafikiwa na Miundombinu ya Umeme (Densification)

80.     Mheshimiwa Spika, Mradi huu unahusisha kuongeza wigo wa usambazaji umeme katika vijiji, vitongoji na maeneo ambayo tayari yana miundombinu ya umeme katika vijiji 4,395 vilivyounganishwa umeme. Mradi  utatekelezwa katika Mikoa yote ya Tanzania Bara na utahusisha: ujenzi wa kilomita 18,625 za umeme wa msongo wa kV 33; kilomita 35,614 za umeme wa msongo wa kV 0.4; ufungaji wa transfoma 13,622; pamoja na uunganishaji wa wateja wa awali 992,373 kwa kipindi cha miaka mitano (5) kuanzia mwaka 2016/17 hadi mwaka 2020/21 sawa na wateja 300,000 katika utekelezaji wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza.
81.     Mheshimiwa Spika, Mradi huu unatekelezwa kwa awamu  ambapo Awamu ya Kwanza (Densification – Round I) ilianza mwezi Aprili, 2017 katika mikoa nane (8) ya Pwani, Tanga, Arusha, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe na Mara na hadi kufikia mwezi Mei, 2018 imekamilika kwa asilimia 98. Katika Awamu hii jumla ya vijiji 300 kati ya 305 vimepatiwa umeme pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 12,084 kati ya 53,000. Gharama ya utekelezaji kwa awamu hii ni Shilingi bilioni 62. Aidha, Mradi wa Densification – Round II utahusisha vitongoji vilivyomo katika vijiji 4,090 vilivyosalia na unakadiriwa kugharimu jumla ya Shilingi bilioni 1,938. Awamu hii itaanza kutekelezwa mwezi Julai, 2018.

(ii)      Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (Grid Extension) – Mzunguko wa Kwanza

82.   Mheshimiwa Spika, Mradi huu unatekelezwa katika vijiji 3,559 vya Mikoa yote ya Tanzania Bara na unahusisha ujenzi wa takriban kilomita 15,600 za njia ya msongo wa kV 33; kilomita 16,420 za njia za usambazaji wa msongo wa kV 0.4; ufungaji wa transfoma zenye ukubwa tofauti zipatazo 6,740 na uunganishaji wa wateja wa awali 300,000. Aidha, maombi ya vijiji 1,541 vilivyorukwa yamepokelewa na yanafanyiwa tathmini kwa ajili ya utekelezaji baada ya kupitia taratibu husika. Ongezeko hilo litafanya jumla ya vijiji vitakavyopelekewa umeme katika Mzunguko huu wa Kwanza kufikia 5,100 na kubaki na vijiji 2,773 vitakavyofikishiwa umeme katika Mzunguko wa Pili. Mradi huu wa REA utaanza mwezi Julai, 2019 na kukamilika mwaka 2020/21.
83.   Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Mei, 2018 katika kipindi cha miezi mitatu (3) ya ujenzi baada ya kukamilika kwa kipindi cha miezi mitatu (3) cha uhakiki wa vijiji na miezi mitatu (3) mingine ya uingizaji wa vifaa na maandalizi ya ujenzi, jumla ya vijiji 502 vinajengwa miundombinu ya umeme ikiwa ni pamoja na kusimikwa nguzo na kufungwa transfoma katika Mikoa yote Tanzania Bara isipokuwa Mikoa ya Kigoma na Katavi. Vijiji hivi vinatarajiwa kuwashwa umeme hivi karibuni na vingine vinaendelea kuwashwa umeme.  Mbali na vijiji hivyo vilivyojengwa miundombinu, hadi kufikia mwezi Mei, 2018 vijiji vingine 545 vimewashwa umeme sawa na wastani wa vijiji 182 kwa mwezi ambayo ni asilimia 92 ya lengo la kuwasha wastani wa vijiji 197 kwa mwezi. Pia, katika vijiji vilivyowashwa umeme wateja 15,073 wameunganishwa sawa na asilimia 90 ya lengo la kuunganisha umeme wateja 16,666. Utekelezaji wa Mradi huu kwa upande wa Mkoa wa Kigoma Mkandarasi CCC – ETERN-HEI Consortium amepatikana na ataanza kazi mwezi Juni, 2018. Aidha, kwa upande wa Mkoa wa Katavi Mkandarasi atapatikana mwezi Juni, 2018 na kuanza kazi mara moja.

(iii)       Mradi wa Kusambaza Umeme katika Vijiji vilivyopo pembezoni mwa Mkuza wa Njia ya Msongo wa kV 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga

84.     Mheshimiwa Spika; Mradi huu unahusisha usambazaji wa umeme katika vijiji 121 vilivyo pembezoni mwa mkuza wa Mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kV 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga ambapo jumla ya wateja 25,000 wa awali wanatarajiwa kuunganishiwa umeme. Mradi pia unahusisha upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Mtera. Hadi kufikia mwezi Mei, 2018, jumla ya vijiji 25 vimefikiwa na umeme na kufanya jumla ya wateja waliounganishiwa umeme kufikia 861. Kwa upande wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Mtera usanifu unatarajiwa kukamilika mwezi Mei, 2018. Shughuli za ujenzi wa kituo zitaanza mwezi Julai, 2018 na kukamilika mwezi Machi, 2019. Mradi huu unagharimu Shilingi bilioni 57 ambazo ni msaada kutoka Serikali za Sweden na Norway.

(iv)        Miradi ya Uendelezaji wa Nishati Jadidifu (Off-Grid Renewable Projects)

85.     Mheshimiwa Spika, Mradi huu unahusisha uwekaji wa mifumo midogo (mini grids, micro grids and stand-alone systems) katika maeneo ambayo yana vyanzo vya nishati mbadala kwa ajili ya kuzalisha umeme. Vilevile, Mradi unahusisha ufungaji wa mifumo ya umeme-jua katika Taasisi za Serikali na maeneo ya huduma za jamii zilizoko vijijini pamoja na kuwezesha ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa bayogesi katika Taasisi za Umma kwa ajili ya kupikia na kuwashia taa ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa ambavyo vina athari kubwa kwa mazingira.
86.     Mheshimiwa Spika, Mradi wa Uendelezaji wa Nishati Jadidifu umegawanyika katika makundi mawili ambapo Kundi la Kwanza linahusisha usambazaji wa umeme vijijini kwa maeneo yaliyopo nje ya gridi kwa mfumo wa Malipo kwa Matokeo (Results Based Financing - RBF). Katika Kundi la  Kwanza, Mikataba ya miradi 22  yenye uwezo wa kuzalisha jumla ya MW 24.4 zitakazosambazwa katika vijiji 139 na kuunganisha wateja 33,939 imesainiwa kati ya REA na Waendelezaji wa Miradi na kazi zinaendelea katika maeneo ya Mikoa ya Iringa, Njombe, Tanga, Dodoma, Singida, Lindi, Mtwara, Tabora, Mwanza, Geita na Kagera.
87.       Mheshimiwa Spika, Kundi la Pili la Mradi huu linahusu kufunga mifumo ya umeme-jua (solar PV systems) katika Taasisi za Umma zikiwemo shule za sekondari, vituo vya afya na zahanati zilizopo mbali na gridi pamoja na masoko ili kuboresha huduma zinazotolewa katika taasisi hizo. Mradi huu unatekelezwa katika Wilaya nane (8) za Biharamulo, Bukombe, Chato, Sikonge, Kasulu, Kibondo, Tunduru na Namtumbo. Hadi kufikia mwezi Mei, 2018 utekelezaji wa Mradi umefikia  asilimia 92 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2019.

