Featured Post

BAJETI YA MADINI 2018/2019 NI SHILINGI BILIONI 58


HOTUBA YA WAZIRI WA MADINI, MHESHIMIWA ANGELLAH JASMINE MBELWA KAIRUKI (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA WA FEDHA WA 2018/19



1.0 UTANGULIZI


1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba, kufuatia Taarifa iliyowasilishwa leo Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Bunge lako Tukufu sasa likubali kupokea, kujadili, na kupitisha Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu, Mpango na Bajeti ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18. Aidha, ninaomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19.

2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi  Mungu,  mwingi  wa  rehema,  kwa  kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana tena. Aidha, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu Hotuba ya Bajeti ya Wizara yangu kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19.

3. Mheshimiwa Spika, vilevile, ninakushukuru kwa kunipa fursa hii adhimu ya kuwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu kwa mara ya kwanza Bajeti ya  Wizara  ya  Madini.  Kama  unavyofahamu  Wizara


hii iliundwa mwezi Oktoba, 2017 baada ya kuvunjwa kwa iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini, na hivyo kufanya bajeti hii kuwa ndiyo ya kwanza ya Wizara mpya ya Madini. Wizara ya Madini inategemea sana mawazo, ushauri na maelekezo ya Bunge lako Tukufu ili kuimarisha na kukuza Wizara hii mpya.

4. Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniteua kuwa Waziri wa Madini; Wizara ambayo ni muhimu kwa uchumi wa Nchi yetu pamoja na Manaibu wangu, Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo (Mb.), na Mheshimiwa Doto Mashaka Biteko (Mb.). Tunamuahidi tutatekeleza maelekezo anayoyatoa kwa ufanisi na uadilifu na tutatekeleza  majukumu  yetu  vyema  na  tutatumia ujuzi na maarifa yote tuliyopewa na Mwenyezi Mungu na tuliyojifunza kusimamia Sekta hii ipasavyo ili Taifa letu linufaike na rasilimali za madini.

5. Mheshimiwa Spika, napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa uongozi wake makini katika usimamizi wa rasilimali za nchi. Sote ni mashahidi wa jinsi uongozi wake unavyogusa wananchi wa Tanzania hususan katika matumizi sahihi ya rasilimali za Taifa katika kuwaletea maendeleo.

6. Mheshimiwa Spika, pia ninawashukuru Makamu wa  Rais,  Mheshimiwa  Samia  Suluhu  Hassan  na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) kwa miongozo wanayonipatia katika kutekeleza majukumu yangu kikamilifu.


7. Mheshimiwa  Spika,  katika  suala  hili  la usimamizi wa rasilimali za nchi na hususan katika Sekta ya Madini ninayoisimamia, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais na wewe binafsi kwa kuunda Kamati ambazo zilishughulikia changamoto zilizopo katika Sekta ya Madini. Mapendekezo ya Kamati zote yamefanyiwa kazi na baadhi ya mapendekezo mengine yanaendelea kutekelezwa. Nawahakikishia kuwa, Wizara yangu itatekeleza mapendekezo yote kama yalivyotolewa na Kamati hizo.

8. Mheshimiwa Spika, vilevile, nikupongeze wewe binafsi, Mheshimiwa Job Yustino Ndugai (Mb.), Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson (Mb.), na Wenyeviti wa Bunge kwa kuendesha Bunge kwa weledi mkubwa, hekima, busara na kwa umahiri.

9. Mheshimiwa Spika, ninachukua fursa hii pia kuwashukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula (Mb.), Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Mariam Ditopile Mzuzuri (Mb.) na Wajumbe wote wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, kwa  michango  yao  mahsusi  wakati  wa  uchambuzi wa Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18 na Mpango na Makadirio ya Bajeti ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19. Kamati imetoa maoni mbalimbali na ushauri mzuri unaoboresha utekelezaji wa majukumu yetu na kuhakikisha Sekta ya Madini inanufaisha Taifa. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa Wizara ya Madini itafanya kazi  kwa karibu na Kamati hii kwa manufaa na maslahi ya Taifa.


10. Mheshimiwa  Spika,  sina  budi  kuwashukuru kwa dhati Viongozi wenzangu wa Wizara ya Madini Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo (Mb.), Naibu Waziri, Mheshimiwa Doto Mashaka Biteko (Mb.), Naibu Waziri na Profesa Simon Samwel Msanjila, Katibu Mkuu. Viongozi hawa na Watendaji wote wa Wizara  wananipa ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yangu na kutekeleza majukumu yao kwa kujituma, tija na ufanisi. Naahidi Bunge lako kuwa  kwa ari na kasi tuliyonayo tutahakikisha rasilimali za madini zinanufaisha Taifa na mchango wa Sekta ya Madini unaongezeka katika Pato la Taifa, maendeleo ya jamii na kupunguza umaskini nchini.

11.   Mheshimiwa Spika,  napenda kutoa pole  kwa Bunge lako Tukufu, familia, ndugu, jamaa na wananchi wa jimbo la Songea Mjini kwa kuondokewa na mpendwa wao,  Mheshimiwa  Leonidas  Tutubert  Gama  (Mb.), na Jimbo la Buyungu, Kigoma kwa kuondokewa na mpendwa wao Mhe. Kasuku Samson Bilago (Mb). Aidha, naomba kuungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuwapongeza Mheshimiwa Janet Masaburi kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Mbunge, Mheshimiwa Dkt. Godwin Ole Mollel, Mbunge wa Jimbo la Siha, Mheshimiwa Stephen Lemomo Kiruswa, Mbunge wa Jimbo la Longido, Mheshimiwa Dkt. Damas Daniel Ndumbaro, Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Mheshimiwa Justin Joseph Monko, Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini na Mheshimiwa Maulid Said Mtulia,  Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, kwa kuchaguliwa na kuwa wawakilishi wa wananchi katika Majimbo hayo. Kuchaguliwa na kuteuliwa kwao ni kielelezo cha kuaminiwa na wananchi ili kuwawakilisha ipasavyo katika Bunge hili.


12.   Mheshimiwa Spika,  napenda kipekee kabisa kuchukua nafasi hii kumshukuru Mume wangu Mpenzi Balozi Mbelwa Kairuki pamoja na watoto wetu wapendwa kwa kunivumilia, kuniunga mkono na kuniombea kwa Mwenyezi Mungu ili niweze kutekeleza majukumu niliyopewa na Mheshimiwa Rais ya usimamizi wa sekta hii nyeti ya madini.

13.   Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, naomba sasa kuwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti  ya  Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18; na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19.


2.0   DIRA, DHIMA NA MAJUKUMU YA WIZARA

Dira na Dhima ya Wizara

14.   Mheshimiwa Spika, Dira ya Wizara ni kuwa Wizara inayoheshimika Afrika katika kuendeleza rasilimali za madini ili ziweze kuchangia kwa ufanisi katika uchumi wa Taifa na ustawi wa Watanzania. Aidha, Dhima ya Wizara ni kuzibadili rasilimali za madini ziweze kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa na maendeleo endelevu.

Majukumu ya Wizara

15.     Mheshimiwa   Spika,   kulingana   na   Hati Idhini (Na.144 ya tarehe 22 Aprili, 2016 iliyofanyiwa marekebisho tarehe 15 Oktoba, 2017, majukumu ya Wizara ya Madini ni: -

(i)  Kubuni, kuandaa na kusimamia Sera, Mikakati na Mipango ya kuendeleza Sekta ya Madini;
(ii) Kusimamia  migodi  na  kuhamasisha  shughuli
za  uchimbaji  pamoja  na  utafutaji  wa  madini kwa kutumia tafiti za kijiofizikia na kijiolojia (Geophysical na Geological surveys);
(iii) Kuratibu        na     kusimamia        uongezaji       thamani
madini kwenye biashara ya madini; kukuza ushiriki wa Wazawa (local content) kwenye shughuli za utafutaji, uchimbaji na biashara ya madini nchini;
(iv) Kusimamia na kuratibu shughuli na maendeleo
ya wachimbaji wadogo; kusimamia Taasisi na
Mamlaka zilizoko chini ya Wizara; na
(v) Kuratibu na kusimamia maendeleo na utekelezaji wa majukumu kwa watumishi wa Wizara.


3.0   MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA WA 2017/18

(a)      Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18


16. Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa katika Mwaka wa Fedha wa 2017/18 iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini iliidhinishiwa Bajeti ya jumla ya shilingi 998,337,759,500. Kati ya fedha hizo, shilingi
938,632,006,000 sawa na asilimia 94 ya Bajeti yote ilikuwa ni kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo na shilingi 59,705,753,500, sawa na asilimia 6 ya Bajeti yote ilikuwa ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida.

(b)       Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18


17. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2017/18 ukiondoa fedha zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za Sekta ya Nishati, Sekta ya Madini ambayo sasa inasimamiwa na Wizara ya Madini, iliidhinishiwa na Bunge lako Tukufu jumla ya shilingi 52,445,367,000. Kati  ya  fedha  hizo,  shilingi  21,783,000,000  sawa na  asilimia  41.53  ya  Bajeti  yote  zilikuwa  ni  kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo na shilingi
30,662,367,000 sawa na asilimia 58.47 ya Bajeti yote zilikuwa ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida kwa Wizara na Taasisi zake. Kwa upande wa fedha za Matumizi ya Kawaida, shilingi 13,912,800,000 sawa na asilimia 45.37 zilitengwa kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (O.C) na shilingi 16,749,567,000 sawa na asilimia 54.63 zilitengwa kwa ajili ya Mishahara


(P.E) ya watumishi wa Wizara na Taasisi zilizopo chini yake.  Aidha, Wizara ilipangiwa kukusanya maduhuli ya Serikali ya kiasi cha shilingi 194,663,501,763.

18. Mheshimiwa            Spika,        hadi      kufikia       tarehe
31 Machi, 2018 Wizara   ilipokea jumla ya Shilingi
19,173,608,450.31  kutoka  Hazina  sawa  na asilimia 36.56 ya Bajeti yote ya Wizara ya Shilingi
52,445,367,000 kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18. Kati ya fedha zilizopokelewa, Shilingi 834,976,618 ni fedha za Maendeleo sawa na asilimia 3.83 ya bajeti yote ya Maendeleo ya Shilingi 21,783,000,000. Kwa upande wa Matumizi ya Kawaida, Shilingi 18,338,631,832.31 zilipokelewa sawa na asilimia 59.81 ya fedha zote za Matumizi ya Kawaida zilizotengwa ambazo zilikuwa Shilingi 30,662,367,000. Kati ya fedha  za Matumizi ya  Kawaida  zilizopokelewa  Shilingi  8,227,481,851 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (O.C) na Shilingi
10,111,149,981.31  ni kwa ajili ya Mishahara (P.E)
kwa watumishi wa Wizara na Taasisi zake.

19. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18, ulizingatia pamoja na mambo mengine: Hati Idhini ya kuanzishwa kwa Wizara ya Madini Namba 144 ya tarehe 22 Aprili,
2016 iliyofanyiwa marekebisho tarehe 15 Oktoba, 2017; Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025; Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka
2015 - 2020; Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21); Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030; Sera ya Madini ya Mwaka 2009; Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017 na Kanuni zake. Vilevile, umezingatia maoni na ushauri wa Kamati Maalum ya Mheshimiwa Rais ya kuchunguza aina, wingi na thamani ya madini


mbalimbali yaliyopo kwenye mchanga wa madini (Makinikia) unaosafirishwa nje ya nchi iliyoongozwa na Profesa Abdulkarim Hamis Mruma; Kamati Maalum ya Mheshimiwa Rais ya kuchunguza masuala ya kisheria na kiuchumi kuhusiana na mchanga wa madini unaosafirishwa nje ya nchi iliyoongozwa na Profesa Nehemiah Eliakim Osoro; Kamati Maalum ya Spika ya kuchunguza Biashara ya Tanzanite iliyoongozwa na Mheshimiwa Doto Mashaka Biteko (Mb.) ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri wa Madini; Kamati Maalum ya Spika ya kuchunguza Biashara ya Almasi iliyoongozwa na Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu (Mb.); na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

20. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18, maeneo yafuatayo yalipewa kipaumbele: kuimarisha ukusanyaji wa Mapato ya Serikali yatokanayo na rasilimali madini; kudhibiti utoroshaji wa madini; kuendeleza wachimbaji wadogo na wa kati wa madini; kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini; kuimarisha usimamizi, ufuatiliaji na ukaguzi wa migodi ikiwemo ukaguzi wa afya, usalama, mazingira na uzalishaji wa madini katika migodi midogo, ya kati na mikubwa; kuendelea kuhamasisha   uwekezaji   katika   Sekta   ya   Madini na kuboresha Sera, Sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali kuhusu rasilimali madini. Vilevile, kipaumbele kiliwekwa katika kuimarisha Taasisi zilizo chini ya Wizara hususan Tume ya Madini, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST),  Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Chuo cha Madini (MRI), Kituo cha Jimolojia Tanzania (TGC) na Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi asilia (TEITI). Maeneo mengine ya   kipaumbele   yalikuwa   ni   kuwajengea   uwezo


watumishi wa Wizara katika fani mbalimbali pamoja
na kuendelea kuboresha mazingira ya ofisi.

(c)       Ukuaji na Mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa


21. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2017, Sekta ya  Madini  ilikua  kwa  asilimia  17.5  ikilinganishwa na asilimia 11.5 ya Mwaka 2016. Kuongezeka kwa kiwango cha ukuaji wa Sekta ya Madini kulitokana na kuimarishwa kwa udhibiti wa biashara haramu na utoroshwaji wa madini; kuimarishwa kwa ukaguzi na usimamizi katika sehemu za uzalishaji, biashara ya madini; na usafirishaji wa madini nje ya nchi; kuongezeka kwa viwango vya mrabaha na kuanzishwa kwa ada ya ukaguzi wa madini kufuatia marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 yaliyofanyika Mwaka 2017 na Kanuni zake.

22. Mheshimiwa Spika, vilevile, mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa umeendelea kuimarika ambapo  katika Mwaka 2017 mchango huo ulifikia asilimia 4.8. Kwa upande wa thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi, mauzo yalifikia Dola za Marekani
1,810,697,000 mwaka 2017. Ni matarajio yetu kuwa thamani ya mauzo itaendelea kuongezeka tena baada ya kukamilisha mageuzi makubwa ambayo tuliyaanzisha ikiwa ni pamoja na uongezaji thamani madini ndani ya nchi.

