Featured Post

WANAOPINGA MAENDELEO WANA WIVU KAMA MASHETANI



*Asema Tanzania imechelewa sana, lazima isonge mbele

Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli, amesema watu wanaopinga maendeleo yanayofanywa na serikali yake wana wivu na kwamba hawana tofauti na mashetani.
akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa usimikaji wa radar nne za kuongozea ndege jijini Dar es Salaam Jumatatu, Aprili 2, 2018, Dkt. Magufuli alisema kwamba, watu wanaopinga jitihada za serikali wanaumia, lakini hilo haliwezi kumfanya yeye na serikali yake wasiwaletee Watanzania maendeleo.
"Nchi hii uwezo wake sasa ni mkubwa mno, ni wa maajabu. Ndiyo maana watu wengine wenye wivu wivu hivi wanaumia sana. Na wenye wivu wapo tu, hata Mungu aliumba malaika pakatokea wenye wivu mashetani yakagoma yakatupwa huku duniani. Nayo lazima yawe na wafuasi fuasi wa aina fulani wenye wivu wivu," alisema.

Awali, Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, alisema makataba wa mradi wa kusimika radar nne uliingiwa tangu Agosti 22, 2017 baina ya Serikali na Kampuni ya Ufaransa ambao utagharimu jumla ya Shs. 77.3 bilioni ambapo Mamlaka ya Usafirishaji wa Anga (TCAA) itagharamia 45% na Serikali Kuu itagharimia 55%.
"Mradi huu umezingatia uendelevu hivyo umeweka dhamana ya miaka 3 ili kuhakikisha mkandarasi analeta vipuri endapo hitilafu yoyote itatokea. Pia mkandarasi atahakikisha vipuri vinapatikana kwa miaka 12 baada ya hapo," alisema Prof. Mbarawa.
Profesa Mbarawa aliipongeza TCAA kwa matokeo mazuri ya ukaguzi wa kimataifa wa ICAO (International Civil Aviation Organization) wa viwango vya udhibiti wa kiusalama wa anga.
"Matokeo yameonyesha Tanzania imepanda katika viwango vya Udhibiti wa Kiusalama wa Anga kutoka 37.8% za 2013 hadi 64.35% za 2017," alisema Prof. Mbarawa.
Lakini Dkt. Magufuli alisema kwamba, pamoja na jitihada hizo, kuna watu wanaonyesha wazi kwamba hawafurahishwi na wamekuwa wakifanya kila njia kupinga mambo yote mema yanayofanyika.
"Kwa sababu ni maajabu kwa nchi kama hii Tanzania ambayo katika miaka mingi heshima yake ilipotea. Ulikuwa huwezi ukayaona mawingu ya kitu kinapaa huko angani kilichoandikwa Tanzania.
"Nchi kubwa, watu milioni 55 hata ndege tulikuwa tumekosa. Na ndege ndio heshima ya nchi. Tumeingia madarakani tukaamua lazima tuwe na ndege. Wakasema pesa atapata wapi. Nikasema pesa ziko kwa mafisadi na watazitema hata ikibidi kwa kutapika.
"Tukanunua ndege 6 bila kukopa. Zilipokuja hao hao waliokuwa wanaponda ndio wa kwanza kupanda hizo ndege. Tunawasamehe sana," alisema Dkt. Magufuli.
Aidha, Dkt. Magufuli alisema kwamba, kwenye nchi zilizostaarabika, huwa wanaungana hata wakiwa na itikadi tofauti.
"Tunajenga hivi vitu kwa ajili ya Watanzania wote na si familia zetu tu," alisema. Akaongeza: "Sekta ya madini imechangia 11.5% hadi 17% baada ya sisi kubana wanyonyaji."
Rais Magufuli alisema kwamba, wapo watu duniani hata ukiwabeba mgongoni ukawavusha mto wakifika ng'ambo watasema "limgongo lake lilikuwa linanuka jasho".
" Tuwaombee tu, tusiyumbishwe tuko pazuri mno," alisema. "Wako watu waliokuwa wamezowea fedha za bure za kuwaibia maskini hao ndio wanapiga kelele sana. Ninafahamu hata makanisani zaka zimepungua sababu zilikuwa zinatolewa na mafisadi."
Dkt. Magufuli akaongeza: "Watendaji wangu wanafanya kazi sana. Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wanafanya kazi ndiyo maana tuko salama leo. Ilifikia kipindi hata kwenda Kibiti ilikuwa shida, hatukuona mtu yeyote analaani."
Alisema wakati wa mauaji ya Kibiti hakuna aliyelaani wala kutoa waraka, na sasa Kibiti kumekuwa salama watu wamekaa kimya.
"Ingawaje sipendi sana kulizungumzia hili kwa sababu ninalijua wala halina msingi wala halitafanikiwa wala hakuna lolote. Kwa sababu Serikali ipo nimekabidhiwa na wananchi kuilinda kwa nguvu zote. Na ninasema kweli kweli; Wengine nawaangalia tu nawacheki nasema "Hiiiiiiiiii"," alisema.
Aliongeza kwamba, Baba wa Taifa (Mwalimu Julius Nyerere) alishasaidia nchi nyingine kupata uhuru, hivyo jukumu lake sasa ni kujenga uchumi wa taifa.
"Katika juhudi hizi watatokea wa kunung'unika, wa kupiga kelele hata sitawasikiliza," alisema.
Aliongeza: "Kazi ya uongozi ni ngumu sana, unageuka huku unakuta watu wanalalamika. Hata Wakina Musa walipata shida, unawavusha watu unakuta wengine wameshajenga na sanamu la dhahabu."
Alitolea mfano miradi ya maendeleo kama Stiegler's Gorge, Ndege 6, SGR ambayo haikuwepo miaka iliyopita na sasa inakwenda kwa kasi kwa manufaa ya Watanzania.

Comments