(v)           Mradi wa Usambazaji Umeme katika Vijiji vilivyopo Pembezoni mwa Miji (Peri-Urban Rural Electrification Program)

88.       Mheshimiwa Spika, Mradi huu unalenga kusambaza umeme katika vijiji vilivyopo pembezoni mwa miji ili kuboresha huduma za kijamii na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa katika maeneo hayo. Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umekamilisha usanifu wa mradi wa majaribio utakaotekelezwa katika Mkoa wa Pwani na Wilaya ya Kigamboni Mkoani Dar es Salaam. Mradi huu utavinufaisha vijiji/vitongoji zaidi ya 250 na kuwaunga wateja wa awali wapatao 37,000. Mradi huu unafadhiliwa na Serikali ya Norway kwa gharama ya Shilingi bilioni 83. Mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili, 2019.
89.     Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Aprili, 2018 REA ilikuwa imepokea jumla ya Shilingi bilioni 313.5 kati ya Shilingi bilioni 469 zilizopangwa kwa mwaka 2017/18 sawa na asilimia 67 ya bajeti. Aidha, katika mwaka 2018/19 fedha zilizotengwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Usambazaji Umeme Vijijini ni jumla ya Shilingi bilioni 412.08, kati ya hizo, Shilingi bilioni 375.38 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 36.70 ni fedha za nje.

D.     SEKTA NDOGO YA NISHATI JADIDIFU

90.    Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhamasisha uwekezaji katika vyanzo vya kuzalisha umeme nchini kwa miradi midogo ya nishati jadidifu isiyozidi MW 10. Katika mwaka 2017/18 EWURA imekamilisha uandaaji wa Kanuni za Uendelezaji wa Miradi Midogo chini ya MW 10 (The Electricity (Development of Small Power Projects) Rules, 2018, GN No. 77 of 2018). Kanuni hizi zinarahisisha uwekezaji katika miradi hiyo ambapo hupunguza muda na gharama za majadiliano ikilinganishwa na miradi mikubwa. Vilevile, EWURA imekamilisha uandaaji wa Kanuni za Kuhamasisha Matumizi Bora ya Umeme Unaozalishwa na Wateja kwa Kutumia Umeme-jua na Upepo chini ya MW 1 (Electricity (Net Metering) Rules, 2018, GN No. 76 of 2018). Kanuni hizi zinatoa mwongozo kwa wateja wa umeme wanaowekeza katika mitambo ya uzalishaji umeme-jua na upepo katika majengo yao kwa dhumuni la kupunguza matumizi ya umeme kutoka katika gridi.

(i) Nishati inayotokana na Nguvu ya Jua (Solar Energy)
91.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Serikali iliwasilisha miradi mbalimbali ya umeme-jua katika Fungamano la Kimataifa la Nishati ya Jua (International Solar Alliance). Kupitia Fungamano hilo Serikali ya India imetenga jumla ya Dola za Marekani milioni 385 sawa na takriban Shilingi bilioni 888.77 kwa ajili ya kuendeleza miradi ya kuzalisha umeme wa jua katika Mikoa ya Shinyanga, Singida, Dodoma, na Kilimanjaro. Katika mwaka 2018/19, Serikali itakamilisha taratibu za kuridhia makubaliano ya International Solar Alliance na kuanza maandalizi ya utekelezaji wa Mradi ikiwa ni pamoja na kufanya Upembuzi Yakinifu.
92.     Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TANESCO inashirikiana na Serikali ya Morocco kupitia taasisi yake ya nishati endelevu (Moroccan Agency for Sustainable Energy –MASEN) kuendeleza miradi ya kuzalisha umeme-jua nchini yenye jumla ya MW 300. Katika mwaka 2017/18 Wizara ya Nishati, TANESCO na MASEN walifanya tathmini ya awali katika maeneo ya Zuzu (Dodoma), Manyoni (Singida) na Same (Kilimanjaro) ili kufahamu ukubwa wa maeneo na kiasi cha umeme unaoweza kuzalishwa. Katika mwaka 2018/19 kazi zitakazofanyika ni kukamilisha Upembuzi Yakinifu, tathmini ya mazingira na kukamilisha taratibu za upatikanaji wa fedha za kutekeleza Mradi.
93.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Serikali iliendelea kushirikiana na Sekta Binafsi katika kukuza uzalishaji na matumizi ya teknolojia ya nishati ya jua ambapo hadi sasa kupitia mfumo wa umeme-jua katika kaya na taasisi za huduma za jamii (shule, vituo vya afya n.k) yaani Solar Home System, umeme wa MW 16 unazalishwa. Aidha, usambazaji wa umeme kwa kutumia gridi ndogo za umeme katika maeneo ambayo hayajafikiwa na Gridi ya Taifa na maeneo ya visiwani uliongezeka kutoka MW 1 mwaka 2016/17 na kufikia hadi MW 2 kwa mwaka 2017/18.
94.     Mheshimiwa Spika, kufuatia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika utekelezaji wa Mradi wa awali wa majaribio wa Solar PV Generators kutokana na fedha za mkopo nafuu kutoka Benki ya Serikali ya Austria, Serikali itaendelea na Utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi katika maeneo mbalimbali nchini. Kupitia Mradi huu jumla ya wateja 2,015 watanufaika. Kazi zitakazotekelezwa katika Mwaka 2018/19 ni kuainisha vijiji na maeneo mengine ambayo hayapo katika Gridi ya Taifa ikiwemo visiwa pamoja na kuanza ujenzi. Jumla ya Shilingi bilioni 2 fedha za nje zimetengwa Mwaka 2018/19 kwa ajili ya utekelezaji wa kazi hizo.

(ii)          Miradi ya Tungamotaka na Bayogesi
95.       Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea na uhamasishaji wa Sekta Binafsi ili kuongeza uzalishaji wa umeme unaotokana na Tungamotaka. Katika kipindi cha mwaka 2017/18, Uzalishaji wa umeme kutokana na chanzo hicho umefikia MW 42 kutoka MW 38 za mwaka 2016/17. Aidha, uhamasishaji wa matumizi ya bayogesi katika mikoa yote ya Tanzania Bara ulifanyika ambapo mitambo 2,000 ilijengwa. Kwa mwaka 2018/19 miradi hii itatekelezwa kupitia Programu ya Uendelezaji wa Nishati Endelevu kwa wote.

(iii)   Maporomoko Madogo ya Maji
96.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 kiwango cha uzalishaji wa umeme kupitia maporomoko madogo ya maji kilifikia MW 42 kutoka MW 36.99 zilizokuwa zinazalishwa hadi mwaka 2016/17 sawa na ongezeko la asilimia 13.5. Ongezeko hili lilitokana na miradi ya Kiliflora (Arusha), Darakuta (Manyara) na Matembwe (Njombe). Aidha, matumizi ya nishati inayotokana na maporomoko madogo ya maji kwa ajili ya kukuza shughuli nyingine za kiuchumi ikiwemo umwagiliaji yaliongezeka kufutia uhamasishaji wa matumizi ya nishati hiyo.