(d)    Uzalishaji na Ukusanyaji wa Maduhuli ya
Serikali kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18


23.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwezi
Julai, 2017 hadi Machi, 2018 jumla ya kilo 30,953.59


za dhahabu zilizalishwa na Migodi Mikubwa na ya Kati ya Bulyanhulu, Buzwagi, Geita, New Luika, North Mara na STAMIGOLD na kusafirishwa nje ya nchi. Vilevile, kilo 2,021.4 za dhahabu zilizalishwa na wachimbaji wadogo wa madini na wachenjuaji wa marudio. Aidha, kiasi cha karati 248,083.94 za almasi kilizalishwa katika Mgodi wa Almasi wa Mwadui (Williamson Diamond Limited) uliopo Shinyanga, pia kiasi cha karati  43,285.31  kilizalishwa  katika  Mgodi  wa  El Hilal na Tanzanite (ghafi) yenye kilogramu 535.99 ilizalishwa na Mgodi wa TanzaniteOne. Vilevile, kiasi cha kilo 516,408.93 cha madini mengineyo ya vito kilizalishwa. Kwa upande wa makaa ya mawe jumla ya tani 385,352 zilizalishwa kwenye Mgodi wa Ngaka Mkoani Ruvuma. Aidha, tani 3,125,399 za madini ya ujenzi na viwandani zilizalishwa. Uzalishaji huu kwa ujumla wake uliiwezesha Serikali kukusanya mrabaha wa Shilingi 175,518,751,221.49.

24. Mheshimiwa Spika, kutokana na mageuzi ambayo tumeyafanya, Wizara iliratibu mnada wa madini ya vito ya tanzanite uliofanyika tarehe 18 hadi
21 Desemba, 2017. Lengo la mnada huo lilikuwa ni kukuza biashara ya ushindani baina ya wachimbaji na wauzaji wa madini haya na wanunuzi wa kimataifa ili kupata bei bora zaidi na ya ushindani kwa njia ya uwazi na kuwapatia wachimbaji wa madini ya tanzanite soko la uhakika. Katika mnada huo, tanzanite yenye uzito wa kilo 47 iliuzwa kwa jumla ya Dola za Marekani 820,744 sawa na shilingi 1,839,476,075. Mapato yaliyokusanywa na Serikali ni mrabaha wa shilingi  110,368,564.50,  ada  ya  ukaguzi  shilingi
18,394,760.75 na ushuru wa   huduma wa shilingi
5,518,428.20.


25.  Mheshimiwa Spika, kwa upande wa maduhuli ya  Sekta  ya  Madini,  katika  Mwaka  wa  Fedha  wa
2017/18 Wizara ya Madini, ilipangiwa kukusanya jumla ya shilingi 194,663,501,763 na Bunge lako Tukufu kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vikiwemo mrabaha; ada ya mwaka; ada za kijiolojia; ada ya uchambuzi wa madini; uchapishaji na uuzaji wa nyaraka za zabuni; stakabadhi nyinginezo; marejesho ya fedha za Serikali; tozo mbalimbali zinazotokana na adhabu na ada za ukaguzi. Napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2018 jumla ya maduhuli ya shilingi 225,006,324,173.21 yalikuwa yamekusanywa. Kiasi hiki ni sawa na asilimia
115.59 ya lengo lililowekwa katika Mwaka wa Fedha wa 2017/18.

26.  Mheshimiwa Spika, ongezeko la makusanyo ya maduhuli limetokana na kuongezeka kwa viwango vya mrabaha kutoka asilimia nne hadi sita kwa madini ya metali, na kutoka asilimia tano hadi sita  kwa madini ya vito; kuanzishwa kwa tozo ya ukaguzi ya asilimia moja ya mauzo ya madini; usimamizi wa biashara ya madini na kuimarisha udhibiti wa utoroshwaji wa madini kwa kushirikiana na wananchi na Vyombo vya Ulinzi na Usalama.

(e)    Udhibiti wa Biashara ya Madini


27.   Mheshimiwa  Spika, Wizara  imeendelea kufanya ukaguzi wa uzalishaji wa madini kwenye migodi mbalimbali ili kuhakikisha kuwa Serikali inapata  takwimu  sahihi  za  madini  yanayozalishwa na kuuzwa  ndani na nje ya nchi; thamani halisi ya madini hayo; na mrabaha stahiki unaopaswa kulipwa. Ukaguzi huo hususan kwenye migodi na mitambo ya


uchenjuaji  umekuwa  ukifanyika  kwa  kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama. Kufuatia jitihada hizo, makusanyo ya mrabaha yameongezeka. Kwa mfano, hadi kufikia mwezi Machi, 2018 Ofisi ya Madini (Chunya)  imeweza  kukusanya  kiasi  cha  shilingi
718,667,100.41 na Ofisi ya Madini (Mwanza) kiasi cha
shilingi 9,843,380,762.80 ikilinganishwa na shilingi
416,968,335.28 na shilingi 6,181,589,371.75 zilizokusanywa na Ofisi hizo kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/17, sawia. Wizara pia imeanzisha utaratibu mpya wa uombaji wa vibali vya kusafirisha madini nje ya nchi, ambapo mchimbaji au mfanyabiashara wa madini hulazimika kuwasilisha sampuli GST kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara ili kufahamu ubora stahiki wa sampuli au madini yanayoombewa kibali cha kusafirishwa nje ya nchi. Vilevile, katika kudhibiti shughuli za uzalishaji na biashara ya madini ya tanzanite ambayo hupatikana Tanzania pekee, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, ilijenga ukuta wenye mzingo wa kilomita 24.5 katika Migodi ya Mirerani kwa lengo la kudhibiti utoroshwaji wa madini ya tanzanite kwenda nje ya nchi.

28. Mheshimiwa  Spika,  Serikali  kupitia  Wizara ya Madini ilizuia uingizaji wa madini yanayopatikana nchini kama vile makaa ya mawe na jasi ili kuhakikisha madini haya yananunuliwa hapa nchini kwa lengo la kukuza soko la ndani la madini hayo. Kutokana na udhibiti huo, jumla ya tani 431,029.14 za makaa ya  mawe  zenye  thamani  ya  Dola  za  Marekani
18,314,709.53 ziliuzwa hadi kufikia Machi, 2018 ikilinganishwa na tani 429,682.85 zilizouzwa Mwaka wa Fedha wa 2016/17 zenye thamani ya Dola za Marekani 16,931,162.29. Vilevile, tani 121,186.82 za


jasi zenye thamani ya Dola za Marekani 3,120,024.09
ziliuzwa kufikia Machi, 2018 ikilinganishwa na tani
181,080.34 zilizouzwa Mwaka wa Fedha wa 2016/17 zenye thamani ya Dola za Marekani 5,283,526.13. Wizara imeanza maandalizi ya uanzishwaji wa masoko ya madini ya dhahabu na vito ikiwemo tanzanite, almasi na madini mengine. Maandalizi haya yanashirikisha Timu ya Wataalamu na wadau mbalimbali wa biashara ya madini na Serikali.

29. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha udhibiti dhidi ya utoroshwaji wa madini, Serikali imeendelea na mkakati wa kukabiliana na biashara haramu ya madini ambapo Wizara kwa kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) inaendelea kufanya ukaguzi kupitia madawati yaliyopo katika viwanja vya ndege, Bandari na mipaka ya nchi. Kufuatia kaguzi hizo, jumla ya matukio 9 ya biashara haramu ya madini yenye thamani ya Dola za Marekani 229,037.85 na shilingi
1,500,000,000 yaliripotiwa kutokea katika Vituo vya
Kutokea (Exit Points) nchini katika kipindi cha Julai,
2017  hadi  Aprili,  2018  ikilinganishwa  na  matukio
11 ya biashara haramu ya madini yenye thamani ya shilingi 268,700,000 yaliyotokea Mwaka wa Fedha wa 2016/17. Aidha, Serikali imekuwa ikiwafikisha wahusika wa matukio hayo katika Vyombo vya Sheria. Wizara bado inaona kuna changamoto ya utoroshwaji wa madini pamoja na kupungua kwa matukio ya ukamataji kwa watoroshaji madini. Hivyo, azma ya Wizara ni kuimarisha udhibiti kwenye mipaka yote ili hatimaye kuondoa kabisa mianya ya utoroshwaji wa madini nchini.


30. Mheshimiwa  Spika,  pamoja  na  uimarishaji huo, bado kuna changamoto mbalimbali katika udhibiti wa shughuli za madini nchini. Hivyo, natoa rai na kuwaomba wadau wote wa Sekta ya Madini na wananchi wote kushiriki katika ulinzi wa rasilimali madini ili ziweze kuwa na manufaa makubwa zaidi kwa Taifa.

(f )       Ujenzi wa Ukuta kwenye Migodi ya Mirerani


31. Mheshimiwa   Spika,   itakumbukwa   kuwa mwezi Juni, 2017 uliunda Kamati Maalum ya Bunge iliyoshughulikia namna shughuli za uchimbaji na uuzaji wa madini ya tanzanite zinavyofanyika nchini. Kamati hiyo ilitoa mapendekezo mbalimbali ikiwemo kuwepo kwa mfumo mpya wa udhibiti wa madini ya tanzanite.

32. Mheshimiwa Spika, kutokana na mapendekezo hayo, tarehe 20 Septemba, 2017 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli aliliagiza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kujenga ukuta kuzunguka eneo la migodi ya tanzanite Mirerani ili kudhibiti utoroshwaji wa madini hayo. Kufuatia agizo la Mheshimiwa Rais, Ukuta huo ulianza kujengwa kuanzia tarehe 1 Novemba, 2017 na kukamilika tarehe 15 Februari, 2018 na kuzinduliwa na Mheshimiwa Rais tarehe 6 Aprili, 2018.

33. Mheshimiwa Spika, kutokana na udhibiti huo, katika kipindi kifupi cha miezi mitatu tu cha Januari hadi Machi 2018, Wizara imefanikiwa kukusanya mrabaha wa kiasi cha jumla ya shilingi 714,670,000. Katika kiasi hicho, shilingi 614,670,000 zinatokana na makusanyo kutoka kwa wachimbaji wadogo. Kiasi


hicho kilichokusanywa kinazidi jumla ya makusanyo ya   mrabaha   wa   miaka   mitatu   iliyopita   kutoka kwa wachimbaji wadogo. Pia, Bunge lako Tukufu litapendezwa kufahamu kwamba katika Mwaka 2015 tulikusanya mrabaha wa shilingi 166,850,000; Mwaka 2016 shilingi 71,860,000; na Mwaka 2017 shilingi 147,140,000 kutoka kwa wachimbaji wadogo.

(g)    Kuimarisha Usalama Migodini


34. Mheshimiwa Spika, pamoja na majukumu mengine Wizara hii ina wajibu wa kuhakikisha usalama wa shughuli za uchimbaji migodini. Kwa msingi huo, Wizara imeendelea kufanya kaguzi mbalimbali ambapo kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18 jumla ya leseni za migodi 2,204 zilikaguliwa. Kati ya leseni hizo, 6 ni za uchimbaji mkubwa, 134 za uchimbaji wa kati na 2,064 za uchimbaji mdogo. Wizara pia iliendelea kufanya uchunguzi wa ajali na matukio yanayotokea migodini kwa lengo la kubaini changamoto za kiusalama ili kuweza kuzuia matukio ya aina hiyo katika migodi. Katika Mwaka wa Fedha wa 2017/18, jumla ya ajali 14 ziliripotiwa na kuchunguzwa katika migodi. Uchunguzi huo uliofanyika ulibaini kuwa wachimbaji 33 walifariki dunia; 50 walijeruhiwa, kutibiwa na kuendelea na kazi zao. Matukio hayo ni kama ifuatavyo: Kanda ya Kati (Singida na Dodoma) matukio 5; Kanda ya Kaskazini (Arusha, Manyara na Kilimanjaro) matukio 3; Kanda ya Kusini Magharibi (Mbeya, Songwe na Iringa) matukio
2; Kanda ya Kati Magharibi (Shinyanga na Tabora) tukio 1; na Kanda ya Ziwa Victoria Mashariki (Mara na Simiyu) tukio 1. Uchunguzi wa ajali hizo, ulibaini kuwa chanzo kikubwa cha ajali hizo ni kutozingatia kanuni za usalama. Kufuatia uchunguzi huo, ripoti ziliandaliwa


na wahusika walipewa nakala ya ripoti husika ili kuboresha usalama katika maeneo yao na wengine
42  leseni  zao  zilisimamishwa  hadi  waliporekebisha na  kufuata  kanuni  za  usalama  migodini  ambapo jumla ya leseni 38 zilikidhi matakwa ya kiusalama na kuruhusiwa kuendelea na kazi. Mathalan, katika eneo la Irasanilo - Solemba, Buhemba shughuli za uchimbaji zilisimamishwa kwa muda wa mwaka mmoja ili kurekebisha kasoro za kiusalama.

35. Mheshimiwa Spika, kanuni ya 71 ya Kanuni za Afya, Usalama na Utunzaji wa Mazingira za Mwaka
2010 inaelekeza wachimbaji kutoa taarifa ya kusudio la kubadilisha teknolojia yoyote katika shughuli za uchimbaji na uchenjuaji na kuwasilisha taarifa hiyo kwenye Ofisi za Madini. Hata hivyo, kumekuwa na hulka ya wachimbaji kutumia teknolojia ya vifaa mbalimbali katika shughuli za uchimbaji bila kuzingatia uwezo na ubora wa vifaa hivyo. Hali hii inasababisha uwepo wa ajali nyingi ambazo zingeweza kuepukika. Mathalan, ajali iliyotokea tarehe 06 Aprili, 2018 Wilayani Bahi, ilisababishwa na winchi inayotumika kubebea mizigo kutumika kubebea watu. Katika uchunguzi ilibainika kuwa wahusika walikuwa hawafanyi ukaguzi wa kamba mara kwa mara. Timu yangu ya ukaguzi ilipowahoji wahusika walionusurika kwenye ajali hiyo, ilibaini kuwa wahusika hao hawakuwa na taarifa kuhusu uwezo wa winchi husika kunyanyua mizigo ila yalikuwa ni mazoea ya kutumia chombo hicho. Natoa rai kwa wachimbaji na wawekezaji wote katika Sekta ya Madini nchini kufuata maelekezo ya Kanuni za Afya, Usalama na Utunzaji wa Mazingira zilizopo ili wawe salama katika shughuli zao za uchimbaji.