(iv)    Uendelezaji wa Jotoardhi (Geothermal)
97.     Mheshimiwa Spika, rasilimali ya jotoardhi hapa nchini inakadiriwa kuwa na uwezo wa kuzalisha hadi MW 5,000 za umeme. Serikali kupitia Kampuni ya Uendelezaji wa Rasilimali ya Jotoardhi Nchini (TGDC), imekamilisha tafiti nne (4) za kina (detailed surface studies) za uendelezaji wa rasilimali hiyo katika maeneo ya Ngozi na Kiejo-Mbaka Mkoani Mbeya, Songwe Mkoani Songwe na Luhoi Mkoani Pwani. Ili kuharakisha uendelezaji wa rasilimali ya jotoardhi, Serikali inatarajia kununua mitambo kwa ajili ya uchorongaji wa visima vya utafiti na uvunaji wa jotoardhi. Jumla ya gharama za ununuzi wa mitambo hiyo ni Shilingi bilioni 80.50, kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 66.70 ni gharama za ununuzi wa mtambo mkubwa na Shilingi bilioni 13.80 ni gharama za ununuzi wa mtambo mdogo.
98.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 Serikali itaendelea na utekelezaji wa Mradi wa jotoardhi katika eneo la Ngozi. Kazi zitakazofanyika ni pamoja na: kuajiri Mshauri Mwelekezi wa kuandaa Mpango Kazi na kusimamia uchorongaji wa visima vya utafiti; kufanya tathimini ya ardhi hitajika na kulipa fidia; kuajiri Mkandarasi wa uchorongaji; na ujenzi wa miundombinu ya barabara na maji. Aidha, Serikali itakamilisha Upembuzi Yakinifu katika eneo la Songwe kwa ajili ya uzalishaji wa umeme na matumizi mbadala. Jumla ya Shilingi bilioni 40.20 zimetengwa katika mwaka 2018/19 ili kutekeleza kazi zilizopangwa. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 32.50 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 7. 70 ni fedha za nje.

(v)        Matumizi Bora ya Nishati (Energy Efficiency)
99.           Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Serikali kupitia ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) iliandaa Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi Bora ya Nishati (Energy Efficiency Strategy) pamoja na kukamilisha maandalizi ya Mpango Kazi wa Matumizi Bora ya Nishati (Energy Efficiency Action Plan). Umoja wa Ulaya umetenga Euro milioni 8 sawa na takriban Shilingi bilioni 20.14 kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango Kazi huo. Katika mwaka 2018/19 itachaguliwa Taasisi ya Umma ya Mafunzo ambayo itajengewa uwezo (Centre of Excellence) kwa ajili ya kutoa mafunzo ya uangalizi wa matumizi ya nishati (energy management) na ukaguzi wa upotevu wa nishati (energy audit).  Aidha, wananchi wataelimishwa ili waweze kufahamu umuhimu na njia za kuepuka upotevu wa nishati kwa lengo la kuokoa fedha na kuipunguzia Serikali gharama za uwekezaji katika miundombinu ya umeme. Fedha za nje Shilingi bilioni 1.35 zimetengwa katika mwaka 2018/19 kwa ajili ya utekelezaji wa kazi hizo.

(vi)    Programu ya Nishati Endelevu kwa Wote (Sustainable Energy for All - SE4ALL)
100.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Serikali iliingia makubaliano na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa ajili ya ufadhili wa utekelezaji wa Programu ya miaka mitano (5) ya Nishati Endelevu kwa Wote (SE4All) ambapo UNDP itachangia Dola za Marekani 350,000 sawa na takriban Shilingi milioni 807.97 na kusaidia upatikanaji wa fedha kutoka vyanzo vingine. Katika kuendeleza vyanzo vya nishati jadidifu, Programu ya SE4All ilisaidia upatikanaji wa taarifa za vyanzo vya nishati ya jua na uandaaji wa miradi katika maeneo ya Zuzu (Dodoma); Manyoni (Singida); na Same (Kilimanjaro) ambapo maeneo haya kwa ujumla yana uwezo wa kuzalisha MW 300. Taarifa hizo zitasaidia Serikali kutafuta wawekezaji katika miradi hiyo.
101.      Mheshimiwa Spika,  katika mwaka 2018/19, kazi zitakazotekelezwa kupitia Programu hiyo ni pamoja na: kuendelea na uboreshaji wa miongozo mbambali itakayosaidia upatikanaji wa nishati endelevu nchini; kuandaa Mkakati wa Tungamotaka na utekelezaji wake;  kujenga uwezo kwa watendaji katika kusimamia utekelezaji wa mipango na miradi ya nishati hapa nchini; kuandaa mazingira bora yatakayosaidia kukuza uwekezaji katika miradi ya Nishati Jadidifu na Matumizi Bora ya Nishati; na kuandaa mfumo wa ukusanyaji na utunzaji wa takwimu za Nishati Jadidifu. Jumla ya Shilingi bilioni 3 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi huu katika Mwaka 2018/19, ambapo Shilingi bilioni 2.5 ni fedha za nje na Shilingi milioni 500 ni fedha za ndani.

E.     SEKTA NDOGO YA MAFUTA NA GESI ASILIA
Shughuli za Utafutaji, Uzalishaji na Usambazaji wa Mafuta na Gesi Asilia Nchini
102.    Mheshimiwa Spika, Kazi za utafutaji wa mafuta na gesi asilia zinaendelea ambapo jumla ya kampuni nane (8) zinafanya utafutaji wa mafuta na gesi asilia kupitia mikataba kumi na moja (11) ya Uzalishaji na Ugawanaji Mapato (Production Sharing Agreement -PSA). Katika mwaka 2017/18 Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kushirikiana na Kampuni ya Statoil zimechoronga kisima kimoja (Pilipili-1) katika kitalu Na. 2 kilichopo Bahari ya Hindi na hivyo kufanya jumla ya visima vilivyochorongwa  kufikia 96. Vilevile, TPDC ikishirikiana na Kampuni ya Ndovu Resources ilifanya uhakiki wa mashapo ya gesi asilia katika kitalu cha Ruvuma, uhakiki huo umeongeza kiasi cha gesi asilia kufikia futi za ujazo bilioni 466 kutoka futi za ujazo bilioni 178 mwaka 2016/17. Hadi kufikia sasa kiasi cha gesi asilia kilichogunduliwa nchini ni Futi za Ujazo Trilioni 57.54.
103.      Mheshimiwa Spika, Kampuni za Heritage Rukwa (TZ) Ltd na Swala Oil and Gas Tanzania zimeendelea na maandalizi ya kuchoronga visima vya utafutaji mafuta katika vitalu vya Rukwa Kusini na Kilosa-Kilombero sawia. Aidha, Kampuni ya Ndovu Resources imeendelea na maandalizi ya Mpango wa Uendelezaji (Development Plan) wa gesi asilia iliyogunduliwa katika eneo la Ntorya - Mtwara. Vilevile, Kampuni ya Dodsal Hydrocarbons imeendelea na uchukuaji wa data za mitetemo (seismic) katika Kitalu cha Ruvu ili kuhakiki ukubwa wa mashapo ya gesi asilia iliyogunduliwa katika kitalu hicho. Kwa upande mwingine, Kampuni za PanAfrican Energy na Maurel et Prom zimeendelea na uzalishaji wa gesi asilia katika Vitalu vya Songo Songo na Mnazi Bay kwa wastani wa futi za ujazo milioni 95 na milioni 80 kwa siku sawia. Gesi inayozalishwa inatumika kuzalisha umeme katika mitambo ya TANESCO.


MIRADI YA UTAFITI KATIKA VITALU VYA KIMKAKATI VYA SHIRIKA LA MAENDELEO YA PETROLI NCHINI (TPDC)
(i)       Vitalu Namba 4/1B na 4/1C

104.      Mheshimiwa Spika, TPDC imeendelea na utafiti katika vitalu vyake namba 4/1B na 4/1C sambamba na taratibu za kuwapata Wabia wa Kimkakati (Strategic Partners) ili kushirikiana nao katika kuendeleza vitalu hivyo. Katika mwaka 2017/18 kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kufanya tathmini ya kifedha na kiuchumi na kukamilisha tathmini ya awali kwa kutumia data za mitetemo za 2D ambazo zinaonesha uwepo wa mashapo mazuri ya gesi asilia katika vitalu hivyo. Kazi zitakazotekelezwa kwa mwaka 2018/19 ni ukusanyaji, uchakataji na tathmini ya data za mitetemo ya 3D zenye ukubwa wa kilomita za mraba 2,500. Fedha za ndani Shilingi bilioni 2 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi.

(ii)  Kitalu cha Eyasi – Wembere
105.    Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TPDC imekusanya data za kijiolojia na kijiofizikia kupitia data za mgandamizo (Airbone Gravity Gradiometry-AGG) na sumaku (Magnetic) katika Bonde la Eyasi-Wembere. Lengo la utafiti huu ni kubaini uwepo wa mashapo yenye kuhifadhi mafuta au gesi asilia katika eneo hilo. Katika mwaka 2017/18 wataalam wa Wizara ya Nishati na TPDC wameendelea kufanya mashauriano na wataalam kutoka sekta ya mafuta nchini Uganda. Aidha,  mwezi Oktoba, 2017 wataalamu hao walitembelea eneo la utafiti pamoja na kuandaa mpango kazi wa kufanya tafiti za kina za kijiolojia na kijiofizikia. Kwa mwaka 2018/19, TPDC imepanga: kutafuta Mbia na kuomba leseni ya utafiti; kufanya Tathmini ya Athari za Mazingira (EIA) kwa ajili ya ukusanyaji wa data za mitetemo za 2D; pamoja na kukusanya, kuchakata na kutafsiri data za mitetemo zenye  urefu wa kilomita 150 katika eneo la Manonga. Fedha za ndani Shilingi bilioni 2 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji kwa shughuli za Mradi.

(iii)       Kitalu cha Mnazi Bay Kaskazini
106.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, shughuli zilizotekelezwa katika kitalu hiki ni: kufanya tathmini ya kifedha na kiuchumi; kuomba leseni ya kitalu; kumpata Mshauri Mwelekezi wa kuchakata na kutafsri data za mitetemo za 3D; maandalizi ya kuchukua zaidi data za mitetemo za 3D; kuandaa Mkataba Kifani wa Ushirikiano (Model Joint Operating Agreement) utakaozingatia maboresho ya mikataba inayopitiwa na Serikali ili kuiboresha; na kuanza mchakato wa kumpata Mbia wa Kimkakati wa Mradi. Kwa mwaka 2018/19, shughuli zilizopangwa kufanyika ni pamoja na: kufanya maandalizi ya uchorongaji kwa kushirikiana na Mshauri Mwelekezi; kuanza ununuzi wa vifaa vya awali vitakavyotumika katika kuchoronga kisima; kutafuta mkandarasi wa kukusanya data zaidi za mitetemo za 3D; na kuandaa na kutafsiri data zenye ukubwa wa kilomita za mraba 141.63. Fedha za ndani za Shirika Shilingi bilioni 13.28 zimetengwa kwa ajili ya shughuli hizo.

(iv)    Kitalu cha Songo Songo Magharibi
107.      Mheshimiwa Spika, Kitalu cha Songo Songo Magharibi kimeonesha kuwa na mategemeo chanya ya uwepo wa gesi asilia. Katika kipindi cha mwaka 2017/18, TPDC imekamilisha kutafsiri  data za mitetemo za 2D na kubaini maeneo yatakayochorongwa visima. Vilevile, TPDC imeanza taratibu za kumtafuta Mbia wa Kimkakati ambapo Mkataba Kifani wa Ushirikiano (Model Joint Operating Agreement) umeandaliwa utakaozingatia maboresho ya mikataba inayoendelea kufanyiwa mapitio na Serikali kwa lengo la kuiboresha. Kwa mwaka 2018/19 shughuli zilizopangwa kufanyika ni pamoja na kumpata Mbia wa Kimkakati wa kukusanya, kuchakata na kutafsiri data zaidi za mitetemo za 3D katika eneo la kilomita za mraba 306. Fedha za ndani za Shirika Shilingi bilioni 11.3 zimetengwa kwa ajili ya shughuli hizo.

MIRADI YA USAMBAZAJI WA GESI ASILIA NCHINI

108.    Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TPDC inatekeleza miradi ya usambazaji wa gesi asilia kwa kuunganisha miundombinu ya usambazaji wa gesi hiyo katika matoleo ya bomba linalotoka Madimba Mkoani Mtwara na Songo Songo Mkoani Lindi hadi Dar es Salaam. Uunganishaji wa wateja umeongeza matumizi ya gesi asilia hadi kufikia wastani wa futi za ujazo milioni 175 kwa siku (mwaka 2017/18) kutoka futi za ujazo milioni 145 kwa siku (mwaka 2016/17) sawa na ongezeko la asilimia 17.

(i)      Miradi ya Kusambaza Gesi Asilia Viwandani
109.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, TPDC imeendelea kutafuta wateja zaidi wa gesi asilia kwa matumizi ya viwanda pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kusambazia gesi hiyo kwa wateja. Shirika limepitia na kuhakiki michoro (Design Drawings) ya awali iliyowasilishwa na Mkandarasi kwa ajili ya kuunganisha gesi asilia katika viwanda vya Lodhia Steel, Knauf Gypsum na Bakhressa Food Products vilivyopo Mkuranga.  Mkandarasi wa ujenzi wa bomba la kusambaza gesi asilia katika viwanda vya Coca-Cola Kwanza Limited na BIDCO Industry vilivyoko eneo la viwanda Mikocheni ameanza kazi mwezi Aprili, 2018. Kiwanda cha Goodwill Ceramic Tanzania Limited kilichopo Mkuranga kimeendelea kutumia gesi asilia kwa ajili ya shughuli za uzalishaji kiwandani hapo. Aidha, awamu ya kwanza ya ujenzi wa miundombinu ya kupeleka gesi asilia katika kiwanda cha Dangote Cement Tanzania Limited kilichopo Mtwara ulikamilika mwezi Septemba, 2017. Hivi sasa Kampuni ya Dangote inaendelea na maandalizi ya awali ya utumiaji wa gesi asilia (Testing and Commissioning).
110.      Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2018/19, TPDC itakamilisha majadiliano na kuingia mikataba ya kusambaza gesi asilia katika kiwanda cha Knauf Gypsum kilichopo Mkuranga Mkoani Pwani. Vilevile, TPDC itafanya majadiliano na wateja wapya wa viwanda walioonesha nia ya kuunganishiwa gesi asilia wakiwemo LN Future Building Materials Co. Ltd na Kings Alluminium vilivyopo Mkuranga-Pwani pamoja na MM-1 Intergrated Steel Mills Ltd kilichopo Mikocheni.