(h)      Kuimarisha Masuala ya Afya Migodini


36. Mheshimiwa Spika, ili kupunguza athari za kiafya zinazoweza kuwapata wafanyakazi migodini kutokana na uvutaji wa vumbi na hewa chafu kuzidi kiwango stahiki kwa muda mrefu; ukaaji wa muda mrefu kwenye eneo lenye kelele nyingi; na kutumia vifaa vyenye viwango vya chini kulingana na mahitaji ya eneo husika, Wizara yangu imeimarisha ukaguzi wa mazingira ya kazi migodini pamoja na kuhamasisha uwepo na matumizi ya vifaa kinga. Ikumbukwe pia, utumiaji wa vifaa vya kinga ni sehemu ya kuzuia athari za kiafya. Kutotumia vifaa vya kinga kunaweza kusababisha matatizo ya kiafya kama kuathiri mfumo wa kupumua au kuambukizana magonjwa kama Kifua Kikuu (TB) ikizingatiwa kuwa wanafanya kazi kwenye maeneo yenye changamoto ya ujazo wa hewa. Ukaguzi wa mara kwa mara kuhusiana na utumiaji wa vifaa vya kinga umekuwa ukifanyika migodini. Aidha, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaendelea na utafiti ili kubaini ukubwa wa changamoto ya TB migodini na kutoa ushauri wa namna bora ya kujikinga na maradhi hayo.

37. Mheshimiwa   Spika,   kwa   kushirikiana   na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu; na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto tunaendelea kuimarisha ukaguzi wakati wa kuajiriwa; na upimaji wa afya mara kwa mara kwa wafanyakazi wote wa migodini. Pia, Wizara inaendelea kuweka utaratibu wa kuchunguza afya wakati mfanyakazi anaacha au kuachishwa kazi. Lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha kuwa shughuli za uchimbaji na uchenjuaji madini zinafanywa kwa kujali afya za wafanyakazi.


(i)       Kuimarisha Utunzaji wa Mazingira Migodini na Kwenye Miradi ya Uchenjuaji Madini


38. Mheshimiwa Spika, Sheria ya Madini ya Mwaka
2010 pamoja na Marekebisho yake ya Mwaka 2017 na  Kanuni  zake  zinasisitiza  umuhimu  wa  utunzaji wa mazingira. Kama nilivyoeleza awali, shughuli za utafiti, uchimbaji na uchenjuaji wa madini zinapaswa kuhakikisha usalama wa watu na mazingira katika maeneo wanayofanyia kazi. Kwa mujibu wa Kifungu cha 60 cha Sheria ya Madini, moja ya masharti ya leseni zitolewazo kwa wachimbaji madini ni kutoa tamko la utunzaji wa mazingira ambapo kwa mchimbaji mdogo hutakiwa kuwasilisha Mpango wa Utunzaji wa Mazingira (Environmental Protection Plan) kwa Afisa Madini  Mkazi.  Kwa  upande  wa  uchimbaji  wa  kati na  mkubwa,  wamiliki  hutakiwa  kuandaa  Tathmini ya Athari za Mazingira na Mpango wa Kutunza Mazingira (Environmental Impact Assessment (EIA) and Environmental Management Plan (EMP)). Lengo kuu la kuwa na maandiko haya ni kuhakikisha mwenye mradi anatambua  kuwa  shughuli  anazofanya  zina  athari kwa mazingira na kufahamu maandalizi yake kwenye utunzaji na uhuishaji wa mazingira ili kuwa rafiki kwa matumizi ya binadamu akiwa bado anaendelea kuwekeza au anapomaliza uchimbaji katika eneo husika.

39. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Kanuni ya 177
– 184 za Mwaka 2010 za Uchimbaji Salama, Afya na Utunzaji wa Mazingira zinazoelekeza migodi kuwa na miundombinu muhimu ya kutupa mabaki ya miamba, mabwawa ya kutunzia maji na mabaki yenye kemikali yatokanayo na uchenjuaji wa madini (Waste Rocks


Dumps and Tailings Storage Facilities). Katika Mwaka wa Fedha wa 2017/18, Wizara yangu ilimuelekeza mmiliki wa Mgodi wa Dhahabu wa Nyarugusu kulipa fidia kwa waathirika kutokana na bwawa la kuhifadhia maji yenye kemikali zilizotumika kuchenjua madini ya dhahabu kumwaga maji hayo katika mashamba na kuathiri mazao ya wakulima kutokana na mvua kubwa kunyesha ndani ya muda mfupi. Licha ya kulipa fidia kwa waathirika, mmiliki alielekezwa kufanya usanifu mpya wa bwawa hilo ili liweze kuhimili mvua kubwa pamoja na kuandaa mpango wa dharura wa ukusanyaji maji hayo wakati wa mvua. Pia, Wizara imeendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye maeneo hayo ili kuona uhimilivu wa miundombinu husika.

40. Mheshimiwa Spika, hali kadhalika, Wizara yangu imeendelea kuhakikisha kuwa migodi ya madini inapofungwa, mazingira ya eneo husika yanaachwa katika hali ya usalama. Kwa mujibu wa Kanuni ya 206 ya Kanuni za Madini (Usalama wa Afya Mgodini na Utunzaji wa Mazingira) za Mwaka 2010, Migodi ya kati na mikubwa inatakiwa kuwasilisha Mpango wa Ufungaji Migodi (Mine Closure Plan). Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, Kampuni ya ACACIA inayomiliki Migodi ya dhahabu ya North Mara, Bulyanhulu na Buzwagi ilishawasilisha Mpango wake wa Ufungaji Mgodi na kuweka Hati Fungani ya Mazingira. Pia, Mgodi  wa  Dhahabu  wa  Geita  Gold  Mining  Limited (GGM)  uko kwenye hatua za kukamilisha utaratibu wa kuweka Hati Fungani. Vilevile, Migodi ya Dangote, TanzaniteOne, New Luika na Williamson Diamonds nayo inakamilisha majadiliano ili kuhakikisha usalama na utunzaji wa mazingira unazingatiwa.


(j)        Usimamizi wa Matumizi ya Baruti


41. Mheshimiwa  Spika,  udhibiti  wa  matumizi ya baruti kwenye shughuli mbalimbali zikiwemo za utafutaji wa mafuta na gesi na uchimbaji wa madini ili kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa usalama na kwa madhumuni yaliyokusudiwa uliendelea kufanyika. Katika ukaguzi uliofanywa na Wizara, ilibainika kuwa jumla ya tani 22,474 za baruti na vipande 1,749,203 vya fataki vilitumika kwenye shughuli mbalimbali. Aidha, jumla ya maghala 37 ya kuhifadhia baruti na fataki yalikaguliwa katika Mikoa yote yenye shughuli za uchimbaji wa madini ili kubaini utunzaji salama kwa mujibu wa matakwa ya Sheria ya Baruti ya Mwaka
1963 na Kanuni zake.

(k)      Uendelezaji wa Wachimbaji Wadogo


42. Mheshimiwa Spika, kwa kutambua kuwa Sekta ya Madini inatoa ajira kati ya 500,000 na 1,500,000 kutokana na utafiti uliofanywa na UNEP Mwaka 2012, Wizara itaendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo kujiajiri kupitia Sekta ya Madini kwa kuwatambua, kuwaendeleza, kuwarasimisha na kuwapatia maeneo ya uchimbaji wa madini. Vilevile, Wizara itaendelea kuwapatia taarifa za kijiolojia, kiufundi na kuwawezesha kupata huduma za kifedha na masoko. Aidha, Wizara itaendelea   kuwapatia   mafunzo   ya   teknolojia   na maarifa ya kisasa kwa ajili ya kuendeleza shughuli za uchimbaji ili wakue na waweze kuwa wachimbaji wa kati na wakubwa katika siku za usoni. Serikali inaamini kuwa uchimbaji mdogo siyo hadhi ya kudumu bali ni hatua ya mpito kuelekea katika uchimbaji wa kati hadi mkubwa. Sababu za kufanya hivyo zipo wazi kwa kuwa wachimbaji wadogo endapo watafanikiwa kukua,


mapato yao yanaweza kuwekezwa zaidi  kwenye Sekta ya Madini na sekta nyingine nchini na hivyo kuchangia zaidi kwenye ukuaji wa Sekta ya Madini, ukuaji wa uchumi na Pato la Taifa na hatimaye kuwanufaisha watanzania wengine.

43. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia GST na STAMICO chini ya Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) ilikamilisha utafiti wa kina wa kijiosayansi uliohusisha uchorongaji na ukadiriaji wa mbale katika maeneo ya wachimbaji wadogo kwenye maeneo sita ya ujenzi wa Vituo vya Umahiri vya Katente (Bukombe), Itumbi (Chunya), Kona Z (Tanga), Kapanda (Mpanda), Buhemba (Musoma) na Kyerwa (Bukoba). Vituo hivyo vitatumika kwa ajili ya mafunzo ya uongezaji thamani madini na uchimbaji salama pamoja na kuongeza uzalishaji, tija na hivyo kuongeza mapato kwa wachimbaji wadogo. Ukadiriaji wa mbale umeonesha  kuwepo  kwa  takriban wakia
47,605 za dhahabu katika maeneo ya Mpanda (D – Reef na Kapanda); wakia 10,737.33 za dhahabu katika eneo la Buhemba; wakia 46,663 za dhahabu eneo la Chunya (Itumbi); na wakia 9,459 za dhahabu katika eneo la Katente. Aidha, ukadiriaji wa mbale katika maeneo  ya  Tanga  (Kiomoni,  Kange  na  Mkulumuzi) na Kyerwa (Kaborishoke) umeonesha uwepo wa tani
403,056,469  za  miamba  chokaa  yenye  ubora  wa zaidi ya asilimia 48 ya chokaa (calsium); na tani
1,409,742.15 za bati sawia. Maandalizi ya ujenzi wa Vituo hivyo yanaendelea.   Aidha, matokeo ya utafiti huo yatatumika kuainisha njia bora za uchenjuaji kwenye kila eneo na kuwasaidia wachimbaji wadogo kupunguza upotevu wa madini wakati wa uchenjuaji.

44. Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Mgodi wa Mfano wa  Lwamgasa  unaendelea  kujengwa  ambapo  kwa


sasa umefikia asilimia 70. Gharama za mgodi huo ni Dola za Marekani 584,800. Mgodi huu utawezesha Chama cha Washirika wa Kijiji cha Lwamgasa na wachimbaji wanaozunguka Mgodi huo kuchimba na kuchenjua dhahabu kwa kutumia teknolojia sahihi na yenye gharama nafuu. Vilevile, mafunzo mbalimbali yamekuwa  yakitolewa  kwa  wachimbaji  wadogo ambapo kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18. Jumla ya wachimbaji wadogo 4,468 walipatiwa mafunzo katika Mikoa 13 ambayo ni Manyara, Morogoro, Tanga, Pwani, Shinyanga, Geita, Mara, Katavi, Singida, Dar es Salaam, Mbeya, Lindi na Mtwara. Vilevile, STAMICO kwa kushirikiana na Tanzania Gender Network Program  (TGNP)  na  Women  in  Mining  Association (WIMA) ilitoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo katika eneo la Mwalazi mkoani Morogoro ambapo jumla ya wachimbaji 37 walipatiwa mafunzo kuhusu namna ya kuchakata madini ya dolomite kwa kuzingatia matumizi na mahitaji ya soko.

45. Mheshimiwa Spika,  mafunzo mengine yalito- lewa na Ofisi ya Madini Mirerani kwa kushirikiana na Wakala wa Usalama Mahali pa Kazi (OSHA) katika eneo la Mirerani; Ofisi ya Madini Geita kwa kushirikiana na OSHA katika Mkoa wa Geita; Ofisi ya Madini Shinyanga kwa kushirikiana na OSHA na TRA katika Mkoa wa Shinyanga; Ofisi ya Madini Chunya kwa kushirikiana na Kampuni ya PAULSAM katika Wilaya ya Chunya; Ofisi ya Madini Singida kwa kushirikiana na Vyama vya Wachimbaji Wadogo na Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) katika Mkoa wa Singida; Ofisi ya Madini Mpanda katika Wilaya ya Mpanda; Ofisi ya Madini Songea; Ofisi ya Madini Musoma katika Wilaya za Butiama, Tarime na Bunda; Ofisi  ya  Madini  Mtwara  katika  Mikoa  ya  Lindi  na


Mtwara; na Ofisi ya Madini Dar es Salaam katika Mikoa ya Morogoro, Tanga na Pwani. Mafunzo hayo yalihusu usalama na afya mahali pa kazi.

(l)     Sera, Sheria na Miongozo mbalimbali kuhusu Rasilimali Madini


46. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2017/18, Serikali chini ya uongozi makini wa Mheshimiwa Rais, imefanya mageuzi makubwa na ya msingi kwenye Sekta ya Madini. Tunalishukuru Bunge lako Tukufu kwa kuridhia na kupitisha Marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kupitia Marekebisho ya Sheria mbalimbali yaliyofanywa na Sheria ya Marekebisho Na.7 ya Mwaka 2017. Katika kuwezesha utekelezaji wa Sheria hiyo, Wizara ya Madini ilitengeneza Kanuni za Madini zipatazo saba ambazo ni:-

(i)  Kanuni za Madini (Haki Madini) za Mwaka 2018;

(ii)  Kanuni       za    Madini      (Biashara      ya    Madini      na
Makinikia) za Mwaka  2018;

(iii)  Kanuni za Madini (Huduma na Bidhaa Madini zinazotolewa na Watanzania) za Mwaka 2018;

(iv)  Kanuni  za  Madini  (Madini  Mionzi)  za  Mwaka
2018;

(v)  Kanuni za Madini (Uongezaji Thamani Madini) za
Mwaka 2018;

(vi)  Kanuni za Madini (Utafiti wa Kijiolojia) za Mwaka
2018; na

(vii)  Kanuni za Madini (Ukaguzi na Uchunguzi wa
Nyaraka) za Mwaka 2018.


47. Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 105 (1) na (2) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017 kinamtaka mmiliki wa leseni ya utafutaji na uchimbaji wa madini kuandaa Mpango wa Mwaka wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR). Mpango huo lazima ukubalike kwa pamoja na Mamlaka ya Serikali ya Mtaa husika au Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kushauriana na Waziri anayehusika na Serikali za Mitaa na Waziri anayehusika na masuala ya fedha. Aidha, Kifungu cha 105(4) kinaitaka kila Halmashauri ya Serikali ya Mtaa kuandaa Mwongozo wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii, kusimamia utekelezaji wa Mpango Kazi wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii na kutoa elimu kwa umma kuhusu miradi iliyopo katika maeneo yao. Hivyo, Wizara ya Madini inawahimiza wadau wote wa Sekta ya Madini wazingatie Sheria ya Madini wanapotekeleza majukumu yao.

(m)  Uimarishaji wa Usimamizi wa Sekta ya
Madini


48. Mheshimiwa  Spika,  Marekebisho  ya  Sheria ya Madini ya Mwaka  2017 yamewezesha kufanyika kwa mabadiliko katika usimamizi wa Sekta ya Madini ambapo majukumu ya iliyokuwa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na baadhi ya majukumu ya Kamishna wa Madini yamehamishiwa Tume ya Madini. Pia, Ofisi zilizokuwa za Kanda na Ofisi za Maafisa Madini Wakazi zipo chini ya Tume ya Madini. Kutokana na mabadiliko hayo, kila Mkoa utakuwa na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi na kila mgodi mkubwa na wa kati utakuwa na Afisa Mgodi Mkazi. Mabadiliko hayo yamelenga kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara hususan kuimarisha ukusanyaji wa  maduhuli  ya  Serikali;  kuondoa  muingiliano  wa


majukumu na kuimarisha usimamizi wa rasilimali madini ili kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

(n)   Uongezaji Thamani Madini


49. Mheshimiwa  Spika,  Serikali  imeendelea  na jitihada mbalimbali za kuhakikisha shughuli za uongezaji   thamani   madini   zinafanyika   ndani   ya nchi  ikiwa  ni  pamoja  na  kusimamia  ipasavyo  zuio la kusafirisha madini ghafi nje ya nchi. Wizara ilitoa matangazo ya kukaribisha uwekezaji katika ujenzi wa vinu vya uchenjuaji kwa ajili ya kusafisha na kuongeza thamani madini ya metali - smelter na refineries hapa nchini. Jumla ya maombi 27 ya uwekezaji kwenye smelter na refineries yaliwasilishwa na uchambuzi unaendelea kufanyika ili kupata mwekezaji atakayekidhi vigezo.

50. Mheshimiwa Spika,   kwa upande wa madini ya vito, Wizara imeendelea kukijengea uwezo Kituo cha   Jimolojia   Tanzania   (TGC)   kilichopo   Arusha kwa kuimarisha miundombinu yake. Vilevile, Kituo kimepata usajili wa kudumu kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kwa namba ya usajili REG/SAT/033 wa kutoa mafunzo ya Diploma in Gem
& Jewellery Technology mwezi Oktoba, 2017. Mafunzo
hayo yatakuwa ya muda wa miaka 3 na yanatarajiwa kuanza   mwezi   Agosti,   2018.   Katika   kuwajengea uwezo wakufunzi wazawa, Wizara iliingia Mkataba na Kampuni ya Centre for Development of Gem & Jewellery Technology kutoka nchini India kuleta wakufunzi saba (7) ambao watatoa mafunzo mbalimbali ya vito na usonara katika Kituo hiki wakishirikiana na wakufunzi wazawa. Aidha, Kituo kimeendelea kutoa mafunzo ya usanifu wa madini ya vito (lapidary) katika ngazi ya Astashahada ambapo jumla ya wanafunzi wanawake


18 walidahiliwa chini ya ufadhili wa Wizara ya Madini pamoja na Kamati ya maonesho ya Madini ya Vito ya Arusha (Arusha Gem Fair).

(o)    Kazi zilizotekelezwa kupitia Mradi wa
Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini
- SMMRP


51. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2017/18 kazi zilizotekelezwa kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) ni pamoja na upatikanaji wa Washauri Waelekezi kwa ajili ya kusanifu na kusimamia ukarabati na upanuzi wa Ofisi 7 za Madini za Mikoa kuwa Vituo vya Umahiri ambazo ni Bariadi, Bukoba (Tazama Picha Na.1), Chunya, Mpanda, Musoma, Tanga na Songea. Pia, Mradi uligharimia upatikanaji wa Mshauri Mwelekezi kwa ajili ya upanuzi wa miundombinu ya Chuo cha Madini  Kampasi  ya  Dodoma.  Michoro  ya  majengo hayo imekamilika na makadirio ya gharama za ujenzi yanaendelea kufanyika. Kazi nyingine iliyofanyika ni kusimamia ujenzi wa Mgodi wa Umahiri katika eneo la Lwamgasa - Geita ambao utagharimu Dola za Marekani 584,800 kwa ajili ya Wachimbaji Wadogo ambapo ujenzi wa shimo la uchimbaji (mining shaft) umefikia asilimia 70 (Tazama Picha Na.2); kuiwezesha GST kufanya utafiti wa kijiolojia kwa ajili ya ukadiriaji wa mbale katika maeneo yanayokusudiwa kuanzishwa Vituo vya Mfano. Maeneo hayo ni Bukombe (Katente); Chunya (Itumbi); Mpanda (D-Reef na Kapanda); Musoma (Buhemba); Kyerwa (Kyerwa); na Tanga (Kiomoni, Kange na Mkulumuzi). Taarifa ya utekelezaji wa utafiti huo imebainishwa kwa kina katika sehemu ya taarifa ya utekelezaji wa kazi zilizofanywa na Taasisi ya Jiolojia na Utafutaji Madini Tanzania.

52. Mheshimiwa Spika, ili kuboresha mazingira ya kazi na kuimarisha utendaji kazi katika Sekta ya Madini, Mradi ulinunua vifaa mbalimbali vya ofisi ambavyo ni vifaa vya ukaguzi, maabara na kemikali kwa ajili ya Wizara, Taasisi za GST, MRI, TGC na Ofisi za Madini za Mikoa. Vifaa hivyo ni vya kupimia viwango vya madini kwenye sampuli mbalimbali na vya ukaguzi wa migodi. Thamani ya vifaa hivyo ni Dola za Marekani 350,000. Vilevile, Mradi uliwezesha kuandaa Mwongozo wa namna bora ya uchimbaji wa madini kwa wachimbaji wadogo nchini (Training Manual Handbook). Mwongozo huo utawasaidia wachimbaji wadogo namna ya kufanya utafiti wa awali; uchimbaji na uchenjuaji endelevu; kuzingatia afya na usalama migodini; utunzaji bora wa mazingira; utunzaji wa kumbukumbu za fedha na ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali. Mwongozo huo utakamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2018.

(p)       Ajira na Maendeleo ya Watumishi


53.  Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka wa Fedha wa 2017/2018, Wizara imepata Kibali cha Ajira Mpya chenye jumla ya nafasi 16 katika kada za Katibu Mahsusi 3, Jiokemia 1, Mjiolojia 1, Wahandisi Migodi 2, Watunza Kumbukumbu Wasaidizi 2, Madereva 6 na Mkutubi Msaidizi 1.  Vilevile, katika Ikama  ya  Watumishi  kwa  Mwaka  wa  Fedha  wa
2017/18, Wizara imeidhinishiwa nafasi za ajira mpya
53, kuwapandisha vyeo watumishi 196, kubadilisha kada watumishi 7 na nafasi za uteuzi 3. Aidha, katika Ikama ya Watumishi kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18, STAMICO iliidhinishiwa nafasi 36 za kuwapandisha vyeo watumishi. Pia, GST imeidhinishiwa nafasi 36 za kuwapandisha vyeo watumishi, kuwabadilisha kada watumishi 3 na nafasi 6 za uteuzi.


54. Mheshimiwa   Spika,   Wizara    imeendelea kuwajengea uwezo watumishi wake 44 katika fani mbalimbali ikiwemo Jiolojia na Utafutaji wa Madini; upimaji wa ardhi (jomatikia); Sayansi ya Mazingira; Uhasibu; Utawala; Sera za Uchumi; Takwimu na Uhazili. Kati ya hao, watumishi 40 wamehudhuria mafunzo ya muda mrefu katika ngazi za Stashahada, Shahada na Shahada za Uzamili. Watumishi 4 walipata mafunzo ya muda mfupi kuhusu utafiti wa kijiolojia na usimamizi wa rasilimali madini yaliyofanyika nchini China.

55. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutoa huduma ya lishe, chakula na malipo ya dawa zilizo nje ya orodha ya dawa zinazogharamiwa na Bima ya Afya kwa watumishi wanaoishi na virusi vya UKIMWI na UKIMWI, ikiwa ni utekelezaji wa Waraka wa Watumishi wa Umma Namba 2 wa Mwaka 2006 na Mwongozo wa Kudhibiti UKIMWI Katika Utumishi wa Umma wa Mwaka 2007.


KAZI ZILIZOTEKELEZWA NA TAASISI ZILIZO CHINI YA WIZARA


56. Mheshimiwa   Spika,   Wizara   ya   Madini inasimamia jumla ya Taasisi 6. Taasisi hizo ni Tume ya Madini, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti Madini Tanzania, Shirika la Madini la Taifa, Chuo cha Madini, Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia na Kituo cha Jimolojia Tanzania.

(a) Tume ya Madini

57. Mheshimiwa Spika, Tume ya Madini imeundwa kwa  mujibu  wa  Kifungu  cha  21  cha  Sheria  ya


(Marekebisho ya Sheria mbalimbali) ya Mwaka 2017 iliyorekebisha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, na ilianza kutekeleza majukumu yake tarehe 30 Aprili,
2018. Kazi zilizotekelezwa na Tume ni pamoja na kupitia, kuchambua na kuhakiki maombi ya leseni za utafutaji, uchimbaji na biashara ya madini yaliyowasilishwa na waombaji wa leseni baada ya tarehe 4 Julai, 2017. Uhakiki uliofanywa na Tume umebaini kuwepo kwa jumla ya maombi 4,394 ya Leseni za Uchimbaji Mdogo (PML)  yaliyokuwa  yamependekezwa  kupewa  leseni. Pia, kulikuwa na maombi 549 ya leseni za biashara ya madini yaliyokidhi vigezo vya kupewa leseni hizo. Maombi hayo yote yanaendelea kuandaliwa leseni husika.

58. Mheshimiwa Spika, vilevile, Tume ilichambua na ilihakiki maombi ya leseni za utafutaji na uchimbaji wa kati wa madini yaliyowasilishwa baada ya tarehe
4 Julai, 2017. Uhakiki huo ulibaini uwepo wa jumla ya maombi 150 ya leseni za utafutaji wa madini na
15 za uchimbaji wa kati za madini. Aidha, uchambuzi wa maombi ya leseni ulibaini kuwepo kwa migogoro
4 katika maeneo yaliyoombewa leseni; taarifa za upembuzi yakinifu zisizojitosheleza; kutokuwepo kwa taarifa za Mpango wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii katika kutoa huduma (Corporate Social Responsibility – CSR); kutokuwepo kwa Mpango wa Ushirikishwaji wa Wazawa katika miradi ya madini (Local Content Plan); na kutokuwepo kwa tamko la kiapo cha uadilifu – “Integrity Pledge”. Waombaji wa leseni wamejulishwa kupitia Vyombo vya Habari kuhusu mapungufu hayo ili wawasilishe taarifa hizo zinazohitajika kwa mujibu wa Sheria.


(b)        Taasisi ya Jiolojia na Utafiti Madini
Tanzania (GST)


59. Mheshimiwa  Spika,  majukumu  ya msingi  ya
Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania ni:-

(i)      kukusanya,  kuchambua,  kutafsiri  na  kutunza takwimu na taarifa mbalimbali za jiosayansi (jiolojia, jiokemia na jiofizikia) na za upatikanaji madini;

(ii)      kutengeneza na kusambaza ramani mbalimbali za jiosayansi; kufanya uchunguzi wa maabara kwa sampuli mbalimbali za miamba, madini, maji, mimea na udongo kwa ajili ya tafiti mbalimbali;

(iii)      kutoa  idhini  ya  maandishi  kwa  sampuli  za miamba, udongo na sampuli zilizo katika hali ya vimiminika kwa ajili ya kusafirisha nje ya nchi;

(iv)     kusaidia wachimbaji wadogo hasa katika kubaini umbile na aina ya mbale, kutambua aina na ubora wa madini pamoja na namna bora ya uchenjuaji;

(v)      kuratibu  majanga  asilia  ya  jiolojia  (kama  vile matetemeko                      ya  ardhi,   milipuko   ya  volkano, maporomoko ya ardhi) na kutoa ushauri wa namna bora ya kujikinga;

(vi)      kuboresha kanzidata ya Taifa ya jiosayansi na madini;

(vii)      kufanya tafiti maalum za jiosayansi;

(viii)      kufanya tafiti za jioteknolojia na kutoa ushauri unaostahili                          katika   masuala   ya   ujenzi   wa miundombinu na makazi; na


(ix)       kutoa ushauri wa jiosayansi na utafutaji madini kwa wadau.

60. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2017/18, GST ilipanga kukusanya maduhuli ya Shilingi 350,000,000 kutoka kwenye vyanzo vyake mbalimbali. Vyanzo hivyo ni ada ya ushauri elekezi, tozo za ramani au machapisho ya jiosayansi na tozo za huduma za maabara. Hadi kufikia tarehe 31 Machi,
2018  GST  ilikuwa  imekusanya  jumla  ya  shilingi
294,700,000. Kiasi hiki ni sawa na asilimia 84.2 ya lengo ililowekewa kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18.

61. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu yake, GST imepima na kuchora ramani za jiolojia na jiokemia za mfumo wa QDS kwa skeli ya 1:100,000 kwenye maeneo mapya (QDSs 264, 265) yaliyoko Wilaya ya Mahenge na Malinyi; na kufanya ugani (field checks) wa jiolojia na jiokemia ili kuboresha ramani 2 za QDS 64 na 65 za Wilaya ya Shinyanga. Vilevile, kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo, GST ilifanya tafiti mbalimbali za jiosayansi. Katika kipindi husika, GST kwa kushirikiana na Geological Survey of China ilifanya utafiti wa kina wa jiokemia katika maeneo ya Mbeya (QDS 244 na 245) na  utafiti wa awali (Regional Scale Surveys) katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Dar- es-Salaam na Morogoro (Tazama Picha Na.3), Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Manyara, Arusha na Mara kwa lengo la kutafuta madini mbalimbali. Kwa ufadhili wa Serikali ya Marekani, GST ilikusanya taarifa na sampuli katika maeneo ya Wilaya za Kondoa na Chemba ili kupata vyanzo vya nishati ya joto ardhi kwa ajili ya maeneo ambayo yako mbali na gridi ya Taifa.