(ii)   Miradi ya Kusambaza Gesi Asilia Majumbani
111.      Mheshimiwa Spika, hadi sasa jumla ya nyumba 70 zilizopo maeneo ya Mikocheni, Dar es Salaam zimeunganishwa na miundombinu ya gesi asilia. Katika mwaka 2017/18, miundombinu ya kuunganisha gesi asilia majumbani imeanza kutandazwa katika Jiji la Dar es Salaam. Maeneo yanayoanza kupelekewa gesi kupitia Mradi huu ulioanza mwezi Aprili, 2018 ni pamoja na Ubungo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Makongo Juu, Survey, Sinza, Shekilango, Mwenge, Viwanda vya Coca Cola na maeneo ya Mikocheni. Mradi huu ni endelevu kutegemeana na mahitaji yatakavyokuwa yanajitokeza katika maeneo husika. Zaidi ya wateja 1,000 wanatarajiwa kufikiwa na miundombinu ya kuunganishia gesi katika awamu ya kwanza.
112.      Mheshimiwa Spika, Mradi mwingine unaofanyiwa maandalizi utakaotekelezwa pamoja na Mradi huu ni usambazaji wa gesi asilia katika maeneo ya Magereza, Magomeni, Hospitali Kuu ya Mkoa na Chuo cha Ualimu katika Manispaa ya Mtwara. Kazi inayofanyika sasa hivi ni ukamilishaji wa taratibu za kuunganisha bomba lenye msukumo mdogo (low pressure) kwa ajili ya kupeleka gesi asilia katika nyumba. Kazi hizi zitakamilika mwezi Juni, 2018 na kazi ya usambazaji wa gesi asilia itaanza mwanzoni mwa mwezi Julai, 2018 ambapo wateja wa awali wanatarajiwa kuwa zaidi ya 580. Kazi hii itakuwa endelevu ambapo maeneo mengine yataendelea kusambaziwa gesi asilia baadae ikiwemo vijiji vinavyopitiwa na bomba la gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
113.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, TPDC inatarajia kuweka miundombinu itakayowezesha zaidi ya nyumba 2,000 kuunganishiwa gesi asilia pamoja na kusambaza gesi asilia katika Mgahawa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Soko la Feri la Jijini Dar es Salaam na Kampuni ya Usimamizi wa Mabasi ya Mwendokasi Jijini Dar es Salaam (UDART). Ili kuwezesha uunganishwaji wa wateja hao, uchambuzi wa kifedha pamoja na Tathmini ya Athari za Mazingira na Jamii (Environmental and Social Impact Assessment-ESIA) utaendelea kufanyika. Fedha za ndani za TPDC Shilingi bilioni 20.9 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi huu.

Ujenzi wa Miundombinu ya Usambazaji Gesi Asilia katika Mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Pwani, Morogoro, Tanga na Dodoma
114.      Mheshimiwa Spika, Mradi huu unajumuisha usambazaji wa gesi asilia kwa njia ya bomba (Piped Natural Gas-PNG), ujenzi wa vituo vya gesi asilia iliyoshindiliwa (Compressed Natural Gas (CNG) stations) na miradi midogo ya gesi kimiminika (Mini-LNG). Katika mwaka 2017/18, TPDC imeandaa Mkataba wa Ushirikiano wa Ubia (Joint Venture Agreement) pamoja na Hati ya Zabuni (Tender Document) ili kuwapata wawekezaji kwa njia ya ushindani. Aidha, Mpango wa utekelezaji wa Mradi huu upo katika hatua za mwisho za mapitio kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) pamoja na kitengo cha PPP cha Wizara ya Fedha na Mipango. Awamu ya kwanza ya utekelezaji, inahusisha utafutaji wa Mbia atakayeshirikiana na TPDC kutekeleza Mradi kwa Mkoa wa Dar es Salaam. Mikoa mingine ya Lindi, Mtwara, Morogoro, Tanga na Dodoma iliyoainishwa katika Mpango itafuata baada ya kukamilika kwa Upembuzi Yakinifu. Katika mwaka 2018/19, fedha za ndani Shilingi bilioni 2 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi. Mradi unatarajiwa kuanza mwezi Novemba, 2018 baada ya taratibu zote kukamilika na utatekelezwa kwa muda wa miaka mitano (5).

Mradi wa Ujenzi wa Kiwanda cha Mbolea Mkoani Lindi
115.    Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TPDC imeendelea na majadiliano kuhusu Mradi wa kujenga kiwanda kikubwa cha Mbolea katika eneo la Kilwa Masoko, Mkoani Lindi ambacho kitazalisha mbolea ya Amonia tani 2,200 na Urea tani 3,850 kwa siku. Mradi utatekelezwa na Kampuni ya Ubia ya Mradi Tanzania Mbolea and Petrochemicals Company Limited (TAMPCO) (inayohusisha kampuni za Ferostaal ya Ujerumani, Fauji ya Pakistani, Haldo Topsoe ya Denmark na TPDC), ambayo imeundwa na kupata hati ya uwekezaji (Certificate of Incentive). Mradi huu pamoja na mambo mengine utasaidia upatikanaji wa mbolea kwa urahisi ili kukuza Sekta ya Kilimo na uchumi wa nchi kwa ujumla. Mradi unakadiriwa kugharimu Dola za Marekani bilioni 1.92 sawa na takriban Shilingi trilioni 4.43 katika utekelezaji wake.
116.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 Serikali itaendelea na majadiliano ya bei ya gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya uzalishaji wa mbolea nchini. Serikali kupitia TPDC itasimamia tathmini ya utwaaji ardhi na usanifu wa kihandisi wa upelekaji wa gesi asilia kwa njia ya bomba kuanzia Nangurukuru hadi Kiwandani. Kazi hizi zitatekelezwa kwa kutumia fedha za ndani za Shirika ambapo kiasi cha Shilingi milioni 266.4 kitatumika.

Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (LNG Project)
117.    Mheshimiwa Spika, Mradi wa LNG unalenga kusindika gesi asilia iliyogunduliwa katika kina kirefu cha Bahari ili iweze kutumika ndani na kusafirishwa na kuuzwa nje ya nchi. Jumla ya gharama za Mradi zinakadiriwa kuwa Dola za Marekani bilioni 30 sawa na takriban Shilingi trilioni 69.25. Katika mwaka 2017/18 kazi zilizofanyika ni pamoja na marudio na ukamilishaji wa uthamini ya eneo la mradi, kukamilisha tafiti za kihandisi na uchaguzi wa teknolojia (concept selection) ya uzalishaji na usafirishaji wa gesi asilia kutoka baharini hadi nchi kavu na kuendelea kwa majadiliano ya kimkataba (Host Government Agreement - HGA) kati ya Serikali na wawekezaji. Katika mwaka 2018/19, kazi zinazotekelezwa ni pamoja na: kufanya Usanifu wa Awali wa Kihandisi (Pre-FEED) kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha LNG; kuendelea na majadiliano ya HGA na ulipaji wa fidia kwa wananchi watakaopisha Mradi.
118.    Mheshimiwa Spika, faida zinazotarajiwa kutokana na Mradi huo ni pamoja na kuongezeka kwa mapato ya Serikali kupitia mauzo ya gesi asilia katika soko la kimataifa, upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa ajili ya matumizi ya ndani, upatikanaji wa ajira kwa wazawa, ukuaji wa Miji ya Lindi na Mtwara ikiwa ni pamoja na upanuzi wa bandari na uwanja wa ndege, upatikanaji wa malighafi za viwanda kama vile mbolea, plastiki na kemikali (Petrochemicals). Fedha za ndani Shilingi bilioni 6.5 zimetengwa kwa mwaka 2018/19 kwa ajili ya kazi hizo na ujenzi wa Mradi unatarajiwa kuanza mara baada ya kukamilika kwa majadiliano ya HGA.

Mradi wa Kusafirisha Gesi Asilia kutoka Tanzania kwenda Uganda 
119.         Mheshimiwa Spika, Mradi unahusu ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Dar es Salaam (Tanzania) kwenda nchini Uganda kupitia Mikoa ya Pwani, Tanga, Manyara, Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Geita na Kagera. Utekelezaji wa Mradi huu utasaidia upatikanaji wa gesi asilia katika mikoa itakayopitiwa na bomba hilo na mikoa mingine ya jirani. Katika mwaka 2018/19 fedha za ndani Shilingi bilioni 1.5 zimetengwa kwa ajili ya Upembuzi Yakinifu utakaobainisha gharama za Mradi na namna bora ya utekelezaji wake. Kulingana Mpango Kabambe wa Matumizi ya Gesi Asilia (NGUMP) kiasi cha futi za ujazo trilioni 3.2 kinakadiriwa kusafirishwa kwa njia ya bomba kwenda nchi za jirani ikiwemo Uganda.  Serikali za Tanzania na Uganda zinaendelea na majadiliano ili utekelezaji wa mradi huu uende sambamba na ule wa EACOP.

MIRADI YA USAFIRISHAJI WA MAFUTA
Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Kabaale (Uganda) hadi Bandari ya Tanga (Tanzania)
120.    Mheshimiwa Spika, Ujenzi wa Mradi huu utatekelezwa na Kampuni Maalum ya Mradi (Special Purpose Vehicle) itakayoundwa na wabia wa Mradi ambao ni Kampuni za Total (Ufaransa), Tullow (Uingereza), CNOOC (China) pamoja na Serikali za Tanzania na Uganda. Gharama za Mradi zinakadiriwa kufikia Dola za Marekani bilioni 3.5 sawa na takriban Shilingi trilioni 8.07.
121.    Mheshimiwa Spika, Hatua za awali za utekelezaji wa Mradi huu zilianza mwezi Januari, 2018. Kazi zilizotekelezwa ni pamoja na: Usanifu wa Kihandisi wa Mradi (Front End Engineering Design); kuridhiwa kwa Mkataba wa Intergovernmental Agreement (IGA) na Mabunge ya nchi za Tanzania na Uganda; kulipa fidia ya utwaaji ardhi kwa eneo la Chongoleani, tathmini ya fidia kwa maeneo ya kambi za wafanyakazi na hifadhi ya mabomba; utafiti wa Geological, Geotechnical na Geophysical katika eneo la Chongoleani; na utafiti wa Geological na Geophysical kwenye njia ya bomba. Katika kipindi hiki majadiliano ya HGA pamoja na maandalizi ya majadiliano ya mkataba wa Ubia (Shareholding Agreement - SHA) yameendelea kufanyika. Kazi zilizopangwa kutekelezwa kwa mwaka 2018/19 ni pamoja na: kukamilisha majadiliano ya HGA na SHA; kukamilisha Usanifu wa Kina wa Kihandisi (Detailed Engineering Design); na kuwalipa fidia wananchi watakaopisha utekelezaji wa Mradi. Kiasi cha Shilingi bilioni 54.2 fedha za ndani zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji. Ujenzi wa Mradi unatarajiwa kuanza mwezi Juni, 2018 na  kukamilika mwaka 2020.

Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Safi (White Petroleum Products) kutoka Dar es Salaam (Tanzania) hadi Ndola (Zambia)
122.    Mheshimiwa Spika, Mradi huu upo katika hatua za awali na unahusu ujenzi wa bomba lenye urefu wa kilomita 1,710 litakalojengwa sambasamba na bomba la TAZAMA linalosafirisha Mafuta Ghafi (Crude Oil) baada ya kuridhiwa na Serikali za nchi za Tanzania na Zambia. Ili kuleta manufaa katika maeneo yatakayopitiwa na bomba hili, Mradi utahusisha ujenzi wa matoleo ya mafuta (take–off points) katika maeneo ya Morogoro, Iringa, Njombe, Mbeya na Songwe. Katika mwaka 2017/18, Andiko la Awali la Mradi (Project Concept Paper) kuhusu namna Mradi utakavyotekelezwa na faida zake liliandaliwa. Aidha, eneo kwa ajili ya ujenzi wa matenki ya hifadhi ya mafuta Morogoro limepatikana na hatua za utwaaji ardhi zinaendelea. Katika mwaka 2018/19, shughuli iliyopangwa kutekelezwa ni kufanya Upembuzi Yakinifu (Feasibility Study) utakaoonesha gharama halisi za Mradi na namna bora ya kutekeleza Mradi. Jumla ya Shilingi bilioni 1.5 fedha za ndani zimetengwa kwa ajili ya kugharamia shughuli hizo.

Mradi wa Hifadhi ya Kimkakati ya Mafuta ya Akiba ya Dharura Nchini

123.    Mheshimiwa Spika, uanzishaji na usimamizi wa Hifadhi ya Kimkakati ya Mafuta ya Akiba ya Dharura (Strategic Petroleum Reserve - SPR) ni muhimu kwa nchi ili kujilinda na mabadiliko hasi ya upatikanaji wa mafuta Duniani yanayoweza kutokea. Katika utekelezaji wa Mradi huu, miongozo mbalimbali ikiwemo kanuni (SPR regulations), mwongozo wa usimamizi (SPR manual) na mfumo wa bei (price template) imekamilika. Katika mwaka 2017/18, kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kumpata Mshauri Mwelekezi na Mkandarasi wa kuondoa mabaki ya mafuta (sludge) katika Tenki Na.8 la TPDC lililopo TIPER litakalotumika kutunzia mafuta ya dharura. TPDC imeendelea na taratibu za kupata ardhi kwa ajili ya ujenzi wa matenki mengine ya kuhifadhia mafuta katika Manispaa za Kigamboni na Tanga. Kazi zilizopangwa kutekelezwa kwa mwaka 2018/19 ni kukarabati Tenki Na. 8 ili kufanikisha uanzishwaji wa hifadhi hiyo nchini. Shilingi bilioni 14.5 fedha za ndani zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa shuguli za Mradi.

Mradi wa Usimamizi wa Rasilimali za Mafuta na Gesi Asilia Nchini

124.    Mheshimiwa Spika, Mradi huu unalenga kuchochea maendeleo ya tasnia ya uziduaji (extractive industry) katika sekta ya mafuta na gesi asilia nchini na kuimarisha uendelezaji wa rasilimali hizo zinazotoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi. Mradi huu utaiwezesha Serikali kuimarisha uwezo wa kukusanya na kusimamia mapato yanayotokana na rasilimali za mafuta na gesi asilia hususan katika maeneo ya utafutaji, uzalishaji na uendelezaji wa rasilimali hizo. Mradi unatarajiwa kugharimu Dola za Marekani milioni 29.53 sawa na takriban Shilingi bilioni 68.17. Katika Mradi huu Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) itachangia Dola za Marekani milioni 26.58 sawa na takriban Shilingi bilioni 61.35 zikiwa ni mkopo wa masharti nafuu na Serikali itachangia Dola za Marekani milioni 2.95 sawa na takriban Shilingi bilioni 6.8.
125.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Taasisi za Serikali zinazohusika na Mradi huu zitajengewa uwezo katika maeneo ya usimamizi wa rasilimali za mafuta na gesi asilia. Jumla ya Shilingi bilioni 14 zimetengwa ambapo Shilingi bilioni 2 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 12 ni fedha za nje. Mradi unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu (3) kuanzia mwezi Juni, 2018.

Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu wa Mafuta na Gesi Asilia Nchini

126.      Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2017/18, Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (Petroleum Upstream Regulatory Authority -PURA)  imeendelea kusimamia shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa gesi asilia katika kampuni nane (8) kupitia PSA 11 zinazofanya shughuli hizo nchini. Katika kutekeleza jukumu hilo kazi zilizotekelezwa ni: kusimamia na kudhibiti uchorongaji wa kisima cha Pilipili-1 katika kitalu Na. 2 unaotekelezwa na Kampuni ya Statoil ikishirikiana na TPDC; kufanya uhakiki na kuidhinisha Mpango Mkakati na Bajeti kwa PSA 10; na kuanza ukaguzi wa hesabu za PSA ambapo ukaguzi wa PSA ya kitalu Na.2 umekamilika.
127.      Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2018/19, Serikali kupitia PURA itasimamia shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia zikiwemo uchorongaji wa kisima cha Hammerkop-1 katika kitalu cha Rukwa kusini na kisima cha Kito-1 katika kitalu cha Kilosa-Kilombero. Mamlaka itasimamia ukusanyaji, uchakataji na tathmini ya data za mitetemo za 2D yenye jumla ya urefu wa kilomita za mstari 840 zitakazokusanywa katika vitalu vya Ruvuma na Eyasi-Wembere. PURA itatathmini pia data za mitetemo za 3D zenye jumla ya kilometa za mraba 1,357.63 katika vitalu vya Kiliwani Kaskazini, Ruvuma, Songo Songo Magharibi, Mnazi Bay Kaskazini na 4/1B. PURA itaendelea kusimamia uzalishaji wa gesi asilia katika Vitalu vya Songo Songo na Mnazi Bay na kufanya ukaguzi wa hesabu za PSA 10.  Fedha za ndani Shilingi bilioni 1.69 zimetengwa kwa ajili ya kugharamia kazi hizo.

Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (Petroleum Bulk Procurement System) Nchini

128.    Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (Petroleum Bulk Procurement Agency- PBPA) imeendelea kusimamia Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (Bulk Procurement System – BPS). Kwa kipindi cha Mwezi Januari hadi Desemba, 2017 jumla ya lita bilioni 5.36 za mafuta ziliingizwa nchini. Lita bilioni 3.19 sawa na asilimia 60 za mafuta yaliyoingizwa zilikuwa kwa ajili ya matumizi ya ndani na lita bilioni 2.17 sawa na asilimia 40 zilikuwa kwa ajili ya nchi jirani. Mafuta kwa ajili ya matumizi ya ndani yalipungua kwa asilimia 3.3 kutoka lita bilioni 3.302  mwaka 2016 hadi lita bilioni 3.19 mwaka 2017. Kupungua huko kulitokana na mitambo ya kuzalisha umeme pamoja na baadhi ya viwanda kutumia gesi asilia kuzalisha nishati badala ya mafuta ya Dizeli na Mafuta mazito (HFO). Mafuta yaliyoagizwa kwa ajili ya nchi jirani za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rwanda, Uganda na Zambia yalipungua kwa asilimia 0.8 kutoka lita bilioni 2.185 mwaka 2016 hadi lita bilioni 2.168 mwaka 2017. Upungufu huo ulitokana na baadhi ya kampuni za mafuta kubadili matumizi ya mafuta yaliyoagizwa kwa ajili ya nchi jirani na kutumika hapa nchini (localization of transit fuel) Kielelezo Na 10.
129.    Mheshimiwa Spika, katika kupunguza upotevu wa mafuta na gharama zinazotokana na muda unaotumika kwa meli kupakua mafuta bandarini (Demurrage Charges), Serikali inatarajia kuanza upokeaji mafuta sehemu moja (Single Receiving Terminal - SRT). Katika kipindi cha mpito utaratibu wa SRT utaanza kwa kutumia miundombinu ya kuhifadhia mafuta ya TIPER ambayo Serikali inamiliki hisa asilimia 50 hadi hapo Serikali itakapojenga miundombinu yake. Utaratibu wa SRT utakuwa chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA). Katika kufanikisha utaratibu huo, kazi zinazotekelezwa kwa sasa ni pamoja na: uboreshaji wa Kanuni za Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja za Mwaka 2017; uandaaji wa Kanuni za Usimamizi wa SRT; uundaji wa Timu itakayofanya ufuatiliaji na tathmini ya utaratibu wa SRT; na uandaaji wa mikataba itakayotumika katika kutekeleza utaratibu wa SRT.

Matumizi ya Bandari za Tanga na Mtwara katika Upakuaji wa Mafuta

130.      Mheshimiwa Spika, kutokana na mafanikio yaliyopatikana kwa kuanza kutumia Bandari ya Tanga kupokea mafuta kwa ajili ya matumizi ya Mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara, Serikali itaanza kutumia Bandari ya Mtwara kupokea mafuta kwa ajili ya matumizi ya Mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi pamoja na nchi za jirani. Bandari ya Mtwara itaanza rasmi kupokea mafuta kwa kutumika mfumo wa uagizaji kwa pamoja mwezi Juni, 2018. Utaratibu wa kupanga bei ya mafuta yatakayoingizwa kupitia Bandari hiyo utazingatia taratibu zilizotumika katika Bandari ya Tanga. Miundombinu ya kuhifadhia mafuta iliyopo katika Bandari hiyo ina uwezo wa kutunza lita milioni 26 zinazotosheleza mahitaji ya ukanda huo kwa sasa. Hata hivyo, kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo, Serikali inawakaribisha wawekezaji kuwekeza zaidi katika ujenzi wa miundombinu ya kuhifadhia mafuta katika Bandari za Tanga na Mtwara.

Matumizi ya Gesi inayotokana na Petroli (Liquified Petroleum Gas – LPG)

131.    Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kukamilisha utaratibu wa uagizaji wa  LPG  kwa  mfumo  wa   pamoja   ambapo kwa mwaka 2017/18 Mshauri Mwelekezi anakamilisha  utafiti kuhusu viwango vya ubora wa LPG unaohitajika kwa ajili ya matumizi nchini na ujenzi wa miundombinu ya kupokelea na kuhifadhia gesi hiyo. Kwa mwaka 2018/19 EWURA itaandaa mwongozo wa uagizaji wa LPG kwa mfumo wa pamoja baada ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kupitia na kuidhinisha viwango vitakavyopendekezwa na Mshauri Mwelekezi. Aidha, Serikali imeendelea kutoa elimu kuhusu matumizi bora ya LPG katika maeneo mbalimbali nchini ili kulinda afya, usalama na mazingira ya watumiaji. Vilevile, Serikali kupitia EWURA imeendelea kusimamia biashara ya LPG ili kubaini wafanyabiashara wasio waaminifu na kuwachukulia hatua stahiki. Kwa mwaka 2017 kumekuwa na ongezeko la uagizaji wa LPG ikilinganishwa na mwaka 2016 ambapo kuanzia mwezi Januari hadi Desemba 2017, gesi iliyoagizwa nchini ilikuwa tani 107,263  ikilinganishwa na tani 90,296 za mwaka 2016, sawa na ongezeko la asilimia 19.

F.        UIMARISHAJI WA MAWASILIANO KATI YA WIZARA NA JAMII

132.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Wizara ya Nishati na Taasisi zake imeendelea kuelimisha umma kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Sekta ya Nishati ili kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu shughuli zinazotekelezwa na Wizara. Njia mbalimbali zimetumika kutoa elimu hiyo zikiwemo magari ya matangazo, redio, magazeti, televisheni, tovuti na mitandao ya kijamii. Aidha, elimu imeendelea kutolewa kupitia Jarida la kila wiki la Wizara (MEM News Bulletin) ambapo hadi kufikia mwezi Aprili, 2018 jumla ya Matoleo 42 yamechapishwa na kusambazwa kwa wadau mbalimbali zikiwemo Ofisi za Balozi za Tanzania. Taarifa zaidi kuhusu Wizara zinapatikana kupitia Tovuti (www.nishati.go.tz), ukurasa wa Facebook (Wizara ya Nishati), Twiter (Wizara ya Nishati); na You Tube (Wizara ya Nishati Tanzania).
133.      Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2017/18 Wizara imeshiriki katika vipindi mbalimbali vya Redio na Televisheni kwa lengo la kuwaelimisha wananchi kuhusu mipango inayotekelezwa na Serikali mathalan kipindi maalum cha ‘TUNATEKELEZA’ kinachoratibiwa na Idara ya Habari (MAELEZO) kwa kushirikiana na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