62. Mheshimiwa Spika, vilevile, GST na Serikali ya Jamhuri ya Korea Kusini ilisaini Hati ya Makubaliano kwa ajili ya kufanya utafiti kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kuainisha maeneo yenye uwepo wa madini kwenye maeneo ya Tunduma na Mtwara (QDS 257,
312, 313, 319, 320) yanayopakana na Zambia na Malawi. Aidha, GST ilitengeneza ramani mbalimbali za jiosayansi na kuzisambaza kwa wadau mbalimbali kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji katika Sekta ya Madini pamoja na matumizi mengine.

63. Mheshimiwa Spika, GST iliendelea kuboresha huduma za maabara ambapo mfumo wa kompyuta kwa ajili ya kuratibu uchunguzi wa sampuli kwenye maabara   uliandaliwa   na   kusimikwa   (Laboratory


Information Management System - LIMS). Pia, GST imeendelea kutengeneza Internal Reference Standards za limestone, phosphate na dhahabu. Vilevile, GST ilifanya uchunguzi wa kemia, petrolojia, minerolojia, uchenjuaji  madini  na jioteknolojia  kwenye  sampuli
13,633 za miamba choronge, udongo na madini. Pia, vyungu (cupels) 4,558 na crucibles 4,626 vilitengenezwa kwa ajili ya kutumika kuyeyushia sampuli za dhahabu ambapo hapo awali vilikuwa vinanunuliwa nje ya nchi kwa gharama kubwa. Vilevile, GST ilifanya uchunguzi wa kimaabara wa jumla ya sampuli 361 za udongo, madini na miamba na taarifa zake ziliandaliwa ambapo ziliwasaidia wateja kupata vibali (export permits) vya kusafirisha sampuli nje ya nchi kwa uchunguzi zaidi.


64. Mheshimiwa Spika, GST iliendelea na kazi ya kuratibu majanga asilia ya jiolojia ambapo takwimu kutoka vituo 8 vya kudumu vya kupimia matetemeko ya ardhi vilivyopo Dodoma, Mbeya, Arusha, Mtwara, Geita, Singida, Babati na Kibaya – Manyara zilikusanywa, kuchakatwa na kuhifadhiwa kwenye kanzidata. Kwa kutumia takwimu hizo, GST iliainisha maeneo yenye vitovu (epicentres) vya matetemeko na kuboresha ramani inayoonesha maeneo yenye vitovu vya matetemeko ya ardhi. Aidha, taarifa kuhusu matetemeko ya ardhi yaliyotokea katika maeneo mbalimbali ya nchi katika kipindi cha mwezi Oktoba, 2017 hadi Machi, 2018 ilitolewa kwa wananchi na kwenye vyombo vya habari. Matukio hayo yameainishwa kwenye Jedwali Na.1.

65. Mheshimiwa Spika, vilevile, GST ilifanya utafiti
maalum wa kuangalia ubora na wingi wa madini ya


jasi katika maeneo ya Makanya na Bendera (Same), Mwanga (Mwanga), Itigi (Manyoni), Msagali (Mpwapwa) na Manda (Chamwino), Mpindiro, Mandawa, Mbaru, (Kilwa-Lindi) na Mkomole (Sumbawanga); utafiti maalum katika Wilaya ya Mufindi, Kijiji cha Isalavanu kwa maombi ya Serikali ya Wilaya ili kubaini uwepo wa madini yaliyofichwa katika maeneo hayo wakati wa Utawala wa Wajerumani kama ilivyokuwa inadhaniwa na wana kijiji hicho; utafiti wa jiosayansi ulifanyika katika mahandaki yaliyopo katika Kijiji cha Gibeshi Mkoani Simiyu ili kujua kama ni mahandaki ya asili au yamechimbwa na binadamu; utafiti wa jiosayansi katika  eneo  la  Nholi  -  Dodoma  ili  kubaini  chanzo na uwepo wa madini ya dhahabu katika eneo hilo; uchunguzi wa malikale katika Wilaya ya Same Kata ya Lugulu na Kitongoji cha Vumba pamoja na Mkoani Tanga katika Kata ya Pongwe; kukusanya taarifa za uwepo wa madini na utafiti wa miamba katika Mkoa wa Iringa, Wilaya za Mufindi, Iringa Vijijini na Kilolo; na pia GST ilishiriki katika ukaguzi wa taarifa zilizotumika kupata kiwango cha almasi kilichopo kwa sasa katika Mgodi wa almasi wa Mwadui na kuhakiki uwepo wa kiwango hicho cha almasi na kutoa mapendekezo kwa Serikali.

66. Mheshimiwa Spika, Pia, katika tafiti nyingi zilizofanywa na wataalam wa jiosayansi ya uchenjuaji zimebainisha kuwa madini mengi hubakia kwenye visusu  (tailings)  baada  ya  kuchenjuliwa.  Sababu za madini kubakia kwenye mabaki ni kutokana na kutofikiwa kwa kiwango cha ukubwa wa chembe (particle size) za mbale kinachotakiwa baada ya mwamba kuvunjwa na kusagwa; matumizi yasiyo sahihi ya kemikali zitumikazo kuchenjua na utumiaji wa vifaa visivyostahili.  Hii inatokana na wachimbaji


wadogo kutofahamu tabia tofauti za miamba na mbale hivyo kupelekea kutotumia njia bora za uchenjuaji. Ni vyema wachimbaji wadogo wakafahamu njia bora za uchenjuaji kwa kufanya majaribio ya sampuli za mbale katika maabara mara kwa mara ili kutambua mtiririko mzuri, aina ya miamba, kiwango cha usagaji, njia na mbinu za uchenjuaji.

67. Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa wachimbaji wadogo, kama hawajui tabia za mbale ya sehemu wanayochimba, kabla ya kuanza uchenjuaji wapeleke sampuli za mbale (bulk samples) kwenye maabara za GST kwa ajili ya uchunguzi ili waweze kutambua njia bora za uchenjuaji. Lengo ni kupunguza madini kubaki kwenye visusu (tailings), kuongeza wingi wa uvunaji wa madini, kipato na faida kwa wachimbaji wa madini.

68. Mheshimiwa  Spika,  GST  ilifanya  kazi  ya kuboresha Kanzidata ya jiosayansi na madini, ambapo jumla ya machapisho 412 yalibadilishwa kutoka katika mfumo wa karatasi na kwenda kwenye mfumo wa digitali; ramani 93 za jiosayansi zilikuwa ‘‘scanned’’ na kuhaririwa na kuwekwa kwenye mfumo wa utunzaji wa taarifa na machapisho (GMIS); Ramani 17 za jiolojia za mfumo wa QDS zimebadilishwa kutoka mfumo wa karatasi kwenda mfumo wa digitali (digitization) kwa lengo la kurahisisha usambazaji na utumiaji. Aidha, GST ilisambaza ramani na machapisho mbalimbali kwa wadau wa Sekta ya Madini kwa matumizi mbalimbali. Vilevile, GST imepokea na kuhakiki taarifa 205 kutoka kwa wamiliki wa leseni za utafutaji na uchimbaji madini kwa ajili ya kujua uhalisia wake na kuzitunza kama ilivyoelekezwa  kwenye  Sheria  ya  Madini  ya  Mwaka
2010 na Marekebisho yake ya Mwaka  2017.


69. Mheshimiwa Spika, GST ilifanya utafiti wa uchenjuaji mbale za madini ya dhahabu katika maeneo ya Londoni na Sambaru (Singida) kwa ajili ya kusaidia wachimbaji   wadogo;   na   kukamilisha   uchakataji wa taarifa za awali za jiosayansi (Geotechnical and seismological) ili kuainisha maeneo hatarishi na salama kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika Jiji la Dodoma ikizingatiwa kuwa maeneo hayo yapo katika ukanda wa matetemeko ya ardhi. Aidha, GST ilitoa  ushauri  elekezi  wa  jiosayansi  kwa  kampuni
10 za utafutaji na uchimbaji madini ya metali na ya viwandani. GST pamoja na hayo ilipokea taarifa zenye jumla ya  leseni 247 za utafutaji madini (Prospecting licences), leseni 12 za uchimbaji wa kati wa madini (Mining licences) na leseni 6 za uchimbaji mkubwa kwa ajili ya kuhakiki ili kujua uhalisia wake na kutunza kama ilivyoelekezwa kwenye Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka  2017. Kati ya taarifa za leseni   zilizofanyiwa tathmini zimebainisha  kuwa taarifa za kampuni 10 hazikidhi vigezo vilivyotolewa na GST na vilivyoainishwa kwenye Sheria. GST imezielekeza kampuni hizo kuziboresha taarifa hizo.

(c)     Chuo cha Madini – (MRI)


70. Mheshimiwa Spika,  Chuo cha Madini kimeen- delea na majukumu yake ya kutoa  mafunzo ya muda mrefu ya utaalam wa kada ya kati (Ufundi Sanifu) katika fani za madini, mafuta na gesi asilia; kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wachimbaji wadogo wa madini hasa katika nyanja za jiolojia na utafutaji madini, uhandisi uchimbaji madini, uhandisi uchenjuaji madini, uhandisi na usimamizi wa mazingira migodini; kutoa


mafunzo maalum (tailor-made courses) kwa wadau kulingana na mahitaji yao; kufanya tafiti katika Sekta za Madini, Mafuta na Gesi; na kutoa ushauri elekezi (consultancy) katika Sekta hizo.

71. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2017/18, Chuo kimedahili jumla ya wanafunzi 542 katika mafunzo ya muda mrefu katika fani za Jiolojia na Utafutaji Madini; Uhandisi Uchimbaji Madini; Uhandisi Uchenjuaji Madini; Sayansi za Mafuta na Gesi; Uhandisi na Usimamizi wa Mazingira Migodini; na Upimaji wa Ardhi na Migodi. Katika kutoa mafunzo ya muda mfupi, Chuo kimeweza kufundisha na kutoa vyeti kwa wafanyakazi 33 wa migodini ili kuwajengea uwezo wa kufanya kazi kwa ubora.  Aidha, katika kutoa mafunzo maalum, Chuo kimeingia Mkataba wa Makubaliano (MoU) na Kampuni ya Acacia North Mara kwa ajili ya kuwafundisha wafanyakazi wake 20 kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia mwezi Januari,
2018. Pia, Chuo kina Mikataba ya Makubaliano na Taasisi ya Jiolojia na Utafutaji Madini Tanzania (GST), Earth Sciences Institute of Shinyanga (ESIS), Zimbabwe School of Mines (ZSM), Dedan Kimathi University of Technology (DeKUT), Dar es Salaam Marine Institute (DMI), Tanzania Geothermal Development Company (TGDC), Chuo cha C̩gep Limoilou РCanada, Chuo Kikuu cha Montpellier РUfaransa, Mgodi wa Dhahabu wa Acacia North Mara na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

72. Mheshimiwa Spika, Vilevile, Chuo cha Madini kimeanzisha mafunzo ya fani mpya ya Upimaji wa Ardhi na Migodi (Land and Mine Surveying) kwa ngazi ya Astashahada na Stashahada. Jumla ya wanafunzi


24 wamedahiliwa na kuanza masomo ya Astashahada mwezi Januari, 2018. Mafunzo haya yatazalisha Mafundi Sanifu wa kupima ardhi na migodi.

73. Mheshimiwa   Spika,   katika    kuhakikisha mafunzo yatolewayo na Chuo cha Madini yanakidhi matakwa ya mtaala na mfumo wa ufundishaji, Serikali imeboresha maabara za Jiolojia, Uhandisi Uchimbaji na Uhandisi Uchenjuaji kwa kutoa vifaa vya maabara (Tazama Picha Na.8) kupitia mradi wa SMMRP ulio chini ya Wizara vyenye thamani ya Dola za Marekani
514,924.81 Maabara hizi zitakiwezesha Chuo kutoa mafunzo kwa vitendo na kufanya tafiti mbalimbali. Aidha,  kupitia  Mradi  wa  Improving  Skills  Training for   Employment   Program    (ISTEP)    unaotekelezwa kwa kushirikiana kati ya Chuo cha Madini na Chuo cha Cégep Limoilou kilichopo nchini Canada, Chuo kimepata vifaa vya kisasa (Tazama Picha Na.9) vya kusaidia kutoa mafunzo ya vitendo katika fani mpya ya Upimaji Ardhi na Migodi. Vifaa hivi vimegharimu jumla ya Dola za Kanada 40,000.








74. Mheshimiwa Spika, katika kusaidia wachimbaji wadogo Chuo kina mpango wa kufanya tafiti kuhusu kutengeneza   njia   mbadala   ya   uchenjuaji   madini ya  dhahabu  kwa  wachimbaji  wadogo.  Madhumuni ya utafiti huu ni kusaidia upatikanaji wa njia bora yenye ufanisi wa kuchenjua madini ya dhahabu kwa wachimbaji wadogo nchini na kuondoa matumizi ya kemikali ya Zebaki kwenye uchenjuaji wa dhahabu kama inavyotakiwa na Mikataba ya Kimataifa ikiwemo Makubaliano ya Minamata kuhusu utunzaji wa mazingira na afya za watu na viumbe mbalimbali katika mazingira yetu.

(d)  Shirika la Madini la Taifa – (STAMICO)


75. Mheshimiwa Spika, majukumu ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ni pamoja na kuwekeza kwenye shughuli za uchimbaji na utafutaji madini; kuwekeza katika uchenjuaji, uongezaji thamani na uuzaji madini; na kutoa huduma na ushauri wa kitaalamu na kiufundi katika Sekta ya Madini wakiwemo wachimbaji wadogo kwenye nyanja za kijiolojia, kihandisi, kimazingira na uchorongaji miamba.

76. Mheshimiwa  Spika,  STAMICO  imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya uchimbaji wa madini nchini ikiwemo ya uwezeshaji wa wachimbaji na miradi ya ubia. Utekelezaji wa shughuli hizo unahusisha uzalishaji wa makaa ya mawe katika Mgodi wa Kabulo; uzalishaji wa madini ya Tanzanite katika Mradi wa Ubia wa TanzaniteOne; uzalishaji wa madini ya dhahabu katika Kampuni Tanzu ya STAMIGOLD; na uendelezaji wa Mradi wa uchimbaji wa dhahabu wa Buhemba.

(i)     Mradi wa Makaa ya Mawe wa Kabulo, Kiwira

77. Mheshimiwa Spika, Shirika lilianza uchimbaji wa makaa ya mawe katika kilima cha Kabulo kilichopo eneo la Kiwira, Mkoani Songwe mwezi Aprili, 2017. Lengo ni  kukidhi mahitaji ya makaa ya mawe nchini.

78. Mheshimiwa Spika, tangu mradi uanze mwezi Aprili, 2017 hadi kufikia mwezi Machi, 2018, Shirika limezalisha jumla ya tani 8,674 za makaa ya mawe yenye thamani ya shilingi milioni 555.1 na kiasi cha tani 2,827.7 za makaa ya mawe zimeuzwa kwa jumla ya shilingi 180,972,800. Aidha, kiasi cha tani 5,846.30 za makaa ya mawe zimehifadhiwa katika eneo la mgodi wakati jitihada za kutafuta wateja zikiendelea.

79. Mheshimiwa Spika, vilevile, Shirika lilifanya ukarabati wa maabara ya kupima ubora wa makaa ya mawe katika Mgodi wa Kiwira sanjari na matengenezo ya vifaa vya maabara ikiwemo kuweka mfumo mpya wa umeme. Ukarabati huo uligharimu kiasi cha shilingi
7,566,000. Pia, Shirika lilifanya ukadiriaji wa mashapo ya makaa ya mawe katika leseni yake ya utafiti ya Kabulo PL Na. 9963/2014 iliyopo wilayani Ileje, Mkoa wa Songwe ambapo ukadiriaji huo umeonesha uwepo
wa tani milioni 300 za makaa ya mawe.

(ii)    Mgodi wa TanzaniteOne

80. Mheshimiwa   Spika,   migodi   ya   Tanzanite iliyopo Mirerani ni pamoja na mgodi unaomilikiwa kwa ubia baina ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Kampuni ya TanzaniteOne Mining Limited (TML). Ipo pia, migodi mingine inayomilikiwa na wachimbaji wazawa wenye leseni za uchimbaji mdogo na wa kati. Uendeshaji wa mgodi baina ya STAMICO na TML umekuwa  na  changamoto  nyingi  zilizosababishwa na kasoro katika Mkataba wa Ubia na Mkataba wa Uendeshaji. Kutokana na kasoro zilizobainishwa na Kamati Maalum ya Spika ya Kuchunguza Uchimbaji na Biashara ya Madini ya Tanzanite, Serikali iliagiza Timu ya Majadiliano ya Serikali kukutana na wamiliki wa TML na STAMICO kujadiliana ili kubaini kasoro hizo na kupendekeza namna bora ya uchimbaji, biashara  na  uendeshaji  wa  mgodi  huo  kwa  lengo la kulinufaisha Taifa kuliko ilivyo sasa. Kufuatia kukamilika kwa majadiliano hayo, Serikali imeagiza Leseni ya Uchimbaji wa Ubia baina ya STAMICO na TML irudishwe Serikalini ili utaratibu mpya uandaliwe utakaowezesha Serikali, TML na mwekezaji wa kimkakati kushirikiana katika uchimbaji, uendeshaji na biashara ya madini ya Tanzanite katika mgodi huo kwa kuzingatia masharti ya Sheria ya Madini, Sura ya
123 kama ilivyorekebishwa na Bunge Mwaka 2017. Aidha, majadiliano na wachimbaji wadogo yanaendelea baina ya Timu ya Majadiliano ya Serikali na wamiliki wa migodi hiyo kwa lengo la kuleta manufaa zaidi kwa Taifa kutokana na madini ya Tanzanite. Vilevile, kwa kutambua umuhimu na upekee wa madini ya Tanzanite duniani kwamba yanapatikana Tanzania tu, Serikali inakamilisha utaratibu wa kuyatangaza madini ya Tanzanite kuwa madini maalum (specified minerals).

Utaratibu wa kuyatangaza utakamilika katika Mwaka huu wa Fedha wa 2017/18.

(iii)      Mgodi wa Dhahabu wa STAMIGOLD

81. Mheshimiwa Spika, Kampuni ya STAMIGOLD ni Kampuni tanzu ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO)  iliyoanzishwa  Oktoba,  2013.  Kampuni hii inamilikiwa kwa ubia kati ya STAMICO asilimia
99.98 na Msajili wa Hazina asilimia 0.02. Kampuni hii ilipewa jukumu la kuendeleza Mgodi wa dhahabu wa STAMIGOLD Biharamulo Mine (SBM) ambao ulirithiwa kutoka kampuni ya Pangea Minerals LTD iliyokuwa mmiliki wa awali kupitia Leseni ya Uchimbaji Mkubwa Na. SML 157/2003.

82. Mheshimiwa Spika, wakati STAMICO inakabidhiwa mgodi huu, gharama za uendeshaji zilikuwa juu ikilinganishwa na mapato yaliyotokana na mauzo ya dhahabu kwa kuwa katika kipindi hicho bei ya dhahabu ilikuwa chini kutokana na mdororo wa uchumi duniani hususan katika Sekta ya Madini. Pamoja na tatizo hilo, Kampuni ilijiendesha kwa hasara na kusababisha deni la takriban shilingi bilioni 64 hadi kufikia mwezi Machi, 2018. Hata hivyo, deni hili linahakikiwa na Vyombo vya Serikali ili kujua uhalali wake na namna ya kuondokana nalo.

83. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwezi Julai,  2017  hadi  Machi,  2018  Mgodi  umezalisha na kuuza jumla ya wakia 3,967.92 za dhahabu na wakia 400.85 za  fedha  zenye  thamani  ya shilingi
11,459,212,821.83. Kutokana na mauzo hayo, Serikali imepokea mrabaha wa shilingi 802,144,897.53.

84. Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine Menejimenti ya Mgodi imeweza kuchukua sampuli 10 za visusu (old tailings) vilivyoachwa mgodini hapo na kupeleka kwenye Maabara ya African Minerals and Geoscience Centre (AMGC) iliyopo Kunduchi, Dar es Salaam ili kuthibitisha kitaalamu kiasi cha dhahabu kilichomo. Kiasi cha visusu kilichopo ni tani 8,600,000. Kwa mujibu wa ripoti ya maabara, visusu hivyo vya dhahabu vina wastani wa gredi ya gramu 1.15 kwa tani ambapo ni sawa na takriban wakia 300,000Vilevile, thamani ya visusu hivyo itatambuliwa kwenye vitabu rasmi kuwa ni mali ya Kampuni kwa ajili ya kumbukumbu na udhibiti wa mali hiyo.

(iv)      Mradi wa Dhahabu wa BUHEMBA

85. Mheshimiwa Spika, Mradi wa Dhahabu wa Buhemba uliopo Wilaya ya Butiama, Mkoa wa Mara unahusisha uchenjuaji wa mabaki ya mchanga wa dhahabu na uchimbaji wa dhahabu katika miamba migumu. Katika Mwaka wa Fedha wa 2017/18, Shirika limeendelea na utafiti kwa lengo la kuendelea kubaini kiasi kingine cha mashapo ya dhahabu kilichopo katika miamba ambapo kazi zilizofanyika zilihusisha uchorongaji wa miamba.

(v)        Mradi wa Dhahabu wa BUCKREEF

86. Mheshimiwa Spika, Mgodi wa Buckreef unamili- kiwa kwa Ubia kati ya STAMICO na Kampuni ya TANZAM 2000 kwa asilimia 45 kwa 55. Katika Mwaka wa Fedha wa 2017/18, STAMICO kwa kushirikiana na Wizara ya Madini na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inaupitia upya mkataba wa ubia. Hii ni kutokana na mbia kuchelewa kuanza uzalishaji kwa

mujibu wa makubaliano ya Mkataba.  Pia, STAMICO kwa kushirikiana na mbia mwenza ilifanya tathmini ya maeneo yanayofaa kuachiwa kwa wachimbaji wadogo katika maeneo ya leseni za utafiti Namba PL 6430/2010 (Lwamgasa West); PL 6549/2010 (Nyamalimbe 2); na PL
6547/2010 (Lwamgasa South 2). Matokeo ya tathmini hiyo yalibainisha kuwa maeneo hayo yanafaa kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Utaratibu unaandaliwa wa kuyaachia maeneo hayo kwa wachimbaji wadogo.

(vi)   Mradi wa Kokoto - Ubena Zomozi

87. Mheshimiwa Spika, Shirika lilifanya utafiti wa wingi na ubora wa miamba katika leseni zake kumi (10) za uchimbaji kokoto zilizopo Ubena Zomozi, mkoani Pwani. Utafiti huo ulibaini uwepo wa miamba yenye kiasi cha mashapo yanayokadiriwa kufikia tani milioni 41.5 za kokoto zinazoweza kuchimbwa kwa zaidi ya miaka 50. Shirika linaendelea na taratibu za kutafuta fedha au kumpata mbia kwa ajili ya mradi huo.

(vii)  Huduma kwa Wachimbaji Wadogo

88. Mheshimiwa Spika, Shirika kwa kushirikiana na Wizara  limeendelea kusimamia ujenzi wa Mgodi wa Mfano katika eneo la Lwamgasa kwa ajili ya wachimbaji wadogo, ambapo hadi kufikia Machi, 2018, ujenzi wa shimo la uchimbaji (mining shaft) na usimikaji wa mitambo ya kuchenjulia dhahabu umefikia asilimia 70 (Tazama Picha Na.10 na 11). Mgodi huu utawanufaisha wachimbaji wadogo katika eneo hilo kwa kuwawezesha kujifunza teknolojia sahihi ya uchimbaji na uchenjuaji wa madini. Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) ulihusika kufanya upembuzi yakinifu katika eneo la

mgodi wa mfano. Aidha, hadi sasa Mradi wa SMMRP umeshatumia jumla ya Dola za Marekani 293,881.2 katika ujenzi wa mgodi huo wa mfano.

(e)       Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia – (TEITI)


89. Mheshimiwa Spika, Tanzania ni Mwanachama wa Mpango wa Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (Extractive Industry Transparency Initiative) tangu mwaka 2009. Katika kutekeleza mpango huo, Serikali ilianzisha Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI) chini ya Sheria ya TEITA ya Mwaka 2015. Taasisi hii ina jukumu la kuhamasisha Serikali kuweka mifumo ya uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia ili kuongeza mapato na manufaa yatokanayo na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa rasilimali hizo.


90. Mheshimiwa Spika, Taasisi hii pia ina jukumu la kuwajengea uwezo wananchi katika kutumia takwimu zinazotokana na shughuli za uendeshaji wa kampuni za madini, mafuta na gesi asilia kwa kuhoji na kuhamasisha mijadala kuhusu manufaa ya shughuli za rasilimali madini; utoaji wa leseni na mikataba, uchimbaji wa madini, mafuta na gesi asilia; usimamizi na uendeshaji wa kampuni za madini, mafuta na gesi asilia; ukusanyaji wa mapato yatokanayo na madini, mafuta na gesi asilia; na mgawanyo wa mapato na matumizi yake.

91. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2017/18, TEITI ilikamilisha na kutoa kwa umma ripoti ya ulinganisho (Reconciliation report) wa malipo yaliyolipwa na Kampuni za madini, mafuta na gesi asilia  na  mapato  yaliyopokelewa  na  Serikali  kwa

Mwaka wa Fedha wa 2015/16. Ripoti hiyo ambayo ni ya 8 imewasilishwa kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa ajili ya uchunguzi. Aidha, TEITI  ilikamilisha  muhtasari  wa  takwimu  za  ripoti hiyo zilizowekwa katika vielelezo (Inforgraphics) kwa lugha ya kiswahili na kiingereza. Lengo ni kurahisisha ufikishaji wa matokeo ya ripoti za TEITI kwa wadau na kujenga uwezo wa wananchi katika kutumia takwimu zinazotokana na shughuli za uendeshaji wa kampuni, kuhoji Serikali na kuhamasisha mijadala kuhusu uongezaji wa manufaa ya uchimbaji madini, mafuta na gesi asilia nchini.

(f )     Kituo cha Jimolojia Tanzania – (TGC)


92. Mheshimiwa  Spika,  Kituo  cha  Jimolojia Tanzania (TGC) kina majukumu ya kutoa mafunzo ya uongezaji thamani madini na miamba na utengenezaji wa bidhaa za urembo na mapambo kwa kutumia miamba (Tazama Picha Na. 12). Kituo kinatoa mafunzo katika fani za usanifu wa madini ya vito, usonara na uchongaji vinyago vya miamba.
Kazi zilizotekelezwa na Kituo hiki ni pamoja na uchongaji wa vinyago 69 vya miamba;    kutengeneza marumaru (tiles) za ukutani 250, table mats 80; tiles kubwa 100 kutokana na mawe ya Tanga  (Tanga stones/slates); kutengeneza bidhaa mbalimbali za mapambo kwa kutumia mawe ambazo ni vikuku (bracelets)   50, hereni 65, mikufu 89, vidani 120 na pete 60; kung’arisha sampuli za madini ya tanzanite za ubora wa chini (reject) za uzito wa kilo 6 kutoka kwa watu mbalimbali; kukata na kusanifu madini ya vito ya taasisi na watu mbalimbali. Kiasi cha madini kilichokatwa na kusanifiwa ni gramu 20 za madini ya tanzanite; gramu 30 za amethyst; na gramu 300 za quartzred aventurine. Pia, TGC imeendelea kutoa mafunzo ya ukataji na ung’arishaji wa madini ya vito ambapo wanafunzi 38 walidahiliwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai, 2017 hadi Mei, 2018. Vilevile, kabla ya Julai, 2017 wanafunzi 65 walikuwa wamedahiliwa na kupata mafunzo ya aina hiyo.



4.0   MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA WA FEDHA WA 2018/19


93. Mheshimiwa Spika, Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19 umezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 - 2020; Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21); Malengo Endelevu ya Maendeleo 2030; Ahadi za Serikali Bungeni za Mwaka wa 2017/18; Mwongozo wa Kutayarisha Mpango na Bajeti wa Mwaka wa Fedha wa
2018/19; Maagizo ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa kwa nyakati tofauti; Ushauri na Maoni ya Kamati Maalum zilizoundwa na Mheshimiwa Rais kama zilivyoainishwa katika aya ya 12 na ushauri uliotolewa na Bunge pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa nyakati tofauti, na Ushauri wa Kamati Maalum za Mheshimiwa Spika.