G.     AJIRA NA MAENDELEO YA RASILIMALIWATU

134.    Mheshimiwa Spika, katika kuongeza tija na motisha kwa watumishi wa Wizara, kwa mwaka 2017/18 Wizara iliwapandisha madaraja jumla ya watumishi 10 katika kada mbalimbali. Katika kipindi cha mwaka 2018/19 Wizara inatarajia kuwapandisha madaraja watumishi 100 ambao wamepata sifa za kitaaluma na wenye utendaji mzuri wa kazi. Aidha, Wizara pamoja na Taasisi zake inatarajia kuajiri jumla ya watumishi 207 katika kada mbalimbali. Kati ya watumishi hao, 43 wataajiriwa na Wizara, 116 TPDC na 48 PURA.
135.    Mheshimiwa Spika, ili kuhahakikisha kuwa Nchi inakuwa na wataalamu wa Kitanzania wa kutosha katika Sekta ya Nishati, Wizara imeendelea kushirikiana na Washirika wa Maendeleo kutoa ufadhili wa masomo kwa Watanzania wanaokidhi vigezo kwenda kusoma nchi mbalimbali kwa ngazi za Shahada, Uzamili na Uzamivu. Kwa mwaka 2017/18 watanzania 22 walipata ufadhili wa masomo kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China katika masuala ya mafuta na gesi asilia. Aidha, kupitia Programu za Uendelezaji wa Rasilimaliwatu (Capacity Building), Development in Oil and Gas Industry na Energy Sector Capacity Building Program watumishi 16 walipata ufadhili katika fani mbalimbali zikiwemo: usimamizi katika masuala ya  mafuta na gesi asilia, sheria na uhasibu na fedha. Kwa mwaka 2018/19, watanzania 22 watapatiwa ufadhili wa masomo kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.
136.      Mheshimiwa Spika, katika kujali afya za watumishi, Wizara imeendelea kutekeleza Waraka wa Utumishi wa Umma Na. 2 wa Mwaka 2006 kwa kuwahudumia watumishi wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (VVU) na wenye UKIMWI waliojitokeza kwa kuwapatia lishe na dawa maalum.  Aidha, Wizara itaendelea kutoa elimu mahali pa kazi ili kuzuia maambukizi mapya na kuwahudumia waathirika wa UKIMWI kadri watakavyojitokeza. Sambamba na jitihada hizo, Wizara pia itaendelea kuhamasisha watumishi kupima afya hususan kwenye Magonjwa Sugu Yasiyo ambukiza (MSY) ikiwemo shinikizo la damu, kisukari na saratani. Aidha, Wizara imeanzisha utaratibu wa kuwahamasisha Watumishi kufanya mazoezi baada ya saa za kazi ili kuimarisha afya zao na kuwawezesha kufanya kazi kwa ufanisi.
137.    Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutekeleza agizo la Serikali la kuhamishia shughuli zake Makao Makuu Dodoma ambapo hadi sasa watumishi 50 kati ya 153 wamehamia Dodoma. Wizara inaendelea kukamilisha taratibu husika ili watumishi wote waweze kuhamia Dodoma katika kipindi cha mwaka huu wa fedha.

H.USHIRIKIANO WA KIMATAIFA

138.         Mheshimiwa Spika, Wizara ya Nishati imekuwa ikishirikiana na Washirika wa Maendeleo katika utekelezaji wa Programu, Mikakati na Miradi mbalimbali ya maendeleo. Kwa niaba ya Serikali, napenda kutambua mchango wa: Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Benki ya Dunia (WB), Benki ya Exim ya China, Benki ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Japan (JBIC), Benki ya Unicredit Austria, Economic Development Cooperation Fund (EDCF- Korea), Mfuko wa Uendelezaji Jotoardhi (Geothermal Risk Mitigation Facility - GRMF), pamoja na Taasisi na Mashirika ya: JICA (Japan), KfW (Germany), AFD (Ufaransa), OfD (Norway), DFID (Uingereza) Sida (Sweden), Umoja wa Ulaya (EU), Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), na  USAID  (Marekani). Vilevile, natoa shukrani kwa Serikali za China, Sweden, Ufaransa, Finland, Ujerumani, Iceland, Norway, Korea ya Kusini, Uganda na Ethiopia. Kwa kipindi cha mwaka 2018/19 Serikali kupitia Wizara ya Nishati itaendelea kushirikiana na Washirika hawa pamoja na wengine katika uendelezaji wa Sekta hii muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa Nchi yetu.  

I.     SHUKRANI

139.      Mheshimiwa   Spika,   kipekee namshukuru kwa dhati Mhe. Subira Khamis Mgalu, Mbunge wa Viti Maalum, na Naibu Waziri wa Nishati kwa namna anavyonisaidia katika kusimamia Sekta ya Nishati. Hakika tangu ameteuliwa kuwa Naibu Waziri amekuwa na mchango mkubwa katika kusimamia Sekta hii ambayo ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi na ujenzi wa viwanda nchini.
140.    Mheshimiwa Spika, usimamizi bora wa Sekta ya Nishati nchini unategemea ushirikiano unaotolewa na watendaji mbalimbali wa Wizara. Hivyo, naomba nitumie nafasi hii kumshukuru Katibu Mkuu wa Wizara Dkt. Hamisi Hassan Mwinyimvua, Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na Watumishi wote wa Wizara kwa ushirikiano wanaonipatia kuniwezesha kuzisimamia shughuli mbalimbali zilizo ndani ya Sekta ya Nishati. Ni matumaini yangu kuwa ushirikiano huu utazidi kuimarika.
141.      Mheshimiwa  Spika,  naomba nitumie nafasi hii kuwashukuru  Wenyeviti na Wajumbe wa Bodi, Wakuu wa Taasisi na Watumishi  wote wa  Taasisi  zinazosimamiwa na Wizara kwa ushirikiano wanaonipatia. Ni wazi kuwa ushirikiano huo umekua chachu katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu yangu.
142.      Mheshimiwa Spika, mwisho lakini siyo kwa umuhimu, nawapongeza wananchi wa Jimbo la Chato kwa uvumilivu wao hasa wanaponikosa Jimboni nikiwa natekeleza shughuli hizi muhimu. Naipongeza sana familia yangu ikiongozwa na mpendwa wangu mama Kalemani kwa ustahimilivu wao hasa ninapokuwa mbali nao kifamilia nikiwa katika majukumu haya ya kitaifa, nawaomba waendelee kuwa wavumilivu kwa kuwa kazi hizi ni muhimu kifamilia na kitaifa.

J.      HITIMISHO

143.      Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19 pamoja na matumizi mengine imeelekezwa katika kutekeleza Miradi Mikubwa ya Nishati ya Kielelezo ambayo itakapokamilika itasaidia upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini.
144.      Mheshimiwa Spika, naomba Bunge lako Tukufu sasa likubali kupitisha Makadirio ya Jumla ya Shilingi 1,692,286,014,000 kwa ajili ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake. Mchanganuo wa fedha hizo ni kama ifuatavyo:
                           (i)     Shilingi 1,665,141,000,000 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi 1,489,741,000,000 ni fedha za ndani na Shilingi 175,400,000,000 ni fedha za nje; na

                        (ii)     Shilingi 27,145,014,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida. Kati ya fedha hizo Shilingi 15,025,821,000 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (OC). Shilingi 12,119,193,000 ni kwa ajili ya Mishahara (P.E) ya watumishi wa Wizara na Taasisi zilizo chini yake.
145.    Mheshimiwa Spika, naomba tena nitoe shukrani zangu za dhati kwako na kwa Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza. Hotuba hii pia inapatikana katika Tovuti ya Wizara kwa anuani ya www.nishati.go.tz. Vilevile, Hotuba hii ina vielelezo mbalimbali kwa ajili ya ufafanuzi wa masuala muhimu yanayohusu Sekta ya Nishati.
146.    Mheshimiwa   Spika,  naomba kutoa hoja.

Comments