94. Mheshimiwa Spika, kazi zilizopangwa kuteke- lezwa kwa Mwaka wa Fedha   wa 2018/19 na Wizara ya Madini na Taasisi zake ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa Mapato ya Serikali yatokanayo na rasilimali madini; kuwaendeleza wachimbaji wadogo na wa kati wa madini; kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani  madini;  kuimarisha  ufuatiliaji  wa  ukaguzi wa usalama, afya, mazingira na uzalishaji wa madini katika migodi midogo, ya kati na mikubwa; kuendelea kuhamasisha uwekezaji katika miradi ya kimkakati ya Sekta ya Madini; kuendelea kuboresha mazingira ya kuwawezesha wananchi kufaidika na rasilimali madini; kuelimisha Umma na kuboresha mawasiliano

kati ya Wizara na wadau mbalimbali kuhusu masuala ya madini;  kusimamia, kufuatilia na kuboresha Sera, Sheria,  Kanuni,  Mikakati  na  Miongozo  mbalimbali ili kuleta ufanisi na tija katika Sekta ya Madini; kuendeleza rasilimali watu na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi; na kuwezesha Taasisi  zilizo chini ya Wizara.

(a)    Kuimarisha Ukusanyaji wa Mapato ya
Serikali yatokanayo na Shughuli za Madini


95. Mheshimiwa    Spika,    Wizara    itaendelea kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli yatokanayo na shughuli za madini ambapo kwa Mwaka wa Fedha wa
2018/19lengonikukusanyaShilingi310,598,007,000, ikiwa ni ongezeko la asilimia 59.57 ikilinganishwa na Shilingi 194,663,501,763 zilizopangwa kukusanywa kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18. Katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali yanayotokana na shughuli za madini, Wizara inatarajia kuimarisha ukaguzi wa migodi mikubwa, ya kati na ya uchimbaji mdogo ili kupata taarifa sahihi za uwekezaji, uzalishaji, mauzo na kodi mbalimbali; kudhibiti utoroshwaji wa madini katika maeneo ya uzalishaji na kutokea nchini (Exit Points); kuimarisha ukaguzi wa madini ya ujenzi na viwandani; kufuatilia taarifa za ununuzi na uuzaji (returns) kwa wafanyabiashara wa madini (Dealers & Brokers); kufuatilia wadaiwa wa tozo mbalimbali za madini kwa mujibu wa Sheria kwa wakati; kudhibiti uchimbaji na uchenjuaji haramu wa madini; na kuboresha na kuimarisha mfumo wa kutoa leseni za madini na kutunza taarifa zake.

96. Mheshimiwa  Spika,  natoa  rai  kwa  wamiliki wa leseni za madini kuacha kukwepa au kuchelewa kulipa kodi, kulipa mrabaha stahiki na tozo nyingine zilizopo kwa mujibu wa Sheria za nchi. Kwa wale watakaobainika kukiuka matakwa ya kisheria, Serikali itawachukulia hatua kali  ikiwa ni pamoja na kufuta leseni zao na kuwafikisha mahakamani.

(b)    Kuwaendeleza Wachimbaji Wadogo wa
Madini

97. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mpango wa kuwaendeleza wachimbaji wadogo, Wizara itaendelea kutenga maeneo yanayofaa ambapo jumla ya maeneo
4 yanatarajiwa kutengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Aidha, GST itabainisha uwepo wa mashapo ya madini katika maeneo yatakayotengwa. Vilevile, Wizara kupitia STAMICO, itawaelimisha  wachimbaji wadogo namna ya kutumia teknolojia ya kisasa na rahisi katika kuongeza uzalishaji na tija wakati wa uchimbaji na uchenjuaji wa madini. Pia, Wizara kupitia mradi wa SMMRP itajenga Vituo vya Mfano 4 ambavyo ni Katente (Bukombe); Itumbi (Chunya); Kona Z (Tanga);  na Lindi. Vituo hivyo vitatumika kwa ajili ya mafunzo ya uongezaji thamani madini, uchimbaji salama pamoja na kuongeza uzalishaji na tija na hivyo kuongeza mapato kwa wachimbaji wadogo. Vituo hivi pia vinatarajiwa kutoa huduma za uchenjuaji wa madini kwa wachimbaji wadogo.

(c)     Kuhamasisha Shughuli za Uongezaji
Thamani Madini

98. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka wa Fedha wa 2018/19, Wizara itaendelea kuhamasisha uwekezaji katika shughuli za uongezaji

thamani madini na kuendelea kutoa leseni za uchenjuaji na uyeyushaji wa madini ya metali. Pia, Wizara itakamilisha kazi ya kuwapata wawekezaji katika Vinu vya uchenjuaji na usafishaji wa madini. Aidha, Wizara itaandaa  Muswada wa Sheria ya Uongezaji Thamani Madini  ili  kukuza  na  kusimamia  vyema  shughuli za uongezaji thamani madini nchini. Viwanda vya uyeyushaji, usafishaji wa madini na shughuli nyingine za uongezaji thamani zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali, kuongeza ajira na kukuza matumizi ya teknolojia nchini.

99. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa madini ya vito, Wizara itaendelea kukiimarisha Kituo cha Jimolojia Tanzania ili kiweze kutoa wataalam kwenye fani za ukataji na ung’arishaji wa madini ya vito, jimolojia na usonara watakaosaidia kufanya shughuli za uongezaji thamani madini hayo hapa nchini.

(d)       Kuimarisha Ukaguzi wa Usalama, Afya, Mazingira na Uzalishaji wa Madini Migodini


100. Mheshimiwa Spika, shughuli za uchimbaji wa madini zinapaswa kusimamiwa kwa karibu kwani huweza  kuambatana  na  athari  za  kiafya,  usalama na uharibifu mkubwa wa mazingira.  Ili kuondokana na athari hizo, Wizara itaendelea kuimarisha kaguzi migodini na maeneo ya uchenjuaji wa madini, kuongeza huduma za ugani hususan kwa wachimbaji wadogo, kuimarisha ushirikiano na taasisi nyingine za Serikali zinazohusika na usimamizi wa masuala ya Afya, Usalama na Utunzaji wa Mazingira katika kufanya kaguzi mbalimbali migodini ikiwemo utekelezaji wa Mkataba wa Minamata wa kupunguza na hatimaye kuzuia  matumizi  ya  Zebaki  katika  uchenjuaji.  Pia,

Wizara itaendelea kukagua na kuhakiki kiasi na ubora wa madini yanayozalishwa na migodi mikubwa, ya kati na midogo.

101. Mheshimiwa   Spika,   nitoe   rai   kwa wachimbaji wa madini na wale wanaofanya shughuli za uchenjuaji hususan madini ya dhahabu kuhakikisha wanaimarisha miundombinu ya mabwawa ya kuhifadhi mabaki  yenye  kemikali  (Tailings  Storage  Facility  – TSF)  kwa  mujibu  wa  Sheria  ya  Madini  ya  Mwaka
2010 kama ilivyofanyiwa marekebisho Mwaka 2017. Pia, Wachimbaji Wakubwa na wa Kati wahakikishe wanawasilisha Mpango wa Ufungaji Migodi kwa wakati kama ilivyoainishwa katika Kanuni ya 206 ya Kanuni za Madini kuhusiana na Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira za Mwaka 2010. Wachimbaji wakubwa na wa kati wanapaswa pia kuweka Hati Fungani ya Uhifadhi wa Mazingira (Environmental Rehabilitation Bond) kama ilivyoainishwa katika Kanuni ya 207 ya Kanuni za Madini kuhusiana na Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira za Mwaka 2010.

102. Mheshimiwa  Spika, Wizara  yangu  kupitia STAMICO  imekuwa  ikishiriki  kwenye  uwekezaji katika madini mbalimbali. Katika kutekeleza jukumu hilo,   STAMICO   imetengewa   kiasi   cha   shilingi
8,600,000,000 kwa ajili ya kuendeleza Mradi wa Dhahabu wa Buhemba wa kuchenjua visusu. Pia, STAMICO itaendelea kutafuta fedha kutoka taasisi mbalimbali za kifedha na wabia kwa ajili ya kuendeleza miradi ya Makaa ya Mawe ya Kiwira na Kabulo; Uchimbaji na Uuzaji wa  Kokoto wa Ubena Zomozi (Pwani) na Chigongwe (Dodoma). Vilevile, STAMICO itaendelea kuimarisha usimamizi wa Mradi wa Ubia wa TanzaniteOne na Kampuni Tanzu ya STAMIGOLD;

kuimarisha biashara ya shughuli za uchorongaji na utoaji wa ushauri wa kitaalam katika Sekta ya Madini; na kuratibu uboreshaji na uendelezaji wa shughuli za wachimbaji wadogo nchini.

(e)       Kuendelea Kuboresha Mazingira ya Kuwawezesha Wananchi Kunufaika na Shughuli za Madini


103. Mheshimiwa  Spika,    Sera  ya  Madini  ya Mwaka 2009 na Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 pamoja na Marekebisho yake ya Mwaka 2017 zinatoa mwongozo wa namna Kampuni za madini zinavyopaswa kufungamanisha Sekta ya Madini na sekta nyingine za kiuchumi. Wizara itasimamia Sheria katika kukuza ushiriki wa Watanzania (local content) kwenye shughuli za utafutaji, uchimbaji,   biashara ya madini nchini na Uwajibikaji wa Kampuni za Uchimbaji Madini kwa Jamii (Corporate Social Responsibility - CSR).

104. Mheshimiwa  Spika,   katika  Kifungu  cha
102 cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 pamoja na Marekebisho yake ya Mwaka 2017, maombi ya leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini yanapaswa kuambatana na Mpango wa Matumizi ya Bidhaa na Huduma za Ndani katika maombi ya leseni husika. Iwapo bidhaa hizo hazipatikani ndani ya nchi, bidhaa hizo  zinapaswa  zipatikane  kwa  kutumia  Kampuni ya ndani ya nchi iliyoingia ubia na Kampuni ya nje. Mmiliki wa Leseni anapaswa kuwasilisha katika Tume ya Madini taarifa inayoonesha matumizi ya bidhaa na huduma za ndani ya nchi katika kipindi cha siku
60 baada ya kuisha kwa mwaka wa kalenda. Wizara itaendelea kusimamia Kampuni hizo ili kuhakikisha kuwa Kifungu hicho cha Sheria kinatekelezwa.

105. Mheshimiwa    Spika,     vilevile,    Wizara itaendelea kushirikisha jamii katika shughuli za kiuchumi ambazo jamii inaweza kuzimudu.  Katika Kifungu  cha  105  cha  Sheria  ya  Madini  ya  Mwaka
2010 pamoja na Marekebisho yake ya Mwaka 2017, kinamtaka kila mmiliki wa leseni ya uchimbaji wa madini, uchenjuaji, uyeyushaji na usafishaji wa madini kuandaa Mpango wa Mwaka wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii. Mpango huo unapaswa kuwasilishwa kwa Mamlaka za Serikali za Mtaa husika kwa rejea na idhini. Nawasihi Viongozi katika kila Halmashauri kuandaa Miongozo ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii na kusimamia utekelezaji wake. Vilevile, Halmashauri zinapaswa kuwaelimisha wananchi katika maeneo yao kuhusiana na Mipango ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii.

106. Mheshimiwa Spika,  natoa rai kwa Mamlaka nyingine  za  Serikali  hususan  Mamlaka  ya  Serikali za Mitaa kushiriki kuziandaa jamii zilizopo katika maeneo ya migodi kushirikiana na Kampuni za madini ili kufanikisha malengo ya mipango hiyo.

(f )       Kuelimisha Umma na Kuboresha Mawasiliano baina ya Wizara na Wadau wa Sekta ya Madini


107. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu itafanya mikutano ya ana kwa ana na wawekezaji na itatoa elimu kwa umma kuhusu rasilimali madini. Kwa kutambua hilo, kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19 Wizara yangu itatoa elimu kwa umma kuhusu rasilimali madini, uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini kupitia vipindi mbalimbali vya redio na televisheni; majarida na machapisho mbalimbali; tovuti; mitandao ya kijamii ya Wizara; na kushiriki katika maonesho mbalimbali

ya kitaifa na kimataifa na kupitia njia nyingine za upashanaji habari kwa umma. Lengo ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata   elimu ya kina kuhusu masuala ya rasilimali madini.

(g)      Kusimamia na Kuboresha Sera, Sheria, Kanuni, Mikakati na Miongozo

108. Mheshimiwa  Spika, Wizara  itafanya  mapitio ya Sera ya Madini ya Mwaka 2009 na kuandaa Sera ya Uongezaji Thamani Madini na Dira ya Taifa ya Kuendeleza Sekta ya Madini (Tanzania Mining Vision
2019 - 2035). Vilevile, Wizara itaandaa Muswada wa kutunga Sheria ya Uongezaji Thamani Madini na Kanuni zake. Aidha, Wizara itaandaa Miswada ya Marekebisho ya Sheria zifuatazo:

(i)        Sheria ya Baruti ya Mwaka 1963 na Kanuni zake za Mwaka 1964;

(ii)    Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali
Madini, Mafuta na Gesi Asilia ya Mwaka 2015; na

(iii)   Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017.

(h)      Kuendelea Kuvutia Wawekezaji Wakubwa kwenye Sekta ya Madini


109. Mheshimiwa Spika, Katika Mwaka wa Fedha wa 2018/19, Serikali itaendelea kuvutia wawekezaji kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji kwa wadau kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo katika Sekta ya Madini ikiwemo kuandaa Jukwaa la Wawekezaji katika Sekta ya Madini (Tanzania Mining Forum); kuwezesha upatikanaji  wa  taarifa  za  kijiolojia  zinazohitajika

katika shughuli za utafutaji wa madini na kushiriki kwenye mikutano na warsha za ndani na nje ya nchi zinazohusu shughuli za madini.

(i)     Kuboresha Utoaji na Usimamizi wa Leseni za
Madini


110. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2018/19, Wizara yangu itaendelea kuboresha Mfumo wa Kielektroniki wa Utoaji na Usimamizi wa Leseni za Madini ili kuendana na Marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 yaliyofanyika Mwaka
2017 na Kanuni zake. Pia, Wizara kupitia Tume ya Madini  itaendelea  kushughulikia  maombi  ya  leseni za madini kwa wakati na kuhakikisha kuwa maombi yote yanayowasilishwa yanashughulikiwa na kujibiwa mapema iwezekanavyo. Aidha, Wizara itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017 kwa kufuta leseni zote zinazokiuka matakwa ya Sheria hiyo ili kutoa nafasi kwa wawekezaji wengine wenye uwezo wa kuyaendeleza na maeneo mengine zaidi kutengwa kwa wachimbaji wadogo.

(j)        Mipango itakayotekelezwa kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini – SMMRP


111. Mheshimiwa Spika, kazi zilizopangwa kuteke- lezwa na Mradi wa SMMRP kwa kipindi cha Mwaka wa Fedha wa 2018/19 ni pamoja na: kuanza ukarabati na upanuzi wa majengo ya Ofisi 7 za Madini ili zitumike kama vituo vya umahiri vya masuala ya madini. Ofisi hizo ni Mpanda, Songea, Chunya, Tanga, Bariadi, Bukoba na Musoma. Vilevile, Mradi utagharimia upanuzi wa

miundombinu  ya  Chuo  cha  Madini  (Dodoma)  kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa shughuli za madini zinazotekelezwa na WIMA; kuendelea kukamilisha ujenzi wa Mgodi wa Mfano Lwamgasa - Geita kwa ajili ya wachimbaji wadogo na kusimika mitambo ya uchenjuaji; na kuiwezesha TEITI kutengeneza mfumo wa kuunganisha na kuzijumuisha pamoja taarifa za malipo na za uchimbaji mdogo, wa kati na mkubwa.

(k)       Kuendeleza Rasilimali Watu, Kuboresha Mazingira ya Kufanyia Kazi na Kuziwezesha Taasisi zilizo Chini ya Wizara


112. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majuk- umu yaliyopangwa, Wizara itahakikisha inajenga ujuzi wa watumishi kwenye nyanja mbalimbali na itaboresha mazingira ya kazi, na kuwapatia vitendea kazi bora na kwa wakati. Aidha, watumishi watapatiwa elimu kuhusu afya bora, uadilifu, rushwa na madhara yake katika utumishi wa umma na Taifa kwa ujumla.

113. Mheshimiwa  Spika kwa  kuzingatia  kuwa Wizara ya Madini ni mpya katika Mwaka wa Fedha wa 2018/19 Wizara na Taasisi zake inatarajia kuajiri jumla ya watumishi 314 wa kada mbalimbali ikiwemo Wahandisi Migodi; Wajiolojia; Maafisa Rasilimali Watu; Wakufunzi wa fani za Madini; Mafundi Sanifu; Madereva na Makatibu Mahsusi. Kati ya hao, watumishi 208 ni kwa ajili ya Wizara, 28 kwa ajili ya GST na 78 ni kwa ajili ya Chuo cha Madini.

114. Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea   kutoa elimu kuhusu masuala ya UKIMWI; na kuendelea kuwahudumia watumishi wenye ulemavu na wanaoishi na  virusi  vya  UKIMWI  na  UKIMWI.  Aidha,  Wizara

itaendelea  kuwahamasisha  watumishi  kupima  afya zao ili kutambua hali za afya zao ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi mara kwa mara.

KAZI ZITAKAZOTEKELEZWA NA TAASISI ZILIZO CHINI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA WA 2018/19

(i)     Tume ya Madini


115. Mheshimiwa    Spika,    kazi    zilizopangwa kutekelezwa na Tume ya Madini kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19 ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa Mapato yatokanayo na rasimali madini; kutathmini na kushughulikia changamoto katika utekelezaji wa Sheria ya Madini   ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017; kutoa Mwongozo wa namna ya kutoa vibali vya kusafirisha madini nje ya nchi; kuimarisha ufuatiliaji wa ukaguzi wa usalama, afya, mazingira, utafutaji na uzalishaji wa madini katika migodi midogo, ya kati na mikubwa; kuimarisha mfumo wa kielekroniki wa kutoa na kusimamia taarifa za leseni za madini ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa leseni na kuondoa migogoro inayotokana na leseni za madini; kuimarisha udhibiti wa utoroshwaji wa madini nje ya nchi; kuimarisha  shughuli za uongezaji thamani madini; kuimarisha usimamizi wa biashara ya madini na kushughulikia migogoro yote inayotokana na shughuli za madini.

(ii)    Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini
Tanzania – (GST)


116. Mheshimiwa Spika, GST inatarajia kutekeleza shughuli zifuatazo kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19:

kuboresha Kanzidata ya miamba na madini ya Taifa ili kuongeza uelewa wa jiolojia ya nchi na ya upatikanaji wa madini mbalimbali nchini ili kuchochea uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini; kuratibu shughuli za utafutaji na uchimbaji madini nchini kwa kupitia taarifa za robo mwaka za shughuli hizo ili kuhakiki usahihi wa taarifa hizo na kuboresha Kanzidata ya Taifa ya madini; kufanya uchunguzi wa sampuli za madini na miamba ili kujua viwango vya madini kwenye sampuli zinazokusanywa na watafiti na watafutaji madini kwa ajili ya kutoa  idhini ya maandishi  ya kusafirisha sampuli hizo nje ya nchi; kuwaendeleza wachimbaji wadogo kwa kufanya tafiti za kijiosayansi katika utafutaji, uchimbaji salama, uhifadhi wa mazingira na uchenjuaji ili kuongeza tija katika uzalishaji; kuboresha huduma za maabara  kwa wadau wa Sekta ya  Madini,  Kilimo  na  Ujenzi;  kuboresha  Kanzidata ya majanga asilia ya jiolojia na kuelimisha wananchi kuhusu namna bora ya kujikinga na majanga hayo; kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya GST kutoka katika vyanzo vyake mbalimbali; kuendeleza rasilimali watu na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi.

(iii)   Chuo cha Madini – (MRI)


117. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2018/19, MRI inategemea kutekeleza shughuli zifuatazo: kuendelea na Mpango wa kukiimarisha Chuo cha Madini;   kuendelea kutoa mafunzo kwa wanafunzi ambapo udahili wa wanafunzi wapya unatarajiwa kuongezeka kutoka wanafunzi 542 hadi
850; kuangalia uwezekano wa kuanzisha kozi mpya kwenye maeneo yanayohusiana na uchimbaji mdogo, madini ya vito na madini ya viwandani; kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya Chuo kwa kujenga jengo

la wakufunzi ambalo litakuwa na ofisi za wakufunzi pamoja na Ofisi za WIMA; na kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalam.

(iv)    Shirika la Madini la Taifa – (STAMICO)


118. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2018/19, STAMICO imepanga kuendeleza Mradi wa Dhahabu wa Buhemba kwa kuanza kuchenjua visusu; kufanya uchorongaji ili  kujiridhisha na kiasi cha mashapo kilichopo; kufanya topographic survey ya eneo zima la mradi; na ununuzi na usimikwaji wa vifaa vya  uchimbaji na uchenjuaji pamoja na shughuli za uendelezaji wa mradi. STAMICO pia itaendeleza Mradi wa Kiwira wa kuchimba makaa ya mawe katika kilima cha Kabulo.  Aidha, ili kufanikisha lengo la kuzalisha makaa ya mawe yatakayokidhi mahitaji ya soko, Shirika linatarajia kutafuta mtambo wa kusafisha makaa ya mawe (washing plant) katika Mradi wa Kabulo ikiwa ni sambamba na  kununua mtambo wa kusaga makaa (crusher)  hayo, kulingana na vipimo vya mteja husika. Vilevile, STAMICO inatarajia kuanza Mradi wa kuchimba kokoto katika eneo la Ubena Zomozi mkoani Pwani.  Shirika pia litaendelea kuimarisha shughuli za kibiashara za uchorongaji na utoaji wa ushauri wa kitaalam katika Sekta ya Madini   na kuratibu uendelezaji wa wachimbaji wadogo nchini.

(v)        Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia – (TEITI)


119.  Mheshimiwa Spika, kazi zitakazotekelezwa na TEITI kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19 ni pamoja na kutoa kwa umma ripoti ya malipo ya kodi yaliyofanywa

na kampuni za madini, mafuta na gesi asilia kwa Serikali kwa kipindi cha Mwaka wa Fedha wa 2016/17; kuendelea kuelimisha umma kuhusu matumizi ya takwimu  zinazotolewa  katika  ripoti  za  TEITI  kwa njia ya matangazo, vipindi vya Redio na Televisheni, makala pamoja na  warsha; kufanya marekebisho ya dosari zilizobainishwa katika tathmini ya utekelezaji wa masharti ya uanachama wa EITI ili kutimiza vigezo vya uwazi vya kimataifa vya EITI vya Mwaka 2016; na kuanzisha Rejista ya taarifa na majina ya watu wanaomiliki hisa katika kampuni za madini, mafuta na gesi asilia.

(vi)    Kituo cha Jimolojia Tanzania – (TGC)


120.   Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2018/19, Kituo cha Jimolojia Tanzania kinatarajia kutekeleza yafuatayo: kuanza kutoa mafunzo ya Stashahada ya teknolojia ya Vito na Usonara (Diploma in  Gem  and  Jewellery  Technology) kutoa  mafunzo ya muda mfupi katika fani za Jimolojia; Gem and Jewellery Appraisal; Gem and Jewellery Marketing; Gemstone  Faceting;  Cabochon  Cutting;  Utengenezaji wa bidhaa za usonara; na uchongaji wa vinyago vya miamba. Kituo pia kitaendelea na shughuli za ukataji na ung’arishaji wa madini ya vito ya wateja mbalimbali yanayowasilishwa kituoni; utengenezaji wa marumaru za mawe ya Tanga (Tanga stones/slates); pamoja na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za usonara na mapambo kama vile mikufu, hereni, bangili, vidani, vikuku na pete kwa kutumia madini mbalimbali.

5.0  SHUKRANI


121.   Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2017/18, Wizara ya Madini ilinufaika kwa misaada na ushirikiano kutoka kwa Washirika mbalimbali wa Maendeleo. Naomba nitumie fursa hii kuwashukuru washirika wetu wote wa maendeleo ikiwa ni pamoja na Benki ya Dunia, Umoja wa Nchi za Ulaya,  Serikali za Jamhuri ya Watu wa China,  Kanada, Marekani, Jamhuri  ya  Watu  wa  Korea  Kusini,  Misri,  Japan na Australia. Serikali itaendelea kushirikiana na washirika hao na wadau wengine wa maendeleo katika kuendeleza Sekta ya Madini nchini.

122.  Mheshimiwa Spika,   pia, naomba kutoa Shukrani kwa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)-Taifa, UWT  Mkoa wa Dar es Salaam, Viongozi  na  Wanachama  wote  wa  CCM  na  UWT kwa kushirikiana nami na kuendelea kuniamini. Nawashukuru pia, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi kwa kuniamini kuwa mwakilishi wao katika Bunge na kwa ushirikiano wanaonipatia. Vilevile, naishukuru familia yangu kwa ushirikiano wanaonipatia katika kutekeleza majukumu yangu.

123.  Mheshimiwa Spika, niwashukuru Manaibu wangu Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo (Mb.) na Mheshimiwa Doto Mashaka Biteko (Mb.) kwa ushirikiano wao thabiti katika kusimamia utekelezaji wa shughuli za Wizara. Aidha, nawashukuru Katibu Mkuu, Profesa Simon Samwel Msanjila, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Suleiman Kikula, Makamishna  wote  wa  Tume  ya  Madini,  Kamishna wa Madini na Makamishna Wasaidizi, Wakurugenzi, Wakuu wote wa Idara na Vitengo, Viongozi wa Taasisi

zilizo chini ya Wizara wakiwemo Wenyeviti, Wajumbe wa  Bodi  na  Watendaji  Wakuu  na  Watumishi  wote kwa ushirikiano wao na kuhakikisha kuwa  rasilimali madini zinanufaisha wananchi na Taifa kwa ujumla. Vilevile, ninalishukuru Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania chini ya uongozi mahiri wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance S. Mabeyo kwa kujitolea katika ujenzi wa ukuta wa Mirerani na kwa ulinzi wanaoutoa katika ulinzi wa ukuta huo.


6.0  HITIMISHO


124. Mheshimiwa Spika, Sekta ya Madini ni muhimu katika kukuza uchumi na kutoa mchango mkubwa kwa Taifa na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka
2025. Aidha, ili kuhakikisha Sekta hii inainufaisha Nchi  ipasavyo,  Wizara  itaimarisha  usimamizi  wake na kudhibiti utoroshwaji wa madini. Vilevile, Wizara itaendelea  kuhamasisha  uwekezaji  katika  shughuli za utafutaji, uchimbaji na uongezaji thamani madini nchini ili kuongeza mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa.

Maombi ya fedha kwa kazi zilizopangwa kutekelezwa kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19

125. Mheshimiwa  Spika, baada ya kueleza kwa kina utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18 na Mpango na Bajeti ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19, sasa naliomba Bunge lako Tukufu likubali na kuidhinisha mapendekezo yBajetyFung10lWizaryMadinyjumlykiasi cha Shilingi 58,908,481,992  kwa  ajili  ya  matumizi ya  Wizara  na  taasisi  zake  kwa  Mwaka  wa  Fedha wa 2018/19. Mchanganuo wa Bajeti hiyo ni kama

ifuatavyo:-
(i)           Bajeti ya Maendeleo ni Shilingi 19,620,964,000: Kati ya fedha hizo, Shilingi 16,800,000,000 ni fedha za ndani na Shilingi 2,820,964,000 ni fedha za nje; na

(ii)       Bajeti  ya  Matumizi  ya  Kawaida  ni  Shilingi
39,287,517,158,          ambapo           Shilingi
18,334,255,000  ni  kwa  ajili  ya  Mishahara na Shilingi 20,953,262,992 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (OC).

126. Mheshimiwa Spika, naomba tena nitoe shukrani zangzdhatkwWaheshimiwWabungwotkwa kunisikilizaHotubhiinapatikankatika Tovutya Wizara    kw anuan ya   www.madini.go.tz Vilevile, Hotubhiinmajedwalnvielelezmbalimbalkwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa masuala na takwimu muhimu kuhusu Sekta ya Madini.

127 Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.



Comments